Walaani Polisi kuua mahabusu kwa risasi na kusingizia alipigwa na wananchi

WANANCHI wilayani Geita mkoani Geita wamelaani vikali kitendo cha askari polisi wa kituo kikubwa cha wialaya kwa kumpiga risasi ya mbavu na kumuua maabusu na kumjeruhi mwingine wakati wakiwapanga kurudi gerezani.

Mmoja wa shuhuda wa tukio hilo ambaye hakutaka kuandikwa jina lake kwa sababu za kiusalama alisema kuwa tukio hilo lilitokea tarehe 18 mwezi huu majira ya saa saba mchana katika viwanja vya mahakama ya Wilaya mara baada ya watuhumiwa kuanza kupangwa kwa ajili ya kurudi Gerezani.

Shuhuda huyo aliongeza kuwa wakati maabusu huyo akipewa karanga na ndugu yake aliyekuwa mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza kesi walishtukia Askari mmoja ambaye hakujulikana jina lake mara moja akimfyatulia risasi ya mbavu mahabusu huyo na kumjeruhi mwingine mguu wake wa kushoto.

Kaim Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoani Geita Pita Kakamba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kumtaja aliyeuawa kuwa ni Masumbuko Shikombe (25), Msukuma na aliyejeruhiwa ni Mashaka Josefu (29), Msukuma na aliyetoroka ni Godfrey Marwa na wote walikuwa mahabusu na walikuwa wanakabiliwa kesi za unyang’anyi wa kutumia silaha na mauaji.

Kaimu Kamanda aliongeza kuwa watu hao walipigwa na wananchi wa Mtaa wa Katoma wakati wakijaribu kukimbia kwa kutaka kutokomea.

Naye Mganga Mfawidhi wa HosptaLi ya wilaya ya Geita Adam Sijaona alikiri kupokea maiti ya mtu huyo na vipimo vya mwanzo vilionyesha kuwa alikuwa ametobolewa sehemu za mbavu na kuongeza kuwa majeruhi hakuletwa katika Hospitari hiyo. Amelilalamikia jeshi la polisi kwa kuchelewesha kibali ili wafanye postmortem na kubaini kilichomuua.

Valence Robert
via Malunde1 blog, 
Geita