Mbinu anazotumia mwajiri ili uendelee kumtumikia

Ajira ni kitu kizuri sana, maana kupitia ajira ndio tunapata watu wa kutufanyia kazi mbalimbali na pia kutupatia huduma mbalimbali. Na kuna kipindi ajira ilikuwa kitu muhimu sana kiasi kwamba aliyekuwa na ajira alionekana kuyashinda maisha. Lakini nyakati hizo zimepita sasa na tumeingia kwenye kipindi ambacho ajira zimekuwa na changamoto kubwa sana.

Kwanza nafasi za ajira zimekuwa chache kuliko idadi ya wanaozihitaji hivyo kufanya idadi ya wasiokuwa na ajira kuwa kubwa.

Na pili, hata waliopo kwenye ajira hawaridhishwi na ajira zao kwa maana kwamba wanajikuta wanafanya kazi miaka mingi lakini hawaoni mabadiliko makubwa kwenye maisha yao.

Pamoja na changamoto hizi za ajira, kuna fursa nyingi ambazo zipo nje ya ajira, ila waliopo kwenye ajira na hata wanaotafuta ajira bado hawahangaiki kuzitumia vizuri. Bado mtu atang’ang’ania kufanya kazi aliyoanza kuifanya miaka 10 iliyopita japo hakuna chochote anachoweza kukionesha kwa miaka hiyo kumi zaidi ya madeni na msongo wa kila siku hasa linapokuja swala la fedha.

Jambo hili limenifanya kufanya utafiti wa ndani zaidi ili kujua kwa nini waliopo kwenye ajira hata kama haiwaridhishi hawapo tayari kutafutra fursa nyingine? Na pia kwa nini vijana wanaomaliza masomo yao, wapo tayari kukaa nyumbani mwaka mzima, kuzunguka na bahasha ya kuomba kazi badala ya kufikiria kutumia fursa nyingine?

Katika kulitafiti hilo nimegundua mbinu mbili ambazo waajiri wote wanazitumia kuhakikisha waajiriwa wanaendelea kuwa watumwa wao. Naposema watumwa, iko wazi kwamba kama mtu anafanya kazi ambayo haimridhishi na wala haifurahii hakuna neno rahisi la kutumia zaidi ya utumwa.

Mbinu hizi mbili zimetumiwa vizuri sana na waajiri na zimeingia kwenye akili ya waajiriwa kiasi kwamba ni vigumu sana kunasua kwenye mtego walioingia.

Mara nyingi unakutana na mtu anayeanza ajira na anakuambia atafanya kwa miaka kadhaa na baadae ataacha afanye mambo mengine makubwa, ila kadiri miaka inavyozidi kwenda ndivyo anavyozidi kuwa na hofu ya kuacha ajira ile. Hii yote inatokana na mbinu hizi zilizotengenezwa na waajiri.

Mbinu ya kwanza; Kuwashawishi kwamba kupitia ajira ndio wataweza kumudu maisha yao.

Kupitia mbinu hii waajiri wanawafanya waajiriwa kuamini kwamba kupitia ajira ndio wanaweza kuyamudu maisha yao. Wanafanya hivi kwa kumhakikishia mfanyakazi mshahara wake wa mwezi, iwe kampuni au taasisi imefanya kazi kwa faida au la. Mfanyakazi hata kama ana mshahara mdogo kiasi gani ana uhakika wa kuupata kila inapofika mwisho wa mwezi.

Pia kupitia mbinu hii waajiri wanawahakikishia wafanyakazi wao maisha mazuri hata baada ya kustaafu. Wanawachangia katika mfuko wao wa mafao ya uzeeni na pia mfuko huu unawafanya waajiriwa kuona kuna kitu kizuri na kikubwa mbeleni, hivyo kuendelea kuwa wafanyakazi watiifu.

Mbinu ya pili; Kumwogopesha mwajiriwa kwamba hakuna maisha nje ya ajira.

Kupitia mbinu hii waajiri wameweka sheria mbalimbali ambazo zinamfanya mwajiriwa aendelee kuwa mtumwa kwa mwajiri wake. Kwa mfano mwajiriwa ameshakaa kwenye ajira kwa miaka kumi na ameshachangia kiasi kikubwa kwenye mafao yake, ataambiwa akiacha kazi au kufukuzwa kazi mafao yake, ama anayapoteza au atayadai akishafikisha umri halali wa kustaafu. Hiki ni kifungo kikubwa sana kinachomhakikishia mwajiri kwamba anaendelea kuwa na watu wanaomtumikia hata kama hawataki kufanya hivyo.

Mbinu hizi mbili zimeshaingia kwa wafanyakazi ambao ni wakongwe kazini na ndio maana wengi wanaweza kupanga kuacha kazi na kufanya mambo mengine lakini wanashindwa. Swali la kushangaza ni je mbinu hizi mbili zimepandikizwaje kwa vijana ambao bado hawajaingia kwenye ajira kabisa?

Kwa vijana ambao bado hawajaingia kwenye ajira kabisa nao wameshanasa mtego huu. Wameshaoneshwa kwenye ndoto kwamba kupata ajira kwanza ndio kujiwekea usalama wa maisha na hata kama ni kuangalia fursa nyingine basi ni baada ya kuwa kwenye ajira kwanza. Hivyo wanakazana kuingia, wakifikiri wataweza kutoka watapotaka, ila wakishanasa mtego wanaishia kuwa watumwa kwa kipindi kirefu kwenye maisha yako.

Unahitaji maarifa na nguvu ya ziada ili kunasua kwenye mtego huu. Unahitaji kuangalia uhalisia ili uweze kujua kwamba lolote linawezekana iwe ni kwenye ajira au nje ya ajira. Na unahitaji uweze kufanya maamuzi yako mwenyewe, kuyasimamia na kutokusikiliza wanaokukatisha tamaa ndio utaweza kuondoka kwenye mtego huu.

