Taarifa ya Jussa: Tundu Lissu ajitolea kumtetea Mansoor Himid

Kinyume na ilivyotarajiwa, Mhe. Mansoor Himid hakufikishwa Mahkamani leo, pamoja na kwamba ni zaidi ya saa 48 tokea alipokamatwa.

Kutokana na hali hiyo, Mawakili wake wakiongozwa na Fatma Karume leo wamewasilisha ombi maalum linalojulikana kisheria kama habeas corpus mbele ya Mahkama Kuu ya Zanzibar wakitaka Mahkama iiamuru Polisi kumfikisha Mhe. Mansoor Yussuf Himid mbele ya Mahkama hiyo ili kujibu tuhuma anazotuhumiwa nazo kama zipo.

Kwa upande mwengine, mwanasheria maarufu Tundu Lissu amejitolea kuungana na wanasheria
wengine watakaomtetea Mhe. Mansoor Yussuf Himid, pale atakapofikishwa Mahkamani.

Kama tulivyotangulia kuwaarifu katika taarifa zilizopita, jitihada nyengine zinaendelea kuchukuliwa na viongozi wetu na pia familia yake kufuatilia yanayoendelea katika kadhia hii.

Wakati tunawashukuru Wazanzibari wote kwa kuitikia wito wetu wa kuwataka wawe watulivu katika kufuatilia suala hili, tunaendelea kurudia kuwasisitiza tena Wazanzibari wenzetu kuendeleza utulivu wao na kutuachia kulifuatilia suala hili kupitia njia za amani na za kisheria huku tukiamini kwamba haki itashinda.

Pamoja Daima!

Ismail Jussa
Katibu
Kamati ya Maridhiano

via Mzalendo.net