Tarehe ya Kongamano la kujadili mchakato wa Katiba yasogezwa

Magreth Kinabo, Habari Maelezo via Tz Gov - Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania limesema kwamba kongamano la kujadili chakato wa kutunga Katiba mpya na changamoto zake lililopangwa kufanyika Agosti 9 na 10 mwaka huu limesogezwa mbele, hivyo litatangaza tarehe ya kufanyika.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa baraza hilo, Peter Mziray katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari mjini Dodoma.
“Kutokana na uzito wa kongamano hilo na kazi kubwa ya maandalizi yake, inayotokana na uwingi na uzito wa wageni waalikwa, kongamano hilo halitafanyika siku ya tarehe 9 na 10 Agosti, mwaka 2014 kama lilivyopangwa awali. Hivyo basi tarehe ya kufayika kongamano hilo imepelekwa mbele na baraza litatangaza,” 
Aliongeza kuwa kongamano hilo litakuwa tukio kubwa na muhimu kwa nchini yetu, kwani litajadili kwa kina mchakato wa kutunga Katiba mpya unaoendelea na changamoto zinazoendelea kukabiliana nazo.

“Wadau wote wanaohusika na mchakato huu wataalikwa na watoa maoni yao,” alisisitiza.

Aidha, Mziray alisema kongamano hili litaibuka na maazimio ambayo baraza hilo linaamini yatakuwa na uzito na ushawishi katika mchakato huo kwa kuwa yatazingatia maslahi mapana ya taifa, hali halisi ya siasa, uchumi, utamaduni, jamii na haja ya kudumisha Muungano wetu na hatima ya nchi kwa miaka mingi inayokuja.

Mwenyekiti huyo amesema kongamano hilo litamhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete atakayelifungua, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe . Mohammed Gharib Bilal, Marais wastaafu, wabunge, majaji, maspika, viongozi wote waliowahi kushika madaraka, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa dini zote.