Vinginevyo utakuwa unaweka mipango kila siku ya kujikomboa lakini ikifika kuchukua maamuzi, unajikuta upo kwenye mtego aliokuwekea mwajiri wako.

Mwaka 2014 umeisha, je umefanya nini? Umefikia malengo uliyopanga? Na je umejipangaje kwa mwaka 2015? Karibu kwenye semina ya siku 21 za mafanikio makubwa mwaka 2015 itakayoendeshwa kwa njia ya mtandao. Semina hii itakuwezeshakuweka malengo ambayo utaweza kuyafikia, kubadili fikra mbaya ulizopandikizwa zinazokufanya uendelee kuwa mtumwa na pia kukupa mbinu za kuboresha kazi au biashara unayofanya. Kushiriki semina hii andika email kwenda [email protected]

Nakutakia kila la kheri katika kujiandaa na mwaka 2015, naamini utakuwa mwaka bora sana kwako.
TUPO PAMOJA.
Makirita Amani
[email protected]

Hakimu ajitoa kwenye kesi ya ugaidi dhidi ya Sheikh Farid

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Hellen Riwa amejitoa kusikiliza kesi ya ugaidi inayomkabili kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), Shekhe Farid Hadi Ahmed na wenzake.

Hakimu Hellen alitangaza kujitoa kusikiliza kesi hiyo jana kutokana na uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ulioamuru Mahakama ya Kisutu kusikiliza na kutolea uamuzi ombi, lililowasilishwa na Shekhe Farid na wenzake.

Akitangaza kujitoa jana Hakimu Hellen alisema:

“Mahakama Kuu ndiyo ina uwezo wa kusikiliza kesi hii…kwa kuwa Mheshimiwa Jaji ni mkubwa, mimi binafsi siwezi, najitoa”.

Katika ombi lao, washitakiwa waliomba Mahakama ya Kisutu ifute mashitaka ya ugaidi dhidi yao, pia walihoji uhalali wa kushitakiwa Tanzania Bara wakati Zanzibar ni nchi ambayo ina Mahakama Kuu na kuomba wakashitakiwe katika sehemu walizokamatwa.

Hakimu Hellen alisema kwa mujibu wa sheria, ushahidi hautoki hewani, unatoka kwenye hati ya mashitaka na kwa maoni yake maelezo ya kesi yalikuwa sahihi, lakini alikuwa anashangaa kwanini washitakiwa waliletwa Tanzania Bara.

Hata hivyo, alisema baada ya kusoma Sheria ya Ugaidi aligundua wanaweza kushitakiwa sehemu yoyote na hati ya mashitaka imeeleza wazi kuwa wanadaiwa kufanya matukio katika maeneo ya Tanzania Bara.

Awali kabla Hakimu hajajitoa, upande wa Jamhuri ulidai hawakuridhika na uamuzi wa Mahakama Kuu na wameshawasilisha kusudio la kukata rufaa ili Mahakama ya Rufaa itoe ufafanuzi wa uamuzi huo lakini kwa sasa wapo tayari kutekeleza kilichoamuliwa.

Upande wa utetezi ulidai Mahakama imeelekezwa kutoa uamuzi wa hoja zilizotolewa Oktoba 19 mwaka huu na wakaomba hakimu ajitoe ili Hakimu mwingine asikilize hoja hizo kwa kuwa hakimu Hellen alishatoa uamuzi.

Hata hivyo, Wakili Kongola alidai hakuna sababu za msingi za hakimu kujitoa na kama ikiwa ni hivyo, watamaliza mahakimu wote wa mahakama hiyo.

 • HabariLeo

Zanzibar: Wawili mbaroni wakituhumiwa kuwavamia Madaktari toka Cuba

Balozi Seif akibadilishana mawazo na Madaktari wa Cuba hapo nyumbani kwao Vuga alipokwenda kuwafariji na kuwapa pole baada ya kuvamiwa na Majambazi.

Kamanda wa Polisi Mkoa Mjini Magharibi Msaidizi Kamishna wa Polisi {ACP} Mkadam Khamis Mkadam alisema Jeshi la Polisi Mkoa huo linawashikilia watu wawili miongoni mwa majambazi wanaotuhumiwa kuhusika na uvamizi wa Madaktari Bingwa wa Cuba katika maeneo kati ya Kikwajuni Wireles na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar {SUZA} mapema juzi usiku.

Alisema polisi ilianza uchunguzi mara moja baada ya kupata taarifa ya kuvamiwa kwa Madaktari hao walionyang’anywa mikoba,vitu pamoja na Fedha zao ambapo mmoja kati yao Profesa Ulpiano alijeruhiwa kwa panga kichwani.

Kamishna Msaidizi wa Polisi {ACP} Mkadam Khamis Mkadam alieleza hayo wakati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika nyumbani kwa Madaktari hao Vuga Mjini Zanzibar kuwafaribi baada ya kupatwa na mkasa huo.

Kamanda Mkadam alisema Mkoa wa Mjini umekuwa na matukio ya kuibuka kwa vitendo vinavyoashiria kuichezea amani baadhi ya wakati jambo ambalo jamii inahusika kwa kiasi kikubwa katika kushirikiana na Jeshi la Polisi kukabiliana na vitendo hivyo.

Alisema ulinzi ni jukumu la watu wote, hivyo miundo mbinu iliyopo hivi sasa Duniani ya mitandao ya mawasiliani katika uwekaji wa Kamera za CCTV inahitajika kutumika kwa lengo la kuwabaini watu wanaojihusisha na matendo maovu.

Kamanda huo wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi alizishauri Taasisi za Umma, Binafsi na hata watu wa kawaida wakakijengea utamaduni wa kutumia mfumo huo mpya ili kuwa na maisha ya salama.

