Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif ahutubia Mwanza

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad akiwasili mjini Mwanza, Jumamosi, Septemba 6, 2014.

Khamis Haji, MWANZA — Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amewahimiza wananchi wa mkoa wa Mwanza kujiweka tayari kukipa talaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na waunge mkono Umoja wa vyama unaotetea Katiba ya Wananchi (UKAWA) katika uchaguzi wa 2015 uwaletee mabadiliko ya kimaisha.

Maalim Seif ameyasema hayo alipokuwa akihutubia katika mikutano ya hadhara katika vijiji vya Ngudu na Hungumalwa Wilaya ya Kwimba, akiwa katika zaiara ya siku nne, ambapo pia amefuatana na viongozi waandamizi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa mkoa wa Mwanza.

Maalim Seif alisema katika kipindi cha miaka 53 tangu nchi ilipopata uhuru kila siku zinavyokwenda mbele hali za maisha ya wananchi zinazidi kuwa mbaya, kutokana na nchi kukosa uongozi bora chini Chama cha
Mapinduzi.

“Ujumbe wetu kwenu ni kuwa CCM imeshalewa madaraka haiwezi tena kuwaletea mabadiliko ya kimaisha, kipeni talaka CCM na mchague vyama vyenye uwezo wa kuwaletea maendeleo”, alisema Katibu Mku wa CUF.

Alisema uthibitisho wa CCM kukosa uwezo wa kuwaletea mabadiliko ya kimaisha wananchi ni namna wanavyo vuruga mchakato wa kupata Katiba Mpya ambao wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar walitarajia uweke misingi bora ya maisha yao, ikiwemo matumizi ya maliasili za ardhi, madini, kilimo, elimu bora na utawala bora kwa jumla.

Maalim Seif alisema CCM wamebadilisha maoni ya wananchi yaliyowasilishwa na Tume ya Mbadiliko ya Katiba chini ya Jaji Mstaafu Warioba, maoni ambayo msingi wake ni mfumo wa Serikali tatu baada ya wananchi hao kubaini ndio wenye maslahi kwao.

Katibu Mkuu huyo wa CUF alisema badala yake CCM kimepindua maoni hayo bila ya kujali fedha nyingi zilizotumika, lengo lao likiwa ni kulinda maslahi ya wachache na kupuuza shida zinazowakabili Watanzania ambao wameshaona mfumo wa Serikali mbili hauwafai tena.

Alieleza kuwa wanafanya hivyo kuendeleza ufisadi unaofanywa na baadhi ya viongozi wa chama hicho kama ule wa kuiba fedha nyingi za wananchi na kwenda kuzificha katika mabenki ya nje kama nchini Uswis.

“Vyama vya CUF, CHADEMA na NCCR Mageuzi vina viongozi makini wenye uwezo wa hali ya juu na vimedhamiria kikweli kuwaletea mabadiliko ya kimaisha wananchi wote wa Tanzania, bila ya ubaguzi, kama inavyofanyika chini ya CCM”, alisema.


Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia mkutano wa hadhara Wilayani Kwimba mkoa wa Mwanza
Naye, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Ilemela, Greyson Wanzagi Warioba akihutubia katika mkutano wa Ngudu alisema CCM imejidhihirisha wazi hakikuwa upande wa wananchi kwa miaka yote tangu kupatikana uhuru kutokana na kitendo chao cha kujifungia Dodoma na kupindua maoni ya wananchi wa Tanzania.

Alisema chama hicho kinajali maslahi yao binafsi, na Umoja wa Kutetea maoni ya Wananchi (Ukawa) utaendela kufichua maovu wanayofanya, ili wananchi wayaelewe na wakikatae katika uchaguzi mkuu ujao.

Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Hamis Kambaya alisema Serikali ya CCM haiwajali wananchi wa Kanda ya Ziwa kutokana na kitendo cha kuwapatia wananchi hao mbegu zisizofaa za zao la Pamba.

Mbali na hilo alisema bei ya zao hilo hivi sasa ni ya chini ambayo haiwezi kumsaidia mkulima anayekabiliwa na hali duni ya maisha na kumfaya ashindwe kupata mlo kamili wa siku, mbali na huduma nyengine kadhaa wa kadhaa muhimu za kijamii zinazomkabili.

Mwenyekiti wa Wanawake wa CHADEMA katika mkoa wa Mwanza, Suzan Masele alisema umefika wakati wanawake waepuka kulaghaiwa kwa Khanga na Vitenge kunakofanywa na viongozi wa CCM wakati wa uchaguzi kwa sababu mambo hayo tayari yamepitwa na wakati.