BUNGE LA TANZANIA
OFISI YA MBUNGE WA JIMBO LA KIGAMBONI
TAARIFA KWA UMMA
MREJESHO WA KIKAO CHA MASHAURIANO KUHUSU MPANGO KABAMBE WA UENDELEZAJI WA MJI MPYA WA KIGAMBONI KILICHOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA CHUO CHA MWALIMU NYERERE, KIGAMBONI, TAREHE 10.08.2014
1. Siku ya Jumapili, tarehe 10 Agosti, 2014 saa 4.00 asubuhi kilifanyika kikao cha mashauriano kuhusu Mpango Kabambe wa Uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni uliotishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Profesa Anna Kajumulo Tibaijuka (Mb) na kuhudhuriwa na mimi, Dkt Faustine Ndugulile (Mbunge, Jimbo la Kigamboni), Waheshimiwa Madiwani wa kata za Kigamboni, Tungi, Mji Mwema, Kibada, Madiwani Viti Maalum pamoja na baadhi ya Watendaji wa Kata zilizo kwenye mradi wa Mji Mpya wa Kigamboni.
2. Madhumuni ya kikao hicho ilikuwa ni:
i) Kutoa elimu na ushawishi kwa waliohudhuria kikao hicho kukubaliana na utaratibu wa wananchi waliomo ndani ya eneo la Mpango Kabambe wa Uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni kukatwa asilimia kumi (10) ya fidia watakayolipwa kama hisa wakati utekelezaji wa mpango huo utakapoanza.
ii) Kutoa taarifa kwa waalikwa kuhusu kuanza rasmi kwa mikutano ya hadhara ya kuomba ridhaa ya kuipitisha Rasimu ya Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni (Public Hearings) kuanzia tarehe 24-29 Agosti 2014 katika kata za Kigamboni, Tungi, Mji Mwema, Somangila,Vijibweni na Kibada.
3. Suala la hisa kutoka kwenye fidia za wananchi lilijadiliwa kwa kirefu na kuibua maswali mengi kuliko majibu. Baadhi ya maswali ni pamoja:
a. Ni sheria ipi mahsusi inayotumika kumlazimisha mwananchi wa Kigamboni kukatwa asilimia kumi kama hisa?
b. Ni lini wananchi wa Kigamboni walishirikishwa na kuazimia sharti hilo?
c. Fedha hizo za hisa zitapelekwa wapi?
d. Ni taasisi gani itakayosimamia hisa hizo?
e. Mfumo na usimamizi wa taasisi hiyo ukoje?
f. Fedha hizo zitatumikaje?
g. Kwa nini hisa isiwe ardhi inayomilikiwa na mwananchi?
h. Kwa nini iwe asilimia kumi na isiwe chini au zaidi?
i. Masharti ya kumiliki hisa hizo yakoje?
j. Gawio la faida au hasara litaanza baada ya muda gani na litakuwaje?
Hatimaye iliazimiwa kuwa wakati utakapowadia wananchi wataelimishwa ipasavyo kuhusu hisa na litakuwa la hiari na si lazima. Suala la hisa lisiwe ni kigezo au sharti la kupokea fidia.
4. Kuhusu mikutano ya hadhara ya kuomba ridhaa ya kuipitisha Rasimu ya Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni (Public Hearings), washiriki wa kikao waliochangia katika mjadala huu walimtahadharisha Mhe. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusu ugumu wa zoezi hili kutokana na madhila yaliyojitokeza katika mitaa ya Kifurukwe na Uvumba, alikoanza kufanya uthamini tangu mwezi Machi 2013, na kubaki na hoja ambazo hazina majibu hadi hivi sasa, Mhe. Waziri alishauriwa kusitisha zoezi hilo katika kata nyingine na badala yake ajikite kutatua kero za wananchi wa Kifurukwe na Uvumba kwanza. Vile vile Mhe. Waziri alikumbushwa kuzingatia maagizo na maelekezo ambayo hajayatekeleza hadi sasa ikiwa ni pamoja na:
i) Kurudisha mrejesho kwa baraza la madiwani la Manispaa ya Temeke kuhusu hoja zilizotolewa katika kikao chao cha mwisho kilichofanyika baina ya madiwani na Mhe. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenye ukumbi wa Manispaa.
ii) Maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Mazingira yaliyomo katika hotuba yao iliyowasilishwa tarehe 28 Mei 2014 katika mkutano wa 15, kikao cha 20 cha Bunge mjini Dodoma.
Kamati hiyo ilitoa maagizo kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kama ifuatavyo:
a. “Kuanza mara moja kukamilisha maandalizi ya mpango kabambe na kuanza urekelezaji wa mradi. Lakini ili hilo lifanikiwe kuna haja ya Serikali kubadili mkakati wake wa utekelezaji wa mradi huu. Kamati inashauri Serikali ijishughulishe na ujenzi wa miundombinu na maendeleo mengine yaachiwe wawekezaji na wananchi wanaomiliki ardhi Kigamboni.
a. “Kuanza mara moja kukamilisha maandalizi ya mpango kabambe na kuanza urekelezaji wa mradi. Lakini ili hilo lifanikiwe kuna haja ya Serikali kubadili mkakati wake wa utekelezaji wa mradi huu. Kamati inashauri Serikali ijishughulishe na ujenzi wa miundombinu na maendeleo mengine yaachiwe wawekezaji na wananchi wanaomiliki ardhi Kigamboni.
