RAIS Jakaya Kikwete amewapongeza vijana wa vyuo vikuu, ambao wamejiunga kwenye kikundi na kufanya shughuli za kilimo kwa kutumia teknolojia mpya ya green house, ambapo baada ya kuvuna wanatarajia kupata shilingi milioni 23.
“Ni kazi gani itakayokupa shilingi milioni 23 kwa mwaka labda uwe na mshahara mkubwa sana,” alisema.
Pamoja na kuwapa pongezi vijana hao, pia aliahidi kukipatia kikundi hicho msaada wa kuchimbiwa kisima kirefu cha maji na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi na kuwa na masoko ya uhakika wa bidhaa zao.
Alisema kuwepo kwa kikundi hicho ni utekelezaji wa sera ya serikali iliyopo madarakani, ambayo
inatoa fursa ya maisha bora kwa kila Mtanzania kwa kuangalia fursa zilizopo.
Alisema hayo juzi wakati akihutubia wananchi wa Tarafa ya Mundemu Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, ambapo pia alizindua Kituo cha Rasilimali za Kilimo na Mifugo. Alisema kitendo cha vijana hao wasomi ni cha kupigiwa mfano.
Aliwataka vijana kutopuuza kilimo, kwani kina uwezo mkubwa wa kuwainua kiuchumi.
“Unaweza kwenda kijijini ukakutana na mtu unamuuliza anafanya kazi gani, anasema hana kazi ila analima tu, bila kujua kuwa kilimo nacho ni kazi ya maana sana,” alisema.
Alisema huu ni wakati wa kila moja, kubadili mtazamo juu ya kilimo, kwani wengi wanatamani kuajiriwa, bila kufahamu kuna fursa kubwa zaidi katika kujiajiri.
Aidha, alisema serikali iliyopo madarakani, imetekeleza kwa kiasi kikubwa kwa vitendo ahadi zake; na miradi mingi ya maendeleo imewafikia wananchi. Rais Kikwete alisema asingependa kuona CCM ikisutwa, kwa kushindwa kuwaletea maendeleo wananchi wake.
“Nisingependa Chama Cha Mapinduzi kisutwe kwa kushindwa kuwaletea maendeleo watu wake, lakini wa kusema na kuzoza wapo tu; na kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kulala,” alisema