Mgando wa mawazo kuhusu uraia-pacha

(image: kbaxi.net)

Katika wiki chache zilizopita kumekuwa na mjadala kuhusu moja ya vipengele muhimu vya rasimu ya Katiba ya nchi yetu, uraia pacha. 

Ni jambo linalofurahisha kuona kuwa tumeanza kutambua kwamba mjadala wa Katiba sio tu unatakiwa kuzunguka suala la muundo wa muungano kama tulivyokuwa tunaaminishwa na baadhi ya vyombo vya habari, bali kuna mambo mengi muhimu yanayotakiwa kujadiliwa na kufanyiwa maamuzi. 

Lakini kwa mara nyingine tena, wasiwasi unatuingia baadhi yetu, hasa pale tunapoona watu waliopewa dhamana ya kufanya maamuzi kwa niaba yetu wanashindwa kufanya maamuzi sahihi. Zaidi ya hapo tunaingiwa na wasiwasi zaidi, na kufikiri kuwa inawezekana kuna maamuzi mengine yamefanywa kwa niaba yetu bila sisi kujua, lakini si maamuzi sahihi.

Sijawahi kujiuliza hata siku moja; watu wanaopewa dhamana ya kufanya maamuzi kwa niaba yetu na kwa ajili ya manufaa yetu, wanatumia kigezo gani kufikia maamuzi? Ni busara, elimu, ujuzi au ufahamu wa hali halisi wa jambo wanalofanyia uamuzi? Au ni kuangalia wenye hali ya watu wao au mawasiliano ya moja kwa moja na watu hao kuhusu mambo yanayowakera? Au ni kusikia tu nani amesema nini, au mkumbo tu wa mwenzangu anaamua nini? Katika suala la kuamua muundo wa muungano tumeona kuwa wabunge wakifanya maamuzi kwa kutumia vigezo ambavyo havieleweki kabisa. Si busara, akili, ujuzi, ufahamu, hali halisi au kuwasikiliza wanaowawakilisha. Hali hii imeanza kuonekana tena kwenye kipengele cha uraia. Inatia hasira kusikia baadhi ya wabunge wanasema wamefikia uamuzi wa kupinga hoja hii baada ya maofisa wa uhamiaji kuwaambia hatari za uraia pacha, na si baada ya kuchimba uraia pacha ni nini, una manufaa gani, hasara gani, hatari gani, na kwanini jambo hilo limeingizwa kwenye rasimu ya Katiba. Kama kweli tunafanya maamuzi kwa mtindo huo, basi nadhani kila mtanzania hata asiyejua kusoma na kuandika anaweza kuteuliwa kufanya maamuzi kwa niaba ya wengine.

Serikali yetu, na hasa waziri wa mambo ya nje Mh. Bernard Membe ambaye kabla ya kuwa balozi alifanya kazi katika balozi za Tanzania nje, na rais Kikwete mwenyewe ambaye alikuwa waziri wa mambo ya nje wa Tanzania kwa muda mrefu, wanajua vizuri sana matatizo yanayowakuta watanzania wanaoishi nje. Kwa hiyo msimamo wa wizara ya mambo ya nje, na kubariki suala la uraia pacha, si wa kukurupuka. Lakini vile vile ni lazima tukubali kuwa wasiwasi wa idara ya uhamiaji kuhusu hatari inayoweza kuletwa na suala la uraia pacha, una msingi. Kwa kuwa wao ndio wanajua raslimali gani wanazo katika kusimamia mambo ya raia na uraia, na watakuwa na uwezo gani kushughulikia suala hilo endapo tutakuwa na uraia wa nchi mbili. Kwa akili nyepesi tu ambayo haihitaji shule, wafanya maamuzi wetu walitakiwa kufikia uamuzi baada ya kuweka kwenye mizani mapendekezo ya wizara ya mambo ya nje na wizara ya mambo ya ndani (uhamiaji). Si kutegemea upande mmoja tu.

Sipendi kutaja undani wa manufaa anayoweza kupata mtanzania na Tanzania kwa kuwa na uraia pacha, au hata kwa kuwa na uraia wa nchi nyingine bila kuwa na ule wa Tanzania. Kuna manufaa kwenye kupata elimu kwani ukiwa raia wa nchi fulani unaweza kusoma hadi shahada ya uzamivu katika fani yoyote kwa gharama za chini na bila vikwazo, huduma za afya kwa gharama za chini, ajira za maana na sio kuishia vipindoni, na hata “access” ya baadhi ya mambo ambayo inakuwa vigumu kupata ukiwa na raia wa kigeni. Haya mambo kama mtanzania akinufaika nayo, akiwa na pasipoti ya Tanzania au hata kama hana pasipoti ya Tanzania, kuna uwezekano mkubwa kwa Tanzania kunufaika pia.

