Hotuba ya Mzee Nyangaki Shilungushela, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Nyangaki Shilungushela akizungumza na Wanahabari.

HOTUBA YA MWENYEKITI WA TAIFA WA BARAZA LA WAZEE WA CHADEMA MZEE NYANGAKI SHILUNGUSHELA KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA BARAZA LA WAZEE WA CHADEMA TAREHE 6 SEPTEMBA 2014 KATIKA UKUMBI WA MLIMANI CITY DAR ES SALAAM


Waheshimiwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Wazee wa CHADEMA Taifa,

Waheshimiwa Waasisi wa CHADEMA mliohudhuria mkutano wa leo,

Waheshimiwa Wasimamizi wa Uchaguzi wa Baraza la Wazee wa CHADEMA Taifa,

Waheshimiwa Wawakilishi wa Chama Taifa na Makao Makuu,

Waheshimiwa Wageni waalikwa; mabibi na mabwana:

Waheshimiwa Wazee;

Niungane nanyi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha siku ya leo katika Mkutano Mkuu wa Baraza la Wazee wa CHADEMA Taifa. Niwasalimu kwa kauli mbiu ya Baraza letu: Wazee, Hazina ya Hekima na Busara.

Tumekutana katika Mkutano Mkuu huu tukiongozwa na dhumuni kuu la Baraza la Wazee wa CHADEMA kwa mujibu wa kipengele cha 1.1 cha kuwa chombo kikuu cha ushauri wa busara na
hekima kinachowezesha CHADEMA kufikia na kuendeleza madhumuni ya CHADEMA kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Mkutano huu mara baada ya ufunguzi utajadili ajenda kuu nne: Mosi, Taarifa ya Utendaji wa Baraza la Wazee wa CHADEMA, Pili, Marekebisho ya Mwongozo wa Baraza la Wazee wa CHADEMA, Tatu, Mpango Kazi wa Baraza la Wazee wa CHADEMA kwa mwaka 2014-2016 na Nne, Uchaguzi wa Viongozi wa Taifa wa Baraza la Wazee wa CHADEMA.

Wajibu wangu katika hatua ya sasa ni kufungua mkutano huu rasmi na nimeona nichukue fursa hii kuzungumza machache kabla ya Taarifa ya Sekretariati ya Wazee ambayo itatoa maelezo juu ya Utendaji wa Baraza la Wazee katika kipindi cha kati ya mwaka 2009 mpaka 2014 na ajenda nyingine ambazo zitatoa mwelekeo wa 2014 mpaka 2016.

Kabla ya kuendelea na hatua hiyo, niwaomba tusimame kwa dakika moja ya ukimya kuwakumbuka Wazee wenzetu viongozi na wanachama wa Baraza la Wazee waliotangulia mbele ya haki katika kipindi cha tangu tulipokutana katika Mkutano Mkuu wa Wazee.

Wazee hao ni pamoja na Hayati Mzee Mohamed Bob Makani aliyekuwa muasisi, Katibu Mkuu wa kwanza na Mwenyekiti wa Pili wa CHADEMA, marehemu Wazee Balozi Pastor Ngaiza, Philip Shilembi na Shida Salum waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya chama, viongozi na wanachama wengine; Mwenyezi Mungu awalaze mahali pema.

Waheshimiwa Wazee;

Niwapongeze kwa kuchaguliwa kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Wazee kwa mujibu Taratibu za Kuongoza Baraza la Wazee wa CHADEMA kipengele 4.7.4.

Nitumie nafasi hii pia kuwaomba mfikishe salamu zangu za pongezi kwa viongozi wote wa Baraza la Wazee wa CHADEMA walioshinda katika ngazi mbalimbali kuanzia misingi, matawi, kata/wadi, wilaya na Mikoa.

Hakika ushindani katika chaguzi hizo na kiwango cha wagombea waliojitokeza kwenye uchaguzi wa ngazi ya taifa ni ushahidi wa ukuaji wa CHADEMA na namna ambavyo wazee wanazidi kujiunga na CHADEMA na kuwa mstari wa mbele kuwezesha mabadiliko nchini.

Hali hii inapaswa kuendelezwa na viongozi wa kitaifa watakaochaguliwa katika Mkutano Mkuu huu. Hali hii ni matokeo pia ya msukumo ulioongezwa na muundo wa Kanda na Programu ya CHADEMA ni Msingi.

Hivyo, ni muhimu katika maeneo ambayo hayajakamilisha uchaguzi ngazi ya chini, mara baada ya Mkutano huu; nyinyi, viongozi wa kitaifa watakaochaguliwa na kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi mbalimbali kwenda kukamilisha chaguzi katika maeneo machache yaliyobaki hususan katika vitongoji, vijiji na mitaa kupitia mwendelezo wa Programu ya CHADEMA ni msingi.

