Shibuda: "Wote nawazidi kiwango cha kufikiri na busara na ndiyo sababu nimerejea katika bunge"

Shibuda alipoulizwa kuhusiana na kauli kwamba yeye ni msaliti na atachukuliwa hatua, alisisitiza kuwa wana fikra chakavu wanaofikiria na kuamini kuwa mtu ukipishana naye mawazo ni msaliti.

Alisema ingekuwa hivyo madaktari baada ya kudundua dawa ya Asprin wasingegundua dawa nyingine kama Panadol, Paracetamol, Dakika Tatu na nyinginezo kwani hizo zote zilitokana na kuchanganya mawazo tofauti.
"Wana uchakavu wa mawazo... ndiyo maana nasema wote nawazidi kiwango cha kufikiri na busara na ndiyo sababu nimerejea katika bunge, hawana uchungu na wananchi, wanaishi maisha ya anasa," 
Shibuda alitoa kauli hiyo leo mchana mjini Dodoma, wakati akiingia kwenye viwanja vya
Bunge akiwa ameambatana na viongozi 44 wa jamii ya wafugaji kutoka mikoa mbalimbali ya Kanda ya Magharibi na Kanda ya Kusini, walioenda kukutana na Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta.
"Nimekuja na jamii hii ya wafugaji kuzungumza na Mwenyekiti maana kama vikao vya Bunge Maalum la Katiba visipofanyika ni kuwanyima haki wafugaji. Hao wanaokataa vikao vya Bunge wengi wao wanatoka katika maisha ya starehe na wamekulia maisha ya anasa, sasa wanataka kuwadhulumu wafugaji. Ni kundi la maslahi binafsi," 
alisema na kuongeza kuwa yeye ni mlezi wa wakulima na wafugaji.