Kuna hoja mbili zilizotajwa kupinga au kukosoa hoja zinazounga mkono uraia pacha, ya kwanza ni ile inayohusu “usalama wa taifa”, na nyingine ni ile iliyotaja suala la uzalendo. Kati ya hoja hizi mbili, ya uzalendo sidhani kama ina mashiko hata kidogo, kwa kuwa hata sasa tuna watanzania wengi ambao hata pasipoti hawana na hawafikiri kusafiri nje ya Tanzania, lakini hawana uzalendo hata kidogo kwa Tanzania. Uzalendo wao unaelekezwa kwenye dini au vitu vingine kabisa vya kigeni. Na kuna wengine wenye pasipoti za Tanzania ambao wanaishi na kufanya kazi nje ya Tanzania, wengine wameishi nje huku wakiwa na fursa ya kuwa raia wa nchi nyingine zenye neema na manufaa kwao kuliko Tanzania, lakini walichagua uzalendo kwa Tanzania. Mfano mzuri ni ule wa Mzee Amir Jamal aliyepoteza maisha yake chini Canada, kwa kuushikilia utanzania wake na kumfanya asinufaike na mfumo wa afya kwa raia wa Canada. Kuna watanzania wengi tu “waliojilipua” Ulaya, na wana pasipoti za nchi za huko lakini roho zao bado ziko Tanzania, na wengine wengi waliokuwa na fursa za “kujilipua” Ulaya lakini walichagua Tanzania. Tusidanganyane hata kidogo kuwa kama leo vumbi likitimka Ulaya, baba zetu, kaka zetu na dada zetu kutoka Kariakoo, au wadogo zetu na watoto wetu waliojilipua na kuwa na pasipoti za Ulaya, wakija Tanzania tutawaambia hamruhusiwi kwa kuwa nyie sio watanzania, na hamkuonesha uzalendo “mlipojilipua”. Kwa hiyo kutumia suala la uzalendo kama kisingizio cha kukwamisha uraia pacha, ni aidha ufinyu wa mawazo, au kutojua hali halisi ya changamoto zinazowakabili watanzania walio nje, au ni ajenda fulani ambayo hatujui lengo lake ni nini.

Hoja kuhusu usalama wa taifa ina mashiko, na hii ndio inatakiwa kujadiliwa kwa makini. Lakini inatakiwa kujadiliwa kwa angle sahihi ili tusipotoshe lengo, na isiwe kisingizio cha kuzuia uraia pacha. Kwa dunia ya sasa ambayo mali asili na raslimali zimekuwa za kugombea, watu na nchi wanatafuta kila njia ya kwenda kwenye nchi nyingine kutafuta raslimali hizo. Kwa hiyo kama Tanzania itakuwa na sheria legelege za uhamiaji, basi matatizo yanayotokana na uhamiaji yatakuwa makubwa. Mfano mzuri ninaoweza kuutaja ni ule wa Malaysia. Baada ya nchi hiyo kutumia sheria za kurithi kutoka Uingereza kuruhusu wageni kuingia nchini humo na kupata ukazi na uraia, wimbi kubwa la wageni liliingia, kuzaliana na kuwa wenyeji na idadi yao ikiongezeka na kupita ile ya wazawa wamalayu. Baada ya muda wageni hao wakawa na wingi kiasi cha kuwa na maamuzi kwenye upigaji kura na hata kwenye umiliki wa njia kuu za uchumi baada ya kuingia na fedha kutoka walikotoka na kudhibiti uchumi. Matokeo yake ni kuwa wazawa sasa wamekuwa wachache, na pole pole wanaelekea kuwa watu wa daraja la pili. Lakini baada ya kuona hatari hiyo walichukua hatua ambazo kwa sasa zimekuwa vigumu kuwa na matokeo ya haraka yaliyotarajiwa.

Mfano mwingine wa wazi tumeona hivi karibuni kwenye eneo letu la Afrika mashariki, na kutukumbusha kuwa hatuwezi kuendelea kuwa wajinga na kuamini kuwa mtu anaweza kuukana uraia wake wa damu na kuwa raia wa nchi nyingine (hata kama anajilipua au makaratasi ya kisheria yanayonesha hivyo) kwani vumbi likitimka watu huwa wanabadilika mara moja. Kuna watu tuliowaamini kuwa watanzania wenzetu na kuishi, kusoma nao na kuwaruhusu kufanya kazi hata kwenye ofisi kubwa za nchi yetu, lakini wametutelekeza na kurudi kwao ambako wana uraia wa damu, na sasa wanaishi na kufanya kazi huko. Utanzania kwao ulikuwa daraja tu na sasa umekuwa historia tu.

