Buriani Mtaalamu Bingwa wa Menejimenti ya Fedha na Uhasibu, Prof. Rwegasira

http://www.msm.nl/resources/uploads/2014/08/Kami-Rwegasira.jpg http://dailynews.co.tz/images/THELATERWEGA.jpg
Mwaka 2012 nilipata neema ya kusoma stashahada ya juu katika utafiti katika moja ya vyuo bora vya masomo ya menejimenti barani Ulaya kilichoko katika iimbo ya Lumburg nchini Uholanzi kijulikanacho kama Maatristch School of Management (MsM). 
Siku moja nikiwa katika harakati za kupata ushauri wa kimasomo kutoka kwa Profesa aliyekua ananisamia, aliniuliza iwapo namfahamu Profesa mwenye asili ya kitanzania aliyeko katika chuo hicho. Alinielekeza ofisini yake na kwa kiu ya kukutana na mtanzania mwenzangu katika nchi ya ugeni nilikwenda kumtafuta mtu huyu nisiyemfahamu. Huyu hakua mwingine bali Profesa Kami S. P. Rwegasira ambaye alikua mtaalamu gwiji wa mambo ya fedha na uhasibu (A Senior Professor in Finance and Accounting). P
amoja na kwamba hakua mtaalamu wa fani yangu ya mifumo ya kompyuta alitaka kujua utafiti wangu
unahusu kitu gani na ndani ya dakika chache alinishauri na kunipa andiko lililoandikwa na mwanafunzi aliyemaliza shahada ya uzamivu katika chuo hicho miaka michache iliyopita ili nilisome kwani lilikua na dhima inayoendana na utafiti wangu.

Siku chache zilizofuata wanafunzi wa kitanzania tuliokua kwenye chuo kile, tulipata mwaliko wa kuhudhuria sherehe fupi iliyoandaliwa kuheshimu mchango na utumishi uliotukuka wa Profesa Kami wa miaka 25 katika ukuaji wa chuo kile. Ilikua ni nafasi nzuri ya kuona tamaduni za matukio ya kisomi katika nchi ya ugeni na hivyo nilihakikisha nimehudhuria. Pamoja na mambo mengi yaliyoendelea pale, ulisomwa wasifu mfupi wa Profesa Kami ambao ulinipa maswali na changamoto kubwa juu ya jinsi gani nchi yetu inatumia vema rasilimali watu tulizonazo. Kami (kama alivyozoea kujiita) alikua mhimili mkubwa wa MsM tangu kuanzishwa kwake na alikua ameshika nafasi kadhaa za uongozi wa chuo. Alihusika na uanzishwaji wa programu za shahada za uzamili na uzamivu katika chuo kile na katika vyuo vingine chini ya mwevuli wa MsM kwenye nchi nyingi duniani
ikiwepo Tanzania (Esami Arusha), Misri, Kuwait, Afrika Kusini, Namibia na kwingineko. Kama vile haitoshi, Kami alikua amefanya tafiti na kuandika machapisho mengi sana ikiwa ni pamoja na vitabu vitano na machapisho ya kitafiti kwenye zaidi ya majarida (Journals) 70. Alikua ametoa ushauri wa kitaalamu kwa mashirikika mengi ya kimataifa na serikali kadhaa ikiwa ni pamoja na kuzishauri nchi kadhaa za Ulaya namna bora ya kumeneji mapato na matumizi ya serikali zao. Uzoefu wake wa kitaalamu katika mambo ya fedha ulizisaidia nchi nyingine kama vile Norway, Marekani, China, Brazil, Peru, Mashariki ya Kati, Mashariki na Kusini mwa afrika pamoja na Kusini Mashariki mwa Asia. Kutokana na uwezo wake, Prof Kami alikua ametambuliwa kama mtu mwenye uwezo na utaalamu wa juu na taasisi kubwa za kimataifa duniani kwa vipindi tofautitofauti.

