Afisa Usalama wa Taifa Mstaafu azungumzia Urais: Sifa, Tahadhari na Nyerere, Mwinyi, Mkapa

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa na Waziri wa kwanza wa Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Dk. Hassy Kitine, amewataka Watanzania kuwa macho dhidi ya watu wanaojitangaza kutaka urais kwani wengi wao huwa na ajenda binafsi na hawajui kuwa urais siyo lelemama.

Dk. Kitine ambaye pia ni miongoni mwa makada wa miaka mingi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amekosoa harakati za kusaka urais zinazofanywa na baadhi ya wanachama wa chama hicho, akieleza hofu yake kuwa wanaofanya hivyo hawaonyeshi kuwa na ajenda ya dhati ya kutaka kuutumikia umma wa Watanzania.

Akizungumza na NIPASHE katika mahojiano maalum mwishoni mwa wiki, Dk. Kitine alisema: "Mtu anayetangaza (mwenyewe) kuwa anataka kuwa rais anakuwa hajui anachokisema... anakuwa hajui matatizo ya urais. Na mtu asiyejua matatizo ya urais anaweza kujisemea tu kwa sababu haelewi urais maana yake ni nini," alisema Dk. Kitine.

"Pili, mtu anayejua maana na changamoto za urais hawezi kutangaza anautaka urais. Ataogopa kwa sababu ya changamoto (nyingi) za urais... kwa hiyo hawezi kujitangazia ovyo kuutaka."

Alisema anachoamini ni kwamba siku zote, rais bora wa nchi hawezi kutangaza kirahisi kuwa anataka kuwa rais kwa sababu hiyo si kazi lelemama na mara nyingi huwa haina shukrani.

"Kumpata rais bora kutatokana na watu wengine wanasema fulani anaweza kutusaidia... na wala siyo yeye (mhusika) kuanza mbinu na kutafuta hela ... na kununua kura, na kufanya mbwembwe na vituko vingi. Hao wote wanaofanya hivyo hawana ajenda yoyote ya kuwatumikia wananchi na taifa.

"Ajenda zao ni nyingine. Wanatafuta urais wanufaike wao, familia zao na watoto wao," alisema Kitine.

NYERERE, MWINYI, MKAPA

Kitine alisema hata Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hakuanza kuutafuta urais bali wazee wa mkoa wa Dar es Salaam ndiyo waliomuomba na kumpendekeza kuwa awe kiongozi wa nchi.

Alisema aliyekuwa kiongozi wa chama cha Tanganyika Africa Association (TAA), Abdul Sykes pamoja na viongozi wengine wa wakati huo kama Takadiri, ndiyo walioamua kumteua Mwalimu Nyerere ili aongoze shughuli za ukombozi. "Kwa hiyo walimsukuma watu wengine na siyo yeye."

Alisema hata rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, hakuutafuta mwenyewe urais bali watu wengine walimwomba kushika wadhifa huo kwa sababu waliona kuwa anafaa.

"Nakumbuka aliyekuwa Katibu Mkuu wa ASP, Thabit Kombo, alikuwa amelazwa KCMC. Ilibidi akachukuliwe kwa ndege ya serikali, akaletwa Dodoma. Halmashauri Kuu ikamuuliza... tusaidie, unadhani ni nani anaweza kuwa Rais wa Jamhuri, akamtaja Mzee Mwinyi. Watu wote, wajumbe wa Bara na Unguja wakakubaliana na mapendekezo ya Mzee Thabiti Kombo. Ninachosema ni kwamba Mzee Mwinyi hakuutafuta urais," alisema.

"Alikuwa hana habari kabisa kama vile ilivyokuwa Mwalimu Nyerere. Hakuanza yeye. Ni watu wengine walianza kusema tunaona (huyu) awe kiongozi wetu."

Dk. Kitine alitoa mfano mwingine kwa Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa; akisema kuwa naye hakuwa anataka kuwa rais bali aliombwa na kushinikizwa na Baba wa Taifa (Mwalimu Nyerere).

"Walikuwa kama watu 17 hivi. Kila mmoja anakwenda kwa Mwalimu... Mwalimu anawaambia tu nendeni, ni haki ya kila mmoja," alisema.

Alisema baada ya vikumbo vingi, kila aliyekwenda kwa Mwalimu Nyerere alijitangaza kwamba anaungwa mkono.

Hata hivyo, Dk. Kitine alisema alichokuwa anakifanya Mwalimu Nyerere ni kusema ukweli kuwa hana uwezo wa kumzuia mtu yeyote kugombea bali wanachama na wananchi ndiyo watakaoamua.

Alisema yeye anakumbuka vyema kuwa Mkapa hakuutaka urais na kwamba, (Mkapa) alikuwa wa mwisho kujaza fomu za maombi ya kuwania nafasi hiyo baada ya kushinikizwa sana na Mwalimu Nyerere.

"Kwanza Mkapa alikataa... akamwambia (Mwalimu), Mzee mimi naogopa... kwa kweli naona tabu sana. Mwalimu akamwambia hili jambo siyo lako na Anna (mke wa Mkapa)... ni letu sote. Kwa hiyo nenda haraka kajaze fomu."

