Meena akamatwa Dar kwa kujifanya Afisa Usalama wa Taifa

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAMBO YA NDANI

JESHI LA POLISI TANZANIA

PRESS RELEASE
02/09/2014

ANAYEJIFANYA AFISA USALAMA WA TAIFA ANASWA DAR ES SALAAM

Mtu mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kutokana na makosa mbalimbali ya kujifanya ni mtumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa. Mtu huyo anayejulikana kwa jina la GUNNER S/O SAIMON MEENA, Miaka 40, Mkazi wa Kinyerezi Segerea anatuhumiwa kuwasumbua wafanyabiashara mbalimbali jijini Dar es Salaam kwa kuwasingizia au kuwatuhumu kwamba wanahusika na makosa yenye kuhatarisha usalama.

Kwa muda mrefu Jeshi la Polisi limekuwa likimtafuta mtu huyo kutokana na malalamiko mengi
ambayo yamekuwa yakijitokeza na uchunguzi unaonyesha kwamba jina lake halipo katika orodha ya watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Tukio la mwisho lililomfanya akamatwe ni pale alipomtishia mfanyabiashara mwenye asili ya kisomali aitwaye ABDI S/O MOHAMED DALMAR. Katika tishio hilo la kutishia mtuhumiwa GUNNER S/O SAIMON MEENA ambaye ni Afisa Usalama feki alidai apatiwe kiasi cha fedha za kitanzania TSHS 25,000,000/= (SHILINGI MILLIONI ISHIRINI NA TANO) ama sivyo angechukuliwa hatua chini ya sheria ya Usalama wa Taifa.

Mlalamikaji alitoa taarifa na ndipo mtuhumiwa akakamatwa katika mtego wa Polsi. Uchunguzi zaidi wa shauri hili unafanyika na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya jalada la kesi yake kupitiwa na mwanasheria wa Serikali.

S. H. KOVA
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM