Mwanachuo UDSM kizimbani akituhumiwa wizi wa milioni 51/=

Meneja wa kituo cha mafuta cha Gudal Petrol Station cha Ubungo, Kibangu Saadi Mohamed (21) pamoja na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),  Edwin Mbuya (21), wamepandishwa kizimbani kwa mashitaka mawili.

Watuhumiwa hao wakazi wa Ubungo-Kibangu walipandishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la wizi wa fedha taslimu Sh milioni 51.6 mali ya kituo hicho.

Mbele ya Hakimu Kwey Rusema, Wakili wa Serikali, Credo Rugaju, alidai kuwa katika shitaka la kwanza, washtakiwa hao walikula njama ya kutenda kosa katika tarehe na muda usiyojulikana maeneo ya Kinondoni.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Julai 28 mwaka huu, washtakiwa waliiba fedha taslimu Sh 51,689,500, mali ya Kituo cha Gudal Petrol Station kilichopo Ubungo Kibangu. Washtakiwa walikana. Upelelezi umekamilika. Kesi imepangwa kusikilizwa Agosti 19 mwaka huu. -- via HabariLeo