Wanafunzi 10 wa Uuguzi Tanzania kupelekwa kujifua Marekani

CHAMA cha Wauguzi Tanzania (TANA), kimesaini mkataba wa makubaliano na Shirika la Colom Foundation Inc kuendesha mafunzo ya uuguzi yatakayofanyika nchini Marekani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Rais wa chama hicho, Paulo Magesa, alisema wauguzi wanahitaji kutoa huduma kwa ufanisi na kwa wakati, hivyo kwa kulitambua hilo, chama chake kimejitahidi kutafuta fursa ya mafunzo ambayo yatawasaidia kujifunza zaidi namna ya utoaji huduma.

Magesa, alisema wamepata nafasi ya kupeleka wauguzi kumi, ambao watachaguliwa Oktoba na watakwenda mwakani katika Chuo cha Dixie State nchini Marekani.

Mkuu wa Colom Foundation Inc, Wilbur Colom, alisema hiyo ni fursa muhimu kwa wauguzi wa Tanzania kwenda kujifunza mambo mengi zaidi yanayohusu taaluma yao na anaamini mafunzo hayo yataweza kutatua kero mbalimbali zilizopo.

via Tanzania Daima

Shirika la Colom Faundation Inc (CFI) la Marekani limetoa ufadhili wa mafunzo ya muda mfupi kwa wauguzi 20 nchini, watakaokwenda nchini humo kujifunza zaidi masuala ya afya ya uzazi na mtoto kwa lengo la kuboresha huduma hiyo nchini.

Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Rais wa Chama cha Taifa cha Wauguzi nchini (TANNA), Paulo Magesa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Magesa alisema makubaliano hayo, yamefanywa baina yao na CFI. Alisema katika mpango huo wa mafunzo, awamu ya kwanza wauguzi 10, kati ya 20 watakwenda nchini Marekani majira ya joto katika Chuo Kikuu cha Dixie kwa ajili ya mafunzo ya wiki nane.

Alifafanua jinsi ya kuwapata wauguzi hao, kwamba watatangaza nafasi hizo za mafunzo kwenye vyombo vya habari ili kutoa fursa kwa wauguzi nchini, kuomba na kwamba wenye sifa watafanyiwa usaili na watakaoshinda ndio watakaokwenda.

Magesa alisema gharama zote za mafunzo hayo, zitagharamiwa na shirika hilo na kwamba kwa wale watakaopata nafasi za mafunzo, watakaporudi watatakiwa kutoa mafunzo kwa wengine ambao hawakupata fursa hiyo.

Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuboresha huduma za afya nchini, hasa kwa afya ya mama na mtoto.

Alisema kwamba fursa hiyo, itakuwa endelevu ili kutoa nafasi zaidi kwa wengine kushiriki na kurudi kusaidia huduma za afya ya uzazi kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa CFI ambaye pia ni mwekezaji nchini wa Hoteli za Nashera, Wilbur Colom alisema wameingia kwenye mkataba huo, ikiwa ni sehemu ya kusaidia jamii ya Tanzania kutokana na wao kuwekeza hapa nchini.

“Tumeamua kuwa na makubaliano ya ushirikiano na TANNA, tumewekeza nchini, na tuna wajibu wa kusaidia jamii tuliyomo, ili tuendeleza undugu na kusaidiana ili afya ya mama na mtoto iboreke,” alisema Colom.

TANNA ilianzishwa nchini mwaka 1979, ikiwa ni chama cha wauguzi wenye taaluma ambao wamesajiliwa katika baraza ya wauguzi na ina matawi 29 nchini, yenye zaidi ya wanachama 3,500 ambao wanafanya kazi kwenye taasisi mbalimbali nchini.

via HabariLeo