TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
- Asisitiza kuwa tatizo ni wafugaji kulisha ng’ombe mashambani
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameahidi kuwa Serikali yake italipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo sugu la ugomvi kati ya wakulima na wafugaji katika Mkoa wa Morogoro ambalo kimsingi linasababishwa na wachungaji kuingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima.
Aidha, Rais Kikwete amewataka wachungaji kuacha mara moja tabia yao ya kuingiza na kulisha ng’ombe wao katika mashamba ya wakulima akisisitiza kuwa hicho ndicho chanzo cha ugomvi kati ya makundi hayo
mawili.Rais Kikwete ambaye anafanya ziara ya siku saba katika Mkoa wa Morogoro ametoa ahadi ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa ugomvi kati ya makundi hayo baada ya kulalamikiwa kila aliposisima na wananchi kuhusu tabia ya wafugaji kuingiza na kulisha ng’ombe wao katika mashamba ya wakulima.
Akiwa njiani kutoka Ifakara, Wilaya ya Kilombero kwenda Wilaya ya Morogoro, Rais Kikwete ameshuhudia mwenyewe malalamiko hayo ya wananchi dhidi ya tabia hiyo ya wafungaji ambao wengi wao siyo wakazi ama wenyeji wa Mkoa wa Morogoro.
Baada ya kujaribu kuwaeleza wananchi katika maeneo mbali mbali kuhusu chanzo cha ugomvi huo na nini hasa ufumbuzi wa suala hilo, Rais Kikwete amewaambia wananchi katika Kijiji cha Mgalegole-Mngazi, eneo la Duthumu, Tarafa ya Bwakira: “Nakwenda sasa kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili. Ni lazima tukomeshe tatizo hili.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Kimsingi, huu ni ugomvi usiostahili kwa sababu kila mmoja kati ya makundi haya anamhitaji mwenzake. Wafugaji wanahitaji chakula…ugali na mchele..kutoka kwa wakulima. Nao wakulima wanahitaji kitoweo…nyama kutoka kwa wafugaji. Kubwa hapa ni wafugaji kuacha kulisha ng’ombe kwenye mashamba ya watu wengine.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Mnawaachia watoto kuchunga ng’ombe. Wanaingiza mifugo katika mashamba ya watu. Wakiwauliza mnawapiga, mnawajeruhi. Acheni mambo haya.”
Rais Kikwete ameanzia ziara yake ya leo kwa kuweka jiwe la msingi katika upanuzi wa Kituo cha Afya Kibaoni, mjini Ifakara, ambacho kinapanuliwa kuwa Hospitali ya Wilaya na baadaye akakabidhi madawati 278 kwa shule 17 za msingi za Tarafa za Mang’ula na Kidatu katika Wilaya ya Kilombero. Madawati hayo yametolewa na Shirika la Taifa la Hifadhi (TANAPA).
Baada ya hapo, Rais Kikwete ambaye anafuatana na Mama Salma Kikwete katika ziara hiyo amepanda treni ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kwenda Kisaki, Wilaya ya Morogoro, ambako amelakiwa na mamia kwa mamia ya wananchi.
Baadaye, Rais Kikwete amezindua Mradi wa Maji wa Duthumu ambao umefadhiliwa na wanachama wa Lions Clubs za Sweden na pia kuzindua vifaa na huduma ya upasuaji katika Kituo cha Afya katika eneo hilo.
Katika mji mdogo wa Mtamba, Rais Kikwete amezindua soko jipya la kisasa na kuzungumza na wananchi ambako aliahidi kuwa Serikali imeanza kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Barabara ya Bingwa-Mvua kwa kiwango cha lami.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.22 Agosti,2014
Ikulu – Dar es Salaam.22 Agosti,2014