Sehemu ya tatu: Afisa Usalama wa Taifa "Shushushu" ni nani, anafanya nini?


Makala ya Evarist Chahali

Nianze makala hii kwa kuomba samahani kutokana na kuchelewesha mfululizo huu wa makala kuhusu taaluma ya ushushushu. Baadhi ya wasomaji wamehoji ukimya huo, huku wengine wakidhani kwamba 'wahusika' wamenizuwia. Ninapenda kurejea nilichokiandika katika sehemu ya kwanza ya makala hii kwamba mfululizo huu unazingatia sheria na maadili na 'wahusika' hawana sababu ya kuuzuwia.

Kwa kukumbushana tu, sehemu ya kwanza iliitambulisha taaluma ya ushushushu kwa ujumla, wakati sehemu ya pili ilielezea jinsi mashushushu wanavyopatikana (recruitment). Katika sehemu hii ya tatu tutaangalia mafunzo ya mashushushu wanafunzi.

Ninakumbuka siku moja niliwahi kuulizwa swali na rafiki yangu flani huko Twitter iwapo walinzi wa viongozi (bodyguards) nao ni mashushushu kwa maana ya kupitia mafunzi kama 'mashushushu wa kawaida.' Jibu langu kwake litatoa mwelekeo wa makala hii, kwamba, kwanza japo taaluma ya
ushushushu ina maeneo flani yanayofanana mahala popote pale duniani, vitu kama mazingira, mahitaji ya nchi/taasisi ya kishushushu, na pengine uwezo wa kiuchumi hupelekea tofauti kati ya taasisi moja na nyingine. Nitoe mfano. Kwa nchi kama Marekani, taasisi ya kishushushu inayohusika na ulinzi wa viongozi (US Secret Service) 'inajitegemea' kwa maana ya ajira,mafunzo na utendaji kazi. Wanaojiunga na taasisi hiyo ni lazima wapitie kozi ya awali ya upelelezi wa jinai (Basic Criminal Investigator Training) inayodumu kwa wiki 10, na inayofanyika katika chuo cha Federal Law Enforcement Training Centre kilichopo Glynco, Georgia, na kisha kufanya kozi nyingine ya wiki 17 inayojulikana kama Speicla Agent Basic Training, inayofanyika katika chuo cha James J. Rowley Training Centre, nje kidogo ya jiji la Washington DC.
Kwa minajili ya kuepuka mkanganyiko, nitatumia mfumo unaotumiwa na Idara yetu ya Usalama wa Taifa (TISS) katika maelezo kuhusu mafunzo ya mashushushu. Tofauti na Marekani, Idara yetu ya Usalama ni taasisi moja yenye vitengo mbalimbali. Na katika jibu nililompatia rafiki yangu ailiyeniuliza huko Twitter, maafisa usalama wanaolinda viongozi wetu huajiriwa kama afisa usalama mwingine yeyote yule. Katika mazingira ya kawaida, baada ya Idara ya Usalama wa Taifa kumaliza mchakato wa kuwapata mashushushu watarajiwa (process niliyoieleza kwa undani katika makala iliyopita), hatua inayofuata ni mafunzo.

Kwa huko nyumbani, kila shushushu mpya hupatiwa mafunzo kupitia kozi ya awali ya uafisa (Junior Basic Course) katika chuo chao kilichopo pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam. Urefu wa kozi hutegemea vigezo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mahitaji ya Idara yenyewe.

Muundo wa mafunzo:

Kimsingi, na katika mazingira ya kawaida, kozi hiyo ya awali hugawanywa katika sehemu kuu tatu: mafunzo ya kijeshi na ukakamavu, mafunzo ya mapambano pasipo silaha (unarmed combat) na mafunzo ya ushushushu 'halisi.'

