Rais Dk Shein ateua viongozi kujaza nafasi za watendaji

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amefanya uteuzi wa viongozi katika taasisi mbalimbali za serikali ili kujaza nafasi zilizo wazi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, walioteuliwa ni pamoja na CRD Juma Haji Juma kuwa Mkuu wa utawala kikosi maalum cha kuzuia magendo (KMKM). Uteuzi huo ulifanywa chini ya kifungu cha 53 cha katiba ya Zanzibarya mwaka 1984.

Aidha Dk. Shein amemteua Meja Yussuf Khamis Yussuf kuwa Mkuu wa Utawala KVZ.

Wengine walioteuliwa ni Kanali Ali Mtumweni Hamad kuwa Mkuu wa utawala JKU, SACP Ali Abdulla Ali kuwa Naibu Kamishna wa chuo cha mafunzo, Abdulla Ali Ussi kuwa ofisa mdhamini Shirika la Biashara Pemba kuchukua nafasi ya Abdulmalik Mohamed Bakari ambaye atapangiwa kazi nyengine.

Wengine ni Sharifa Khamis Salim alieteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Zanzibar (BTMZ) na Abdalla Suleiman Abdalla kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Utawala wa Umma, Zanzibar.

Uteuzi wa watendaji hao ulianza Julai 16, Agosti 11, 12, 14 na 18 mwaka huu.