Usahihishaji mpya wa mitihani ya Taifa Kidato cha IV na VI

USAHIHISHAJI mpya wa mitihani ya Taifa kwa kidato cha nne na sita, unaoendana na utaratibu mpya wa upangaji wa ufaulu na madaraja, unatarajiwa kuanza kutumika katika mtihani wa majaribio wa kidato cha nne mwaka huu nchini kote, na kufuatiwa na mitihani yote ya kidato cha nne na sita.

Akitangaza mabadiliko hayo muhimu jana Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA), Dk Charles Msonde, alisema tayari maelekezo kuhusu mabadiliko hayo, yameshatolewa kwa wakuu wa shule za sekondari nchini.

Baadhi ya faida ya mabadiliko hayo kwa mujibu wa Dk Msonde, ni pamoja na kuondoa ukadiriaji wa alama za ufaulu, uliokuwa ukitumiwa awali, kuweka uwazi katika usahihishaji na kumwezesha mwanafunzi kukokotoa ufaulu wake hata kabla ya matokeo na hata mwalimu kukotoa ufaulu wa wanafunzi wake kabla hata ya matokeo.

Kwa mujibu wa Dk Msonde, mwalimu na mwanafunzi wataweza kukokotoa alama za ufaulu, kwa kuwa
majibu yanayotumika kusahisha mitihani kila mwaka na namna wanafunzi walivyojibu, yatarejeshwa shuleni, ili mwalimu afahamu hali ya wanafunzi na ufundishaji.

Pili kwa mujibu wa Dk Msonde mabadiliko ya sasa, yatamwezesha mwalimu kufahamu shida ya wanafunzi wake kulingana na taarifa ya ufaulu wa waliopita na kufahamu wapi patumike mbinu gani kuinua ufaulu.

Ukadiriaji

Kwa mujibu wa Dk Msonde, mabadiliko hayo yanaanza katika mfumo wa viwango vya ufaulu, kutoka katika Mfumo wa Viwango vya Ufaulu Vinavyobadilika, kwenda katika Mfumo wa Viwango vya Ufaulu Visivyobadilika.

Mfumo wa Viwango vya Ufaulu Vinavyobadilika, Dk Msonde alisema ulianza kutumia tangu mwaka 1973, wakati Necta ilipoanzishwa mpaka 2011.

Akifafanua kuhusu mfumo huo ulioachwa mwaka 2011 na kuzikwa rasmi kuanzia mwaka huu, Dk Msonde alisema wanafunzi wakifeli sana, Necta ililazimika kukadiria viwango vya ufaulu kuwa vya chini kabla ya kutoa matokeo.

Alisema walikuwa wakiangalia wastani wa ufaulu na kulinganisha na mwaka uliopita, kama ni wa chini waliangalia waliofaulu sana na waliofeli sana, kisha waliangalia tofauti ya alama ya ufaulu kati ya waliofaulu na baada ya hapo walikuwa wakibadilisha viwango vya ufaulu kuwa vya chini kabla ya kutoa matokeo.

Alitoa mfano, kama mwaka uliopita wastani viwango vya ufaulu wa somo kama Historia ulikuwa 60 na mwaka huo wastani huo ukashuka kuwa 40, ilikuwa ishara ya kwanza kuwa somo husika mwaka huo wamefeli sana.

Kutokana na hali hiyo, alisema kama alama A ilianzia 80 mpaka 100, Necta iliweza kushusha ianzie 70 mpaka 100, ili hata waliopaswa kuwa na alama B, wapande kidogo na hivyo hivyo katika alama zinazofuata.

“Hivyo katika mfumo huu, viwango vya ufaulu hupangwa kwa kutegemea watahiniwa walivyofaulu somo husika, hivyo viwango hivyo vya ufaulu hutofautiana baina ya somo na somo na kati ya mwaka mmoja na mwingine,” alisema Dk Msonde.

Matokeo yake, Dk Msonde alisema viwango vya ufaulu vilikuwa siri na Baraza halikuwahi kueleza popote kuhusu usiri huo na wadau walikuwa na habari za kupotosha kuwa A ilikuwa inaanzia 81 na D ikianzia 21, wakati katika hali halisi kuna wakati viwango hivyo vilishuka.

Kuzika ukadiriaji

Kuanzia mwaka huu Mfumo wa Viwango vya Ufaulu Visivyobadilika, unaanza kutumika na viwango hivyo ni vipya baada ya kupangwa kwa kuangalia mwenendo wa ufaulu wa miaka 12, kuanzia 1999 hadi 2011.

