Rais Kikwete akagua enelo na utayari wa kupambana na Ebola

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwaangalia wahudumu waliopata mafunzo maalumu ya kumhudumia mgonjwa wa ebola wakati alipokagua wodi maalumu iliyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa ebola iliyoko katika eneo la hospitali ya Temeke jijini Dar es salaam leo Septemba 9, 2014 mara alipowasili kutokea Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Septemba 9, 2014, amekagua huduma na vifaa, pamoja na maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa hatari wa Ebola, ili kujiridhisha na utayari wa Tanzania dhidi ya tishio kubwa la ugonjwa huo.
Mara tu baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar Es Salaam, akitokea Dodoma, Rais Kikwete amekwenda moja kwa moja kukagua vifaa, huduma na maandalizi ya jinsi Tanzania
inavyojiandaa kubaini na kushughulikia wagonjwa wa Ebola, ambao wanaweza kupitia kwenye Uwanja huo.
Rais Kikwete ameonyeshwa Kamera na Mashine za Kuchanganua Picha (Scanners) ambazo tayari zimefungwa kwenye eneo ambalo abiria hulitumia kuingilia katika Uwanja huo.
Rais Kikwete ameelekeza kuboreshwa kwa taratibu na huduma ili kuhakikisha kuwa wasafiri hawapotezi muda mwingi kwa kujipanga foleni ili waweze kukaguliwa.
“Ugonjwa huo usiwe ni kikwazo kwa abiria kupita kwenye Uwanja wetu huu. Tutengeneze mfumo na utaratibu ambao unawezesha wasafiri kupita katika eneo hilo kama ambavyo imekuwa siku zote, lakini wakati huo mashine zetu zikiwa tayari kugundua haraka ni msafiri yupi ana matatizo ama dalili za ugonjwa huo.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Tusitengeneze mfumo ambao unazalisha msongamano ndani ya Uwanja wa Ndege. Napenda kuona kuwa wasafiri wanaendelea kuutumia Uwanja wetu bila msongamano na ucheleweshwaji wowote. Abiria wasipate taabu kwa sababu ya Ebola.”
Mpaka sasa hakuna hata kesi moja ya Ebola imethibitishwa katika Tanzania, lakini maandalizi ya kiwango cha juu yamekuwa yanafanywa, ili kujenga utayari wa kukabiliana na tishio la ugonjwa huo ambao unaendelea kuua maelfu ya watu katika nchi za Afrika Magharibi za Liberia, Sierra Leone, Guinea, Senegal na Nigeria pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Aidha, ugonjwa Ebola haujapata kuingia katika Tanzania katika historia ya ugonjwa huo ambao asili yake ni DRC, ambako mgonjwa wa kwanza alipatikana eneo la Mto Ebola.
Baada ya kumaliza ukaguzi wake kwenye Uwanja wa Ndege, Rais Kikwete ametembea, akaona na akaelezwa kuhusu maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa huo kwenye Kituo Kikuu cha Kuwatenga na Kuwahudumia Wagonjwa wa Ebola (Ebola Isolation Centre) katika Mkoa wa Dar Es salaam kwenye Hospitali ya Wilaya ya Temeke.
“Nimeanzia Uwanja wa Ndege. Nia yangu ni kuona utayari wetu katika kukabiliana na ugonjwa hatari wa Ebola, kuona jinsi gani mifumo yetu inavyofanya kazi, kwa ujumla wake, kukabiliana na janga hili hatari sana,” amesema Rais Kikwete ambaye amefuatana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mheshimiwa Seif Rashid na Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Said Mecky Sadiq.
Baada ya kukagua huduma mbali mbali kwenye Kituo hicho ikiwa ni pamoja na kuona wodi zinazoandaliwa kwa ajili ya wagonjwa na kuelezwa hatua zinachukuliwa, Rais Kikwete ametoa maagizo kadhaa ikiwa ni pamoja na kutengenezwa mazingira bora zaidi na eneo zuri la watumishi wa afya wa Kituo hicho, kuhakikisha kuwa mfumo wa maji unafanya kazi vizuri na kukarabati vyoo na bafu.
Amesisitiza Rais Kikwete: “Nataka kuona kituo chenye viwango vya kuweza kuhudumia watu wa tamaduni zote na watu wa hadhi zote – kuanzia aliyevaa lubega hadi kwa yule mwenye suti ya sehemu tatu. Aidha, wekeni sehemu ya kupika chakula kwa ajili ya wagonjwa.”
Kwenye Kituo hicho ambacho awali kilijengwa kama Kituo cha Kupokea na Kuhudumiwa Wagonjwa wa ugonjwa wa Kipindupindu, Rais Kikwete ameelezwa kuwa kila mgonjwa mmoja wa Ebola ataweza kuhudumiwa na wafanyakazi wanne wa sekta ya afya, ambao nguo na magauni yao yatachomwa moto kila wanapomaliza kumhudumia mgonjwa.
Aidha, ameelezwa kuwa tayari wanataaluma 1,200 wamepewa mafunzo ya kuhudumia mgonjwa wa Ebola katika Mkoa wa Dar Es Salaam, kwamba vifaa vyenye thamani ya Sh. milioni 119 tayari vimenunuliwa na kuwa daktari mmoja ametumwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC) kupata uzoefu wa kukabiliana na ugonjwa huo.
Waziri Rashid amemwambia Rais Kikwete kuwa kitaifa maandalizi yanaendelea na kuwa mpaka sasa Kamera na Mashine za Kuchanganua Picha tayari zimefungwa katika Viwanja vya Ndege vya Dar Es salaam, Zanzibar, Kilimanjaro na Mwanza na kwenye vituo vya mipaka ya Tanzania na nchi za Uganda, Rwanda, Burundi na Zambia.
Aidha, Waziri amesema kuwa maagizo yametolewa kwa hospitali zote nchini kuwa na vyumba maalum vya kuwatenga na kuwahudumia wagonjwa wa Ebola.
Wiki iliyopita, akizungumza na viongozi na wazee wa Mkoa wa Dodoma kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Mipango, Dodoma, Rais Kikwete ambaye alikuwa amemaliza ziara ya mkoa huo, alizungumzia tishio la ugonjwa huo na hatua zinazochukuliwa na Serikali kukabiliana nalo.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.