Kwa mafanikio haya ya ujenzi wa CHADEMA, napendekeza kwamba Mkutano Mkuu huu wa Wazee upitishe azimio la kutaka Serikali kutangaza haraka uchaguzi wa Vitongoji, vijiji na Mitaa wa mwaka 2014 kwa kuwa kuchelewa kutangazwa kwa uchaguzi huo mpaka hivi sasa sababu mojawapo ni hofu ya CCM kushindwa katika maeneo mengi nchini.

Aidha, mafanikio haya ni dalili njema ya CHADEMA kwa kushirikiana na vyama vingine vya upinzani hususan vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) vya kuiondoa CCM madarakani kupitia chaguzi za udiwani, ubunge na urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Katika muktadha huo, katika kujadili Mpango Kazi wa Baraza la Wazee kwa mwaka 2014 mpaka 2016, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Wazee mtoe mapendekezo yatakayowezesha kukamilisha chaguzi za wazee katika maeneo machache yaliyobaki kwenye ngazi za misingi, matawi, kata/wadi, wilaya na mikoa ili kuwezesha ushindi katika maeneo yote muhimu.

Pamoja na kazi hii, anzeni kujiandaa kuhamasisha wazee kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura. Napendekeza pia Mkutano Mkuu huu upitishe azimio la kuitaka Tume ya Uchaguzi (NEC) kutangaza mara moja ratiba ya uandikishaji wa wapiga kura kwa kuwa iliahidi kwamba zoezi hilo lingeanza maeneo mbalimbali nchini kuanzia mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka 2014.

Kampeni za uchaguzi zitakapoanza Mpango Kazi wa Wazee uwezeshwe uwepo wa wazee kwenye kamati za kampeni katika vituo vya kupigia kura kuwezesha ushindi wa CHADEMA na washirika wake katika chaguzi zote zinazofuata.

Waheshimiwa Wazee;

Muongozo wa baraza la Wazee wa CHADEMA kipengele 1.2 (f) unatoa jukumu kwa baraza letu kubuni mipango na mikakati ya kuhusisha kundi la wazee ndani ya jamii kukagua, kusimika na kuchagua viongozi bora kwenye chaguzi za ndani na nje ya chama.

Nimeweka kipaumbele suala la uchaguzi kwa kuwa tupo katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa ndani ya CHADEMA unaofanyika ikiwa ni takribani mwezi mmoja kutoka kuanza kwa kampeni za uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa wa mwaka 2014 na mwaka mmoja kutoka katika kampeni za uchaguzi mkuu wa udiwani, ubunge na urais wa mwaka 2015. Nimeweka kipaumbele suala la uchaguzi kwa kuwa nchi yetu ipo kwenye mkwamo wa mchakato wa mabadiliko ya katiba.

Wakati sisi tunapokutana hapa, Bunge Maalum linaendelea kupokea taarifa za Kamati mbalimbali huku wanaojiita walio wengi katika Bunge hilo wa CCM na vibaraka wao wakiendelea kupuuza maoni ya wananchi na kubomoa misingi ya rasimu iliyowasilishwa na tume ya mabadiliko ya katiba.

Natambua kwamba rasimu ya katiba itayopendekezwa hatimaye itakuja kupigiwa kura ya maoni ambao hao wanaojiita walio wengi wa CCM katika Bunge Maalum watakutana na wananchi walio wengi waliotoa maoni yao.

Hata hivyo, Baraza la Wazee wa CHADEMA ni muhimu kupitia mkutano mkuu huu lipitishe azimio la kulaani hatua ya Wazee wa CCM wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalum Samuel Sitta na Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete kushindwa kutoa uongozi wa kunusuru fedha za umma kuendelea kutumika huku kukiwa hakuna muafaka wa kitaifa kwenye mchakato.

Kwa upande mwingine, nashauri Mkutano Mkuu wa Baraza la Wazee wa CHADEMA upitishe azimio la kuwapongeza Wazee wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti Jaji (Mstaafu) Joseph Warioba na wajumbe wake akiwemo mzee mwenzetu mteule kupitia CHADEMA Prof. Mwesiga Baregu kwa kuheshimu maoni ya wananchi na kuzingatia sehemu kubwa ya maoni hayo katika rasimu ya pili ya katiba iliyowasilishwa.

