Niko tayari kugombea Jimbo la Mrema mwaka 2015 - Mbatia

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ametangaza rasmi nia yake ya kuwania ubunge katika Jimbo la Vunjo, lililopo Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Mbatia, ambaye pia kwa sasa ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, alitangaza azma hiyo, jana ikiwa ni siku moja baada ya wafuasi wa vyama vya CCM, Chadema, NCCR-Mageuzi na TLP kumwita jimboni humo, wakimtaka achukue maamuzi magumu ya kurejea nyumbani kugombea ubunge.
“Ni kweli kabisa kuna wananchi wameniandikia barua, wengine walikuja Dodoma wakati wa Bunge la Bajeti na wengine wamenifuata Dar es Salaam hivi karibuni kuniomba nikubali kugombea ubunge. Kimsingi, nimewaelewa. Na siyo dhambi nikitamka kwamba, niko tayari kugombea Vunjo mwaka 2015,” 
alisema Mbatia.

Alisema kwa nafasi aliyonayo hivi sasa kama mbunge wa kuteuliwa na Rais kwa mujibu wa katiba na akiwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, ameridhia ombi la wananchi hao kwa kuwa wanathamini mchango wake katika kutetea walalahoi pamoja na rasilimali za nchi.

Hata hivyo, Jimbo la Vunjo kwa sasa linawakilishwa bungeni na Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Augustino Mrema, aliyeshinda kiti hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Juzi kiongozi wa wafuasi hao, Mathew Temu, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kwenye mji mdogo wa Himo, alisema uamuzi huo una baraka za wananchi wa jimbo hilo, ambao wametoa uwakilishi wa viongozi 15 kutoka katika kata zote za jimbo la Vunjo.

Kupitia tamko lao, ambalo NIPASHE inayo nakala yake, wafuasi hao licha ya kumtaka Mbatia agombee ubunge pia walimsihi asijipange kuwania urais kupitia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Tamko hilo linaeleza sababu za kumhitaji Mbatia kuelekeza nguvu zake nyumbani ni pamoja na kusuasua kwa sekta ya elimu, afya na miundombinu katika jimbo hilo.

Mrema alipotakiwa jana na NIPASHE kueleza hatua hiyo ya Mbatia, kwanza alitaka kujua idadi ya watu walioitisha mkutano na wanahabari na kumwita Mbatia aende kugombea ubunge katika jimbo hilo.

Alipojibiwa kuwa watu hao walikuwa zaidi ya 21, Mrema alihoji: “Kwani kuna tatizo gani?”

Mwandishi alipomjibu kwamba, ni yeye ndiye anayetakiwa atoe maoni yake kuhusiana na hatua hiyo ya Mbatia, Mrema alisema: “Nitaeleza baadaye.” na kisha akakata simu.

via NIPASHE