Akiwapa pole Madaktari hao Bingwa wa Cuba wanaotoa huduma katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja pamoja na kusomesha Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar {SUZA} Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hilo ni tukio la ajabu na la kusikitisha katika visiwa vya Zanzibar.

Balozi Seif alisema vitendo hivyo viovu vinavyofanywa na baadhi ya wahuni vimekuwa vikileta sura mbaya kutokana na sifa ya Zanzibar yenye Utamaduni wa kistaarabu wa kupenda wageni tokea karne nyingi zilizopita.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Madaktari Bingwa hao wa Cuba kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia vyombo vyake vya ulinzi inaendelea na uchunguzi wa kina na wahusika wa vitendo hivyo watapopatikana mkondo wa sheria utafanya kazi zake dhidi ya wahalifu hao.

Balozi Seif aliwataka Madaktari hao kuendelea na majukumu yao kama kawaida na Serikali itakuwa makini katika kuwahakikishia usalama wao pamoja na wageni wengine wakati wao wote wawapo hapa Nchini.

Wakitoa shukrani zao kwa faraja hiyo pamoja na juhudi zilizochukuliwa na vyombo vya ulinzi katika kuwasaka wahalifu waliohusika na tukio hilo Madaktari hao wa Cuba waliahidi kuendelea kutoa huduma kama kawaida licha ya mkasa uliowakumba.

Madaktari hao walielezea matumaini yao kwamba Serikali pamoja na vyombo vyake vya ulinzi vitafanya juhudi za ziada katika kuona kwamba matukio kama hayo yanadhibitiwa kabisa.

Madaktari hao wanne wa Cuba ni Dk. Barbara, Dk. Daisy Batle, Dk. Katia wakiwa na Kiongozi wao Profesa Ulpiano walivamiwa ghafla na vijana walioshuka na mapanga kwenye Gari aina ya Noah wakati wakitokea Kikwajuni kuelekea nyumbani kwao Vuga.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimpa pole Kiongozi wa Madaktari wa Cuba Profesa Ulpiano Nyumbani kwake Vuga Mjini Zanzibar baada ya kuvamiwa na majambazi jana usiku yeye na wenzake maeneo kati ya Kikwajuni na SUZA.

 Madaktari wa Cuba waliovamiwa na majambazi kutoka kushoto ni Mke wa Madaktari hao Dk. Ulpiano, Dk. Katia na Dk. Barbara.

 • Picha: Hassan Issa, OMPR – ZNZ
 • Taarifa ya maandishi: Othman Khamis Ame, OMPR – ZNZ

Hadithi ya visiwa viwili: Zanzibar na Cuba

HASHIL Seif ni mwenzangu. Ni rafiki yangu na ijapokuwa si wa damu moja, au pengine kwa sababu hiyo, amekuwa zaidi ya ndugu yangu. Yeye ni mtu wa mambo mengi. Ni mtu wa visa na mikasa. Hayo yako wazi katika mashairi na riwaya zake alizochapisha. Mengine yatadhihirika zaidi kitapotoka kitabu chake kipya cha kumbukumbu za maisha yake ya kisiasa.

Hashil Seif ana dosari moja. Kuna nyakati anaweza kuwa machachari na mapepe. Hata hivyo husameheka kwa wepesi kwa vile daima hufanya mambo kwa moyo safi. Pia ni rahisi kuyasahau machachari yake kwa sababu aghalabu huwa ni zao la akili yake inayofanya kazi kama cherehani isiyosita kufuma.

Juu ya mizaha yake mingi akili yake saa zote huwa macho kuangalia wapi duniani haki za binadamu zinakiukwa. Ndio maana kwa muda wa miaka mingi alikuwa akifanya kazi katika Kituo cha Haki za Binadamu nchini Denmark anakoishi.

Tangu utotoni mwake Hashil amekuwa amejawa na raghba ya kupigania haki na shauku hiyo ndiyo iliyompelekea kuzivaa siasa. Alianza na siasa za kiwananchi, za kizalendo, za kupigania uhuru na kumtoa mkoloni. Halafu siasa zake zikapevuka. Zikawa siasa za kitabaka za kuwapigania wanyonge.

Haikuchukuwa muda akiwa kijana kabisa Hashil akawa miongoni mwa wa wafuasi wakubwa wa Abdulrahman Babu tangu Babu alipokuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) hadi alipotoka na kuunda chama cha Umma Party.

Siasa za Hashil zilikuwa za safari ndefu iliyomtoa kwao na kumfikisha Havana, Cuba, 1962. Alikwenda huko kufunzwa mbinu za kupindua serikali. Wakati huo Babu alikuwa amefungwa gerezani na Waingereza. Kuna wasemao kwamba Waingereza walimfunga kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa ZNP.

Hashil aliifunga safari ya kwenda Havana kwa siri kubwa. Alikuwa katika kundi la mwanzo la vijana wa Kizanzibari waliokwenda Cuba wakiongozwa na Hamed Hilal. Wenzao katika kundi hilo walikuwa Said Seif Rahatileil, Ali Yusuf Baalawy, Salim Saleh na Ali Mshangama.

Makundi mingine yalifuata baadaye. Msaada huo ulipatikana kwa jitihada kubwa za Ali Sultan Issa aliyetumwa na viongozi wa chama cha wafanya kazi cha Federation of Progressive Trade Unions (FPTU), Ahmed Badawi Qullatein na Khamis Abdallah Ameir, ende Cuba kutafuta msaada wa kuwapeleka vijana wa Kizanzibari kujifunza mbinu za kupindua serikali kwa kutumia silaha.

Hadithi hii ni ndefu lakini kwa ufupi Ali Sultan alifanikiwa kuwasili Cuba na kupokewa na Raul Castro, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na ambaye sasa ni Rais wa Cuba baada ya kumrithi kaka yake Fidel Castro. Isije ikafikiriwa kuwa urithi huu ni upendeleo wa kindugu. La, Raul alikuwa miongoni mwa viongozi wa mapinduzi ya Cuba chini ya Fidel walioupindua udikteta wa Fulgencio Batista.

