Tarime: Watoto 984 waozeshwa kwa nguvu; 1,628 wakeketwa


Baadhi ya wanafunzi wakiangalia ujumbe mfupi uliotumwa kwa simu zote zilizosajiliwa kwa njia ya simu za kiganjani na Mjane wa Hayati Nelson Mandela, Bi. Graca Michel kwa kushirikiana na Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Bi. Sophia Simba kupinga ndoa za utotoni kwa watoto wa kike.

JUMLA ya wasichana wenye umri mdogo wapatao 984 wameolewa na kukatishwa masomo huku wasichana wengine 1,628 wakikeketwa wilayani Tarime, Mkoa wa Mara ikiwa ni miongoni mwa vitendo vya kikatili ambavyo amekuwa akifanyiwa mtoto wa kike baadhi ya maeneo nchini Tanzania.

Takwimu hizo za vitendo vya kikatili dhidi ya mtoto wa kike wilayani Tarime zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele kwa niaba ya Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara kwenye hafla ya uzinduzi rasmi wa kampeni za kupinga ndoa za utotoni kwa watoto wa kike zitakazoendeshwa mkoani Mara.

Akizungumza kabla ya uzinduzi wa kampeni hiyo, Henjewele alisema takwimu hizo zavitendo vya kikatili Mkoani Mara ni za kuanzia mwaka 2013 hadi Juni 2014. Alisema baadhi ya familia eneo hilo wanamchukulia mtoto wa kike kama kitega uchumi hivyo wamekuwa wakiwaozesha mapema ili kupata mali (yaani ng'ombe) jambo ambalo bado uongozi wa mkoa huo kwa kushirikiana na wadau anuai wamekuwa wakipinga na kupambana na ukatili huo.

"...Matukio ya vitendo vya unyanyasaji kwa mtoto wa kike kwa mwaka 2013 hadi Juni 2014 ni kama ifuatavyo; watoto wa kike wapatao 984 waliozeshwa, wasichana 1,628 walikeketwa, jumla ya wanafunzi wa kike 4,134 walipewa mimba na kukatishwa masomo yao huku wasichana 1,912 wakifanyiwa ukatili wa vipigo kwenye familia ama kwenye ndoa na jumla ya watoto 11 walibakwa...," alisema Henjewele.

Aidha alisema vitendo hivyo vya kikatili kwa mtoto wa kike vinachangiwa na baadhi ya jamii mkoani humo kuendeleza mila na desturi zilizopitwa na wakati, migogoro ya koo, mwamko duni wa elimu kwa jamii na usiri mkubwa wa kutokubali mabadiliko dhidi ya vitendo vya kikatili kwa jamii hiyo. Akizungumzia jitihada zinazofanywa na viongozi wilayani hapo kukabiliana na vitendo hivyo, alisema wamekuwa wakiendesha semina na vikao mbalimbali na wazee wa kimila, mangariba na jamii kwa ujumla kwa lengo la kutokomeza vitendo vya Ukatili wa kijinsia, ukeketaji pamoja na mila na desturi zilizopitwa na wakati.

Kwa Upande wake mjane wa hayati Nelson Mandela, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Graca Michel Trust, Bi. Graca Michel akizungumza kabla ya kuzindua rasmi kapeni hizo alisema viongozi kwa kushirikiana na wanajamii mkoani Mara wakiamua kwa dhati wanaweza kukabiliana na ndoa za utotoni na vitendo vingine vya kikatili eneo hilo.

Akizungumzia kwa ujumla alisema jamii nyingi ya kiafrika bado zinamthamini mtoto wa kiume zaidi ya yule wa kike ilhali watoto wote wanapaswa kuwa na haki sawa. Aliwataka wazazi wenye mawazo kama hayo kubadilika na kutoa haki sawa kwa watoto bila ubaguzi. Alishauri suala la uamuzi dhidi ya maisha ya mtoto lifanywe kwa ushirikiano kwa familia nzima pamoja na kushirikishwa mtoto.

"...Lazima tukubali kubadilika, umefika wakati suala la uamuzi wa wakati gani wa kuolewa kwa mtoto wa kike ufanywe kwa ushirikiano kati ya wazazi wote pamoja na mtoto mwenyewe tena kwa wakati muafaka...lazima turejeshe maamuzi pia kwa mtoto mwenyewe si kutumia nguvu kwa kila kitu," alisema Bi. Michel.

