Ufafanuzi kuhusu malipo ya posho za Wajumbe wa BMK

Mkurugenzi wa Habari na Itifaki wa Bunge Maalum Bw. Jossey Mwakasyuka (kushoto) akitoa ufafanuzi mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na malipo ya posho za Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba leo katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Bunge mjini Dodoma. Kulia ni Afisa Habari wa Bunge hilo Owen Mwandubya.

Ofisi ya Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma, kupitia Mkurugenzi wa Habari na Itifaki wa Bunge hilo, Bw. Jossey Mwakasyuka imetoa ufafanuzi juu ya taarifa zilizotolewa kwenye vyombo vya habari kuhusu kuchelewa kwa malipo ya posho za Wajumbe wa Bunge hilo.
“Ni vema ikaeleweka kwamba Wajumbe wa Bunge Maalum wote ni watu wenye nafasi zao katika jamii na ni wenye kazi au shughuli zao mahususi zinazowaingizia kipato... Ujumbe wa Bunge Maalum ni nafasi ya muda tu ya kutimiza jukumu la kuliandalia taifa Katiba Mpya,” 
alisema Mwakasyuka kuashiria kuwa ofisi hiyo imekerwa na kuchapishwa kwa taarifa ambazo zinawadhalilisha Waheshimiwa Wajumbe na kuwafanya waonekane wenye kuishi na kufanya kazi kwa kutegemea posho wanazolipwa, jambo ambalo amesema linawavunja Wajumbe moyo na kuwafanya washindwe kuifanya kazi yao vizuri kama ilivyotarajiwa na wananchi.

Amesema Wajumbe wote wa Bunge Maalum ambao wanahudhuria vikao vinavyoendelea wamekwishalipwa posho zao zote kama wanavyostahili.
“Ni vyema ikaeleweka kwamba malipo ya posho yanafuata taratibu za fedha za umma na yanapita kwenye mchakato maalum unaojumuisha kupata orodha za mahudhurio ya Wajumbe kwenye kikao, upatikanaji wa fedha toka Hazina, na upatikanaji wa fedha toka Benki, hivyo wakati mwingine huchukua siku kadhaa hadi kukamilika.”