Raul alivutiwa na msimamo wa Ali Sultan. Wote walikuwa waumini wa itikadi moja. Kila wakati walikipembua walichokuwa wakikijadili kwa uchambuzi wa kisayansi.

Hashil na wenzake walishukia hoteli ya Havana Libre na anasema anakumbuka chumba chake kilikuwa ghorofa ya 14. Siku ya pili baada ya kuwasili Havana kiasi cha saa sita za usiku walichukuliwa kwenye mkutano uliokuwa ukihutubiwa na Che Guevara. Ilikuwa katika sehemu ndani ya ofisi yake.

Pamoja na Hashil walikuwa Hamed Hilal, Rahatileil na Ali Mshangama. Walikuwako pia vijana wengine kutoka nchi za Amerika ya Kusini. Kila mmojawao alipewa cigar avute labda ili wasisinzie. Mkutano huo ulifanywa nyakati hizo za usiku kwa sababu Che alikuwa amezongwa na kazi na hakuwa na nafasi mchana.

Che alizungumza kwa Kispanyola lakini alikuwako mkalimani wa Kiingereza. Alizungumzia umuhimu wa kuwa na umoja miongoni mwa wenye kupigana na ubeberu.

Baada ya hotuba yake Che aliwapa fursa ya kumuuliza maswali. Hashil aliuliza lake akajibiwa na baada ya mkutano kumalizika Che alimpa mkono yeye na wenzake akajiondokea.

Hashil anasikitika kwamba Che alipozuru Zanzibar yeye alikuwa masomoni Indonesia. Akina Ali Sultan na wenzake waliokuwa zamani Umma Party ndio waliokuwa wenyeji wa Che Zanzibar na walimpa Mussa Maisara, mmoja wa vijana wa Afro-Shirazi Party (ASP), dhamana ya kumtembeza.

Kwenda Cuba kulimvutia Hashil kwa vile alikuwa akimuhusudu sana Fidel Castro na akitamani akutane naye uso kwa uso. Bahati hiyo ilimwangukia ghafla siku Fidel alipokwenda hoteli ya Havana Libre.

Alipofika hotelini Fidel alifululiza hadi jikoni. Hashil alisadif kuwapo hapo na alisonga mbele kumpa mkono. Hakuwahi kuzungumza naye kwa kina. Alimwambia tu kwa Kispanyola kwamba alitoka Zanzibar. Anadhani baadaye Fidel aliuliza na kuambiwa kuwa Hashil alikuwa kati ya walio Cuba kwa mafunzo ya kijeshi.

Wenye kumjuwa Fidel wanasema kuwa ni mtu mwenye kupenda kujuwa mambo anayependa kuzungumza na kushindana. Fursa hiyo kwa bahati mbaya Hashil hakuipata.

Vijana wa Kizanzibari waliokuwa Cuba hawakuwa na masihara. Muda mwingi walikuwa wakizungumzia vipi watakaporejea nyumbani watapoweza kuipindua serikali.

Mwaka mmoja kabla Marekani ilijaribu kuupindua utawala wa Castro kwa kufanya uvamizi unaojulikana kama ‘Uvamizi wa Bay of Pigs’. Wakati mmoja baada ya vijana wa Kizanzibari kuwasili kulikuwa na uvumi kwamba Marekani huenda ikajaribu tena kuishambulia Cuba. Kusikia hayo kina Hashil walimpelekea barua Waziri wa Mambo ya Ndani wa Cuba Ramiro Valdés Menéndez wakimueleza kuwa walikuwa tayari kusimama bega kwa bega na wananchi wa Cuba kuihami nchi yao.

Barua hiyo iliwakuna viongozi wa Cuba. Kabla ya barua hiyo kuandikwa Wacuba wakitaka kuwaondosha Wazanzibari kambini na kuwapeleka kuwaficha sehemu nyingine. Lakini Hashil na wenzake walikataa na wakaachiwa wabakie kambini.

Mapinduzi ya akina Castro yalikabiliwa na misukosuko mingi. Mbali na jaribio la 1961 la uvamizi wa ‘Bay of Pigs’ Marekani imeiwekea vikwazo Cuba tangu 1959, vikwazo ambavyo vimeudhoufisha uwezo wa serikali ya Cuba wa kuyakidhi mahitaji ya wananchi wake.

Marekani pia ilivunja mahusiano yake ya kiserikali na Cuba. Na isitosheke ilijaribu hata kumuua Fidel Castro zaidi ya mara 600.

Ni wiki iliyopita tu Rais Barack Obama wa Marekani alipotangaza kwamba Marekani inabadili msimamo kuhusu Cuba na itaitambua na kuwa na mahusiano ya kawaida nayo.

Obama ametambua kwamba sera zao dhidi ya Cuba hazikufua dafu.

Kama kuna utawala unaostahiki kuwa na kaulimbiu ya ‘mapinduzi daima’ basi labda ungekuwa wa Cuba kutokana na vitimbi unavyofanyiwa na Marekani. Kaulimbiu kuu ya Cuba ni ‘patria o muetre, venceremos’ (‘Watani au kifo, tutashinda’), yaani tutaupigania watani wetu, nchi yetu, mpaka tufe na tutashinda. Hiyo ni kaulimbiu ya kizalendo.

Kwa hakika, katika nadharia za Kimarx ipo dhana inayoitwa ‘mapinduzi ya kudumu.’ Dhana hii ilianza kutamkwa na Karl Marx lakini baadaye ikawa moja ya nguzo za madhehebu ya Ki-Trotsky katika itikadi ya Kimarx. Waumini wa fikra hiyo wanamfuata Leon Trotsky, mmoja wa wanamapinduzi wa Urussi ambaye baadaye alihasimiana na Vladmir Lenin.

