Tamasha la Matumaini 2014 kesho, Taifa


Ally Kiba.

SIKU iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa burudani mbalimbali imewadia ambapo kesho Agosti 8, katika Uwanja wa Taifa patakuwa hapatoshi wakati Tamasha la Usiku wa Matumaini litakapokuwa likichukua nafasi.

Akizungumza na Centre Spread, mratibu wa tamasha hilo, Luqman Maloto alisema kuwa maandalizi yote yameshafanyika na tayari mkali wa muziki kutoka Nigeria anayetamba na ngoma ya Johnny, Yemi Alade ameshatua nchini, kinachosubiriwa ni burudani mwanzo mwisho.

“Kila kona ya burudani imeshakamilika hivyo kama wewe ni mpenzi wa ndondi kuna ngumi kati ya mabondia Mada Maugo dhidi ya Thomas Mashali, JB dhidi ya Cloud 112, Said Memba dhidi ya Khalid Chokoraa na wengineo.

Mabondia Mada Maugo na Thomas Mashali wakitunishiana misuli.

“Wapenzi wa Bongo Fleva, kutakuwa na mfalme wao, Ali Kiba akiwa sambamba na mastaa kama Shilole, Madee, R.O.M.A, Meninah, Navy Kenzo, Scorpion Girls, Juma Nature na wengine kibao,” alisema Maloto na kuongeza:

“Kwa wale wapenzi wa soka basi watakutana na mechi kabambe kati ya Wabunge Mashabiki wa Simba dhidi ya wenzao wa Yanga, Azam Fc dhidi ya Mtibwa, Bongo Fleva dhidi ya Bongo Movie na wengine wengi.”

Maloto aliongeza kuwa jukwaa litashambuliwa pia na wanamuziki wa nyimbo za Injili kama Martha Mwaipaja, Upendo Nkone, Angel na wengine wengi.

Tamasha la Usiku wa Matumaini linatarajiwa kuanza kesho saa 5 asubuhi hadi saa 6 usiku ambapo wapenzi wa burudani watainjoi mambo yote kwa kiingilio cha shilingi elfu 5 tu.

Navy Kenzo.