Serikali yawasilisha pingamizi la kesi ya Bunge la Katiba

Upande wa Jamhuri umewasilisha pingamizi dhidi ya ombi la kusimamishwa kwa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba vinavyoendelea mjini Dodoma, lililofunguliwa na Mwandishi wa Habari, Said Kubenea.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju aliwasilisha pingamizi hilo jana mbele ya jopo la Majaji watatu, Augustine Mwarija, Dk Fauz Twaib na Aloysius Mujulizi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akidai kesi hiyo ina mapungufu ya kisheria.

Kubenea kupitia kwa Wakili Peter Kibatala, alifungua kesi ya Katiba akiomba Mahakama itoe tafsiri ya mamlaka ya Bunge hilo, pia aliomba kusimamishwa kwa bunge hilo hadi kesi hiyo itakapotolewa uamuzi.

Katika pingamizi la Jamhuri, wamewasilisha hoja tatu za kisheria ambazo ni pamoja na ombi hilo lina upungufu wa kisheria, kwa kuwa halijataja kifungu cha sheria, ambacho kinaipa Mahakama mamlaka ya kutoa uamuzi wa ombi lao.

Aidha, wanadai ombi hilo halina msingi kisheria na ni batili, kwa kuwa hati ya kiapo inayounga mkono ombi hilo, ina mapungufu ya kisheria.

Majaji hao walisema pingamizi hilo, litasikilizwa leo, Wakili Kibatala aliomba pingamizi hilo pamoja na ombi la kusimamisha vikao vya Bunge, visikilizwe leo, kutokana na umuhimu na uharaka wa ombi hilo.

Mahakama ilikubali ombi la Wakili Kibatala na kuahirisha shauri hilo hadi leo saa 3 asubuhi litakaposikilizwa pingamizi hilo pamoja na ombi hilo.

Kubenea amefungua kesi hiyo, akiomba Mahakama itoe tafsiri ya mamlaka ya Bunge hilo chini ya vifungu vya 25 (1) na 25 (2) vya Sheria ya Marekebisho ya Katiba Namba 83 ya mwaka 2011.

Aidha, anaiomba Mahakama itoe zuio la muda la kusimamisha bunge hilo ili kusubiri uamuzi wa ombi la tafsiri hiyo. Amewasilisha ombi hilo chini ya hati ya dharura.

Katika kesi hiyo ya msingi, anaiomba Mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya masharti ya vifungu hivyo vya sheria na pia itamke kama bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha malengo ya Rasimu ya Katiba, iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa kiwango gani.

via HabariLeo