Alliance for Change and Transparency-Tanzania Maoni ya ACT-Tanzania kuhusu namna ya kutoka katika mkwamo uliopo katika mchakato wa Katiba Mpya.
1. Nchi yetu iliingia katika mchakato wa Katiba kwa kushirikisha wananchi wote ili kupata Katiba bora yenye kuakisi matakwa ya nchi kwa sasa na baadaye. Ili kupata Katiba bora na inayokubalika na wananchi wengi iwezekanavyo, ni lazima mchakato wa kutunga Katiba uwe wazi, shirikishi na wenye kuzaa mwafaka na maridhiano miongoni mwa makundi mbalimbali ya wananchi
2. Chama cha ACT-Tanzania kinaipongeza sana Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyofanya kazi yake kwa bidii, umakini na weledi mkubwa kwa kuwashirikisha wananchi kwa upana wake na kwa kuzingatia maoni ya wananchi na matakwa ya nchi ya sasa na baadaye katika kuandika Rasimu ya Katiba.
3. Chama cha ACT-Tanzania kilitarajia kwamba Bunge Maalumu la Katiba lingeiga na kuendeleza utamaduni wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika kuhakikisha kwamba mwafaka na maridhiano yanapewa nafasi katika kila hatua ya mjadala badala ya kuzingatia misimano ya vyama vya siasa na wingi wa wajumbe wanaounga mkono hoja fulani katika mijadala. Bahati mbaya Bunge Maalumu la Katiba limeshindwa kuzingatia utamaduni wa maridhiano uliojengwa na wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
4. Chama cha ACT-Tanzania kimesikitishwa sana na viongozi wa vyama vya siasa wa CCM na vile vinavyounda kundi la UKAWA kwa kushindwa kwao kupata mwafaka na maridhiano kuhusu muundo wa muungano wa nchi yetu na hata kusababisha kuvurugika kwa mchakato wa Katiba. Ni aibu kwamba mchakato mzima wa Katiba katika Bunge Maalumu umetekwa na sera za vyama vya siasa kuhusu muundo wa serikali ya Muungano badala ya kutafakari na kujadaili Rasimu ya Katiba kwa upana wake na kwa maslahi ya nchi na wananchi kwa ujumla.
5. Chama cha ACT-Tanzania kinasikitika kwamba Bunge Maalumu la Katiba linaendelea na ratiba yake ilihali kundi kubwa la wajumbe likiwa nje ya mchakato. Bila kujali sababu za kundi la UKAWA kuwa nje ya Bunge Maalumu la Katiba, ACT- Tanzania haiamini kwamba mchakato huu utadhaa Katiba bora na yenye kukubalika kwa upana bila makundi yote muhimu kushiriki katika mchakato huu kwa ukamilifu wake mwanzo hadi mwisho. Ni maoni ya ACT-Tanzania kuwa tukiendelea na mchakato kama ulivyo sasa inawezekana tukapata katiba mpya yenye uhalali kisheria. Lakini itakuwa ni katiba isiyo na uhalali wa kisiasa wala kijamii, na kwa maana hiyo itakuwa haina tofauti ya maana na katiba ya sasa na hivyo kuifanya nchi kuingia kwenye hasara kubwa ya fedha za umma.
6. ACT-Tanzania haioni uwezekano wa kupatikana katiba mpya iliyo bora katika kipindi hiki, hasa kwa kuzingatia mkwamo uliomo baada ya wajumbe kujikita katika misimamo ya vyama vyao badala kujadili rasimu ya katiba mpya kwa uhuru, umakini na weledi.
7. Kutokana na mazingira ya mchakato wa Katiba tuliyoeleza hapo juu, ACT-Tanzania inapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe mapema iwezekanavyo ili kunusuru mchakato wa Katiba na kurudisha hali ya kuelewana katika jamii yetu:
a. Bunge Maalumu la Katiba lisimamishwe ili kuendelea kutoa fursa ya mazungumzo ya kutafuta mwafaka na maridhiano.
b. Mchakato wa kuandika katiba mpya uahirishwe hadi baada ya uchaguzi mkuu.
c. Katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu, Bunge la Jamhuri ya Muungano lifanye marekebisho katika katiba ya sasa ili kutengeneza mazingira ya uchaguzi ulio huru na haki.
Tunapendekeza marekebisho ya katiba ya sasa katika maeneo kumi (10) yafuatayo:
i) Tume ya Uchaguzi iwe huru na ionekane kuwa huru,
ii) Kuruhusu mgombea binafsi na wabunge ‘kukatisha kapeti’ bila kupoteza ubunge wao ili kudhibiti ubabe wa vyama vya siasa
iii) Kushusha umri wa mgombea urais ili kuwapa vijana haki na fursa ya kugombea katika nafasi hii muhimu, hasa ukizingatia kwamba karibu theluthi mbili (65%) ya wapiga kura wote Tanzania wapo chini wa umri wa miaka 40, na ukweli kwamba takwimu za Tume ya Marekebisho ya Katiba zinaonyesha kuwa wananchi walio wengi (53.7%) waliotoa maoni kuhusu umri wa mgombea urais walitaka umri huo ushushwe.
iv) Kuweka sharti kwamba ili mgombea atangazwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano lazima apate angalau asilimia 50 ya kura zilizo halali.
v) Kuweka msingi wa kikatiba kwamba wagombea Urais lazima wawe na angalau midahalo mitatu katika kipindi cha kampeni.
vi) Kuondoa suala la Mafuta na Gesi katika mambo ya Muungano ili kuruhusu Zanzibar kuendelea na utafutaji wa Mafuta na Gesi asilia kwa uhuru na bila kuingiliwa na Tanzania bara
vii) Kuruhusu Zanzibar kuwa na mahusiano na ushirikiano wa kimataifa (International Cooperation) kwa faida za maendeleo yake.
viii) Kuweka mipaka ya Mashtaka ya Kesi za Rushwa ili kuruhusu TAKUKURU kufanya uchunguzi na kuendesha kesi hususani kwa kesi ufisadi wa mali umma bila kupita kwa Mkurugenzi wa Mashtaka.
ix) Kuweka msingi wa kisheria wa Tangazo la Mali na Madeni ya Viongozi kuwa wazi kwa Umma na uthibitisho wa uhalali wa mali ambazo mtu anamiliki uwe upande wa mtuhumiwa (reverse of burden of proof).
x) Kuweka msingi wa Kikatiba wa Uhuru wa kupata habari kwa wananchi (Freedom to access information) na kupiga marufuku vyombo vya habari kufungiwa isipokuwa kwa amri ya mahakama.
8 Chama cha ACT-Tanzania kinatoa wito kwa wadau wote wa Katiba kuungana katika kushinikiza mchakato wa Katiba unaoendelea kusimamishwa na kuruhusu mabadiliko hayo machache ya Katiba ya sasa ili kupisha uchaguzi na kuhakikisha Taifa linapata muda wa kutosha wa kuandika Katiba bila shinikizo na katika hali ya utulivu.
8 ACT-Tanzania inawataka mahasimu katika mchakato wa Katiba kutoa fursa kwa majadiliano na kujenga mwafaka na maridhiano ya nchi katika maeneo hayo. Tunasisitiza kwamba tusichoke kuzungumza katika masuala ya nchi yetu kwani mbadala wa mazungumzo ni fujo na upotevu wa amani.
Asanteni kwa kunisikiliza
Ndugu Samson Mwigamba
Katibu Mkuu, ACT-Tanzania.