Bomu larushwa kwa mkono na kujeruhi 6 Morogoro


Hofu ya ugaidi imezidi kutanda katika Wilaya ya Kilombero baada ya watu sita kujeruhiwa vibaya na bomu lililorushwa kwa mkono wakati wakitoka katika maadhimisho ya Mei Mosi katika kijiji cha Msolwa Ujamaa katika Kata ya Sanje wilayani Kilombero mkoani Morogoro.

Katika hospitali ya St. Kizito Mikumi walikolazwa, majeruhi wa tukio hilo wamesema bomu hilo lilirushwa na vijana wawili baada ya kutiliwa shaka na wananchi wa kijiji hicho na kuwaweka chini ya ulinzi kwa ajili ya kuwapekua, ambapo vijana hao walirusha bomu na kujeruhi wananchi pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali waliokuwa kwenye gari la Mweneyekiti wa Halmashauri wakitokea katika maadhimisho ya Mei Mosi.

Wameomba jeshi la polisi kufanya uchunguzi kufuatia matukio yanayoashiria ugaidi kuendelea kuandama wakazi wa Kilombero.

Nao viongozi wa Kata akiwemo Diwani wa kata ya Sanje, David Ligazio wamesema ipo haja ya serikali kuongeza nguvu ya jeshi la polisi ikiwa ni pamoja na magari ya usafiri na kutafuta vifaa vinavyoweza kuchunguza maeneo ya milima ya Udzungwa na Ruaha ambapo wamebaini wahalifu wengi wamewaona wakitokea katika misitu hiyo mara kwa mara.

Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Lenard Paul amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema hadi sasa jeshi la polisi linawatafuta watuhumiwa hao. Amesema bomu hilo limejeruhi dereva wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero,  kuharibu gari ya Halmashauri na kujeruhi wananchi wa kijiji cha Msolwa Ujamaa.

Tukio hilo limetokea ndani ya siku 14 baada ya watuhumiwa wengine  9 kukamatwa Msikitini wakiwa na milipuko 30, sare za jeshi, bendera nyeusi pamoja na vitu mbalimbali vya kufanyia uhalifu, huku mmoja akichomwa moto na wananchi wenye hasira akiwa katika harakati za kutoroka baada ya kumchoma askari kwa jambia shingoni hukko katika Tarafa ya Kidadu wilayani Kilombero.

via ITV