Polisi Zanzibar yamshikilia Mansour Himid kwa kumiliki silahaJeshi la Polisi visiwani Zanzibar linamshikilia aliekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki kupitia tiketi ya CCM Bwana Mansour Yussuf Himid.

Akieleza sababu za kukamatwa kwake Naibu mkurugenzi wa makosa ya jinai Zanzibar wakati akizungumza na Mazrui media, Bwana Salum Msangi amesema wamemshikilia Mansour baada ya kupata taarifa za raia wema kuwa anamiliki silaha.

Alieleza kuwa mara baada ya kupata taarifa hio jeshi hilo liliamua kufanya msako maalumu nyumbani kwa aliekuwa Mheshimiwa huyo mnamo majira ya 2:30 asubuhi huko Chukwani nje kidogo ya mji wa
Zanzibar na ndipo walipokuta silaha za aina mbili.

Akizitaja miongoni mwa silaha hizo Msangi amesema ni Bunduki moja aina shotgun yenye risasi 112 pamoja na bastola aina ya beretta aliokuwa na risasi 295.

Ameleza kuwa licha ya silaha hizo kumilikiwa kihalali na Mansour lakini kisheria hazikutakiwa ziwe na risasi nyingi kiasi hicho kama zilivokutwa nyumbani kwa Mansour.

Aidha ameleza kwa mujibu wa sheria ya Zanzibar silaha aina ya bastola ilitakiwa isizidi risasi 25 na bunduki aina ya shotgun isizidi risasi 20.

Licha hayo Naibu Mkurugenzi huyo amefafanua sheria ya Zanzibar haimruhusu mmiliki yoyote wa silaha kihalali kubaki nayo nyumbani kwake isipokuwa aikabidhi kituo cha polisi na anaweza kuifata wakati akilazimika kuitumia.

Jeshi la Polisi visiwani Zanzibar limetoa wito kwa wamiliki wote wa silaha kuzingatia sheria halali za umiliki wa silaha ili kujiepushia matatizo.