Taarifa ya Sikika kuhusu tuhuma za Madiwani wa Halmashauri ya Kondoa

Mwenyekiti wa Bodi Sikika, Bi. Pili Mtambalike akisoma tamko la Shirika lisilo la Kiserikali la Sikika mbele ya waandishi wa Habari leo Agosti 3, 2014 kufuatia kusikitishwa na taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri wilayani Kondoa ya kusitisha shughuli zake katika wilaya hiyo kupitia barua yenye kumbukumbu namba KDC/LGC/M/3 VOL. II/71 ya tarehe 31/07/2014. Kwa mujibu wa barua hiyo, maamuzi hayo yalitolewa katika mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika 26 Julai, 2014 Kondoa baada ya kuituhumu Sikika kwamba imesema Madiwani hawajasoma. Kutoka Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Sikika Bw. Irenei Kiria na Mjumbe wa Bodi ya Sikika.




Taarifa kwa Vyombo vya Habari, 03 Agosti, 2014

SIKIKA YAKANUSHA TUHUMA ZA MADIWANI, HALMASHAURI KONDOA

Sikika imesikitishwa na taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri wilayani Kondoa ya kusitisha shughuli zake katika wilaya hiyo kupitia barua yenye kumbukumbu namba KDC/LGC/M/3 VOL. II/71 ya tarehe 31/07/2014. Kwa mujibu wa barua hiyo, maamuzi hayo yalitolewa katika mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika 26 Julai, 2014 Kondoa baada ya kuituhumu Sikika kwamba imesema Madiwani hawajasoma.
Sikika inakanusha tuhuma kwamba ilisema Madiwani hawajasoma.
Maamuzi ya kusitisha kazi za Sikika yametolewa na Halmashauri hiyo wakati shirika likiendelea na mchakato wa kuwezesha zoezi la Ufuatiliaji wa Uwajibikaji Jamii (Social Accountability Monitoring – SAM), zoezi ambalo linahamasisha uwazi, uwajibikaji na utawala bora katika kusimamia rasilimali za umma ili kuboresha utoaji wa huduma za jamii, ikiwemo afya.
Pamoja na kukuza ushiriki wa wananchi katika kufuatilia na kusimamia rasilimali zao, SAM pia huwasaidia madiwani kuwawajibisha watendaji wa halmashauri ikiwa
ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za jamii katika kata zao za uchaguzi.
Sikika inatambua kwamba serikali kuu pamoja na wafadhili hupeleka fedha nyingi katika halmashauri zetu kwa lengo la kutoa huduma kwa wananchi, hivyo ni jukumu la madiwani na wananchi kusimamia matumizi mazuri ya fedha hizo na kuhakikisha huduma bora zinapatikana.
Kwa mujibu wa Kiongozi cha Madiwani Juu ya Maswala ya Msingi na Ujuzi juu ya Uendeshaji wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2010, Baraza la Madiwani linawajibika kukuza ushirikiano kati ya Halmashauri, asasi za kiraia na taasisi zingine za kiserikali. Pia, Madiwani wanawajibika kuangalia na kudhibiti rasilimali za umma ndani ya Halmashauri zao.
Sikika inapenda kuwaeleza Watanzania kwamba inafanya kazi za SAM katika wilaya kumi hapa Tanzania kwa ushirikiano mkubwa sana wa Madiwani husika, na kwamba zoezi hili linakwenda vizuri na kwa mafanikio makubwa katika wilaya tisa isipokuwa tu katika wilaya ya Kondoa, kwa sasa. Kwa mfano, Julai 2014 tumekamilisha zoezi la SAM awamu ya pili katika Wilaya za Mpwapwa na Singida Vijijini ambapo SAM ilifanikiwa kutokana na ushirikiano mkubwa wa Madiwani.
Sikika imeandikishwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania kufanya kazi ya kuhimiza utawala bora na uwajibikaji katika sekta ya afya Tanzania kupitia uchambuzi wa sera, mikakati, mipango, bajeti na matumizi ya serikali. Majukumu yetu ya msingi ni kuhimiza uwajibikaji katika sekta ya Afya kwa lengo la kuharakisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote.
Kwa mantiki hiyo basi, Sikika inafanya kazi kwa karibu sana na makao makuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Kamati ya Huduma za Jamii tangu mwaka 2005.
Uamuzi wa kuifungia Sikika wilayani Kondoa unakiuka Kifungu cha 27(1) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kinachompa kila mwananchi  wajibu wa kulinda mali asili ya Jamhuri ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi.
Uamuzi huo pia umekiuka kifungu cha 146(1) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinachoeleza madhumuni ya kuwapo kwa Serikali za Mitaa kuwa ni kupeleka madaraka kwa wananchi. Na kwamba vyombo vya Serikali za Mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki na kuwashirikisha wananchi katika mipango na shuhghuli za utekelezaji wa maendeleo katika sehemu zao na nchini kote kwa jumla.
Tumeshangazwa kwamba barua hiyo inayozuia kazi za Sikika wilayani Kondoa, haikueleza ni sheria gani ambayo Baraza la Madiwani limetumia kufanya uamuzi huo na pia haikuwasilisha ushahidi wowote wa tuhuma zilizoelekezwa Sikika.
Tumeshangazwa pia kuona kwamba Baraza la Madiwani la Wilaya ya Kondoa linafanya uamuzi mzito kama huu kutokana na tuhuma ambazo hazijathibitishwa na kwamba Sikika haijawahi kupewa ushahidi wowote kuhusu tuhuma hizo.
Tumeshangazwa zaidi na taarifa za Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kondoa Hamisi Mwenda kupitia vyombo vya habari kwamba kikao cha Baraza la Madiwani kilichokaa tarehe 26/07/2014 kufanya uamuzi huo kilihudhuriwa na madiwani 39 wakati ukweli ni kwamba waliohudhuria ni 35. Hivyo idadi ya kura alizotangazia umma siyo za kweli.
Sikika imesikitishwa na mwenendo wa Madiwani wa Halmashauri ya Kondoa kuwakingia kifua watendaji wa Halmashauri kila inapojitokeza hoja inayohitaji ufafanuzi kuhusu matumizi ya rasilimali za umma katika Idara ya Afya. Matokeo yake, huduma za afya katika Halmashauri hiyo siyo za kuridhisha na wananchi wanazidi kutaabika.
Sikika inaamini kwamba:
  • Uamuzi wa kusitishwa kwa shughuli za Sikika ni moja kati ya mbinu za kuzuia zoezi la SAM awamu ya pili lisikamilike kwani kukamilika kwake kungesababisha kuhojiwa masuala mbalimbali ya kiutendaji, matumizi ya fedha za umma na uwajibikaji.  
  • Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Kondoa limepotoshwa na Mkurugenzi pamoja na Mwanasheria wa Halmashauri, na kwamba uamuzi ulifikiwa kwa kutumia maneno ya kuzusha bila ushahidi.
  • Kwamba Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Kondoa lina wajibu wa kusimamia watendaji wa Halmashauri na hasa Idara ya Afya ili kuhakikisha matumizi mazuri ya fedha na rasilimali za umma kwa ajili ya kuboresha huduma za afya wilayani hapo.
  • Kama Sikika ilichapisha machapisho yanayohatarisha amani na usalama, taarifa na ushahidi huo zingefikiswa kwenye kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na uamuzi wa kamati ungekuwa umeshawasilishwa kwa Sikika.
  • Kwamba ili kazi za SAM ziendelee katika Halmashauri ya Kondoa kama zinavyoendelea katika Halmashauri zingine kwa mujibu wa dhana ya utawala bora, tunasisitiza umuhimu wa uchunguzi kufanyika ili kubaini ukweli na wapi upotoshaji umefanyika ili kutoathiri uwajibikaji.
  • Kwamba Waziri mwenye dhamana ya Serikali za mitaa atapata nafasi ya kufuatilia suala hili ili kujua ukweli na kulipatia ufumbuzi kwa manufaa ya wananchi wa Kondoa.
  • Kwamba tunaisihi ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu wa fedha (special audit) katika Idara ya Afya ya Halmashauri ya Kondoa.
  • Halmashauri ya Kondoa itajizatiti katika kutekeleza Mpango Mkakati wa TAMISEMI wa kipindi cha 2011/12 hadi 2015/16 unaosisitiza Halmashauri za Wilaya kuzidisha ushirikiano wake na Asasi za Kiraia katika kutimiza wajibu wa kuwahudumia wananchi.


Mwisho, tunasisitiza kwamba tuhuma kuwa Sikika ilisema madiwani wa Halmashauri ya Kondoa hawajasoma si za kweli na hazina ushahidi. Kama upo ushahidi tupatiwe na ujadiliwe. Pia tunasisitiza ushirikiano wetu na madiwani wote wa Halmashauri ya Kondoa katika kusimamia rasilimali na huduma za afya Wilayani humo kwa lengo la kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Kondoa.


Macintosh HD:Users:thomas:Desktop:Pili.jpg
Pili Mtambalike
Mwenyekiti wa Bodi ya Sikika.
03/8/2014



Sikika, S.L.P 12183 Dar es Salaam, Simu: +255 222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua pepe: [email protected],
Twitter: @sikika1, Facebook: Sikika Tanzania, Tovuti: www.sikika.or.tz


Mwenyekiti wa Bodi Sikika, Bi. Pili Mtambalike akisoma tamko la Shirika lisilo la Kiserikali la Sikika mbele ya waandishi wa Habari leo Agosti 3, 2014 kufuatia kusikitishwa na taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri wilayani Kondoa ya kusitisha shughuli zake katika wilaya hiyo kupitia barua yenye kumbukumbu namba KDC/LGC/M/3 VOL. II/71 ya tarehe 31/07/2014. Kwa mujibu wa barua hiyo, maamuzi hayo yalitolewa katika mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika 26 Julai, 2014 Kondoa baada ya kuituhumu Sikika kwamba imesema Madiwani hawajasoma. Kutoka Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Sikika Bw. Irenei Kiria, Mjumbe wa Bodi ya Sikika pamoja na Dokta Eli Nangawe (wa Kwanza Kulia).


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Sikika Bw. Irenei Kiria akitolea ufafanuzi tamko lililosomwa mbele ya waandishi wa habari leo Agosti 3, 2014 kufuatia kusikitishwa na taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri wilayani Kondoa ya kusitisha shughuli zake katika wilaya hiyo kupitia barua yenye kumbukumbu namba KDC/LGC/M/3 VOL. II/71 ya tarehe 31/07/2014.


Waandishi wa Habari wakiwajibika.


Dokta Eli Nangawe akijibu maswali mbele ya waandishi wa habari.