Mtanzania aliyefanya mauaji ya wanawe Australia

Mtanzania anayeishi nchini Australia ahukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kuwaua watoto wake na kisha kuwataarifu Polisi.

Makachero wakamata Waasia watuhumiwa wa ukahaba Dar

Idara ya uhamiaji imewakamata wahamiaji haramu kutoka nchi ya Nepal ambao walikuwa wakiishi Mwananyamala DSM wakifanya kazi za ukahaba.

Mazungumzo ya Rais na Wazee wa Dar es Salaam

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais kuzungumza na Wazee wa Dar es Salaam Jumatatu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete atazungumza na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, mchana wa Jumatatu, Desemba 22, 2014.

Wakati wa mazungumzo yake na Wazee hao, Rais Kikwete atazungumzia masuala mbali mbali ya kitaifa, yakiwemo yale ambayo yamekuwa yanasubiri maamuzi yake tokea alipokuwa anajiuguza kufuatia upasuaji aliofanyiwa mwezi uliopita, Novemba 2014.

Undani zaidi kuhusu mkutano huo kama vile mahali utakapofanyika, saa utakapofanyika na nani wataalikwa utatolewa na mamlaka zinazohusika na maandalizi ya mkutano huo.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.

19 Desemba, 2014

Kiwanda cha sukari Kagera chaanza kuzalisha ziada

Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ikikagua mitambo ya kuzalishia sukari katika Kiwanda cha Sukari cha Kagera.

Kiwanja cha Sukari cha Kagera kimeanza kuzalisha ziada ya sukari inayohitajika katika soko la sukari nchini hali inayopelekea kuweza kupunguza tatizo la upatikanaji wa sukari Tanzania na nchi za jirani zinazotumia sukari kutoka kiwandani hapo.

Hayo yamewekwa wazi na Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho, Bw. Ashwin Rana, wakati alipokuwa akizungumza na Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango.

“Kwa sasa tumeweza kuongeza mauzo katika kanda kufikia tani 40,000, pamoja na kuongeza ununuzi kutoka kwa wakulima wa miwa wa nje zaidi ya tani 100,000 kwa mwaka,” alisema.

Bw. Rana aliongeza kuwa Kiwanda chake kimewekeza zaidi katika upanuzi wa eneo la shamba la miwa la umwagiliaji la hekta 3600 pamoja na kuwekeza zaidi katika teknolojia ya kisasa katika kilimo.

“Kampuni yetu imewekeza kwa kiasi kikubwa katika teknolojia na vifaa vya kisasa ikiwemo matrekta yanayotumia setalaiti katika ufanyaji kazi wake katika kuandaa mashamba,” aliongeza.

Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri amekipongeza Kiwanda hicho kwa kuwekeza kwenye uzalishaji wa kisasa wa miwa hali inayoongeza uzalishaji wa sukari kuwa mkubwa kiwandani hapo.

Bibi Mwanri ameongeza kuwa Kiwanda hicho kinastahili pongezi za kipekee kwa kuweza kuongeza ajira zaidi ya watu 6000 waliopo kiwandani.

“Kwa kweli munastahili sifa kwa kutoa ajira kwa vijana wa Kitanzania pamoja na kuuza umeme kwenye gridi ya Taifa,” alisema.

Kwa mujibu wa Meneja wa Kiwanda hicho, kwa sasa kinakabiliwa na na changamoto za uuzaji haramu wa sukari zinazoingia kimagendo nchini ambao umechangiwa kushindwa kwa kiwanda kuuza sukari ili kurudisha gharama za uzalishaji kutokana bei za sukari zinazoagiwa kutoka nje kuwa bei ya chini sana.

“Bei ya Sukari Duniani imeshuka sana kutokana na Nchi kubwa duniani kusaidia wakulima katika uzalishaji na pembejeo (subsidies) na hivyo sukari kuuzwa katika soko la dunia kwa bei ya chini (Dumping) na kufanya kuwa bei kuwa ndogo kuliko gharama halisi ya uzalishaji,” aliongeza.

Aliongeza kuwa changamoto nyingine ni pamoja na kiwanda kushindwa kulipa mikopo iliyochokuwa benki kutokana na kuwepo sokoni kwa sukari ambayo ni ya magendo na bei ya chini hivyo kiwanda kushindwa kufikia malengo hata ya kiundeshaji na mipango mikakati.