Trotsky alipendekeza dhana ya ‘mapinduzi ya kudumu’ kuelezea jinsi mapinduzi ya kisoshalisti yanavyoweza kutokea katika nchi zisizokuwa na ubepari mpevu.

Huku kwetu ‘mapinduzi daima’ inatumiwa kama dhana ya kihuni, ya kubagua watu kikabila au kisiasa. Wenye uchu wa madaraka wanazificha dhamiri zao ovu nyuma ya ‘mapinduzi daima.’

Hashil Seif na Mapinduzi ya Zanzibar walizaliwa tarehe moja. Januari 12, 1964 Hashil alitimia miaka 24. Alikuwa ameshapikika kisiasa na alikwisharudi Zanzibar kutoka Cuba. Alikuwa ni mmoja wa vijana wachache waliokuwa na ujuzi wa kutumia silaha na waliokuwa na nadharia za kimapinduzi.

Siku ya Mapinduzi alipewa vijana wapatao 15 awafunze kutumia silaha. Pia aliamrishwa na Maalim Aboud Jumbe akiteke kituo cha mawasiliano cha Cable & Wireless (ilipo sasa Serena Hotel). Aliowaongoza walikuwa pamoja na Adam Mwakanjuki na Kadiria Mnyeji, mfuasi mwengine wa Umma Party.

Jukumu jengine alilopewa Hashil pamoja na mwenzake Amour Dugheish aliyekuwa naye Cuba ni kukiteka kituo cha polisi cha Malindi. Hiyo ilikuwa kazi pevu kwani palizuka mapigano makali hapo.

Aidha Hashil alikuwa katika kikundi kilichoongozwa na Hamed Hilal kuiteka jela ya Kiinua Miguu. Walikuwa pamoja na Dugheish, Rahatileil, Tahir Adnan na Tahir Ali Salim.

Hii leo Hashil Seif akikaa na kuyatafakari yote hayo yaliyopita huingiwa na uchungu kuona jinsi Mapinduzi yalivyopotoshwa na Zanzibar ilivyopoteza mamlaka yake.

I wapi Zanzibar ikilinganishwa na Cuba? Chini kabisa. Cuba ina madaktari Zanzibar. Kwa hakika, ina madaktari na wauguzi wapatao 50,000 katika nchi 60. Isitoshe, Cuba inaongoza duniani kupambana na maradhi ya ebola.

Madaktari wa Cuba wamewatibu bure wagonjwa wa macho milioni tatu katika nchi 33. Hata Mario Teran, sajenti wa Bolivia aliyemuua Che Guevara kwa kuamrishwa na shirika la ujasusi la Marekani la CIA, miaka 40 baadae alifanyiwa operesheni ya macho na madaktari wa Cuba. Alikuwa haoni na sasa anaona.

Sisi Zanzibar tuna nini cha kujivunia na kaulimbiu ya ‘mapinduzi daima’?

 • Ahmed Rajab/Raia Mwema

Rais Kikwete ahani msiba wa Sheikh Komorian

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiifariji familia ya Marehemu Sheikh Ali Mzee alipokwenda kuhani msiba huo jana Jumapili Desemba 29, 2014. Marehemu Sheikh Komorian alifariki juzi Jumamosi Desemba 28, 2014 na kuzikwa jana Jumapili Desemba 29, 2014.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiifariji familia ya Marehemu SheikhAli Mzee alipokwenda kuhani msiba huo jana Jumapili Desemba 29, 2014. Marehemu Sheikh Komorian alifariki juzi Jumamosi Desemba 28, 2014 na kuzikwa jana Jumapili
Desemba 29, 2014.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akishiriki katika dua na familia yaMarehemu Sheikh Ali Mzee alipokwenda kuhani msiba huo jana Jumapili Desemba 29, 2014. Marehemu Sheikh Komorian alifariki juzi Jumamosi Desemba 28, 2014 na kuzikwa jana Jumapili
Desemba 29, 2014

 • Taarifa ya Ikulu

Binti ajirusha baharini

Mwanadada mmoja amejirusha baharini katika kivuko cha ferry mapema leo adhuhuri wakati akiwa ameabiri ferry ya MV Harambee kutoka upande wa Mombasa Kisiwani kuelekea Likoni.

Msichana huyo mwenye umri kati ya miaka 20 na 25 amejirusha kutoka eneo la juu ya ferry wakati fery ikiwa katikakati ya bahari ikielekea ufuoni.

Wapiga mbizi wa shirika la Kenya ferry wamejaribu kuokoa maisha yake baada maji kumzidi kutokana na mawimbi makali na akafanyiwa huduma ya kwanza na hatimaye kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Likoni. Kwa sasa anapokea matibabu katika hospitali moja mjini Mombasa.

Kulingana na afisa wa uhusiano mwema wa shirika la Kenya Ferry Harun Mutiso amesema kwamba maafisa wa polisi wanachunguza kilichopelekea msichana huyo kutaka kutoa uhai wake.

Hata hivyo kulingana na walioshuhudia ni kwamba wanadada huyo alionekana mtulivu na hakuna aliyetarajia kwamba anaweza jirusha kutoka eneo la juu ya Ferry hadi ndani ya bahari.

Haya yanajiri siku moja baada ya mwanadada mmoja kutoka mtaa wa wa mbuzi huko Likoni kumtumia rafiki yake wa kiumeujumbe mfupi kutumia simu ya rununu kwamba atajinyonga kutokana na hali ya maisha kuzidi kuwa ngumu kwake.

Albino atekwa; Baba anashikiliwa na Polisi

Binti mwenye asili ya Albino Mkoani Mwanza atekwa na watu wasiojulikana waliovamia nyumba yao na kumuweka chini ya ulinzi baba yake.

Ajali yaua 4 Uchira, Moshi

Watu wanne wamefariki na wengine wamejeruhiwa baada basi walilopanda kupasuka tairi na kugonga basi ndogo huko mkoani Kilimanjaro.

