Tanzania yasaini mkataba wa kuanzisha Kampasi ya "African Institute for Mathematical Sciences - Next Einstein Initiative"Serikali ya Tanzania na Taasisi ya African Institute for Mathematical Sciences - Next Einstein Initiative (AIMS-NEI) wamesaini Mkataba wa Makubaliano kuanzishwa kwa kampasi ya taasisi hiyo nchini itakayofundisha na kuendeleza masomo ya Hisabati na Sayansi.

Mkataba huo umesainiwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome kwa upande wa Serikali na Bwana Thierry Zomahoun, Mkurugenzi Mtendaji wa AIMS-NEI jijini Dar es Salaam.

Profesa Mchome amesema kusainiwa kwa mkataba huo ni jitihada za Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha kuwa Taifa linakuwa na wataalam wa kutosha katika Nyanja za Hisabati na
Sayansi. Mheshimiwa Rais alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa taasisi hiyo alipokuwa ziarani nchini Canada mwishoni mwa mwaka jana.

Akizungumzia mkataba huo, Profesa Mchome alisema “Hii ni nafasi ya pekee maana huwezi kupata Mainjinia bila kujua hesabu, wala Madaktari na Wanasheria bila kuwa na ufahamu wa hesabu, na hesabu ndiyo kila kitu.”

Taasisi ya African Institute for Mathematical Science-Next Einstein Initiative (AIMS-NEI), wameshafungua kampasi zake katika nchi za Afrika Kusini, Senegal, Ghana na Cameroon, na kwa hapa Tanzania tayari wamepata eneo wilayani Bagamoyo katika majengo ya Boma ambayo yatakarabatiwa. Kwa kuanzia masomo hayo yatatolewa katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela kilichopo Arusha ambapo wanafunzi 40 wa awali wameshadahiliwa tayari kwa kuanza masomo hayo mwezi Septemba mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa African Institute for Mathematical Sciences-Next Einstein Initiative (AIMS-NEI), Thierry Zomahoun, alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi bora kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki, ili ijijenge katika misingi ya uchumi imara zaidi, haina budi kuwekeza katika masuala ya hesabu na sayansi ili kupata watalaamu watakaolisaidia taifa kusonga mbele kimaendeleo.

Aidha, Bwana Zomahoun alimpongeza Mheshimiwa Rais Kikwete kwa kukubali kuanzishwa kwa kampasi ya taasisi hiyo hapa nchini ili kukuza na kuendeleza masomo ya hisabati na sayansi na kuzalisha wataalamu wa kutosha watakaokidhi mahitaji ya nchi katika nyanja mbalimbali.