Maamuzi ya mkutano wa Rais Kikwete na Viongozi wa TCD kuhusu Katiba Mpya na Bunge Maalum la KatibaMkutano kati ya Rais Jakaya KIkwete na viongozi wa vyama vya Siasa vinavyounda Kituo cha Demokrasia nchini (TCD) umekubaliana kufany amarekebisho katika katiba iliyopo na inayotumika sasa ( Katiba inayotumika kwa wakati huu ya mwaka 1977) ifanyiwe marekebisho muhimu ili iweze kutumika katika uchaguzi Mkuu wa mwakani, 2015.

Akisoma tamko la TCD mbele ya Wanahabari mjini Dodoma, Mwenyekiti wa Muungano huo Mhe. John Cheyo, amesema mkutano wao na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, umekubaliana kuwa muda uliobakia kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Mwakani hautoshi kwa mchakato huo kukamilika:
"Hakuna muda wa kutosha kukamilisha mchakato wote na kufanya mabadiliko yanayohitajika kwenye sheria na kanuni ili hiyo Katiba iweze ikatumika. Kwa mujibu wa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, mwisho wa mchakato ni kura ya maoni juu ya Katiba inayopendekezwa, na ingepashwa kufanyika Aprili 20, 2015 kama itabidi kura irudiwe, kwa mujibu wa sheria kura itarudiwa mwezi wa Juni au Julai 20, 2015... na ili Katiba Mpya itumike katika uchaguzi Mkuu utakaokuja, itabidi uhai wa Bunge na Serikali uongezwe zaidi ya 2015, jambo ambalo hatuliungi mkono" 
Kwa maamuzi hayo, ni dhahiri kuwa jukumu la Katiba Mpya litaachwa kwa Rais ajaye.

Mambo ambayo vyama vya siasa wamekubaliana ni pamoja na:

  1. Kuwa na tume huru ya uchaguzi na kusimamia uchaguzi wa mwaka 2015
  2. Mshindi wa uchaguzi wa Rais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50% (yaani 50% + 1)
  3. Matokeo ya uchaguzi wa Rais yaweze kupingwa mahakamani 
  4. Kuruhusu mgombea binafsi katika uchaguzi

Mkutano huo ulifanyika kwa njia ya mashauriano yaliyochukua sura ya Kamati ya Makatibu Wakuu, Kamati ya Wenyeviti wa Vyama vya Siasa vya CCM, CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi katika hatua tofauti.

Mhe. Cheyo ameeleza kuwa kamati zote zilitoa taarifa zao kwenye vikao vya Viongozi Wakuu wa Vyama (Summit) ya TCD ambayo wajumbe wake ni Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na Makatibu Wakuu wa Vyama wanachama.
Cheyo amesema, vyama vingine vya siasa ambavyo vinapenda kupendekeza mambo mengine ya kurekebisha katika katiba ya mwaka 1977 vinaombwa kufanya hivyo mapema kwa kuwa muda uliopo wa kufanya mabadiliko ni mdogo.
“Muda tulionao ni kwa mabadiliko yanayopendekezwa kujadiliwa katika Bunge la Novemba na wakichelewa Bunge la Februari 2015."
Kwa makubaliano hayo, kazi inayofanywa na Bunge maalum la katiba (BMK) ya kuandika katiba mpya itakoma Oktoba 4 mwaka huu, siku ambayo Bunge hilo litakuwa halijakamilisha uandikaji wa katiba ambao unafanywa na kamati ya uandishi iliyo chini ya Andrew Chenge.

Uamuzi huo unakidhi baadhi ya madai ya kundi linalojiita umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA) ambao ni wajumbe waliokuwa ndani ya Bunge maalum la katiba lakini walijiondoa kwa kutoridhishwa na mwenendo wa bunge hilo.

Mhe. Cheyo amesema kuwa Bunge Maalum la Katiba kwa sasa linafanya kazi kwa mujibu wa Tangazo la Serikali (Government Notice) Na 254 lililotolewa na Mhe. Rais Kikwete tarehe 1 Agosti, 2014.

“Tangazo hilo litatumika hadi tarehe 4 Oktoba, 2014 ambapo Katiba inayopendekezwa inategemewa kupatikana, Wajumbe walikubaliana hatua hii iachwe ifikiwe”, alisema Mhe. Cheyo.

Kuhusiana na Kura ya maoni, Mhe. Cheyo ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba baada ya Bunge hilo kumaliza kutunga Katiba, ingefuata hatua ya kura maoni kuthibitisha Katiba.

“Kwa kutambua kuwa hatua ya kura ya maoni italazimisha uchaguzi mkuu 2015 kuahirishwa, basi hatua hii ihairishwe, na mchakato wa Katiba uendelee baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015”, alisema Mhe. Cheyo.

Sambamba na hayo, Mhe. Cheyo ameishauri Serikali kuchukua hatua za kisheria ili matayarisho kwa ajili ya Uchaguzi wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa, yaanze haraka iwezekanavyo ili uchaguzi ufanyike mapema hapo mwakani.

Viongozi hao Wakuu wa Vyama wamempongeza Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa ujasiri wake na imani yake katika kuimarisha demokrasia nchini na kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya nchi.

“Tunampongeza kwa kukubali kukutana na kushauriana nasi kuhusu mambo ya muhimu kwa mustakabali wa taifa letu kwa lengo la kudumisha amani, upendo na mshikamano ili nchi yetu iende kwenye uchaguzi ikiwa ni nchi ya kujivunia yenye amani, mshikamano na itakayokuwa na Uchaguzi Huru na wa haki, lakini pia tunajipongeza sisi wenyewe Wakuu wa Vyama kwa kuwa tumetoka mbali na misimamo yetu, lakini utaifa umetufanya tukubaliane katika mambo ya msingi wa Taifa letu”, alipongeza Mhe. Cheyo.