Kiwanda cha Sukari cha Kagera kiko katika sehemu Kaskazini Magharibi ya Tanzania (karibu na mpaka wa Tanzania na Uganda) kilibinafsishwa na Serikali kwa sekta binafsi mwaka 2001.

Malengo ya ubinafsishaji yalikuwa kuboresha upanuzi wa masoko ya ndani na kikanda, uwekezaji wa kisasa, upanuzi na ukarabati na majengo ili kuhakikisha shughuli za kiundeshaji zinaboreshwa.


Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Mwenye kofia ya bluu) akionja sukari inayozalishwa na Kiwanda cha Sukari cha Kagera. Kushoto ni Mratibu wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bw. Senya Tuni.


Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera. Nyuma ni shehena ya sukari iliyo tayari kuingia sokoni.


Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakioneshwa mashine ya kumwagilia maji miwa ijulikanayo kwa kitaalamu kama Centre Pivot System.


Meneja wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera, Bw. Ashwin Rana (Kulia) akiwaonesha Wakaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango mashine mpya zinazotumika kuvutia maji kwa ajili ya kumwagilia miwa.


Msimamizi Mkuu wa Mtambo wa maji wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera, Mhandisi Abdul Adinani (Kulia) akitoa maelekezo ya namna ya maji yanavyochujwa kabla ya kutumika kwa ajili ya umwagiliaji wa miwa. Wanaomsikiliza ni Wakaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango.


Mtaalamu wa uchongaji na usawazishaji wa ardhi kwa ajili ya mashamba ya miwa, Mhandisi Ali Khamis (Kulia) akitoa maelezo ya namna matrekta yanayotumia setalaiti (hayapo pichani) yanavyofanya kazi. Wanaomskiliza ni Prof. Longinus Rutasitara (kushoto) ambaye ni Naibu Katibu Mtendaji anayeshughilikia masuala ya Uchumi Jumla na Katikati ni Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri.


Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakioneshwa kwa vitendo matrekta yanayotumia setalaiti kusawazisha shamba kwa ajili ya uzalishaji miwa. 


Meneja wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera, Bw. Ashwin Rana akiwakaribisha wageni kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango walipotembelea kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo nchini. Anayesalimiana naye ni Prof. Longinus Rutasitara (Naibu Katibu Mtendaji Uchumi Jumla). Katikati ni Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri.

  • Picha, taarifa kutoka kwa Saidi Mkabakuli, Kagera

Utajiri kwako ni lazima ikiwa utafanya 7 yafuatayo


wavuti.com inamshukuru sana Imani kwa kutushirikisha makala hii elimishi.

KAMA UNAFANYA MAMBO HAYA, UTAJIRI KWAKO NI LAZIMA.

Kuwa na mafanikio makubwa na hatimaye kuwa tajiri ni kitu ambacho kinaonekana kuwa kigumu kwa wengi ama hakiwezekani kabisa. Hii yote inatokana na wengi kutokujua njia au mambo muhimu ya kufanya hadi kufikia mafanikio makubwa. Kutokana na hili wengi wamekuwa wakijiuliza wafanye nini au kitu gani kitakachowafanikisha katika maisha yao.

Kiuhalisia, katika maisha kuna vitu ambavyo ukifanya iwe kwa kukusudia au bahati ni lazima uwe tajiri na pia kuna vitu ambavyo ukifanya, sahau mafanikio katika maisha yako. Vitu hivi vinaweza kuwa tabia zetu au mienendo tuliyonayo ambayo inakuwa inaathari kubwa kwetu na hii ndiyo naweza sema ni siri kubwa iliyofichika kati ya watu wenye mafanikio na ambao hawana.

Watu wenye mafanikio wamemudu kwa kiasi kikubwa kufanya mambo yanayowafanya wawe matajiri, huku maskini wakiwa hawajui hilo na kuendelea kufanya vitu vinavyowafanya kuwa maskini. Kwa wewe kulijua hilo tu, tayari una nafasi kubwa ya kufanikiwa na kufanya mambo makubwa katika maisha yako.


Kama kweli umechoshwa na umaskini, na umedhamiria kweli kuwa tajiri hakikisha unafanya mambo haya:-


1. Hakikisha unajiwekea mipango na malengo makubwa.

Kama kweli unataka kufanikiwa na kuwa tajiri ni lazima ufanye hili. Huwezi kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kama una tabia ya kujiwekea malengo kidogo. Watu wote wenye mafanikio huwa ni watu wa kujiwekea malengo makubwa na ambayo huanza kuyafatilia kila siku na kuhakikisha mpaka yanatimia.