Ufafanuzi wa Wizara kuhusu habari katika gazeti la NIPASHE

TAARIFA YA UFAFANUZI WIZARA YA NISHATI NA MADINI

Katika gazeti la NIPASHE la Jumatatu tarehe 08 Desemba, 2014 ziliandikwa habari kuhusu Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo (Mb) chini ya kichwa cha habari “Wanaomtetea Muhongo Wajibu haya”. Hoja zilizotolewa katika gazeti hilo zililenga kupotosha ukweli. Wizara inapenda kutoa maelezo kuhusu hoja zilizotolewa kama ifuatavyo:

Utendaji wa Wizara chini ya Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo (Mb)

Taarifa za gazeti hilo zilieleza kuwa utendaji wa Wizara ya Nishati na Madini hasa katika uongozi wa Waziri Muhongo umekuwa ni wa kukatisha tamaa. Moja ya mifano iliyotolewa ni kuendelea kuwepo kwa wachimbaji madini wanaozidi kutorosha madini kwa nia ya kukwepa kodi. Hoja hii haina ukweli wowote kwani chini ya uongozi wa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo (Mb) utendaji wa Wizara umeimarika kwa kiasi kikubwa. Chini ya Uongozi wake kumekuwepo na uwajibikaji mkubwa kwa watumishi wa wizara ili kuhakikisha kuwa wanawatumikia wananchi ipasavyo. Ni katika kipindi chake kumekuwepo na uanzishwaji wa madawati ya ukaguzi wa madini katika viwanja vikubwa vya ndege vya JNIA, KIA na Mwanza chini ya Wakala wa Ukaguzi wa madini (TMAA) ili kudhiditi wachimbaji madini na watu wengine wenye nia ya kutorosha madini nje ya nchi bila kuzingatia sheria. Kutokana na hatua hiyo madini mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 15 yameweza kukamatwa. Madini yaliyokatwa bila kuwa na vibali halali yametaifishwa na Serikali. Serikali ilianza kuuza baadhi ya madini yaliyokamatwa kwa njia ya mnada kwenye Maonyesho ya Vito yaliyofanyika Mjini Arusha kuanzia tarehe 18 - 20 Novemba, 2014. Katika mnada huo jumla ya zaidi ya shilingi milioni 70 zilipatikana na kuingia Serikalini. Serikali itaendelea kupiga mnada madini mengine yaliyokamatwa kwa manufaa ya taifa. Wizara inaendelea kuimarisha udhibiti ili kuhakikisha kuwa mtu yeyote anayekusudia kutorosha madini anakamatwa na kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na madini yake kutaifishwa na Serikali. Katika kusimamia sheria na taratibu, chini ya Uongozi wa Prof.Muhongo, Wizara imedhibiti tabia ya kuchukua vitalu vya madini na kuhodhi ili wale tu wanaozingatia masharti ya leseni ndio waendelee kuvifanyia kazi vitalu. Hili limewaumiza waliokuwa na tabia hiyo ambao kimsingi walikuwa wanavunja sheria. Baadhi ya vitalu vilivyopokonywa vimekuwa vikigawiwa kwa wachimbaji wadogo.Hivyo, si kweli kwamba utendaji wa Wizara ya Nishati na Madini chini ya Prof. Sospeter Muhongo (Mb) ni wa kukatisha tamaa katika kudhibiti utoroshaji wa madini nje ya nchi na katika ukiukwaji wa masharti ya leseni mbalimbali za madini kama ilivyodaiwa.

Upitiaji Mikataba ya Madini

Taarifa za gazeti hilo la NIPASHE la Jumatatu tarehe 08 Desemba, 2014 zilieleza kuwa chini ya Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo (Mb) Serikali imeshindwa kupitia mikataba ya madini ili taifa linufaike zaidi. Taarifa hizo si za kweli zinalenga kupotosha umma.

Ukweli ni kuwa chini ya Uongozi wa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo (Mb), Wizara imepitia mikataba ya madini kwa kufanya majadiliano na Kampuni za uchimbaji madini zenye mikataba ili kurekebisha vipengele vya mikataba ambavyo vinalenga kuleta manufaa zaidi kwa Taifa. Kazi hiyo imefanyika kwa Kampuni zote zenye mikataba na tarehe 9 Oktoba, 2014 Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) imetiliana saini mkataba wa kurekebisha vipengele katika mkataba uliosainiwa huko nyuma baada ya majadiliano kukamilika. Aidha, majadiliano na Kampuni ya ACACIA (zamani Kampuni ya African Barrick Gold –ABG) yamekamilika na kilichobaki ni pande mbili (Serikali na Kampuni) kusaini marekebisho yaliyofanyika kwa ajili ya mikataba ya migodi yake ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara.

 1. KUKATIKA KWA UMEME

Kukatika kwa umeme kunasababishwa na kuzeeka kwa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme. Ikumbukwe kuwa, kwa kipindi cha karibu miaka kumi TANESCO iliwekwa chini ya PSRC kwa nia ya kubinafsishwa mwaka 1997 – 2007. Katika kipindi hiki TANESCO haikuruhusiwa kuwekeza wala kufanya ukarabati wa miundombinu yake hivyo hali hiyo ilipelekea kuchakaa kwa miundombinu hiyo ikiwemo mfumo wa usafirishaji na usambazaji wa umeme. Hata hivyo baada ya Serikali kubadili mtazamo wake wa kulibinafsisha Shirika, TANESCO mipango kabambe ya kufanya ukarabati wa miundombinu hiyo na kujenga mipya ili kuwa na mfumo wa usafirishaji na usambazaji umeme ulio wa uhakika. Kazi hiyo inaendelea katika sehemu mbalimbali nchini ikiwemo jiji la Dar es Salaam ambako kazi ya kukarabati na kupanua miundombinu ya usambazaji umeme inaendelea. Aidha, TANESCO ilishaelekezwa kutoa taarifa kwa umma kuhusu katizo lolote la umeme lililopangwa kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya umeme. TANESCO imekuwa ikifanya hivyo kwa kutumia vyombo vya habari vikiwemo televisheni, radio na magazeti na pia kwa kutumia magari ya TANESCO kufikisha taarifa kwa maeneo yanayoathirika. Kwa upande wa katizo la umeme usiotarajiwa, TANESCO inacho kikosi cha dharura ambacho watumishi wake wanafanya kazi masaa ishirini na nne kwa zamu ili kuhakikisha kuwa hitilafu ndogondogo zinatatuliwa mara moja zinapojitokeza. Jamii ya Watanzania wanalishuhudia hilo.


