IPTL yafungua kesi kumdai Zitto bilioni 500/=

Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), imefungua kesi ya madai katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakimtaka Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe awalipe fidia ya Sh bilioni 500 kutokana na kutoa kashfa dhidi yao.

IPTL, Kampuni ya Pan Africa Power Solutions Tanzania Limited (PAP) na Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni hayo mawili, Harbinder Seth wamefungua kesi dhidi ya Zitto, Mhariri wa gazeti la Raia Mwema, Kampuni ya Raia Mwema na Kampuni ya Flint Graphics.

Washitakiwa wengine wameshitakiwa kwasababu makala yenye maneno ya kashfa na kuwachafua, iliyochapishwa Agosti 13 mwaka huu katika ukurasa wa 7 na 14 wa gazeti lao, ikiwa na kichwa cha
habari cha "Fedha za IPTL ni Mali ya Umma" na Kampuni ya Flint Graphics kwa kuchapisha gazeti hilo.

Aidha, wanaiomba Mahakama iamuru makala hayo, yalikuwa ya upotoshaji na kuwachafua kwa kudhamiria, pia wadaiwa waombe radhi kwa kuchapisha habari ya kuomba msamaha kwenye kurasa za mbele katika matoleo mawili mfululizo ya gazeti hilo. 

Wadaiwa hao waliiomba Mahakama, itoe zuio kwa wadaiwa, watumishi wao, wafanyakazi, washirika, wawakilishi au watu wengine wanaofanya kazi chini ya wadaiwa, kuchapisha au kuandika makala yoyote ya kuwachafua. 

Wanadai makala hayo yalikuwa na maneno “kwa mara nyingine Serikali kupitia viongozi wake akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wamedai kwamba dola milioni 250 za Kimarekani zilizopaswa kuendelea kuwepo katika akaunti ya “Tegeta Escrow Account’ si mali ya Serikali na hivyo si mali ya umma…. 

Akaunti hiyo ilifunguliwa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la TANESCO pamoja na IPTL”. 

Ilidaiwa kuwa kabla ya kusambaza habari hizo, wadaiwa walitakiwa kufanya juhudi za kuthibitisha ukweli kutoka kwao au kwa maofisa husika wa Serikali, ambao wangethibitisha ukweli kuwa fedha zilizowekwa kwenye akaunti ya Escrow, zilikuwa ni dola milioni 122 za Kimarekani na siyo dola milioni 250, kama walivyodai. 

Aidha, wangejua fedha ziliwekwa katika makubaliano ya Escrow ;na siyo kama fedha za umma, lakini ni kutokana na mgogoro wa malipo, yaliyotakiwa kufanywa na Tanesco kwa IPTL. 

Wadai hao walifungua kesi hiyo Septemba 4, mwaka huu kupitia kwa Wakili Melchisedeck Lutema na Kay Felician Mwesiga.