Waheshimiwa Wazee;

Muongozo wa Baraza la Wazee kipengele cha 1.2 (a) kimetoa jukumu kwa Baraza la Wazee wa CHADEMA kuwa chombo cha ushauri ngazi mbalimbali za chama. Wajibu huu ni wa baraza na wazee wanachama wa baraza letu. Kwa kuzingatia wajibu huo, nimeshiriki kwa niaba yetu katika vikao vya kamati kuu kwa nyakati mbalimbali na katika vikao vya kupanga mikakati ya chama kwa miaka kadhaa.

Kati ya masuala ambayo vikao hivyo vimekuwa vikiyapa kipaumbele ni mchakato wa mabadiliko ya katiba.

Wazee ni hazina ya hekima na busara. Hivyo, ushauri wangu mara nyingi umekuwa ni kwa CHADEMA kuwezesha maridhiano, usuluhishi na utatuzi wa migogoro inayojitokeza kwenye mchakato wa mabadiliko ya katiba.

Hata hivyo, katika hali ambayo imefikia ya mgogoro baina ya CCM kwa upande mmoja na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na wananchi walio wengi waliotoa maoni yao kwa upande mwingine; na kuvunjika kwa mazungumzo yaliyoongozwa msajili wa vyama vya siasa nashauri viongozi wa CHADEMA na UKAWA nashauri wachukue tahadhari kubwa katika mazungumzo na Rais.

Waheshimiwa Wazee;

Kitendo cha Bunge Maalum kuendelea mpaka hivi sasa hata baada ya kuanza mazungumzo ya Rais na vyama yanayoratibiwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) inaweza kuwa ni mchezo wa CCM na Serikali kuchelewesha maridhiano huku wajumbe wake wakiendelea ‘kuchakachua’ rasimu ya katiba kinyume na maoni ya wananchi.

Hivyo, tarehe 8 Septemba 2014 iliyotangazwa na Ikulu kuwa ni mwendelezo wa mazungumzo na Rais inapaswa kuwa nafasi ya mwisho iwapo Bunge Maalum halitasitishwa au kuahirishwa ni muhimu viongozi wa taifa wa CHADEMA wakashauriana wenzao wengine wa UKAWA kufanya maamuzi ya kuwaunganisha wananchi kwa nguvu ya umma kuchukua hatua kwa CCM na Serikali.

Mwelekeo unaonyesha kwamba wazee wa CCM ndani ya chama hicho, Bunge Maalum, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Serikali za pande zote mbili za Muungano wameamua kusaliti maoni ya wananchi na matakwa ya kikatiba kwamba mamlaka na madaraka ni ya wananchi.

Katika muktadha huo, ufumbuzi endelevu ni kuiondoa CCM madarakani na kuweka uongozi bora na chama kitakachokuwa na dhima ya kuleta sera sahihi, mikakati makini na oganaizesheni makini katika mchakato wa mabadiliko ya katiba na maendeleo ya nchi.

Mabadiliko ya Katiba sio mchakato wa kuchukuliwa kwa mzaha. Ni mchakato unaohusu maisha ya wananchi na mustakabali wa nchi. Pamoja na CCM kukataa maoni ya msingi ya wananchi juu ya muundo wa muungano wa Shirikisho la Serikali tatu, chama hicho kupitia wajumbe wake wanaojiita walio wengi kinapinga maoni ya wananchi yaliyoingizwa kwenye rasimu ya katiba ikiwemo uadilifu, uwazi na uwajibikaji kuwa sehemu ya tunu za taifa.

Kwa kuzingatia maoni hayo, CCM na wajumbe wake wanaojiita walio wengi hawana uadilifu, uwazi na uwajibikaji wa kuweza kusimamia masuala ya msingi yanayohusu wazee katika rasimu ya katiba ikiwemo ya kuhakikisha kwamba hifadhi ya jamii hususan pensheni inatolewa kwa wote (universal social security particularly pension).

Waheshimiwa Wazee;

Masuala na maslahi ya wazee chini ya chama kinachotawala sasa yamekuwa yakipewa kipaumbele kwenye ahadi badala ya kuwekwa katika utekelezaji. Matokeo yake ni migogoro ya wazee kama ambavyo inajitokeza kwa nyakati mbalimbali kwa wazee wanaodai mafao yao.

Taarifa ya utendaji ya sekretariati itaeleza namna ambavyo Baraza la Wazee wa CHADEMA limekaa na wazee wenye madai mbalimbali ikiwemo wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika maboresho ya Mpango Kazi 2014 mpaka 2016 natarajia wazee wajumbe wa mkutano huu mtatoa mapendekezo ya namna ya kuwezesha Baraza letu kuongeza msukumo katika kuwawakilisha na kuwatetea wazee nchini.