9 Septemba , 2014.

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na wauguzi waliovalia mavazi maalumu tayari kutoa huduma kwa  abiria  atayekutwa na ugonjwa wa ebola  mara atapowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Septemba 9, 2014 mara alipowasili kutokea Dodoma.

  Baadhi ya wahudumu waliovalia mavazi maalumu wa  wodi maalumu iliyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa ebola iliyoko katika eneo la hospitali ya Temeke  jijini Dar es salaam leo Septemba 9, 2014 mara alipowasili kutokea Dodoma.

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimsikiliza Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Rashid Hemed jinsi Tanzania ilivyojipanga kupambana na ugonjwa hatari wa ebola baada ya kukagua wodi maalumu iliyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa ebola iliyoko katika eneo la hospitali ya Temeke  jijini Dar es salaam leo Septemba 9, 2014 mara alipowasili kutokea Dodoma.

 Baadhi ya wahudumu waliovalia mavazi maalumu wa  wodi maalumu iliyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa ebola iliyoko katika eneo la hospitali ya Temeke  jijini Dar es salaam leo Septemba 9, 2014 mara alipowasili kutokea Dodoma.

  Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwaangalia wahudumu waliopata mafunzo maalumu ya kumhudumia mgonjwa wa ebola wakati alipokagua wodi maalumu iliyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa ebola iliyoko katika eneo la hospitali ya Temeke  jijini Dar es salaam leo Septemba 9, 2014 mara alipowasili kutokea Dodoma.

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipata maelezo ya jinsi vifaa maalumu vinavyofanya kazi ya kutambua wagonjwa wa ebola mara watapowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Septemba 9, 2014 mara alipowasili kutokea Dodoma.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitoa maelekezo ya namna ya kuhudumia abiria wakati wa ukaguzi wa wagonjwa wa ebola mara watapowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Septemba 9, 2014 mara alipowasili kutokea Dodoma.

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipata maelezo ya jinsi madakrai na wauguzi walivyo jiandaa kufanya ukaguzi wa abiria na kutambua wagonjwa wa ebola mara watapowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jueb4: lius Nyerere jijini Dar es salaam leo Septemba 9, 2014 mara alipowasili kutokea Dodoma.

  Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipata maelezo wakati alipokagua wodi maalumu iliyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa ebola iliyoko katika eneo la hospitali ya Temeke  jijini Dar es salaam leo Septemba 9, 2014 mara alipowasili kutokea Dodoma.