Mawaziri 120 ndani ya miaka 10 ya Urais wa Kikwete

Rais Jakaya Kikwete ambaye alianza kipindi chake cha kuongoza nchi mwaka 2005 kwa kuteua jumla ya mawaziri na manaibu 60, anaondoka akiwa ameteua jumla ya watu 118 kushika nyadhifa hizo, Mwananchi inaweza kukuthibitishia.

Mwaka 2005 wakati akitangaza baraza lake la kwanza, Rais Kikwete aliteua mawaziri 29 na manaibu 31, idadi ambayo ilikuwa kubwa kulinganisha na marais waliopita, lakini alipofanya mabadiliko ya kwanza makubwa mwaka 2008, alipunguza ukubwa wa Serikali baada ya kuteua mawaziri 26 na manaibu 21.

Hata hivyo, idadi kubwa ya watu walioteuliwa kuwa mawaziri, imechangiwa na idadi ya mabadiliko aliyofanya tangu alipovunja baraza mwaka 2008 kutokana na Edward Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu.

Ukijumlisha na mabadiliko hayo, tayari Rais Kikwete amefanya mabadiliko makubwa ya mawaziri mara tatu na madogo mengine mara tatu, hali inayoifanya Serikali yake kutumia mawaziri tofauti 118 katika utawala wake hadi sasa.

Rais alifanya mabadiliko makubwa ya kwanza mwaka 2008 kutokana na kashfa ya mkataba wa Richmond iliyosababisha Lowassa kujiuzulu na baadaye mwaka 2012 aliwaacha mawaziri sita kutokana na kashfa iliyotokana na ripoti ya CAG, kabla ya kufanya mabadiliko mengine makubwa mapema mwaka 2014 kutokana na kashfa ya Operesheni Tokomeza, ambayo utekelezaji wake ulitawaliwa na uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu.

Katika kipindi hicho, mawaziri wanne walipoteza maisha, mmoja alipata kazi Umoja wa Mataifa na wengine kujiuzulu na hivyo kulazimika kufanya mabadiliko madogo manne.

“Mabadiliko haya ninayachambua katika sehemu mbili. Kwanza, ili mtu aweze kufanya kazi kwa utulivu na kutekeleza mikakati yake ni lazima awe na muda wa kutosha. Kama akikosa utulivu taasisi (wizara) aliyopo inaweza kuyumba,” alisema Mkuu wa Shule ya Sheria wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Bonaventure Rutinwa.

Hata hivyo, Rutinwa, ambaye alikuwa mmoja wa wasomi waliotakiwa kutoa maoni yao kuhusu idadi ya mawaziri walioteuliwa hadi sasa, alisema mara nyingi mabadiliko hayo yamefanyika kutokana na matatizo yanayotokea katika wizara zilezile, akitoa mfano Wizara ya Nishati na Madini, ambayo alisema imesababisha wizara nyingine kutetereka.

“Ili kuepusha jambo hili. Uteuzi katiza wizara kama hii ya Nishati na Madini unatakiwa kufanywa kwa umakini zaidi ili kuepuka kubadili mawaziri mara kwa mara,” alisema.

“Kama waziri anakuwa na mipango ya muda mrefu na akaondoka ndani ya kipindi kifupi, mambo yanaweza kukwama,” aliongeza.

Kwa upande wa pili, Profesa Rutinwa alisema mabadiliko hayo huondoa fikra kwa baadhi ya mawaziri kuwa uwaziri ni urithi badala ya nafasi hiyo kuwa ya kisiasa.

“Uwaziri utaendelea kuwa wako iwapo tu utafanya vizuri kazi zako. Hata Rais Kikwete wakati akiingia madarakani aliwahi kusema wazi kuwa yeye na Makamu wa Rais ndiyo wenye nafasi za kudumu, si mawaziri aliowateua,” alisema.

Lakini Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Profesa Tolly Mbwete na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana walitofautiana na msomi mwenzao na badala yake kupongeza mabadiliko hayo ya mara kwa mara, wakisema yanaongeza ufanisi.

“Naona ni suala la kawaida tu ili kuondoa ufanyaji kazi wa mazoea,” alisema Profesa Mbwete.

Alisema jambo la muhimu kwa mawaziri ni kufanya kazi ipasavyo na kusisitiza kuwa ndiyo maana mawaziri ambao ni watendaji kazi wazuri wapo mpaka leo.

“Wanaoteuliwa wanatakiwa kutambua wajibu wao, lakini pia waziri kukaa sana katika nafasi hiyo si jambo zuri,” alisema.

Dk Bana alisema: “Mawaziri wanabadilishwa kulingana na uwajibikaji wao. