Shibuda, Arfi, Leticia watakwenda na maji CHADEMA? Arfi ahoji: "Hivi Lissu ni nani?" Aeleza sababu ya kurudi Bungeni

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Said Arfi akitia saini kitabu cha mahudhurio mara baada ya kurejea katika Bunge hilo wiki iliyopita pembeni ni Lweli Lupondo akitoa maelezo jinsi ya kutia saini. (picha via Tz Gov blog)

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa kitawafukuza wabunge wake, John Shibuda (Maswa Magharibi), Said Arfi (Mpanda Mjini) na Leticia Nyerere (Viti Maalum) baada ya kujiridhisha kwamba wameshiriki vikao vya Bunge Maalum.

Hatua hiyo inakuja baada ya wabunge hao kuripotiwa kujisajili na kushiriki vikao vya Bunge hilo kinyume na msimamo wa CHADEMA kupitia kundi lao la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambalo wamesusia wakidiai CCM imechakachua rasimu yenye mapendekezo ya wananchi.

Msimamo wa CHADEMA ulitolewa jana na Mwanasheria wake, Tundu Lissu akisema kuwa
Kamati Kuu ilishatoa maelekezo kwa wabunge wote, hivyo hawamuogopi wala hawataki kumwonea mtu, kwamba ndio maana wanajiridhisha kwanza.
“CHADEMA kama mshirika wa UKAWA, tuliwazia wabunge wetu wasishiriki Bunge hilo wala vikao vya kamati zake, sasa hawa waliokwenda huko Dodoma lazima waseme wako UKAWA au CCM.
“Hawa watu ni mamluki, kwa hili wala hatutahitaji kuwaita wajieleze. Tulisema wasiende, wao wakaenda. Sasa tutuchukua hatua na kama wanataka ubunge wa mahakama wataupata,”
alisema.

Lissu alisisitiza kuwa wabunge hao wameonesha njaa ya ajabu ya kukimbilia posho kwani hata kama ni shida ya kukosa fedha si kwa njia hiyo ya usaliti wanaojaribu kuufanya wakidhani watakidhoofisha CHADEMA.
“Hivi nani asiyemjua Shibuda…nani hamjui Arfi tangu ajiengue umakamu mwenyekiti wa chama au nani asiyejua mwenendo wa Leticia? Sisi hatumwogopi wala hatutamwonea mtu bali siku ya kufanya hesabu ikifika, kila mmoja ataoneshwa zake na kama kuna wengine acha waende tutawashughulikia bila kujali,”
alisema

Posho

Bunge Maalum la Katiba, limeamua kuzuia malipo ya posho za kujikimu kwa baadhi ya wajumbe wa Ukawa waliojisajili bila kushiriki vikao.

Katibu wa Bunge hilo, Yahaya Hamis Hamad, alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kubaini wajumbe hao wanafanya hila ya kujipatia fedha bila kufanya shughuli inayotakiwa.

Alisema kuwa utaratibu huo wanaufanya kujenga uhalali wa kulipwa posho ya kujikimu ya sh. 230,000 inayotolewa kila siku kwa mjumbe aliyeko Dodoma.

Kwa mujibu wa utaratibu wa malipo ya Bunge Maalum kila siku mjumbe aliyejisajili hulipwa sh. 230,000 na atakayehudhuria kikao hulipwa sh. 70,000, hivyo kufanya sh. 300,000 kwa siku.

Hamad alisema mpaka jana asubuhi wabunge wawili wa CHADEMA, John Shibuda na Leticia Nyerere ndiyo waliojisajili lakini hawakuhudhuria vikao.

Alibainisha kuwa mjumbe mwingine kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Clara Mwaituka naye alijisajili lakini hakushiriki kwenye vikao.

Alisema wamebaini kuwa licha ya wabunge hao kujisajili lakini walikuwa hawajalipwa fedha za siku saba kama walivyolipwa wenzao wanaoshiriki vikao.

Alisema kuwa alipokwenda kwa wahasibu kuangalia walivyolipwa UKAWA, alibaini kutofanyika kwa malipo, hivyo akaagiza yoyote atakayekuja asilipwe mpaka kuwe na uhakika wa kuhudhuria vikao.
“Kwa bahati nzuri watu wa uhasibu waliandika pembeni majina ya wajumbe wa UKAWA….hata Shibuda na Nyerere hawakulipwa, sasa tunataka tubane zaidi kukwepa ujanja ujanja,”
alisema.

Katibu aliongeza kuwa Shibuda alitoa taarifa kuwa hatoweza kushiriki kwenye vikao vya kamati kwa madai ana matatizo ya kiafya.
“Shibuda alikuja ofisini kwangu huku mguu wake ukionekana kuwa umevimba hivyo akaomba ruhusa kwenda kupatiwa matibabu, lakini hao wengine wamejiandikisha tu na kuondoka hata hivyo hawajaonekana tena,”
alisema.

Hamad aliwataja wajumbe wengine kutoka Ukawa waliojiandikisha na kuhudhuria vikao vya kamati kuwa ni Fatma Mohamed Hasan na Ally Omary Juma aliodai ni wa CUF.

Tanzania Daima, liliwasiliana na mmoja wa wajumbe wa Ukawa, Ismail Jussa Ladhu, ambaye alisema wajumbe waliotajwa na Hamad, hawatoki CUF.
“Mimi naona Katiba hafuatilii vema taarifa za wajumbe wake maana aliowataja mmoja natoka kundi la 201 mwingine anatoka chama kingine cha upinzani kisichokuamo UKAWA,”
alisema.

Hamad alimtaja mjumbe mwingine aliyeonekana kuwa na msimamo wa Ukawa akitokea kundi la 201 kuwa ni Jamila Abeid, ambaye hakutaja anawakilisha kundi lipi.

Arfi awasili bungeni

Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi (CHADEMA) jana alijisajili kushiriki vikao vya Bunge Maalum huku akidai amefanya hivyo kwa kutimiza haki yake ya kimsingi.

Arfi aliwasili majira ya asubuhi na mara baada ya kukamilisha taratibu za kujisajili alisema anawawakilisha Watanzania Bara.

Alisema amepata fursa na haki ya kuwemo kwenye Bunge hilo kutokana na kuwa mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Arfi alisema licha ya viongozi wa CHADEMA kuwataka wanachama wake wasihudhurie vikao, yeye ameamua kushiriki kwa lengo la kutimiza wajibu wake kwa wananchi waliomchagua.

Alipinga msimamo wa chama chake huku akidai kuwa vyama vinataka kupokonya mamlaka ya wananchi, kwamba iwapo wataendelea kukubali hali hiyo watakuwa wanawanyima wananchi haki yao ya msingi na kikatiba.


Arfi ahoji uhalali wa CHADEMA kuendelea kumbana


SIKU moja baada ya CHADEMA kutangaza uwezekano wa kuwachukulia hatua wabunge wa chama hicho wanaokiuka msimamo wao wa kususa vikao vinavyoendelea vya Bunge Maalumu la Katiba, Mbunge wa Mpanda Kati, Said Arfi amehoji uhalali wa CHADEMA kuendelea kumbana.

Amemtaka Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu kuacha kuwadanganya Watanzania juu ya mchakato huo na kwamba, kama angekuwa na nia njema angeshauri waende mahakamani kusimamisha Bunge ili kupata tafsiri ya sheria na si kutoka nje.

Kauli ya Arfi aliyoitoa jana, imekuja baada ya Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki kukaririwa na vyombo vya habari akisema wasaliti wa Ukawa wajiandae kuwa wabunge wa mahakama, akimaanisha kutengwa na chama hicho.

Arfi aliyeachia ngazi nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA - Taifa mwishoni mwa mwaka jana, alisema ameshangazwa na kauli ya Lissu na kuhoji uhalali alionao katika kumbana.

“Napenda kumkumbusha Lissu kama anapenda kusema, akili yake isiwe ya kusahau. Ni hatari kwa kiongozi na wala hataepuka kuitwa mropokaji …naomba arejee kauli yake iliyoandikwa pia na gazeti la (analitaja) la tarehe 27.06.2014, nanukuu “... kutoruhusiwa kushiriki shughuli za kambi hiyo...” “Sasa Lissu anapata wapi uhalali wa kuhoji matendo na maamuzi yangu wakati wamenitenga kinyume na kanuni za kambi rasmi? Hivi Lissu ni nani..? Angewaachia wengine walisemee, si Lissu,” alihoji Arfi.

Aliongeza kuwa, kukaa kwake kimya si ujinga bali ni busara, lakini si kwa kila jambo na kwamba Lissu anapolazimisha kutoshiriki kwenye bunge hilo hadi hapo uongozi wa bunge hilo utoe ufafanuzi wa kifungu cha 25, cha sheria ya mchakato wa Katiba sura ya 83, anajidanganya na kuwadanganya Watanzania.

Alisisitiza kuwa kazi ya Bunge ni kutunga Sheria na chombo cha Kikatiba cha kutafsiri sheria ni Mahakama na kwamba angemuelewa Lissu kama Mwanasheria, angewashauri kwenda mahakamani kusimamisha Bunge hilo, ili kupata tafsiri ya sheria na sio kushawishi kutoka nje ya bunge.

via gazeti la HabariLeo

Arfi ataja sababu za kurudi Bungeni


Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Said Arfi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amezitaja sababu za kurejea katika bunge hilo, kuwa ni hofu ya Mwenyezi Mungu.

Aidha Arfi ameitaja sababu nyingine ni kwamba amerudi katika Bunge hilo, ili kuhakikisha kwamba anaisadia nchi kupita katika mchakato wa Katiba mpya kwa amani na utulivu kwa kutumia kipaji chake na kuwatumikia Watanzania.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na mjumbe huyo, wakati akihojiwa na kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC).

Akizungumza katika kipindi hicho, huku akinukuu kitabu cha Nabii Musa, Arfi alisema Mwenyezi Mungu hawapendezwi na mtu mwenye jeuri na anayejivuna.

“Nimejitathimini na kuona mimi mwenyewe ni nina nafasi gani… maaskofu, mapadre, wachungaji na masheikh. Viongozi wetu wametusii turudi turudi napata kiburi wapi cha kutokurudi,” alihoji Arfi.

Akirejea katika kitabu cha Quran anasema Mwenyezi Mungu hapendezwi na mtu mwenye kiburi na anayejivuna. Aliongeza kuwa viongozi hao “wana nafasi kubwa pia wanaheshima ndio maana nimeweza kurudi,” alisema.

Mjumbe huyo alisema sasa ni wakati wa kila mtu kueleza ukweli, kwani amerejea katika Bunge hilo, amepata bahati ya kuchangia katika sura ya nne katika kifungu cha 43na 44 kinachohusu haki za msingi.

“Nimepata fursa ya kutoa mapendekezo ya haki za wazee nisingewezakuwasilisha kama ningekuwa nje. Pia haki za wafanyakazi,” alisema.

Akizungumzia kuhusu wajumbe wenzake waliosusia Bunge hilo, aliwataka kutanguliza maslahi ya taifa. Huku akisisitiza kwamba atajitahidi kuwashawishi wajumbe walioko nje ya Bunge hilo ili waweze kurejea.

Mhe.Arfi aliwahakikishia wananchi kuwa wanawatengenezea Katiba itakayowasaidia kubadilisha ya watu wote.

Na Magreth Kinabo, Dodoma via Tz Gov blog

Shibuda asema hatatetea kiti chake, amechoshwa na viongozi CHADEMA


Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda, amesema hatatetea kiti chake cha ubunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika uchaguzi mkuu mwakani kwa madai ya kuchoshwa na kauli za vitisho na kejeli zinazotolewa dhidi yake na baadhi ya viongozi wa chama hicho.

Alitoa kauli hiyo siku chache baada ya kudaiwa kuwa alijisajili kwa ajili ya kushiriki Bunge Maalumu la Katiba kinyume cha katazo na msimamo wa chama chake.

Pia amesema yeye si sehemu ya wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na kwamba hajawahi kuelimishwa juu ya Ukawa.

Shibuda aliyasema hayo kwa nyakati tofauti jana wakati akizungumza na wazee wa mji wa Maswa na Malampaka, Wilaya ya Maswa mkoani Shinyanga.

Wazee hao walitaka kujua hatima yake ya kisiasa ndani ya CHADEMA baada ya chama hicho kutishia kumfukuza kwa madai ya kushiriki vikao vya Bunge hilo vinavyoendelea mjini Dodoma.

