Safu mpya ya uongozi CHADEMA Kilimanjaro; "Ndesa Pesa aitumia CCM salamu"

MBUNGE wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, amefanikiwa kutetea nafasi yake Uenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Mkoa wa Kilimanjaro baada ya kupita bila kupingwa huku akijigamba awamu hii atahakikisha wananyakua majimbo yote ya ubunge yaliyobaki Chama Cha Mapinduzi, (CCM).
 
Ndesamburo ambaye amechaguliwa kwenye nafasi hiyo kwa mara ya nne mfululizo, aliyasema hayo juzi mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa viongozi wa ngazi ya Mkoa.
 
Viongozi wengine:
  • Basil Lema alifanikiwa kutetea nafasi yake ya Ukatibu wa Mkoa aliyoishikilia kwa vipindi viwili.
  • Grace Kiwelu amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa BAWACHA
  • Helga Mchomvu amechaguliwa kuwa Katibu BAWACHA.
  • Samwel Msuya alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee.
  • Eliakimu Kimaro amechaguliwa kuwa Katibu wa Baraza la Wazee.
  • John Minja alichaguliwa kuwa Mweka Hazina wa Baraza la Wazee.
  • Wawakilishi Baraza la Wazee Taifa ni William Maro na Ester Masiramba.
Ndesamburo, aliwashukuru wapiga kura kwa kumpa kura zote za ndiyo kwani hakuwa na mpinzani na fomu yake alichukuliwa na wazee wa Wilaya ya Siha wakati akiwa safarini nchini Uingereza na kusisitiza kuwa uongozi ni mzigo, hivyo wale waliyochaguliwa wahakikishe wanaubeba ipasavyo kwa kufanya kazi ya kuimarisha chama.
 
“Ukiona kiongozi anajipeleka mbele kujichagua huyo si kiongozi, anatakiwa aombwe na wananchi wanaoona anafaa kuwaongoza, na ikiwa hivyo kunakuwa hakuna masuala ya rushwa… mimi nilikuwa Ulaya, nimerudi nimekuta fomu, niwashuruku sana wazee wangu kwa kuniamini…
 
“Mliochaguliwa niwaombe mkafanye kazi ipasavyo, kiongozi mzuri anatafutwa na utatafutwa kwa kazi unayoifanya itakapoonekana na wale unaowaongoza, sasa hivi huko nje CCM wanalia wamepata taarifa Ndesa Pesa (Ndesamburo) kaingia tena,” alisema Ndesamburo ambaye pia ni muasisi wa CHADEMA.
 
Uchaguzi huo ulisimamiwa na Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Mchungaji Israel Natse na Katibu, Amani Golugwa.