Kilio cha wazee wengi kimekuwa ni umaskini na hali ngumu ya maisha kutokana na wenye kupata pensheni kupata kiwango kidogo kwa waliokuwa waajiriwa katika sekta rasmi na wengi zaidi kutokuwa kabisa na pensheni baada ya kustaafu kwao hasa wakulima na wazee waliotumikia taifa katika sekta isiyo rasmi.

Kwa nyakati mbalimbali katika siku ya Wazee Duniani Oktoba Mosi kati ya mwaka 2009, 2010, 2011, 2012 na 2013 Serikali imekuwa ikiahidi kutoa pensheni kwa wazee wote nchini; hata hivyo hakuna mwaka mpaka sasa ambao bajeti imetengwa kuwezesha utekelezaji. Wanachama wa Baraza la Wazee wa CHADEMA wamekuwa wakifuatilia suala hili ikiwemo kupitia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Ahadi za uongo zimekuwa zikitolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na mawaziri wengine kuhusu suala hili. Nitoe mwito kwa viongozi wa wazee kutoka mikoa mbalimbali mlioshiriki mkutano huu kuanza maandalizi mara baada ya kurejea katika maeneo yenu ili kuziunganisha ngazi zenu na za chini yenu katika maadhimisho ya siku ya wazee kwa mwaka huu Oktoba Mosi, 2014 ujumbe ufike kwa watawala kwamba wazee wamechoka kudanganywa na wako tayari kuunga mkono mabadiliko kuchangua uongozi ambao utatekeleza ahadi kwa vitendo.

Wazee wanaweza kuendelea na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi wakiwa na mazingira bora. Hivyo, katika Mkutano huu Taarifa ya Sekretariati ya Baraza la Wazee itawajulisha hatua iliyofikiwa katika mchakato wa kuboresha Sera ya Wazee ya CHADEMA. Nawahimiza kushiriki katika kushiriki michakato yote ya sera mbalimbali zenye kuwagusa wazee kwa namna au nyingine zitakazotekelezwa na CHADEMA kitakapoongoza Serikali.

Waheshimiwa Wazee;

Nimalizie kwa kuwakumbusha majukumu ya msingi ya Baraza la Wazee wa CHADEMA kwa mujibu wa muongozo kipengele 1.2 (b), (c) na (j) ya kuwa chombo cha utatuzi na usuluhishi wa migogoro ndani ya chama ama baina ya viongozi, kuwa chombo cha kupatanisha na kuunganisha viongozi na kushauri viongozi wa CHADEMA katika ngazi mbalimbali.

Katika mkutano huu mtapokea mapendekezo ya maboresho na marekebisho ya muongozo wa Baraza la Wazee wa CHADEMA katika maeneo na masuala mbalimbali. Pendekezo langu jipya ni kuhusu jina la Baraza letu; kumekuwa na changamoto ya kutafuta kifupi cha Baraza hili kuweza kutofautiana na Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA). Kumekuwepo pia na ombwe la kutokuwa na Baraza la Wazee katika taifa letu.

Hivyo, pendekezo langu ni kuwa tujitambulishe kama Baraza la Wazee tu. Baraza la Wazee (BAWA) litabeba sura ya utaifa litaendelea kuwa la kitaifa. Jumuiya ya Wazazi ya CCM imeendelea kujitambulisha kama JUWATA ikighilibu wazazi nchini. Umoja wa Wanawake wa CCM, umeendelea kujitambulisha kama UWT ukihadaa wanawake kuwa ni chombo cha wote. Baraza la Wazee (BAWA) sio tu libebe taswira ya wazee nchini, bali lionyeshe kwa vitendo kuwakilisha na kutetea wazee nchini mpaka pale wazee watakapokuwa na chombo chao cha kuwaunganisha wote bila kujadili tofauti mbalimbali.

Katika kujadili mapendekezo hayo, na katika kutekeleza muongozo huo kumbukeni kuwa pamoja na kuwa wanachama na vikao vya kawaida vya ngazi mbalimbali. Mkazo uwekwe katika kuunda “Caucus ya Wazee” katika ngazi zote. Hili ni kundi maalum la kushauri viongozi wa kuanzia ngazi za msingi hadi taifa. Hili ni kundi la wazee wateule wenye busara na hekima lukuki, wanaokubalika na kuheshimika katika jamii na wenye kupatikana mara kwa mara kutoa ushauri. Kwa kufanya hayo mtakuwa mnatekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Baraza la Wazee wa CHADEMA: Wazee; Hazina ya Hekima na Busara. Na kwa kauli mbiu hiyo, natangaza kwamba Mkutano Mkuu huu umefunguliwa rasmi.

Mungu ibariki Tanzania,

Mungu ibariki CHADEMA,

Mungu wabariki Wazee.