b. Kuanzia sasa Serikali iwashirikishe wananchi wa Kigamboni katika kila hatua ya utekelezaji ikiwa ni pamoja na suala la fidia.
c. Serikali ihakikishe kwamba, wataalamu wa Wizara ya Ardhi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Katiba na Sheria na wadau wengine wote wanaohusika katika ustawishaji wa mipango miji na makazi wahusishwe kikamilifu.
d. Mapendekezo yote yatakayotolewa na wadau wote wakati wa mchakato ni muhimu yaletwe kwenye Kamati ili kujiridhisha, lengo likiwa ni kuepuka kutokea tena kwa utata wa utekelezaji wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni”
iii) Utekelezaji wa kauli ya Mhe. Waziri Mkuu aliyoitoa Bungeni tarehe 28 Mei 2014 katika mkutano wa 15, kikao cha 20 cha Bunge mjini Dodoma, alipoombwa kutoa msimamo wa serikali kuhusu Mradi wa Uendelezaji Upya Mji Mpya Wa Kigamboni ili kunusuru kukwama kwa bajeti ya ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nilipotoa shilingi katika mshahara wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Waziri Mkuu alisema yafuatayo:
“Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme tu kwamba, niliposikiliza taarifa ya kamati na kama mtaona Taarifa ya Kamati na kama mtaona ukurasa wa 22 na 23 na zile kurasa za mwisho kwenye hitimisho, yapo mawazo ambayo nafikiri ni mazuri sana. Kinacholeta tatizo hapa inaonekana pengine Serikali hatujafanya kazi ya kutosha katika kuelimisha jamii juu ya mradi wenyewe, namna utakavyosimamiwa, utakavyoendeshwa na kubwa zaidi dhana hizi mpya za hisa, unajua ni dhana ambazo zinahitaji elimu ya kutosha. Hata haya mambo mengine ambayo yanadaiwa hapa ya kutoshirikishwa na kadhalika, kwa sababu yamesemwa hapa ndani ya Bunge, mimi nadhani jibu sahihi tukubali.
Tukubaliane na aliyosema Mheshimiwa Ndugulile pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba, acha Serikali jambo hili tulichukue upya, tupitie maeneo yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyasema, tutashirikisha Wabunge wenyewe na zile Wizara zote ambazo zinahusika. Kubwa ni Baraza la Madiwani katika Manispaa ya Temeke, maana eneo hili mpende msipende, ni eneo ambalo lipo chini ya Manispaa hiyo. Tulichofanya ni kuchukua eneo kwa madhumuni ya uendelezaji, lakini hatuwezi kuacha lile Baraza bila kulielimisha kiasi cha Kutosha (Makofi).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nikuhakikishie, na niwaombe wenzangu kwamba, Serikali acha ilipe uzito unaotakiwa, naamini tutafikia mahali pazuri tu bila tatizo kubwa (Makofi)…”
5. Mhe. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alishauriwa kuzingatia na kuyafanyia kazi maagizo na maelekezo yaliyoainishwa hapo juu kabla ya kuendelea na zoezi lingine lolote na pia kuelekeza nguvu zaidi kwa maeneo ya Kifurukwe na Uvumba kwa kutatua changamoto zilizojitokeza huko wakati wa zoezi la uthamini.
6. Ikumbukwe kuwa katika zoezi la uthamini lililoendeshwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika mitaa ya Uvumba na Kifurukwe kuna matatizo makuu mawili yaliyojitokeza:
i) Baadhi ya wananchi walikubali kuthaminiwa na wengine walikataa kwa kutokufuatwa kwa sheria na taratibu.
ii) Wizara kutokuwa na fedha za kutosha kulipa fidia toka ilipoanza zoezi hilo mpaka sasa.
iii) Wakati zoezi hilo linafanyika na mpaka sasa, hakuna na Mpango Kabambe (Master Plan) ulioidhinishwa kwa matumizi.
Mhe. Waziri alishauriwa atanzue kwanza changamoto hizi ili kujenga imani kwa wananchi wa maeneo mengine yaliyomo ndani ya mradi.
7. Baada ya majadiliano marefu, yafuatayo yaliazimiwa:
i) Suala la hisa litakuwa ni hiari. Wananchi wapewe elimu ya kutosha ili kufanya maamuzi sahihi bila shinikizo.
ii) Mikutano ya hadhara iliyopangwa kwenye kata nyingine zilizo kwenye eneo la mradi kuhusu kuidhinisha rasimu ya Mpango Kabambe wa Uendelezaji Mji Mpya wa Kigamboni isitishwe na badala yake nguvu ielekezwe kwenye kutanzua changamoto zilizojitokeza mitaa ya Uvumba na Kifurukwe;
iii) Utekelezaji wa maazimio haya uende sambamba na utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na maelekezo ya Mhe. Waziri Mkuu
8. Mwisho, ninawaomba wananchi wote wa Kigamboni, waendelee kudumisha amani na utulivu. Pia ninawaomba wananchi wa mitaa ya Uvumba na Kifurukwe kuwa wavumilivu wakati tunaendelea kuyafanyia kazi maazimio haya na maagizo mengine yaliyotolewa na vyombo vingine ambayo hayajatekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi hivi sasa.
Dkt Faustine Ndugulile (MB)
MBUNGE
JIMBO LA KIGAMBONI
Kwa taarifa zaidi, bofya hapa kupakua Taarifa kwa umma