Acha kujidharau au kujiona hufai eti kwa sababu huna pesa na ukashindwa kujiwekea mlengo yako. Panga mipango yako vizuri, kama ni pesa zitakuja zenyewe wakati unaendelea kutekeleza mambo mengine. Ukiwa na malengo makubwa hii itakusaidia kufanya kazi kwa bidii kubwa na hautaweza kukata tamaa mapema. Chukua tabia hii muhimu ikusaidie kukufanikisha.

2. Hakikisha unatumia muda wako vizuri.

Muda ni kitu muhimu sana katika maisha yetu. Kama wewe ni mtunzaji mzuri wa muda na haupotezi muda hovyo, elewa kabisa kufanikiwa kwako ni lazima. Watu wengi kutokana na kutokujua ama mazoea ambayo wanayo toka mwanzo, ni watu wa kupoteza muda sana. Kama tabia hii ndiyo unayo, kufanikiwa na kupiga hatua mbele itakuwa ngumu katika maisha yako. Jifunze kutunza muda utaona mafanikio makubwa sana ambayo hukufikiri hapo mwanzo.

3. Hakikisha unajifunza vitu vipya kila siku.

Tatizo kubwa walilonalo watu wengi ni kutopenda kujifunza vitu vipya.. Wengi ni wavivu wa kusoma hali ambayo hupelekea kukosa vitu vizuri vyenye uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha yao. Kama unataka mafanikio makubwa katika maisha yako, ni lazima uwe msomaji mzuri pia. Hii itakusaidia wewe kupambana na changamoto kwa kujua wengine waliweza kukabiliana nazo vipi. Ni lazima ujenge utaratibu wa kujisomea vitu vitakavyobadili maisha yako.

4. Usiwe mtu wa kulaumu tu.

Wapo watu ambao siku zote ni watu wa kulalamika tu na kulaumu wengine ndio waliopelekea wao kuwa hivyo. Hawa ni watu ambao mara nyingi hufikiri kuwa wao wamekuwa maskini pengine kutokana na wazazi hawa kuwasaidia au hawakusoma na visingizio vingi tu. Hii ni tabia ambayo haiwezi kukufikisha popote, zaidi ya kukurudisha nyuma. Kama nia yako kubwa ni mafanikio achana na visingizio, chukua hatua za kusonga mbele. Vipo vitu vingi vya kufanya na ukaondokana na kulaumu kwako. (Unaweza ukasoma pia Huu Ndio utajiri mkubwa utakaoupata kama utaamua kufanya biashara hii)

5. Hakikisha unaye ‘mentor’ wa kukuongoza kwenye mafanikio yako.

Asilimia kubwa ya matajiri wote walioko duniani wanao watu waliowaongoza katika maisha yao hadi kufanikiwa. Ni muhimu hata kwako wewe kuwa na ‘mentor’ au mtu ambaye atakuongoza kwenye mafanikio yako. Mara nyingi huwa hatujui kila kitu katika maisha yetu. Kama katika kitu ulichochagua kufanya yupo mtu ambaye tayari amefanikiwa katika hilo eneo ni vizuri ukamtumia ili akakuongoza ili usije ukapotea kiurahisi na kufanya makosa ambayo pengine hukustahili kuyafanya.

6. Hakikisha unaepuka madeni yasiyo ya lazima.

Kama umekopa mkopo benki, hakikisha huo mkopo unakusaidia kuongeza kipato chako. Acha kukopa mkopo halafu unaamua kujengea nyumba au kununua gari, na matokeo yake pesa zote unazipoteza unaanza kuhangaika namna ya kulilipa deni hilo. Kati ya vitu ambavyo vimewafanya wengi kujuta na kujilaumu katika maisha yao ni mikopo. Kama umeamua kukopa, uwe mwangalifu ili usije ukaumia baadae wakati unarudisha hilo deni. Kikubwa jifunze kutumia mkopo vizuri.

