Tabia ya viongozi Afrika kukusanywa ka' mafungu kupelekwa China mara Marekani...

.

MKUTANO wa Kimataifa wa Ushirikiano kati ya Marekani na Bara la Afrika umemalizika mwishoni mwa wiki iliyopita na kuna machache ambayo mwananchi wa kawaida anaweza kuwa amefaidika nayo kutoka huko.

Mkutano huo tayari umeanza kuzua maneno hususani kwa wenzetu wa nchi za Magharibi mwa Afrika. Kikubwa ni aina fulani ya dharau iliyoonyeshwa na serikali ya Marekani dhidi ya viongozi wa Afrika.

Wakati katika mikutano baina ya Afrika na China, Japan au Umoja wa Ulaya (EU) viongozi wa bara hili hupata fursa ya kuonana na kiongozi wa nchi iliyoitisha mkutano kwa minajili ya kufanya majadiliano baina ya nchi mbili (bilateral meetings), Marekani haikutoa nafasi hiyo.

Tumeambiwa tu kwamba hata chakula cha jioni walichoandaliwa viongozi wetu hakikuwa katika
hadhi ya kawaida ya dhifa ambazo zimezoeleka. Huu ni ujumbe mwanana kwa viongozi wetu.

Afrika haina mjomba wala shangazi wa kuisadia kujikwamua kutoka katika umasikini wake. Namna pekee ambayo wageni wanaweza kuja na kusaidia ni pale wanapoona kwamba wao watafaidika zaidi kuliko nchi zetu.

Ndiyo maana, nchi ambazo zinaonekana kuwa mbele kusaidia Afrika, ndizo hizohizo baadaye hubainika kuwa zinafanya mambo mengine yanayochochea uvunjifu wa amani na wizi wa rasilimali.

Afrika itajikwamua kutoka katika umasikini, ujinga na maradhi pale ambapo nchi zenyewe zitaamua kwa dhati kupambana na masuala hayo. Tulipoamua kupambana na adui ujinga katika miaka ya 1970, hatukusaidiwa na mtu hadi yakapatikana mafanikio yaliyopatikana.

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba mambo manne yanahitajika ili nchi iweze kuendelea; Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi. Jambo pekee ambalo lipo na la uhakika ni ardhi.

Serikali za Afrika sasa zinapaswa kuwekeza katika watu kwa maana ya kuwapa elimu bora na ujuzi tofauti wa kuweza kusaidia kusonga mbele na kuhakikisha kwamba siasa za utawala zinakuwa nzuri ili wapatikane viongozi bora.

Tabia hii ya viongozi wa Afrika kukusanywa kwa mafungu na kuhangaishwa kupelekwa mara China, mara Marekani na kwingineko, haitaweza kusaidia lolote.

Nchi zote ambazo zinadai kutaka kusaidia Afrika, nazo sasa zina matatizo makubwa ya kiuchumi na ndiyo maana vyama vyenye mrengo mkali wa kisiasa vinazidi kupata wafuasi na ufuasi katika nchi hizo wafadhili wetu.

Namna pekee ya kujikomboa itatoka miongoni mwetu na si Marekani wala Uchina.

--
Raia Mwema - Si Marekani, China wala EU watakaotukwamua