Ujerumani yakanusha tuhuma za kujihusisha na Katiba Mpya Tanzania

UBALOZI wa Ujerumani nchini, umekanusha kujihusisha kwa namna yoyote kwa taifa la Ujerumani katika kuingilia au kuweka ushawishi katika mjadala unaoendelea wa katiba nchini.

Kauli hiyo ambayo imo katika taarifa ya ubalozi huo iliyosainiwa na mtaalamu wake wa mawasiliano John Merikion.

Taarifa hiyo imesema kwamba Serikali ya Ujerumani kimaadili haiingilii mambo ya siasa za ndani na za nje za nchi zingine.

Taarifa hiyo ilisema kutokana na uhalisia huo, Serikali ya Ujerumani na maafisa wake hawafanyi ushawishi wowote kuhusu mwelekeo wa mjadala wa katiba unaoendelea hivi sasa nchini Tanzania.

Aidha taarifa hiyo ilisema kwamba mashirika mengi ya Kijerumani yanafanya kazi na mawakala wa asasi za kiraia duniani kote kuimarisha shughuli za mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.

Alisema katika taarifa yake kwamba aina hiyo ya ushirikiano hufanyika pia nchini Tanzania kwa kufanya shughuli zilizolenga katika mipango ya elimu na mafunzo kuhusiana na demokrasia ya vyama vingi.

Taarifa hiyo ilisisitiza kwamba utaratibu huo hufanywa kwa wawakilishi wa vyama vyote vikubwa vya siasa nchini Tanzania.

Aidha taarifa hiyo imesema kwamba shughuli za kisiasa huwa hazisaidiwi au kufadhiliwa na mashirika haya, ambayo hutenda kazi zake kwa kutumia pesa zinazotolewa na Serikali ya Ujerumani.

Ubalozi huo umesema kwamba umelazimika kutoa msimamo huo kutokana na habari za mara kwa mara katika vyombo vya habari nchini Tanzania kwamba Ujerumani inaingilia mjadala unaoendelea wa katiba.

Tanzania kwa sasa ipo katika mchakato wa katiba mpya, ambapo kwa sasa rasimu inajadiliwa na Bunge Maalumu la Katiba linalokutana mjini Dodoma.

via Lukwangule blog