Sehemu ya pili: Afisa Usalama wa Taifa "Shushushu" ni nani, anafanya nini?


Makala ya Evarist Chahali

Nianze sehemu hii ya pili ya mfululizo huu kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa wote waliowasiliana nami kuhusiana na mada hii. Kutokana na mawasiliano hayo, nimetambua kuwa mada hii ina umuhimu wa aina yake. Nami ninaahidi kuwaletea kitu kilicho bora kabisa, kwa maana ya 'darasa' kamili lakini pasipo kukiuka wala kukizana na sheria au taratibu zinazolinda fani hii nyeti.

Katika sehemu hii ya pili, tutaangalia jinsi afisa usalama wa taifa anavyopatikana, au kwa kimombo ni recruitment process. Ni muhimu kueleza kwamba taratibu za kujiunga na taasisi za usalama wa taifa duniani kote hupaswa kufanywa kwa umakini mkubwa hasa kwa vile majukumu na wajibu wa shushushu kwa taifa yana umuhimu mkubwa sana.

Kwa nchi 'za wenzetu' kama Marekani na Uingereza, zoezi la uajiri hufanyika kwa uwazi kidogo, kwa
maana kwamba matangazo ya nafasi za kazi huwekwa hadharani. Mifano hai ni matangazo ya ajira za ushushushu katika tovuti ya Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na Shirika la Ujasusi la Uingereza (MI6)
Kwa huko nyumbani Tanzania, zoezi la uajiri wa mashushushu hufanyika kwa usiri mkubwa (angalau taratibu zinapaswa kuwa hivyo). Na hata kwa mashirika ya kishushushu ya nchi nyingine, ajira za wazi kama nilivyoonyesha hapo juu hazimaanishi kuwa waajiriwa wote wa mashirika hayo hupatikana kwa uwazi.

Kimsingi, na pengine tukitumia mfano 'mwafaka' wa Idara yetu ya Usalama wa Taifa huko nyumbani, kinachoangaliwa kwa mtu anayetakiwa kuajiriwa ni 'vitu vya ziada' pengine tofauti na watu wengine. Katika mazingira stahili (ideal situation) shushushu mtarajiwa anatarajiwa kuwa na uwezo mkubwa wa akili, yaani kama nilivyoeleza katika makala iliyopita kwamba kazi yenyewe ni ya matumizi makubwa ya akili, kwahiyo mtarajiwa anapaswa kuwa intelligent kweli kweli.


Tukiendelea na mazingira hayo stahili, taasisi ya ushushushu huanza kitambo 'kumwinda' wanayetaka kumwajiri. Sehemu mwafaka zaidi za kusaka mashushushu watarajiwa ni katika taasisi za elimu. Sababu kuu za msingi za kutumia taasisi za elimu kama 'soko' la 'kuchagua mashushushu watarajiwa' ni, kwanza, umri wa wanafunzi wengi huwa mwafaka kuonyesha tabia zao halisi, na pili, taasisi ya elimu hutoa ushahidi mzuri wa kiwango cha akili cha shushushu mtarajiwa.


Sehemu nyingine iliyokuwa mwafaka kuwasaka mashushushu watarajiwa ilikuwa kwenye kambi za jeshi la kujenga taifa. Wakati taasisi za elimu zinatoa fursa nzuri kutambua uwezo wa akili wa shushushu mtarajiwa, kambi za JKT zilikuwa zikitoa fursa nzuri ya kuangalia uwezo wa kimwili, hususan uvumilivu (indurance). Kwa waliobahatika kupitia JKT wanafahamu bayana kuwa mafunzo ya awali (takriban miezi 6 ya mwanzo) yalikuwa yanaufikisha mwili katika kiwango cha juu kabisa cha uvumilivu. Ni katika mazingira kama hayo ndipo taasisi za kishushushu zinaweza kupata fursa ya kuona 'uwezo wa ziara' au 'usio wa kawaida' wa shushushu mtarajiwa.

Kadhalika, zamani kulikuwa na shule mbili-katika-moja iliyokuwa na mchepuo wa kijeshi. Shulke hiyo ni Tabora School, ambayo kimsingi ni Shule ya Sekondari ya Tabora Wavulana (Tabora Boys) na Tabora Wasichana (Tabora Girls). Shule hizi ambazo kimfumo zilikusanya wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao kutoka takriban kila wilaya ya Tanzania zilitoa fursa nzuri kwa Idara ya Usalama wa Taifa kupata maafisa wake watarajiwa. Uzuri wa shule hizo ni kwamba zilitoa fursa mbili kwa mpigo: fursa kwa mashushushu kupima uwezo wa kiakili wa mtarajiwa na pia kuona uwezo wake kimwili kupitia mazoezi na mafunzi ya kijeshi katika shule hizo. Vilevile, shule hizo ambazo pia zilikuwa na maafisa wa jeshi kama walimu, na wanafunzi wanaovaa sara zinazofanana na za kijeshi , zilitawaliwa na nidhamu ya hali ya juu, sambamba na kuhimiza uzalendo.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora wakiwa katika mafunzo ya kivita

Lakini kwa vile ajira katika taasisi za kishushushu inazingatia zaidi mahitaji ya kimazingira, nyakati nyingine walengwa huwa watu waliopo makazini, kwa mfano wahadhiri, maafisa wa vyombo vingine vya dola - kwa mfano jeshi au polisi- na maeneo mengineyo. Ila ajira za namna hii ni za nadra kwa sababu mara nyingi watu wa aina hiyo 'huajiriwa' kama 'watoa habari' au sources kama wanavyofahamika kiintelijensia. Kinachoweza kuiskumua taasisi ya kishushushu kulazimika kumwajiri mtu ambaye tayari ana ajira nyingine au yupo katika fani tofauti ni unyeti wa nafasi yake na umuhimuwa wake wa muda mrefu.