Haikua rahisi sana kukutana na Profesa Kami ndani ya chuo cha MsM kwani mara nyingi alikua amesafiri na alitumia zaidi ya 60% ya siku zote za mwaka akiwa safarini kufundisha na kutoa shauri wa kitaalamu na mihadhara ya kisomi vyuo vikuu mbalimbali duniani. Siku alizokuwepo chuoni nilibahatika kuzungumza naye mara nyingi tulipokua tunakutana wakati wa chakula cha mchana kwenye mgahawa ndani ya chuo. Waswahili huwa wana msemo wao kuwa watu fulani wameivana damu...nami nadhani nilipata kibali ya kuivana damu na Profesa Kami kwani alikua akitaka sana kujua maendeleo yangu mara kwa mara na kunitia moyo kusoma. Tulitumia muda mwingi tukiongea mambo yahusuyo maendeleo ya Tanzania na baadaye niligundua ni mfuatiliaji mzuri wa Michuzi Blog katika kupata habari za nyumbani.
Profesa Kami akiwa katika mazungumzo na Dada na Shemeji yake Neuwied Ujerumani



Nakumbuka siku moja Profesa aliniambia tukatembee nchini Ujerumani bila kunipa maelezo zaidi. Ilikua kipindi cha baridi kali Ulaya kimeshaanza hivyo kuamka asubuhi na mapema ilihitaji bidii na kujivisha nguo za kutosha. Tulitoka Uholanzi asubuhi na mapema akiendesha gari lake aina ya BMW kwa uangalifu mkubwa na tulikwenda mwendo wa zaidi ya masaa mawili ndani ya Ujerumani hadi kwenye mji mmoja mdogo ulioko eneo la mashambani ujulikanao kama Neuwied. Huku tulikwenda kumsalimia mdogo wake wa kike ambaye ameolewa na Mjerumani na wamekua huko kwa zaidi ya miaka 30 na Kami alikua ana zaidi ya mwaka hawajaonana. Tukiwa njiani nilipata muda wa kuongea mengi na Profesa kuhusu hali ya elimu, uchumi na siasa za nchi yetu na bara la Ulaya. Profesa alinisaidia sana kuelewa kwa nini nchi kama Ugiriki na Spain zilikua zinakabiliana na tatizo kubwa la kuanguka kwa uchumi na hivyo kuwa na migomo na maandamo yasiyokwisha. Alinisaidia kuelewa nini jukumu la Benki Kuu ya Jumuia ya Ulaya katika kusaidia hali iliyokua inaziandama nchi nyingi za Ulaya na kwanini ni vigumu sana kwa nchi kama zetu za Africa Mashariki kukubali kuwa na soko moja la fedha (Benki Kuu moja) kirahisi.

Nilimchokonoa Profesa juu ya mchango wake kwa nchi yetu na nilimuuliza moja ya maswali niliyoyapata siku alipokua anafanyia sherehe ya miaka 25. Nilimuuliza ni kwa nini uzoefu alionao kushauri nchi zilizoendelea za Ulaya na kwingineko kuhusu menejimenti ya fedha hajautumia katika nchi yetu ya Tanzania kusaidia hali iliyoko. Majibu ya Profesa hayakua ya kunifurahisha mimi wala yeye mwenyewe ila kwa kifupi alinionesha jinsi gani nchi yetu isivyothamini sana utaalamu na wataalamu katika kuendesha mambo yake. Alionesha namna gani SIASA imekua na nguvu juu ya kila kitu na hivyo kutokuipa kazi ya kitaalamu heshima inayostahiki. Profesa hakua tu ana uzoefu mkubwa nje ya nchi akiwa kama msomi, bali alikua na uzoefu kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Taasisi cha Usimamizi wa Fedha IFM ambapo alikua kiongozi kabla hajaamua kutumia utaalamu wake nje ya nchi. Tulizungumzia maadili n atulizungumzia uwajibikaji. Kwa kifupi kumsikiliza Profesa Kami ilikua ni zaidi ya kusoma Kitabu. Alingea kwa unyenyekevu na kwa lugha nyepesi yenye lengo la kufundisha.

