Tunaangalia jinsi ya kufuta karo shule zote za sekondari za Serikali - Rais Kikwete


Serikali inajipanga kufuta ada za sekondari, ili elimu kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne, itolewe bure.
 
Rais Jakaya Kikwete, alisema hayo juzi katika mkutano wake na wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Mzumbe cha Morogoro, na wakazi wa vijiji vya jirani na chuo hicho, katika ziara yake inayoendelea katika Mkoa wa Morogoro iliyoanza Agosti 20.
“Sasa hivi tunaangalia jinsi ya kufuta karo katika shule zetu zote za sekondari za Serikali, ili kuhakikisha kila mtoto anayeanza darasa la kwanza, awe na nafasi ya kumaliza
sekondari kwa maana ya kidato cha nne, bila kulazimika kuacha shule kwa sababu ya ada.
“Tunaangalia kuondoa ada hii, ambayo wazazi wanalipa Sh 20,000 kwa shule za kutwa na Sh 70,000 kwa shule za bweni, ili watoto wetu waingie darasa la kwanza, na kwenda moja kwa moja hadi kidato cha nne bila wasiwasi wa kukwamishwa na ada,”
alisema Rais Kikwete.

Kwa hatua hiyo, Rais Kikwete alisema mbali na kulenga kuinua elimu, pia itawapunguzia mzigo wazazi na walezi wa watoto wanaosoma katika shule hizo za sekondari za Serikali.

Alisema zipo sababu za msingi zinazokwamisha wanafunzi wengi wa shule za sekondari, kuendelea na masomo yao kutokana na wazazi wao kushindwa kulipia karo ya shule, kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo za umasikini.

Rais Kikwete alisema pamoja na kejeli nyingi zilizoelekezwa kwa shule za sekondari za kata, kiasi cha kuitwa Yeboyebo katika miaka ya mwanzoni ya shule hizo, bado zimekuwa na mafanikio makubwa, ambayo ni sehemu ya mafanikio ya Sekta ya Elimu katika miaka karibu tisa ya uongozi wake.

Akielezea historia ya kuanzishwa kwa shule za sekondari za kata, Rais Kikwete alisema wakati alipokuwa akiingia madarakani, hali ya watoto kuingia sekondari kutoka shule za msingi ilikuwa mbaya.Kwa mujibu wa Rais Kikwete, hali hiyo ilisababisha asilimia kati ya sita na kumi tu ya wanafunzi waliomaliza darasa la saba, kusonga mbele kwa sababu shule za sekondari zilikuwa chache.
“Kwa miaka mingi, hatukujenga shule mpya za sekondari na kama mnavyojua, Wakoloni wa Kiingereza ndio kabisa hawakujenga shule. Kazi hiyo waliwaachia Wamisionari. Kwa hiyo wakati tunaingia madarakani, hali ilikuwa mbaya ndiyo maana tukaja na Sera ya Shule za Kata,” 
alisema Rais Kikwete.