Njia hii ni kama ya dharura au ya katika mazingira maalumu kwani kuna ugumu wa kumshawishi mhusika akubali kuajiriwa, na pengine mtu huyo anaweza kuwa na mtandao mkubwa wa kijamii - kwa maana ya familia au marafiki - na hilo linafanya sharti kuu la ajira kwenye taasisi yoyote ya usalama wa taifa, yaani USIRI, kuwa mashakani. Ni rahisi kumkanya mwanafunzi wa sekondari, kwa mfano, kwamba asimwambie mtu yeyote kuhusu jukumu atakalokabidhiwa mbeleni, na akalihifadhi - pengine kwa vitisho- kuliko mtu mzima ambaye inaweza kumwia vigumu kumficha mkewe au marafiki wa karibu. Na kama tujuavyo, ajira katika sehemu hizo zina 'ujiko' wa namna flani, kwahiyo si ajabu mtu mzima akiambiwa 'kuna dili' sehemu akaanza kutangaza kabla hata hajapewa mafunzo.

Kimsingi hakuna muda maalumu wa kumfuatilia mtu anayetakiwa kujiunga na taasisi ya kishushushu. Panapo dharura, zoezi la ufuatiliaji laweza kudumu kwa muda mfupi, lakini pasipo haraka yaweza kuchukua miaka kadhaa.


Baada ya kuwatambua 'waajiriwa watarajiwa' - process inayofahamika kama spotting - hatua inayoweza kufuata ni kuwa kuwaendeleza watarajiwa hao (yaani kuwaandaa kwa ajili ya utumishi kwa taasisi husika). Neno mwafaka ni development. Katika hatua hii, mashushushu HALISI wanakutana na mashushushu watarajiwa. Hatua hii inaweza kuchukua muda mfupi kutegemea mabo kahdaa au yaweza kuchukua muda mrefu pia. Hadi hapo, taasisi husika huwa haijafikia uamuzi wa kumwajiri mtarajiwa au la, bali inafanya marejeo ya ufuatiliaji wa awali na maendeleo ya mhusika katika kipindi hicho.

Sambamba na hatua hiyo, ni uamuzi kwa taasisi ya ushushushu kuanza kufanya ufuatiliaji wa kina kuhusu mtarajiwa. Ufuatiliaji huo hujulikana kama VETTING. Hata hivyo, uamuzi wa kufanya vetting hutarajia 'potential' ya mtarajiwa, hasa ikizngatiwa kuwa vetting ni process ndefu na inayoweza kuwa na gharama kubwa. Kwa kifupi, process hiyo inalenga kumfahamu mtarajia 'nje ndani' yaani kila kitu kumhusu yeye. Na hapo ndipo utabaini urahisi wa kutafuta mashushushu wapya wakiwa wadogo mashuleni- kwa vile hufanya vetting kutokuwa ndefu sana kutokana na kutokuwa na mtandao mkubwa wa mahusiano kijamii au kimaisha, ilhali kwa mtu mzima kazini itamaanisha kuwafuatilia watu wengi na pengine kutembelea sehemu nyingi pia. Na pindi vetting isipofanywa kwa umakini, dhamira nzima ya kufanya suala hilo kwa usiri linaweza kuathiriwa. Athari hizo si kwa taasisi ya kishushushu pekee bali pia yaweza kuyaweka maisha ya mtarajiwa hatarini.

Matokeo ya jumla ya vetting ndiyo yatakayoamua hatma ya ajira ya shushushu mtarajiwa. Nimesema 'matokeo ya jumla' kwa sababu hata baada ya kuajiriwa, shushushu huendelea kufanyiwa ufuatiliaji na mwajiri wake katika muda wake wote wa utumishi wake, na pengine hadi atakapoaga dunia. Kadhalika, vetting hujitkeza pia pindi shushushu anapotaka kuoa au kuolewa, ambapo mwenza wake hufanyiwa uchunguzi ili kuthibitika kuwa hatokuwa na madhara kwa utendaji wa kazi wa shushushu husika.

Kwa leo niishie hapa. Makala ijayo itaangalia hatua ya kutoka kuajiriwa hadi mafunzo, na itaelemea zaidi kwenye mafunzo. Endelea kufuatilia makala hii pamoja na habari nyingine mbalimbali, na zinazohusu intelijensia kwa kubonyeza hapo juu ya blogu kwenye kipengele cha INTELIJENSIA