Mafunzo ya kijeshi na ukakamavu hujumuisha 'kwata' za kijeshi (kama zile wanazofunzwa 'makuruta' katika Jeshi la Kujenga Taifa). Kabla ya kuanza kozi hii, mashushushu watarajiwa hufanyiwa uchunguzi wa kiafya kubaini iwapo wataweza kumudu shuruba zinazoambatana na kozi hiyo. Na kwa hakika ni hatua ngumu mno, ambapo kwa takriban kila 'intake' kuna 'wanafunzi' wanaoamua kuomba ruhusa ya kuondoka baada ya kushindwa kustahilimi ugumu wa mafunzo hayo.

Haya ni mafunzo ya kijeshi 'halisi' kwa maana ya drills za kijeshi, mafunzo ya msingi ya kivita ikiwa ni pamoja na usomaji ramani katika uwanja wa mapambano, ulengaji shabaha, uelewa kuhusu silaha mbalimbali, nk. Sambamba na mafunzo hayo ni mazoezi makali ya viungo na ukakamavu. Kadhalika, mafunzo hao huambatana na kujenga nidhamu ya kijeshi pamoja na uvumilivu (ni jambo la kwaida kwa 'wanafunzi kupitisha usiku kadhaa bila kulala). Mafunzo haya huendeshwa na wakufunzi wa kijeshi ambao pia ni waajiriwa wa Idara ya Usalama wa Taifa.

.


Hatua inayofuata ni kozi ya mapambano bila silaha (unarmed combat). Katika kozi hii, mashushushu watarajiwa hufundishwa jinsi ya kupambana na adui kwa kutumia mwili pekee, yaani bila kuwa na silaha. Walimu wa kozi hii huitwa Sensei na kozi hujanyika katika ukumbi ujulikanao kama dojo. Kadhalika, 'wanafunzi' huvaa ' mavazi maalum' yajulikanayo kama Kimono.

Pasipo kuingia ndani zaidi, kozi hii hufuata mfululizo wa hatua zinazojulikana kama 'kata.' Kwa lugha nyepesi, kata ni movements za mtu mmoja mmoja au zaidi, na kila moja ni mfumo wa mapambano. Kila kata ina jina, na majina hayo yana asili ya Mashariki ya Mbali, ambapo fani ya mapambano bila silaha ni sehemu muhimu ya utamaduni kwa nchi kama China,Japan, Korea, nk. Ili kujifunza kata inayofuata ni lazima kuimudu kata ya awali. Ni kama vile hatua za makuzi ya mtoto, hawezi kuanza kukimbia kabla ya kutamaa.

.

Kwa minajili ya kurahisisha maelezo, kozi hii hujumuisha karate, judo, ngumi,nk. Kadhalika, japo mafunzo yanaitwa mapambano bila ya silaha, ukweli ni kwamba kuna baadhi ya kata huhusisha matumizi ya/ kujilinda dhidi ya silaha ndogo japo hatari kama vile visu, jambia la mapambano, minyororo, nk. Katika kozi hii, 'wanafunzi' hufunzwa pia kuhusu 'sehemu za udhaifu katika mwili wa binadamu' (weak points) kwa minajili ya kutambua eneo gani la mwili wa adui likidhibitiwa anakuwa 'hana ujanja.'

.

Hatua ya tatu ni mafunzo 'halisi' ya ushushushu. Kwa ujumla, mafunzo haya humfundisha shushushu mtarajiwa mbinu za kukusanya taarifa za kiusalama kwa siri, kuzichambua na 'kuzifanyia kazi.' Kwa ujumla pia, kozi hii hugawanywa katika makundi mawili: ushushushu ndani ya nchi na ujasusi ushushushu nje ya nchi. Kadhalika, masushushu wanafunzi hufunzwa kitu kinachoitwa 'shughuli za adui' yaani ujasusi (espionage), uzandiki (subversion), hujuma (sabotage) na ugaidi (terrorism). Vilevile, hufunzwa mbinu za kunasa mawasiliano (bugging), ufuatiliaji wa siri (surveillance), jinsi ya kupata watoa habari (recruitment of sources) na jinsi ya kuwamudu, ikiwa na pamoja na jinsi ya 'kuwamwaga' (kuachana nao) pale wanapopoteza umuhimu.