 1. DENI LA TANESCO LAPAA.

Mpaka kufikia mwanzoni mwa mwaka 2014, deni la TANESCO lilikuwa limefikia takribani Shilingi bilioni 695.30. TANESCO kwa kutumia vyanzo vyake vya fedha kutokana na ukusunyaji wa maduhuli ndani ya kipindi cha miezi 11 imepunguza deni hilo mpaka kufika takribani Shilingi bilioni 355.11. Kukua kwa deni la TANESCO kulisababishwa na hali ya ukame uliolikumba taifa kuanzia miaka ya 2011 ambapo TANESCO ililazimika kununua umeme aghali kutoka kwa wazalishaji wa umeme binafsi ikiwemo mitambo ya kukodi ya dharura. Deni hilo lilikua kama ifuatavyo:

Mwaka Deni (Bilioni Sh.)
2011           538.47
2012            563.02
2013           695.30
2014 (9 Disemba) 355,11

TANESCO imeongeza ufanisi wake katika kukusanya maduhuri na kufikia kiwango cha asilimia 97 na fedha inayopatikana inatumika kupanua huduma ya umeme nchini, kuendesha Shirika na kulipa madeni inayodaiwa.

Ukweli ni kwamba deni la TANESCO limeshuka kwa kiasi kikubwa na kwa sasa TANESCO imeweka mkakati maalumu wa kuwalipa wadeni wake wakubwa kiasi cha Shilingi bilioni tatu kwa wiki kwa kila mdai, hivyo ni matarajio ya Shirika kumaliza deni hilo mwaka kesho (2015).

 1. NCHI ITASONGA MBELE

Wazo la kuanzishwa kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) lilibuniwa na watumishi na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini mwaka 2005/6 chini ya uongozi wa Nazir Karamagi akiwa Waziri wa Nishati na Madini. Taratibu za kuanzishwa kwa REA zilikamilika mwaka 2007 ambapo REA ilianza kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Sospeter Muhongo baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini ameisaidia REA kupata fedha kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo na hivyo amesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza kwa kasi ya kupeleka huduma ya umeme vijijini.

Aidha, Ili kufikia lengo la kuwaunganishia umeme asilimia 30 ya watanzania ifikapo mwaka 2015, Chini ya uongozi wa Waziri Muhongo Serikali kupitia TANESCO, ilipunguza gharama za kuunganisha umeme wa njia moja (single phase) kwa wateja wadogo kwa wastani wa kati ya asilimia 30 na 77 kama ifuatavyo:

 1. Kwa wateja watakaojengewa njia moja (single phase) kwenye umbali usiozidi mita 30 bila kuhitaji nguzo, katika maeneo ya vijijini watalipa Shilingi 177,000 na wa mijini watalipa Shilingi 320,960badala ya Shilingi 455,108 zinazolipwa na wateja hao kwa sasa.

 1. Kwa wateja watakaojengewa njia moja (single phase) na kuwekewa nguzo moja, katika maeneo ya vijijini ni Shilingi 337,740 na wa mijini ni Shilingi 515,618 badala ya Shilingi 1,351,884 zinazolipwa na wateja hao kwa sasa.

 1. Kwa wateja watakaojengewa njia moja na kuwekewa nguzo mbili katika maeneo ya vijijini ni Shilingi454,654 na wa mijini ni Shilingi 696,670 badala ya Shilingi 2,001,422 zinazolipwa na wateja hao kwa sasa.


Kwa ujumla katika kipindi hiki huduma ya umeme nchini imepanuka na kuwa bora zaidi kuliko siku za nyuma. Ni matarajio ya Serikali kuwa huduma hii itazidi kuwa bora zaidi katika siku chache zijazo kutokana na juhudi kubwa zinazoendelea katika sekta ndogo ya umeme.

 1. DALALI WA FEDHA ZA ESCROW

Waziri wa Nishati na Madini ndiye msimamizi mkuu wa masuala yanayohusu sekta za Nishati na Madini nchini. Mtambo wa IPTL ulijengwa kwa ajili ya kufua umeme unaotumiwa na jamii ya watanzania. Kuwepo kwa mgogoro kungeweza kuondoa azma ya uwepo wa mtambo huo ya kufua umeme ili kuliepusha Taifa kuingia katika mgawo wa umeme kutokana na upungufu wa upatikanaji wa nishati hiyo, hivyo lilikuwa ni jukumu lake kuona kuwa mgogoro wa wawekezaji wa mitambo ya IPTL unakwisha ili mitambo iendelee kutoa huduma ya umeme kwa Taifa. Jukumu la Waziri ni kusimamia Sera, Sheria na taratibu katika sekta anazozisimamia. Katika kufanya hivyo, Waziri hukutana na wadau na kujadili masuala kwa uwazi bila kificho kwa nia ya kujenga nchi na kuhakikisha kuwa maslahi ya Taifa ndiyo kipaumbele. Kwa hiyo mikutano na Wadau ikiwa ni pamoja na wawekezaji hufanyika si kwa udalali. Suala la fedha za akaunti ya Escrow lilihusu uamuzi wa mahakama iliyojiridhisha kuwa mnunuzi wa hisa zote za VIP na MECHMAR ni halali na alitakiwa kukabidhiwa mali na madeni ya IPTL. Mali ni pamoja na kiasi cha fedha stahiki kwenye Akaunti ya Escrow ambazo hata hivyo ilidhihirika kuwa hazitoshi kukidhi deni halali.