E:\Prof Kami\regermanyphoto\DSC01034.JPG E:\Prof Kami\moreofgermanyphotos\DSC01052.JPG
Safari ya Neuwied Ujerumani: Profesa akimpa dada yake zawadi ya maua toka Uholanzi

Nilishangazwa sana na unyenyekevu, upendo na kujali kwa Profesa Kami ambaye nilibahatika kujenga naye urafiki bila hakujali tofauti kubwa ya umri, utaalamu na nafasi kati yetu. Siku ya mwisho baada ya kumaliza masomo na hivyo kurudi nyumbani, Profesa Kami alitoka safari na kuja kunichukua chuoni kwenda kuninunulia chakula cha jioni cha kuniaga. Pamoja na mafanikio yake nje ya nchi, alikua na ratiba ya kuja kupumzika nyumbani kwake Mikocheni kila baada ya muda wa miezi kadhaa. Miezi michache baada ya mimi kurudi Tanzania, alikuja mapumzikoni na kufika nyumbani kwetu kuijulia familia yangu hali. Mke wangu na mimi tulijisikia kuheshimika sana kwa kupata rafiki kama huyu.

Mwezi October mwaka 2013, Profesa Kami alimua kustaafu kazi katika chuo cha MsM na kuamua kurudi nyumbani kutumikia nchi yake tena kwa utaalamu wake kupitia Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Kutokana na kazi yake kubwa ya kisomi na kitaalumu, Chuo cha MsM kilimtunukia cheo cha juu kabisa katika ngazi ya kitaalamu kiitwacho Emeritus Professor hivyo kumfanya kuwa the Emeritus Professor of Financial Management and Accounting. Cheo cha Emeritus Professor hutolewa na vyuo vikuu kama heshima ya juu kwa maprofesa waliostaafu huku wakiwa wametoa mchango uliotukuka katika fani yao kama wasomi. Professor wa cheo hiki hapangiwi tena kazi kama kawaida kwa wanataaluma, bali hupewa uhuru wa kufanya kile akipendacho na kwa muda wake hadi atakopokosa nguvu au kufariki.

Siku sio nyingi sana, Profesa Kami alinaindikia ujumbe kwa njia ya barua pepe akinitaka tupange moja ya siku ili mimi na familia yangu tukutane naye nyumbani kwake Mikocheni kwani angekua Tanzania kwa muda mrefu kidogo na alitaka tuonane kabla sijasafiri. Tarehe 26 mwezi wa nane nikiwa bado sijatimiza ahadi yangu ya kukutana na Profesa kami, niliamka asubuhi na mke wangu akaniuliza iwapo nimesoma habari za kifo cha rafiki yangu Profesa Kami. Aliniambia hana hakika sana lakini amesoma kwenye moja ya mitandao habari za kifo cha ghafla cha Kami akiwa nchini Rwanda kwa safari ya kikazi chini ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Profesa Kami alifariki tarehe 23 August ikiwa ni siku mbili tu kabla ya kutimiza miaka 66 tangu kuzaliwa kwake.

Habari hii ilinishtua sana, na kwa maumivu sikua na maneno ya kueleza nilichokisikia na kwa bahati mbaya nilipata habari hizi mwili wa Profesa ukiwa umeshasafirishwa kwenda nyumbani kwao Bukoba kwa mazishi. Najua mke na watoto wake wawili wameumia na kushtuka sana kwa kifo hiki cha ghafla cha kiongozi wa nyumba yao; lakini kifo hiki kimeshtua na kimeumiza wengi na majonzi ya kumpoteza Kami ni mazito sana. Ninakichukia kifo maana mara zote kimekua sabab ya maumivu na kilio na hakipendezwi na uhai wa watu wema kwenye jamii yetu.

Kwa heri heri rafiki yangu mwanazuoni Emeritus Professor Kami S.P. Rwegasira

Mwalimu MM