Tangazo la Mafunzo ya Shahada Jumuishi ya Ualimu wa Sayansi na Hisabati

Ili kukabiliana na upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati katika shule za Sekondari nchini, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) imeandaa mafunzo ya stashahada maalumu ya Ualimu katika Sayansi, Teknohama na Hisabati kwa wahitimu wa kidato cha nne na wale wenye sifa mbadala. Mafunzo yatatolewa katika Chuo cha Elimu, Chuo Kikuu cha Dodoma. Mafunzo haya yatakayofuata mfumo wa Tuzo za Elimu ya Ufundi (NTA) unaoratibiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) utamuwezesha mhitimu wa kidato cha nne kupata mafunzo maalumu.

Ili kufanikisha mafunzo haya maalumu, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu itatoa mikopo kwa wanafunzi wote watakaochaguliwa. Pamoja na serikali (wizara) kutoa nafasi ya mikopo kwa watakaofanikiwa kujiunga, programu hii ya mafunzo itawezesha wahitimu kupata ajira baada ya kuhitimu katika ngazi ya stashahada (NTA Level 6). Baada ya kufanya kazi kwa muda usiopungua miaka miwili kama mwalimu mwenye Stashahada, mhitimu atakuwa na hiari ya kurudi chuoni kwa mafunzo zaidi ya Shahada ya Ualimu wa Sayansi, Teknohama na Hisabati (NTA Level 8). Mhitimu wa stashahada anayo hiari pia kupata mafunzo ya mwaka mmoja na kupata stashahada ya juu ya ualimu (NTA Level 7).