7. Hakikisha unaweka akiba ya kutosha.

Kila pesa unayopata hakikisha unajiwekea akiba yako. Wataalamu wengi wa masuala ya mafanikio wanashauri angalau asilimia kumi ya kile unachokipata iweke kama akiba yako. Pesa hii inapokuwa nyingi itakusaidia wewe kuwekeza katika miradi yako mbalimbali. Hakikisha pesa hii unaiwekeza na usiitumie katika matumizi mengine yasiyo ya lazima. Kama ukifanya hivi kwa pesa hii utakuwa upo kwenye nafasi ya kupata mafanikio makubwa katika maisha yako.

Kwa kufanya mambo hayo unao uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha yako kwa jinsi unavyotaka na kuwa tajiri. Kumbuka hukuzaliwa maskini au mlalahoi kama unavyodhani, kikubwa jifunze kuwa na fikra sahihi zitakazo badili maisha yako na kisha chukua hatua sahihi kuelekea malengo yako uliyojiwekea. Hakuna kinachoshindikana kila kitu kinawezekana endapo tu ukiamua.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio na endelea kutembelea mtandao wa DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na kuhamasika zaidi.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035

[email protected]
DiraYaMafanikio.blogspot.com

Taarifa ya Wizara kuhusu Vyama vya Kijamii vilivyosajiliwa

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

TANGAZO KWA WADAU

VYAMA VYA KIJAMII VILIVYOSAJILIWA NA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI


WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI INAPENDA KUVIFAHAMISHA VYAMA VYA KIJAMII VILIVYOSAJILIWA NA WIZARA KUWA KUANZIA TAREHE 01 JANUARI, 2015 MALIPO YOTE IKIWA NI PAMOJA NA ADA ZA UANACHAMA YATALIPIWA KUPITIA KATIKA MATAWI YA BENKI YA NMB A/C NAMBA 20110013811 YENYE JINA “MOHA REVENUE COLLECTION”.

MALIPO YATAKAYOFANYIKA NJE YA UTARATIBU HUU MPYA HAYATATAMBULIWA.

KWA MAELEZO ZAIDI TEMBELEA TOVUTI YA WIZARA www.moha.go.tz AU PIGA SIMU NAMBA 022 2112034-40.

ATAKAYESOMA AU KUSIKIA TANGAZO HILI AMTAARIFU NA MWENZAKE.

IMETOLEWA NA

KATIBU MKUU

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI[video] Kitimtim kilichotokea ndani ya Bunge la KenyaHali ya wasiwasi ilitokea katika Bunge la Kenya Alhamisi Desemba 18 wakati wabunge walipokuwa wakijiandaa kujadili muswada wa sheria kuhusu usalama, ambapo baadhi ya wabunge walionekana wakipigana makonde na kuzuia shughuli za Bunge kuendelea.

Wabunge kutoka muungano wa vyama vya upinzani CORD walifanikisha azma yao ya kuzua ghasia na kuvuruga shughuli Bungeni baada ya kubainika kuwa Bunge lingejadili kupitisha au kufutilia mbali muswada kuhusu usalama.

Wabunge kutoka muungano wa vyama vya upinzani wameikosoa hatua ya serikali ya kuwaweka maofisa wa usalama nje ya majengo ya Bunge, huku wakidai kuwa ilikuwa njama za kuwatishia usalama wao.

Mengi awageukia Masele, Maswi, Wasira

MWENYEKITI Mtendaji wa Kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi, amewashukia Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele kwa madai ya kusambaza taarifa za uongo dhidi yake.

Mengi alisema hayo katika taarifa yake aliyotoa kwenye vyombo mbalimbali vya habari, zilizoeleza kwamba amezushiwa kuwa alimpatia Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, mabilioni ya shilingi kwa lengo la kuwahonga wabunge ili wapinge vikali wizi uliofanyika kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.

Katika taarifa hiyo aliwataja Masele na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi, kwamba wanahusika kutoa taarifa kwamba alitoa fedha hizo ambazo hakutaja kiwango kamili kwa wabunge.

“Ole Sendeka ni rafiki yangu, kwa hiyo nilimwuliza kuhusu taarifa hiyo. Alinijibu kwamba siku moja akiwa amekaa meza moja na Masele kule Dodoma alipigiwa simu na kijana wake ikabidi aombe radhi na kusogea pembeni ili aweze kusikiliza simu hiyo.
“Masele ni mtu wa ajabu kwani alimtuma mhudumu eti aje kusikiliza mazungumzo yake ya simu,” 
ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Mengi.