Shibuda alisema alijiunga na CHADEMA kwa hiari yake akipinga dhuluma zilizokuwa zikifanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema wakati anajiunga na Chadema, alidhani kuna demokrasia na ukombozi wa kweli, lakini alichokikuta ni tofauti kwani kila siku amekuwa akipata misukosuko kutoka ndani ya chama hicho.

Shibuda alisema amekuwa kimya muda mrefu na kwamba ilifika wakati baadhi ya vijana wa CHADEMA walimtukana matusi na kumdhalilisha kwa kumwita majina ya kuudhi, kama vile `msaliti' na `pandikizi wa CCM', huku viongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho wakishindwa kuchukua hatua.

“Pamoja na shutuma zote zinazotolewa juu yangu na kupachikwa majina mbalimbali kuwa mie ni msaliti, mara ni pandikizi la CCM, lakini hata siku moja sijawahi kuitwa katika Kamati Kuu ya Chadema na kuhojiwa,” alisema Shibuda.

Aliongeza: “Nimekuwa nikitukanwa hadharani na vijana wa CHADEMA mbele ya viongozi wa juu wa chama, lakini hawachukui hatua. Mie mtu mzima. Hapo natafsiri kuwa wametumwa na viongozi hao ili kunifanyia fitina hizo.”

Akizungumzia madai ya kukiuka katazo la chama na UKAWA kushiriki Bunge hilo, Shibuda alisema hayana mashiko, kwani hajahudhuria kikao hata kimoja cha Bunge wala hajachukua posho.

Hata hivyo, alikiri kufika mjini Dodoma akitokea jijini Dar es Salaam akiwa njiani kuelekea jimboni kwake mjini Maswa.

Alisema alipita bungeni kufuatilia fedha za matibabu kutokana na kusumbuliwa na mguu.

Shibuda alisema akiwa katika ofisi za Bunge mjini Dodoma, alijaza fomu zinazohusiana na matibabu, kwani wabunge hutibiwa na serikali kupitia Ofisi ya Bunge kwa kipindi chote cha uhai wa ubunge wao.

Alisema tangu madai hayo yaanze kuandikwa na kutangazwa katika vyombo vya habari, hajawahi kuulizwa na kiongozi yeyote wa CHADEMA.

Hivyo alisema amesikitishwa na kauli ya Mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu, ya kutishia kumfukuza katika chama hicho kwa tuhuma za usaliti na kwamba anaamini uongozi ni kutanguliza hekima na busara katika kufikia maamuzi.

“Uongozi si Magereza. Na hata magereza wafungwa wana haki zao. Tundu Lissu amekuwa nani katika nchi hii? Anaongea kama kasuku. Hafanyi utafiti. Anakurupuka na kuongea na kutoa matamko. Mie nitamtaka athibitishe tuhuma hizo anazozitoa dhidi yangu. Nasema CHADEMA si baba wala mama yangu,” alisema.

Alisema amechoka kusikia hukumu dhidi yake kila siku kupitia vyombo vya habari zinazotolewa na viongozi wake wa CHADEMA.

Alitoa mfano akisema alipounga mkono nyongeza ya posho ya vikao vya Bunge, aliitwa msaliti, lakini leo wabunge wote wakiwamo wa CHADEMA waliogomea, wanachukua posho hiyo.

Alisema yeye si sehemu ya UKAWA na wala hajawahi kuelimishwa juu ya umoja huo, bali anachokumbuka ni kuwa kupitia viongozi wa juu wa vyama vya upinzani vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi, walikubaliana katika kikao kuwa wabunge wa vyama hivyo kususia Bunge hadi hapo rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakapojadiliwa.

“Mwislamu hawezi kutetea Uislamu kama hajui nguzo tano za Uislamu. Na pia huwezi kuwa Sheikh bila kupitia madrasa. Na hata katika Ukristo, huwezi kuutetea Ukristo kama hujui Biblia na hukusoma mafundisho. Na mie siwezi kuwa Ukawa wakati sijaelimishwa juu ya kundi hilo,” alisema Shibuda.

Akijibu moja ya maswali ya wazee ni chama gani ambacho atagombea ubunge katika uchaguzi mkuu ujao, alisema wakati ukifika atasema.

