Sababu ya kuchelewa kwa mishahara mwezi Julai


Naibu Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba akiongea na waandishi wa habari kufafanua juu ya malipo ya mishahara.


Serikali imebainisha kuwa mabadiliko ya mfumo wa ulipaji wa mishahara kwa watumishi katika mwaka huu wa fedha ndiyo uliochangia uchelewaji uliojitokeza katika baadhi ya taasisi.
“Nimeagiza watumishi wote wa Serikali malipo yao yafanywe kupitia akaunti zao za benki ili kupunguza malipo hewa yaliyokuwa yanafanywa na wahasibu wasio waadilifu. Awali, tulikuwa tunapeleka fedha katika taasisi husika na wao walikuwa wanafanya malipo hayo,”
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizindua matawi 10 ya Taasisi ya Huduma za Fedha na Mikopo (UTT- Microfinance).

Nchemba ameonya na kuzitaka mamlaka husika ziwe na taarifa sahihi za idadi ya watumishi ili kuondoa makosa ya kulipa mishahara hewa, la sivyo watakaolipa mishahara hewa watachukuliwa hatua za kisheria na kufikishwa mahakamani.