Dk Msonde alisema katika miaka hiyo 12 ya kuangalia, A ya juu ilikuwa mwaka 1999 na 2011, ambapo ilianzia 70 mpaka 90. Alisema hakuna mwaka A ilishuka chini ya 70. Alama D katika miaka hiyo 12, ilianzia 30 mpaka 45.

Baada ya kupata alama hizo, Dk Msonde alisema walitafuta wastani wa A katika miaka hiyo 12 ambao ulikuwa ni 76.2 na wengi waliopata A ya chini katika muda huo ilikuwa 75.

Katika kutafuta wastani wa D katika miaka hiyo 12, ulikuwa 33.3 na D iliyotumika sana katika miaka hiyo ilikuwa 30 ndipo wakaamua kuweka viwango vipya vya ufaulu.

Viwango vipya

Baada ya wastani huo, Dk Msonde alisema walianza kupanga viwango vipya vya ufaulu ambavyo vitatumika katika usahihishaji wa mtihani wa taifa wa kidato cha nne na mtihani wa taifa wa kidato cha sita, ambao hautakuwa na tofauti katika ya mitihani hiyo.

Kabla ya viwango hivyo, kidato cha sita kilikuwa na alama saba za ufaulu, yaani A, B, C, D, E, S na F wakati kidato cha nne kilikuwa na alama sita za ufaulu, yaani A, B, C, D na F.

Katika viwango vipya kutakuwa na alama saba za ufaulu kwa mitihani yote ya kidato cha nne na kidato cha sita, ambayo ni A ambayo itaanzia (75-100), tafsiria yake ni Bora sana.

Kutakuwa na B+ (60-74, vizuri sana); B (50-59, vizuri); C (40-49, wastani); D (30-39, inaridhisha); E (20-29; hairidhishi) na F (0-19, amefeli).

Madaraja zamani

Mbali na mabadiliko katika viwango vya ufaulu, mabadiliko mengine yaliyofanyika ni katika ukokotoaji wa madaraja ya ufaulu, kutoka Mfumo wa Ukokotoaji wa Jumla wa Pointi (TPGS), ambao umekuwa ukitumiwa tangu 1973 mpaka 2014 kwenda Mfumo wa Wastani wa Ukokotoaji wa Pointi (GPA) utakaotumika katika matokeo ya kidato cha nne ya mwakani.

Katika mfumo wa TPGS, alama A ilikuwa na pointi 1; alama B+, pointi 2; B, pointi 3; C pointi 4; D pointi 5; E pointi 6 na F pointi 7.
Kwa kuwa upangaji wa madaraja, uliangalia masomo saba ambayo mwanafunzi alifaulu zaidi, mwanafunzi aliyefaulu sana katika mfumo huo, kwa maana ya kupata alama A masomo yote saba, alipata Daraja la Kwanza lenye pointi saba, kwa maana na kila somo pointi moja.
Madaraja mapya

Katika mfumo wa GPA, Dk Msonde alisema alama A inakuwa na pointi 5; B+, pointi 4, B pointi 3; C pointi 2; D pointi 1; E pointi 0.5 na F pointi 0. Katika hilo, mtahiniwa ataanza kuhesabika amefaulu somo endapo atapata alama D, ambayo ni sawa na pointi 1.

Akielezea namna alama hizo zitakavyotumika kupanga madaraja, Dk Msonde alisema mfumo utakuwa kujumlisha alama za ufaulu za mwanzo katika masomo saba na kugawanya kwa saba, hivyo mwanafunzi atakayefaulu sana na kupata alama A katika masomo saba, atapata jumla ya alama 35, ambayo ikigawanywa kwa masomo hayo saba, atapata pointi 5, ambayo ndiyo utaulu wa juu utakaoitwa ‘Distinction’.

Hivyo madaraja mapya kwa kidato cha nne yatakuwa daraja la kwanza ‘Distinction’ pointi (3.6-5.0); pili ‘Merit’ (2.6-3.5); tatu ‘credit’ (1.6-2.5); nne pass (0.3-1.5) na aliyefeli ‘fail’ (0.0-0.2).

Kwa kidato cha sita, atakayefaulu sana kupata A katika masomo matatu ya ‘combination’, atakuwa amepata jumla ya pointi 15 na ukigawanya kwa tatu, yaani masomo matatu ya ‘combination’, naye atapata 5.

Hivyo madaraja mapya kwa kidato cha sita yatakuwa daraja la kwanza ‘Distinction’ pointi (3.7-5.0); pili ‘Merit’ (3.0-3.6); tatu ‘Credit’ (1.7-2.9); nne ‘pass’ (0.7-1.6) na aliyefeli ‘fail’ (0.0-0.6).

via HabariLeo