Pengine la kuchekesha katika hatua hii ya mafunzo ya ushushushu ni hisia kwamba 'mashushushu hufundishwa kutongoza.' Kuna aina flani ya ukweli katika hilo japo kinachofundishwa sio jinsi ya kutongoza mwanamke bali kutongoza kwa minajili ya kupata taarifa. Na pengine neno 'kutongoza' sio stahili kwani lina connotation na mambo ya ngono.

Japo mbinu za kukusanya taarifa za kiusalama (methods of elicitation) ni maalum kwa matumizi ya mashushushu, kimsingi zinatumika katika fani nyingine, kwa mfano watafiti wanapofanya mahojiano kwa ajili ya tafiti zao.Tofauti ya msingi ipo kwenye usiri unaoambatana na mbinu husika, kwa mfano mtu kuhojiwa pasi kujua anahojiwa na shushushu. Mfano mmoja wa mbinu hizo ni kinachotwa 'incorrect supposition.' Mbinu hii inatumia udhaifu wa kawaida wa binadamu kutotaka kuelezwa isivyostahili. Kwa mfano, katika kutaka kufahamu kama mtumishi wa kawaida tu ana 'fedha zaidi ya uwezo wake.' shushushu anaweza kumwambia mtu huyu "ah inadaiwa wewe ni masikini tu ambaye hata kodi ya nyumba ya kupanga inakusumbua." Katika mazingira mwafaka, mhusika atakurupuka na kujigamba, "ah wapi bwana. Utawaweza waswahili kwa uzushi? Mie nina nyumba kadhaa hapa mjini, na lile duka la spea pale Kariakoo ni langu..." Kwahiyo wakati mwingine ukiskia mtu anang'ang'ania kusema kitu kisicho sahihi dhidi yako, usikimbilie kudhania anakudhalilisha au hajui ukweli.Yawezekana 'anakulengesha' umpatie ukweli anaohitaji.

Mbinu nyingine ni ya 'nipe nikupe.' Nakupa unachodhani ni taarifa za siri (naam, pengine ni za siri kweli lakini hazina madhara) ili nawe unipe taarifa ninazohitaji. Ni kile wanaita 'Quid Pro Quo.'

Jambo jingine ambalo mashushushu wanafunzi hufundishwa muda wote ni kitu kinachofahamika kama constant vigilance of an officer, yaani afisa usalama wa taifa anapaswa kuwa macho muda wote, huku akitambua kuwa uhai wa taifa lake upo mikononi mwake muda wote. Pengine tafsiri ya kanuni hiyo ni 'kujitambua muda wote.' Kutambua dhamana aliyonayo afisa usalama kwa taifa. Kadhalika, mafunzo huhusisha pia kujenga na kuimarisha matumizi ya 'hisia ya sita.' Kama nilvyoeleza katika makala ya kwanza, binadamu tuna hisia tano: kuona kwa kutumia macho, kusikia kwa kutumia masikio, kunusa kwa kutumia pua, ladha kwa kutumia ulimu na kuguswa (touch) kwa kutumia ngozi. Hisia ya sita ni kitu cha zaida ya hivyo vitano. Ni vigumu kueleza katika mazingira ya kawaida ila labda kwakifupi ni ule uwezo wa kwenda mbali zaidi ya uwezo wa kawaida wa hisia: kuamini au kutoamini pale inapopaswa kuamini au kutoamini, kutambua hatari hata bila ya kupewa tahadhari, nk.