Alisema kwa sasa bado anatimiza wajibu wake wa kuwatetea wapigakura wake ambao wengi wao ni wakulima na wafugaji na kwamba yuko tayari kufukuzwa CHADEMA kwa kuwatetea (wapigakura wake).

Wakati Bunge Maalumu la Katiba likiendelea na vikao vyake mjini Dodoma, baadhi ya wajumbe wanaodaiwa kutoka UKAWA wamehudhuria vikao hivyo lakini wamekanwa na vyama vyao na wengine kuonywa kwa usaliti.

Katibu wa Bunge Maalumu, Yahaya, alisema kuwa hadi kufikia Alhamsi wiki iliyopita, tayari kulikuwa na ongezeko la wajumbe wa Ukawa kutoka wawili hadi kufikia sita; watatu wakitoka CHADEMAa na wengine kutoka makundi mengine.

Wajumbe kutoka CHADEMA wanaodaiwa kukaidi maamuzi ya Ukawa kwa kujiandikisha kwa ajili ya kuhudhuria vikao vya Bunge hilo, kuanzia Agosti 5, mwaka huuni Shibuda, Mbunge wa Viti Maalum, Leticia Nyerere na Said Arfi, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa zamani wa CHADEMA, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mpanda Kati.

via gazeti la Nipashe

SHIBUDA AACHIA NGAZI CHADEMA


SIKU chache baada ya Mbunge wa Maswa Magharibi, mkoani Simiyu, Bw. John Shibuda (CHADEMA), kudaiwa kukisaliti chama hicho na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa kurudi katika Bunge Maalumu la Katiba ambalo linaendelea na vikao vyake Mjini Dodoma, mbunge huyo ameibuka na kutangaza rasmi kuachana na chama hicho.


Alisema amechukua uamuzi huo baada ya kuchoshwa na matusi dhidi yake, kuitwa msaliti, mnafiki hivyo matusi yanayotolewa juu yake sasa yanatosha.

Bw. Shibuda aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari pamoja na Baraza la Wazee wilayani humo ambapo alitumia fursa hiyo kutangaza rasmi uamuzi wa kuachana na CHADEMA.


Alisema tangu amejiunga na CHADEMA, amekuwa akitukanwa, kuitwa masaliti na kunyimwa ushirikiano kutoka uongozi wa juu katika chama hicho ili kuchochea maendeleo na wananchi wake.

Aliongeza kuwa, chama hicho kimeshindwa kumpa heshima aliyonayo hivyo hawezi kuendeshwa kama mtoto na wala kupelekwa kama viongozi wa chama hicho wanavyotaka.


"Tangu nimejiunga na chama hiki, kila siku natukanwa hata na watoto wadogo ndani ya chama hiki...sasa nimechoka na siwezi kuvumilia hali hii, nimekuwa mvumilivu kwa muda mrefu hivyo natangaza kuwa, sitagombea ubunge kwa tiketi ya CHADEMA kwani chama hiki si baba wala mama yangu," alisema.


Kuhusu kurudi kwake bungeni

Akizungumzia madai ya kurudi kwake katika Bunge Maalumu la Katiba, alisema si ya kweli na hajawahi kuingia ndani ya Bunge hilo tangu lianze vikao vyake Agosti 5 mwaka huu bali alipita Dodoma wakati akitokea Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.


Alisema wakati akitokea Dar es Salaam, afya yake ilikuwa mbaya pamoja na kuvimba miguu hivyo alilazimika kupita kwa madaktari walioko katika viwanja vya Bunge ili aweze kupatiwa dawa.


"Wakati nikiwa njiani kuja Maswa kwenye msiba, afya yangu ilikuwa mbaya hivyo nililazimika kumpigia simu daktari wa Bunge na kumueleza juu ya afya yangu akaniambia nipite akanicheki.


"Nilipofika bungeni, nikapewa maelekezo ili niweze kupata dawa na kuangaliwa afya yangu, lazima nijiandikishe na mimi nilifanya hivyo na baada ya kujiandikisha, nilipewa dawa na kuangaliwa afya yangu sasa watu waliponiona wakasema nimekisaliti chama na UKAWA jambo ambalo si kweli," alisema.


