Hekaya: Kisa cha Abunuwasi na Mfalme

HEKAYA ZA ABUNUWASI ni kitabu cha hadithi za kusisimua, zinazofurahisha sana kutokana na umahili wa watunzi wa vitabu vya kale. Kutokana na utamu wa hadithi za ABUNUWASI, Blog ya MPIGANAJI itawaletea hadithi hizo ili kuwachangamsha akili...

KISA CHA ABUNUWASI NA MFALME


SIKU moja alfajiri, wakati wananchi wa mji wenye wakazi wengi walipokwenda kuchota maji mtoni, walishangazwa kuuona mkono wa mtu ukiwa katikati ya mto. Mkono huo wa ajabu ulikuwa umenyoosha vidole viwili juu, kuonyesha alama ya mbili.

Wananchi walistushwa sana na kitendo hicho, wakaogopa hata kuchota maji mtoni, kwani hawakuwahi kuona tukio la kuogopesha kama lile. Wengine waliamini kuwa huo ulikuwa mwili wa mtu aliyetupwa mtoni.

Lakini ishara iliyoonyeshwa na mkono huo iliwafanya wananchi waamini kuwa huo ulikuwa
mkono wa ajabu. Katika kiza kinene kilichozunguka ndani ya vichwa vya wananchi, habari zikamfikia Mfalme wao, naye akafika haraka eneo la tukio.

Mfalme wa nchi hiyo baada ya kujiridhisha kuwa ulikuwa mkono wa ajabu na uliwekwa na watu wenye imani za kishirikiana, alitoa siku tatu mkono huo uwe umeondolewe, vinginevyo ataleta wataalam kutoka sehemu mbali mbali duniani kwa ajili ya kubaini wahusika.

Siku tatu zilizowekwa na Mfalme zikaisha, wataalam wa mambo ya asili kutoka sehemu mbali mbali duniani wakaanza kuwasili mtoni hapo kwa lengo la kuundoa mkono huo wakashindwa.

Mfalme akatoa ofa nono, waganga wenye sifa na jeuri ya mambo ya jadi wakamiminika eneo la mto, wakafanya mitambiko na mambo yao kwa ufanisi zaidi, wengine wakalala mtoni kuonyesha umahili wao lakini wakashindwa na kuuondoa mkono huo wa ajabu...

Mfalme na wasaidizi wake wakakuna vichwa, wananchi hawana jinsi ya kupata maji. Maji mtoni hayachoteki, wananchi wanaogopa kutumia maji hayo. Ndipo Abunuwasi akajitokeza mbele ya Mfalme. Akamwambia Mfamle, "Mimi naweza kujaribu.

Mfalme akamfukuza Abunuwasi kwa hasira, akamwambia. "Mpumbavu sana wewe, hapa wameshindwa waganga na waganguzi, wewe Abunuwasi utaweza wapi, usitupotezee muda wetu".

Abunuwasi akaondoka, waganga wakazidi kumiminika mtoni wakitoka sehemu mbali mbali za dunia kutokana na sifa zao. Kila walichofanya kuuondoa mkono huo wakachemka na kuondoka eneo hilo kimya kimya.

Abunuwasi akamrudi Mfalme, akamwambia, "Wacha nijaribu mimi". Mfalme akamjia juu akamwambia. "Nimesema huwezi Abunuwasi, wameshindwa waganga wa dunia, utaweza wapi wewe?, Abunuwasi akasisitiza. "Wacha nijaribu mimi kama walivyojaribu wengine na kushindwa.

Mfalme kwa hasira akamwambia Abunuwasi, "Haya jaribu, maana unataka kutupotezea muda tu hapa, lakini ole wako ukishindwa, nitawaamru askari wakutie ndani".

Abunuwasi akaanza kuuzunguka mto huku umati wa wananchi ukimwangalia kwa makini, alipita huku na huku akikimbia kama mtu aliyepatwa na wazimu, Mfalme akaanza kuchukia, hatmaye Abunuwasi akakaa sambamba na mkono ule, Abunuwasi akachuchumaa chini na kuinua mkono wake juu mfano wa mkono ule.

Mfalme na wananchi walikuwa kimya wakifuatilia kwa makini tukio hilo, Abunuwasi aliuchezesha mkono wake kushoto na kulia, mkono ule ndani ya maji nao ukafanya vile, kama alivyofanya Abunuwasi. Wananchi wakashangazwa mno na kitendo kile.

Abunuwasi akauvuta mkono wake nyuma, mkono huo pia ukafanya hivyo, Abunuwasi akakunja kidole chake kimoja, mkono ndani ya maji nao ukafanya vile. Hatmaye Abunuwasi akaushusha mkono wake chini kama anaudhamisha, mkono ule nao ukadhama na haukuonekana tena.

Mayowe, vigelegele na shangwa vikasikika, Mfalme akasimama akamfuata Abunuwasi, akamuomba radhi, akamtukuza na kuonyesha kufurahishwa. "Ahsante sana Abunuwasi, umetuondolea aibu, nisamehe kwa kukudharau, sikutegemea kabisa".

Wananchi wakaja juu wanamtaka Abunuwasi apewe Ufalme. Maana ameweza kufanya jambo lililowashinda waganga na waganguzi. Mfalme akahamaki. Abunuwasi akaula...

--
Shukurani:
Mpiganaji (Maseypr): HEKAYA ZA ABUNUWASI