Kwa mara ya kwanza wanaotaka Scotland ijitenge na Uingereza waongoza kwa kura

.
 Evarist Chahali, Uskochi — Zikiwa zimebaki siku 11 tu kabla ya wakazi wa hapa Uskochi kupiga kura ya kuamua iwapo taifa hili liwe huru au liendelee kubaki katika 'Muungano wa Uingereza', kwa mara ya kwanza kabisa, kura ya maoni kuhusu 'uhuru' huo inaonyesha wanaotaka 'uhuru' huo wanaongoza kwa asilimia 51.

Japo kitakwimu, hiyo ni sawa na sare, ukweli kwamba haijawahi kutokea kwa wanaotaka uhuru kuongoza katika kura yoyote ile ya maoni unaleta uwezekano japo kidogo wa kura ya 'Ndiyo' kwa wanaotaka uhuru kufanikiwa.

Kura mpya ya maoni iliyofanywa na taasisi ya kura za maoni inayoheshimika sana hapa
Uingereza, YouGov, inayochapishwa Jumapili hiiinaonyesha wanaotaka uhuru wanaongoza kwa asilimia 51 huku wasiotaka uhuru wakiwa na asilimia 49, ukiondoa wapiga kura ambao hawajafikia uamuzi (undecided).

Kadhalika, gazeti la Sunday Times lililoipa kazi ya kusanya maoni taasisi hiyo ya YouGov linaeleza kwamba Malkia wa Uingereza sasa ameshtushwa na ameagiza kupatiwa maendeleo ya kila siku kuhusiana na kura hiyo.

Serikali 'Kuu' ya Waziri David Cameron sasa inatarajiwa kufanya jitihada za dakika za majeruhi kuokoa 'Muungano' huo wa zaidi ya miaka 300 usivunjike, kwa kutoa madaraka zaidi kwa serikali ya Uskochi.

Kampeni ya 'Better Together' inayopigania kuendelea kwa 'Muungano' huo imekuwa ikiongoza katika kura zote za maoni. Kampeni ya 'Yes' inayounga mkono 'uhuru' ilikuwa nyuma kwa asilimia 22 takriban mwezi mmoja tu uliopita.

Endelea kufuatilia blogu ya Chahali kwa taarifa mpya kuhusu hili na mengineyo.