Awali nimetaja kuhusu vitendo vya adui, yaani ujasusi, uzandiki, hujuma na ugaidi. Kimsingi japo hivi ni vitendo vya adui na njia ya kupambana nayo ni kinachojulikana kama counterintelligence au CI kwa kifupi, mashushushu wanafunzi hufunzwa pia mbinu 'za kiadui.' Ni hivi, kuna nyakati serikali au taasisi ya usalama hulazimika kupelekea amshushushu wake nje ya nchi, na kimsingi hawa ndio wanaoitwa spies, na kitendo chenyewe ndio espionage (ujasusi), lengo si 'kutengeneza maadui' bali kuwapatia mashushushu uwezo wa kukusanya taarifa za kiusalama nje ya nchi. Miongoni mwa kanuni anazofundishwa shushushu mwanafunzi ni pamoja na uwezekano wa kukanwa na nchi yake pindi akikamatwa kwenye operesheni za nje ya nchi. Vilevile, mashushushu hufunzwa kuhusu kitu kinachofahamika kama 'kifuniko' (cover ) yaani utambulisho bandia. Kwa mfano, balozi takriban zote duniani huwa na majasusi wanaojipachika vyeo kama 'mwambata wa siasa' au mwabata wa ulinzi.' Ieleweke kuwa japo ushushushu ni fani inayokubalika, serikali rafiki ikitambua shughuli za maafisa usalama wa nchi nyingine rafiki, yaweza kupelekea matatizo makubwa. Na mara nyingi ukisikia serikali imewafukuza maafisa ubalozi flani basi mara nyingi watu hao ni mashushushu 'waliojificha' kama maafisa ubalozi.

Vilevile, katika muda wote wa mafunzo, mashushushu watarajiwa huhamasishwa kuhusu uzalendo, thamani ya nchi yao, umuhimu wa kuilinda muda wote, umuhimu wa taaluma hiyo katika ustawi na mustakabali wa taifa lao,nk. Na siku ya kuhitimua mafunzo, kila shushushu huapa kwa kushika alama muhimu za taifa- katiba/bendera ya taifa, na kuweka kiapo cha kuitumikia nchi yake kwa uwezo wake wote, sambamba na viapo vingine vya kikazi (kwa mfano kamwe kutotoa siri za nchi na za Idara). Japo kuna hisia 'mtaani' kwamba watu walioacha au kuachishwa ushushushu huogopa kutoa siri kwa kuhofia kuadhibiwa, ukweli ni kwamba kiapo wanachokula wakati wa kuhitimu mafunzo ni 'kizito' mno kiasi kwamba katika mazingira ya kawaida, mhusika atajiskia nafsi inamsuta kusaliti kiapo hicho.

Licha ya mafunzo ya darasani, kuna mafunzo ya nje ya darasa ambapo mashushushu watarajiwa 'humwagwa mtaani' kufanya mafunzo ya vitendo.

Kubwa zaidi wakati mafunzo yanaendelea ni usiri wa hali ya juu. Katika mazingira ya kawaida, kila shushushu mwanafunzi huwa amefika ukweli kuwa anaenda/ yupo mafunzoni. Na kuficha huko si kwa marafiki tu bali hata wazazi na ndugu wa karibu. Na hapa ni muhimu kueleza kwamba moja ya vitu anavyokumbushwa afisa usalama wa taifa tangu hatua za mwanzo za kujiunga na taaluma hiyo hadi katika maisha yake ya kila siku ni KUWA MAKINI NA IMANI, au kwa lugha nyingine USIMWAMINI MTU YEYOTE. Wanasema TRSUT WILL GET YOU KILLED, yaani IMANI (kwa mtu au kitu) ITAKUUWA. Kwahiyo si jambo la ajabu kwa shushushu kutomwamini hata mzazi, ndugu au mwenza wake.

Kwa leo ninaomba kuishia hapa. Endelea kufuatilia mfululizo wa makala hii, ambapo toleo lijalo litaangalia kidogo kuhusu aina nyingine za mafunzo na kuangalia kwa undani kuhusu 'maisha ya shushushu mtaani,' yaani baada ya kuhitimu mafunzo yake. Unaweza kusoma habari za intelijensia kirahisi zaidi kwa kuonyeza INTELIJENSIA hapo kwenye menu ya blogu hii.