Lakini kama kweli tunaangalia usalama wa taifa, sheria yetu ya sasa Immigration act 1995 tayari ni hatari kubwa sana kwa usalama wa nchi yetu. Na wageni wanaojua udhaifu wake wanaitumia vilivyo kujinufaisha. Tunatekeleza sheria ya uhamiaji ya mkoloni yenye viraka, ambayo ilitungwa kwa ajili ya maslahi na usalama wa mkoloni, bila kuzingatia kabisa maslahi ya mtanzania na hali halisi ya dunia ya leo. Kutokana na udhaifu wa sheria yetu, kuna baadhi ya watu wanafanya kila wanaloweza ikiwa ni pamoja na kuja Tanzania kuishi kwa mwaka mmoja na kufanya ujanja ujanja mwingine na kusema “wanaukana” uraia wa nchi zao, ili wapate uraia wa Tanzania. Baada ya kupata uraia na pasipoti, wanaitumia kwenda kirahisi katika nchi ya tatu ambako kimsingi ndio lengo lao kuu, na huko wanafanya yoyote wanayotaka kwa jina la utanzania. Tanzania yenyewe hainufaiki kwa lolote na watu hao. Kwa sasa kuna baadhi yao wako hapa Tanzania wengine hata wanapata taabu kuongea Kiingereza achilia mbali Kiswahili, lakini wanajiita watanzania na hata kufikia hatua ya kujitapa kuwa wanamiliki asilimia kubwa ya uchumi wa Tanzania. Hii ni hatari ambayo tayari ipo na imeletwa na sheria ya sasa ya uhamiaji, ni bora tuwazuie watu kama hawa kuingia kwenye nchi yetu.

Hata hoja ya kuukana uraia wa nchi wanazotoka kama inavyoelezwa kwenye sheria yetu, kwa mazingira ya siku hizi ni legevu, kwa sababu watu “wanaoukana” uraia wao wa damu na kuchukua uraia wa Tanzania, wanaporudi kwao wanaweza kurudishiwa uraia huo kwa kutupa pasipoti yetu na kujaza fomu moja tu. Mfano mmoja unaoweza kuthibitisha hili, ni Marekani ambayo inafuata utaratibu wa Jus Sol, unaosema Mmarekani wa kuzaliwa hata kama akiwa na uraia wa nchi nyingine ikiwa ni pamoja na ule wa damu unaopatikana kwa nasaba ya damu ya baba (jus Sangunis) au ule wa kuomba (Naturalization) au wa ndoa (jure matrimonii), uraia wake wa kuzaliwa haupotei kwa sababu yoyote ile. Kwa maana hii ni kujidanganya kuwa mmarekani anaweza kuja Tanzania na kusema ameukana uraia wake. Na kwa sheria yetu ya uraia ya mwaka 1995, mtanzania akizaliwa Marekani hata kama baba yake na mama yake ni watanzania wa damu, yeye si mtanzania. Sababu ni kuwa tayari ana uraia wa nchi nyingine ambao hata kama akiukana kwa kuchoma pasipoti ya Marekani au kusaini fomu yoyote ile na kwa viapo baada ya kufikisha umri wa miaka 18, kwa mujibu wa sheria za Marekani yeye bado ni mmarekani tu.

Sidhani kama itakuwa busara tukikwepa kusema ukweli kuwa kuna watanzania wenye asili ya Asia, ambao wana pasipoti ya Tanzania na nchi nyingine moja, mbili au tatu, na baadhi yao kila likifika joto la uchaguzi wanatumia pasipoti zao kwenda nje ya Tanzania na kurudi baada joto hilo kupungua. Kuna watanzania weusi pia wenye pasipoti za nchi za nje ambao hata kama kuna joto kiasi gani, licha ya kuwa na fursa za kwenda nje ya Tanzania, bado wanaendelea kuwepo Tanzania. Kufanya suala la uzalendo limbane mtanzania mweusi tu, nadhani si haki kabisa.

Kwa maoni yangu ni busara sana kumfungulia milango mtanzania yeyote anayekwenda kupambana nje ya Tanzania, kwa kuwa popote pale akienda hata kama akijilipua au asijilipue, afanikiwe au asifanikiwe roho yake bado inabaki Tanzania. Kuna wengi waliojilipua na kila mwezi wanachangia remittances Tanzania. Ni unafiki sana kusema tunaweza kutoa raia kwa wengine, halafu wetu wanaochukua uraia kwingine tunawakana. Na kibaya zaidi hawa tunaowapa uraia na kutudanganya kuwa wameukana uraia wao, wanatumia pasipoti yetu kwenda kuishi Amerika na Ulaya, na ku-remitt pesa kwenye nchi zao. Kwa hiyo uamuzi wa akili ni kuruhusu watanzania kuwa na uraia pacha, lakini tuangalie kwa makini sheria ya uhamiaji ya sasa ambayo tofauti na ilivyoundwa inaruhusu hata watu wasio na msaada kwa Tanzania kutoka Asia kuingia na kuwa raia wa Tanzania.

Kitu ambacho kidogo kimenitia hofu kwenye mapendekezo ya sheria ya uraia pacha, ni kuruhusu wa mwanamke mtanzania akiwa na mtoto na mgeni, mtoto wake anaweza kuwa mtanzania hii ni hatari kwa kuwa unaweza kuwafanya baadhi ya watu kuja Tanzania kwa “mission” ya kuwazalisha wasichana wa watanzania na kupata utanzania ambao baada ya miaka 20 au zaidi wanaweza kuutumia kwa ajenda kubwa ambayo inaweza kuwa na madhara kwa Tanzania. Nadhani tumeanza kuona baadhi ya wafanyabiashara wageni wanavyozalisha dada zetu hapa Tanzania.

FIKRA PEVU - Uraia pacha: Suala lililoonesha mgando wa mawazo katika kufanya maamuzi yanayohusu maslahi ya Tanzania na watanzania