Aliongeza hata hivyo ipo haja ya kuwa na asasi za ushauri ngazi ya familia ambazo zitakuwa zikitoa ushauri juu ya masuala ya familia kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazotambulika. Alisisitiza katika kampeni za sasa juhudi na elimu ya kutosha itolewe kwa jamii mkoani Mara ili baadaye ifanyike tathmini kwa eneo hilo jambo ambalo linaweza kusaidia mapambano maeneo mengine hapo baadaye.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Valerie Nsoka akifafanua juu ya shughuli za kampeni hizo alibainisha kuwa zitaambatana na utoaji elimu kwa makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, watendaji wa vyombo vinavyosimamia sheria, viongozi wa jamii na jamii kwa ujumla juu ya mapambano ya kampeni hizo. Kampeni hizo baadaye zitaendelea katika maeneo mengine ya Tanzania.

Programu ya kampeni hiyo imefanikishwa kwa kushirikiana na Serikali, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), Shirika lisilo la Kiserikali la Children's Dignity Forum (CDF), Graca Machel Trust (GMT), asasi za mkoani Mara na uongozi wa mkoa.

*Imeandaliwa na www.thehabari.com

Baadhi ya washiriki katika hafla ya uzinduzi rasmi wa kampeni za kupinga ndoa za utotoni kwa watoto wa kike zitakazoendeshwa mkoani Mara. Uzinduzi huo umefanywa na mjane wa hayati Nelson Mandela, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Graca Michel Trust, Bi. Graca Michel leo jijini Dar es Salaam.
 
 
Mjane wa Hayati Nelson Mandela, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Graca Michel Trust (GMT), Bi. Graca Michel (kulia) akishangilia baada ya kutuma ujumbe mfupi kwa njia ya simu za viganjani kwa simu zote zilizosajiliwa nchini Tanzania ikiwa ni ishara ya uzinduzi kampeni za kupinga ndoa za utotoni kwa watoto wa kike zitakazoendeshwa mkoani Mara.

 
Mjane wa Hayati Nelson Mandela na Mwenyekiti wa Taasisi ya Graca Michel Trust (GMT), Bi. Graca Michel akimbusu mmoja ya watoto wa kike kutoka Mkoa wa Mara kuonesha ishara ya upendo katika uzinduzi huo

 
Mjane wa Hayati Nelson Mandela, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Graca Michel Trust (GMT), Bi. Graca Michel akisalimiana na baadhi ya viongozi mbalimbali kutoka mkoani Mara.

Baadhi ya watoto wa kike kutoka Mkoa wa Mara wakizungumzia namna walivyonusurika kufanyiwa vitendo vya kikatili (kukeketwa). Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Valerie Nsoka akiwasikiliza.

 
Viongozi mbalimbali wastaafu wa Serikali, viongozi wa dini Mkoa wa Mara, wawakilishi wa wanafunzi Mkoa wa Mara wakiwa katika hafla ya uzinduzi rasmi wa kampeni za kupinga ndoa za utotoni kwa watoto wa kike zitakazoendeshwa mkoani Mara.

 
Baadhi ya viongozi wa mashirika mbalimbali walioshiriki hafla ya uzinduzi wa kampeni za kupinga ndoa za utotoni kwa watoto wa kike zitakazoendeshwa mkoani Mara. Uzinduzi huo umefanywa na mjane wa hayati Nelson Mandela, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Graca Michel Trust, Bi. Graca Michel leo jijini Dar es Salaam.

 
Mjane wa Hayati Nelson Mandela, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Graca Michel Trust (GMT), Bi. Graca Michel (kulia) akizungumza kabla ya kuzindua rasmi kampeni za kupinga ndoa za utotoni kwa watoto wa kike zitakazoendeshwa mkoani Mara.

 
Baadhi ya wanafunzi wakitumbuiza katika hafla ya uzinduzi rasmi wa kampeni za kupinga ndoa za utotoni kwa watoto wa kike.

 
Moja ya kikundi cha maigizo kikionesha igizo namna mtoto wa kike anavyokabiliana na changamoto za unyanyasaji kutoka kwa jamii katika hafla ya uzinduzi rasmi wa kampeni za kupinga ndoa za utotoni kwa watoto wa kike