Bw. Shibuda aliongeza kuwa, baada ya kupatiwa dawa aliendelea na safari yake ya kwenda jimboni kwa ajili ya msiba hivyo alishangaa kusikia anaendelea na vikao bungeni wakati yuko msibani.


Azungumzia UKAWA


Akiuzungumzia UKAWA, Bw. Shibuda alisema umoja huo hauna masilahi kwa Watanzania ambao asilimia kubwa ni wakulima na wafugaji kwani tangu watoke bungeni na yeye akiwa mmoja wa waliotoka, hajawahi kujulishwa jambo lolote kuhusu mazungumzo kati yao na CCM.


Alisema kitendo cha kutojulishwa lolote, kinampa shida ya kuamua kuendelea na Bunge la katiba au kususia vikao kwani hapewi taarifa za mchakato wa maridhiano lakini wajumbe wengine wamekuwa wakipata taarifa hizo na yeye kubaguliwa.


"Mimi si mkokoteni na siwezi nikaota juu ya maamuzi ya UKAWA ambayo wamekuwa wakiyajadili katika vikao vya maridhiano, wajumbe wengine wamekuwa wakipewa taarifa kila siku juu ya kinachoendelea hadi sasa lakini mimi nabaguliwa kwa nini," alihoji Bw. Shibuda.


Aliuponda umoja huo na kusema hauna dhamira ya kuwasaidia wakulima wa pamba na wafugaji ambao ndiyo wapiga kura wake na ndio walimtuma bungeni kujadili kero zao.


Atangaza kurudi bungeni

Katika hali isiyo ya kawaida, Bw. Shibuda alitangaza rasmi kurudi bungeni ili kuendelea na vikao vya Bunge la Katiba akisema anaenda kuzungumzia kero za wakulima wa pamba na wafugaji ili ziwekwe katika Katiba Mpya.


"Siko tayari kupelekwa na chama chochote cha siasa nchini wala viongozi wake, nitaenda bungeni wiki hii kuendelea na vikao ili niweze kuwatetea wakulima wangu wa pamba na wafugaji ambao ni maskini sana," alisema.


Juu ya viongozi CHADEMA

Akiwazungumzia viongozi wa juu wa chama chake, alisema wamekuwa wakitumia ubabe, vitisho na ubaguzi kukiendesha chama hivyo ni wazi wamekosa hekima na busara.


"Viongozi wa CHADEMA ni wababe, hawana hekima wala busara, wanataka kuendesha chama watakavyo kama cha kwao lakini mimi nimekataa, nataka niwaambie kuwa, waliposikia nimetoka CCM, wao ndiyo walinifuata nijiunge na chama chao," alisema.


Atangaza vita na Lissu

Bw. Shibuda alidai kukerwa na Mwanasheria wa chama hicho ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Bw. Tundu Lissu, akidai amekuwa akimuandama bila ya sababu na kumtaka aache mara moja.


Alisema amemvumilia kwa kiwango kikubwa kwani amekuwa akimsingizia mambo ya uongo na kutangaza vita dhidi yake.


"Amenituhumu mambo mengi na mimi nimemvumilia vya kutosha na sasa, ndani ya siku chache nikirudi Dar es Salaam tutaonana maana siwezi kutukanwa na mtoto mdogo kama Lissu," alisema.


Bw. Shibuda mbali na kutangaza kuachana na chama hicho, hakuwa tayari kuzungumzia chama anachotarajia kuhamia bali alisema chama atakachohamia ni siri yake akisema kitakuwa chama kipya nchini.


Wazee wamuunga mkono

Baada ya wazee hao kumsikiliza Bw. Shibuda, walimuunga mkono kwa uamuzi wake wa kukihama chama hicho na kumtaka arejee bengeni ili kuwatetea wananchi wa Maswa ambao ni wakulima na wafugaji.


"Sisi kama wazee, tunakuunga mkono na tunawataka wabunge wengine kurejea bungeni ili kujadili matatizo ya Watanzania ambayo hayahusiani na muundo wa Serikali...tunataka wakulima na wafugaji wadhaminiwe," Alisema Mohamed Mangasiri ambaye ni Mwenyekiti Baraza la Wazee jimboni humo.