Akaunti hiyo ilikuwa na Sh. 182 bilioni wakati malipo yaliyokubalika kwa pande zote (IPTL na TANESCO) kwa mujibu wa maamuzi ya ICSID I yalikuwa Sh. 306 bilioni. Kumwita Waziri wa Nishati na Madini kuwa ni dalali ni kupotosha ukweli.

Kiwanda cha juisi chafungwa, picha ya uzalishaji inajieleza...

Baadhi ya juisi hizo zikizalishwa

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) imekifungia kiwanda cha Devideic cha mjini Morogoro kwa muda usiojulikana kuendelea na uzalishaji wa juice aina ya Into baada ya vipimo vya kimaabara vya Shirika hilo kubaini kiwango cha sukari inayotumika haifai kwa binadamu pamoja na mazingira ya uchafu.

Matumizi hayo ya sukari isiyofaa na mazingira hayo ya uchafu yanahatarisha usalama wa afya za walaji wengi yakiwemo makundi ya rika mbalimbali na watoto.
Kufungiwa kwa Kiwanda hicho kuendelea kuzalisha bidhaa ya aina hiyo kulifanyika jana ( Des 29),baada ya maofisa wa TBS kutoka makao makuu Jijini Dar es Salaam , kufanya ukaguzi wa kushitukiza katika kiwanda hicho kilichopo eneo la Kihonda, Maniapaa ya Morogoro.

Ukaguzi hu wa kushitukiza ulifanyika chini ya ulinzi wa Polisi na baada ya kufika kiwandani hapo, wafanyakazi kadhaa walikutwa wakijaza juici iliyojazwa kwenye matenki kwa kupitia mabomba yaliyowekwa kiko tofauti na utaratibu wa kiuzalishaji.

Ofisa Viwango na Mkaguzi wa TBS, Lawrence Chenge, baada ya kujilizisha na ukaguzi wake katika maeneo ya stoo, mitambo, matenki , mifumo ya maji na aina ya viwango vinavyohitajika ndani ya juice hiyo , ulibani kuwa na kasoro nyingi na kukosekana kwa aina viwango vinavyohitajika kuihalalisha kuwa na ubora halisi kwa watumiaji.

“ Tumefanya ukaguzi mara kadhaa na mara zote tumetoa kutoa maelekezo maeneo ya sehemu ya kurekebishwa ...lakini hadi sasa hawajafanya juhudi zozote “ alisema na kuongeza
“ ...Tumepima tena juici hii ya Into kwenye maabara zetu na kugundulika kuna kasoro nyingi ya kukosekana viwango muhimu vinavyotakiwa kwenye bidhaa hii na kwa maana hii haijakidhi viwango na haifai kwa matumizi ya binadamu na wengi wakiwa ni watoto “ alisema.

Kutokana na mapungufu hayo, TBS imechukua jukumu la kukifungia kiwanda hicho kisiendelee na uzalishaji wake katika bidhaa hiyo hadi pale uongozi wa kiwanda utakaporekebisha yale yaliyobainika kwenye ripoti kimaabara nay a kiukaguzi na kukaguliwa tena kabla ya kuruhusiwa.

Wakati kiwanda hicho kinafungiwa kuendelea na uzalishaji wa aina hiyo ya juici, tayari katoni 50 zilikutwa zimezalishwa na nyingine kurundikwa kwenye madishi makubwa.

Naye Ofisa Uhusiano wa TBS, Roida Andusamile, alisema kuwa Shirika hilo lina maabara za kisasa na kuwa na uhakika wa matokeo ya majibu ya upimaji wa sambuli ya juici hiyo inayozalishwa na kiwanda hiyo.

Kwa mujibu wa Ofisa huyo, kutokana na ubora wa maabara hizo,matokeo ya majibu ya viwango chake hata upimaji huo ukipelekwa nje ya nchi hakutakuwepo na utofauti wa majibu.

Hivyo alisema, uchunguzi wa kimaabara na matokeo yake ni kwamba juichi hiyo ina uchafu na inatumia ‘sweetner’ kinyume na kiwango kinavyotakiwa na hivyo kuwa na madhara kwa binadamu.

Mbali na hayo ,alisema bidhaa iliyopo sokoni ‘ madukani’ itaondolewa na kutakiwa isiendelee kuuziwa wateja kutokana na mapungufu yaliyomo kwenye juici hiyo.

Kwa mujibu wa Ofisa Uhusiano huyo , kiwanda hicho kimeanzishwa kihalali kupitia mfumo wa viwanda vidogo vodogo vya wajasiliamali chini ya mpango ulioanzishwa na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) mwaka 2011 na kilipewa alama ya TBS kwa masharti ya kuzalisha bidhaa zenye viwango vya ubora kwa mujibu wa sheria na pale kinapokwenda kinyume kitafungiwa kama vinavyofungiwa viwanda vingine vikubwa.

Kwa upande wake Meneja wa Uzalishaji wa Kiwanda hicho, Thadeus Ngonyani, licha ya kujitetea kuwa wanazingatia viwango vya ubora ,alijikuta akilemewa na maswali kuliko majibu huku akitoa lamawa kuwa huo ni uonevu na kuwa ni vita vya kibiashara kwa kukifungia kiwanda chake.

Hata hivyo akilishindwa kujitetea pale alipotakiwa kuanisha aina ya viwango ‘ Ingredients’ iliyomo kwenye juici hiyo aina ya Into na pia kuendelea kujaza juici kwa mfumo wa njia ya kawaida wakati ulipokatika umeme.

 • John Nditi / Habarileo