Serikali imewatelekeza waliokubali Diploma ya Ualimu wakaacha High School

SERIKALI IMEWATEKELEZA VIJANA WALIOKUBALI KUSOMA DIPLOMA YA UALIMU NA KUACHA KUSOMA KIDATO CHA TANO NA SITA

Itakumbukwa kuwa serikali ilifanya kampeni kubwa juu ya suala hili mwaka jana 2014. Na ikasema imejiandaa vya kutosha kuwaendeleza vijana hao wa masomo ya sayansi ili wamalizapo diploma ya “chap chap” warudi kwenye shule zetu kuondoa tatizo la ukosefu na upungufu wa walimu wa sayansi.

Vijana hao walidahiliwa pale Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa ajili ya programu hiyo lakini serikali haikuwa imejipanga kuwapa fedha za mahitaji muhimu kama ilivyohitajika. Taarifa kutoka UDOM zinaonesha kuwa, vijana hao wametangatanga na kuomba pesa za kula na kujikimu kutoka kwa wale “wakubwa zao” wanaosoma Digrii hadi imekuwa kero. Unakuta kisichana cha miaka 17 au 16 kinasoma programu hii na hakijapewa pesa za vitabu, chakula na malazi. Kinazunguka kuwaomba wakaka wa digrii ili kiishi, nani kakipeleka kitoto hiki Dodoma?

Baada ya vijana hao wanaotokea mikoa mbalimbali ya Tanzania kutaabika bila kupata msaada huku hawana pesa kwa muda mrefu, waliamua kuongozana kwenda kwa Waziri Mkuu na ama Mawaziri na viongozi wengine wa serikali ili suala lao litatuliwe. Wamekutana na ukatili wa kutosha kutoka kwa polisi, wengine wamevunjika na kuumia vibaya.

Mimi ambaye nimepitia misukosuko zaidi ya hiyo wakati naongoza UDSM na TAHLISO, nachoweza kusema ni kuwa vijana wa sasa na wazee wetu wa sasa, hii ndiyo hali halisi ya nchi yetu. Tuna serikali isiyo na mipango na isiyo na haja ya kupanga na kutekeleza chochote “unresponsible government”. Iweje tupange kusomesha vijana kwa programu za dharura huku hatuna fedha za kuendesha program hiyo na hasa kutosheleza mahitaji ya gharama za maisha ya wahusika?

Ni hivi karibuni tu Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu imetangaza kwamba imeshindwa kuwapa mikopo wanafunzi zaidi ya 20,000 kwa mwaka huu peke yake. Nikukumbusheni pia kwamba, bunge la bajeti lililokamilisha kazi yake mwezi Juni 2014 tulijionea ripoti za aibu zikionesha kuwa kuna wizara nyingi tu ziliishia kupata 40% - 50% ya bajeti iliyopangwa. Haya yote ni dalili tosha kuwa tunaishi kwenye “taifa linaloangamia” (a failed state). Kwamba hatuna uwezo wa kupanga na kutekeleza mipango yetu. Kwamba hatuna kipaumbele kwa yale tunayoyafanya.

Watoto wa watu tumewadanganya, wameacha kwenda kidato cha tano na sita kwa nia njema ya kulisaidia taifa lao kutokana na vipaji na elimu yao, badala ya kuwalipa neema na mipango thabiti tunawalipa ubabaishaji, ukatili, nia ovu na jeuri. Vijana hawa wanaoteseka leo kwa ajili ya haki zao wanapata mafunzo makubwa sana. Idadi ya vijana watakaoendelea kuichukia CCM inaongezeka kama mchanga wa baharini maana “Colonialism planted the seeds of its own destruction” – Hakika, hata CCM inapanda mbegu ya kujimaliza wenyewe.

Poleni sana wadogo zetu, poleni sana wana UDOM.

J. Mtatiro,
Alhamisi, 15 Januari 2015,
Dar Es Salaam.

Rais Kikwete aliposhuhudia kuapishwa kwa Rais Nyusi

Rais Mpya wa Msumbiji Felipe Jacinto Nyusi akila kiapo cha urais kuiongoza nchi ya Msumbiji jijini Maputo Msumbiji jana.


Rais Jakaya Kikwete akimpongeza Rais Mpya wa Msumbiji Filipe Jacinto Nyusi muda mfupi baada ya kuapishwa jijini Maputo Msumbiji leo.


Rais Kikwete akizungumza na Rais Mpya wa Msumbiji Filipe Jacinto Nyusi pamoja na Rais wa Msumbiji aliyemaliza muda wake Armando Emilio Guebuza katika viwanja vya ikulu ya Maputo baada ya sherehe za kuapisha leo.


Rais Kikwete akisalimiana na Rais Mstaafu wa Zambia Kenneth Kaunda wakati wa kuapishwa kwa Rais mpya wa Msumbiji Felipe Jacinto Nyusi jijini Maputo Msumbiji leo.


Rais Kikwete akifurahia jambo na Mfalme Letsie III wa Lesotho(kushoto), Rais Hifikepunye Pohamba wa Namibia(wapili kushoto) na kulia ni mke wa Rais Mama Salma Kikwete.Viongozi hao walihudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Mpya wa Msumbiji Felipe Jacinto Nyusi zilizofanyika jijini Maputo Msumbiji.

picha: Freddy Maro/Ikulu

Tuhuma zaisababisha PAC kuisimamisha Menejimenti ya RUBADA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC) imeisimamisha kazi kwa muda Menejimenti ya Mamlaka ya Bonde la mto Rufiji  (RUBADA) kwa tuhuma za ubadhirifu, ajira za upendeleo na kuwa na hati mbili za ukaguzi wa hesabu za mwaka 2012/13.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe amesema menejimenti hiyo imesimamishwa kwa kipindi cha miezi mitatu ili kupisha uchunguzi mzima unaoikabili.

Wengine 3 wafikishwa kortini kuhusiana na Tegeta Escrow Account

Watuhumiwa waliofikishwa mahakamani leo kuhusiana na miamala ya Tegeta Escrow Account

Watu watatu wengine wamefikishwa mahakamani jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kuingiziwa fedha za rudhwa zilizotoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imewafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, watu hao waliotambuliwa kuwa ni Mhasibu wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) Steven Urassa, Meneja wa Misamaha ya Kodi wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Leonard Kyabukoba Rutabingwa na Mkurugenzi wa Fesha wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Julius Angelo Ruta.

Urasa yupo nje kwa dhamana wakati watuhumiwa wengine wawili wamepelekwa rumande kwa kushindwa kukidhi masharti ya dhamana.

Hadi sasa, idadi ya watu waliofikishwa kortini kuhusiana na miamala ya akaunti ya Tegeta Escrow ni watano.

TAKUKURU imesema ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) inatakiwa kuchukua hatua ya kuwafikisha mahakamani vigogo wote wakiwamo mawaziri na wale wote watakaobainika kwenye uchunguzi wake kuwa wamehusina na vitendo vya rushwa katika miamala ya akaunti ya Tegeta Escrow.

Rais Kikwete aongoza kikao cha kwanza mwaka huu cha Baraza la Mawaziri

Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiongoza kikao cha Baraza la Mawaziri chakwanza kwa mwaka huu wa 2015 Ikulu jijini Dar es salaam leo January 16, 2015. Kulia kwake ni Makamu wa Rais Dkt Mohamed Gharib Bilali na kushoto
kwake ni Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda.
(picha: Ikulu)