Viongozi hao, James Mbatia wa NCCR MAGEUZI, Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF na Freeman Mbowe wa CHADEMA, wamesema UKAWA inaamini kwamba hakuna katiba itakayotengenezwa kwa kudharau maoni ya wananchi, na bila kuwa na maridhiano hivyo kuendelea na Bunge Maalum la Katiba ni kupoteza fedha nyingi za walipa kodi.
James Mbatia amesoma azimio hilo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Kiongozi mwingine wa UKAWA, Profesa Ibrahim Lipumba amesisitiza kwamba Rais alifanya kosa kubwa kuvunja iliyokuwa tume ya mabadiliko ya katiba kabla ya kumalizika kwa mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya huku Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe akilalamikia alichodai kuyumba kwa uongozi wa nchi katika kipindi hiki muhimu kwa mustakabali wa taifa.
Kundi la UKAWA linalojumuisha wanachama wa vyama vya siasa vya upinzani vimesusia vikao vya Bunge Maalum la Katiba tokea kuanza tena Agosti Tano, mwaka huu kwa madai kwamba rasimu ya katiba inayojadiliwa sio iliyopelekwa Bungeni na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, mgogoro mkubwa ukiwa kwenye muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
via VOASwahili