Alisema baada ya Mkapa kujitetea kadri ya uwezo wake ili kuepuka jambo hilo, Mwalimu Nyerere alimwambia utetezi wake hauna nguvu kwa sababu alikuwa ameshaagiza viongozi wengine wa chama kuhakikisha wenyeviti wa CCM mikoa yote wanamuunga mkono.

Alisema mfano huo wa Nyerere na waliomfuatia unadhihirisha kuwa wote hawakuwahi kujitangaza wenyewe kuwa wanautaka urais hapo kabla bali walishinikizwa na kwamba jambo hilo linampa hofu kuwa harakati za sasa zilizoanza kufanywa na baadhi ya makada wa CCM hazitatoa kiongozi bora.

"Kwa hiyo rais bora ambaye atatusaidia ni yule ambaye hana ajenda ya kuutaka urais, (bali) ataambiwa na kusukumwa na watu wengine," alisema Kitine.

"Hawa (wanaojitangaza sasa) wanazo ajenda nyingine, siyo za kulitumikia taifa," alisema.

SIFA ZA RAIS

Kabla ya kutaja sifa za rais bora, Dk. Kitine alisema anakubaliana na sifa zote zilizotajwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Mzee Cleopa Msuya ambazo zilichapishwa na NIPASHE wiki iliyopita, ambazo zilikuwa ni pamoja na .............

Sifa alizoziongeza Dk. Kitine kwa mtu anayestahili kuwa rais ajaye wa Tanzania ni; Mosi, lazima awe mwadilifu wa asili na siyo wa kujifanya, na pia ambaye amezaliwa huku akiwa tayari Mwenyezi Mungu ameshampa karama hiyo ya uadilifu.

Pili; mzalendo anayeipenda nchi yake na Watanzania na kwamba, hata anapokuwa ikulu, awe na nia ya kusaidiana na Watanzania wenzake kuboresha maisha.

"Tatu; awe rais ambaye tunamtegemea... kwa sababu atakuwa mwadilifu, awe na uwezo wa kufanya maamuzi na kukemea uchafu wote ambao uko katika nchi. Huwezi kukemea kama siyo mwadilifu. Mtu fisadi huwezi kusema ufisadi mbaya wakati na wewe ni miongoni mwao," alisema Kitine.

Nne; Rais awe amesoma. Siyo lazima awe na elimu kubwa sana, lakini angalau awe na shahada ili akiongea na wenzake huko nje awe na uelewa.

"Tano; rais ambaye tutakuwa naye awe ni mtu anayejua utawala bora, utawala wa kufuata sheria... haya mambo ya kujichukulia sheria mkononi, mob justice, na kuua watu.. ni ishara tu kwamba hakuna utawala wa sheria," aliongeza.

Sita; ni lazima ahakikishe na aonekana kuwa anachukia rushwa na ufisadi. Hawezi kuwa mnafiki katika hili.

Saba; rais lazima aijue nchi yake na awe na utaalam wa kuilinda nchi yake. Lazima ajue jeshi sana.

Nane; lazima ajue usalama wa nchi.

"Tisa; ni lazima ajue uchumi wa nchi, tena uwe kwenye kiganja chake. Ajue viwanda, uchumi mkubwa na mdogo na changamoto zake; ajue miundombinu na implications (athari) za gesi, mafuta na madini. Ajue faida zake kwa Watanzania na ahakikishe kila mwananchi anapata nyumba nzuri ya bati na tofali.

Ajenge shule na hospitali haziko umbali wa kilometa tano na serikali ihakikishe kila mwananchi anapata huduma za msingi kama umeme na maji ... ni kwa sababu hili linawezekana kutokana na utajiri mkubwa tulionao," alisema.

Sifa muhimu ya kumi ni kwamba, rais bora awe na kundi moja tu, nalo ni la Wananchi anaowaongoza na siyo anayezungu huku na huko kwa nia ya kuunda makundi.

TAHADHARI KWA CCM

Dk. Kitine alizungumzia pia tabia iliyoanza kuota mizizi ya baadhi ya watu kutumia nguvu ya fedha kupata nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM, akionya kuwa kuruhusu siasa za kutegemea fedha badala ya sifa muhimu za msingi ni kuhatarisha uhai wa chama.

Alisema matumizi makubwa ya fedha ndani ya CCM yanachangia umasikini kwa wanachama na wananchi kwa sababu kiongozi anayetafuta wadhifa kwa kununua hawezi kukubali kuwainua wananchi kwani anajua kuwa wakikombolewa kweli kutoka kwenye lindi la umaskini atashindwa kuwanunua baadaye.

Dk. Kitine amezungumzia ajenda hiyo wakati ambao joto la uchaguzi na harakati za makundi zikiendelea ndani ya CCM huku baadhi ya makada wakitangaza nia yao hadharani kuwa watajitosa kuwania nafasi ya kuwa wagombea wa CCM wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.

* Mbali na kuzungumzia sifa za urais, Dk. Kitine pia alizungumzia mchakato wa katiba na mwelekeo wa Bunge la Katiba. Usikose kile alichokizungumzia kwenye eneo hilo kesho.

RESTITUTA JAMES
NIPASHE - Dk. Kitine: Urais siyo lelemama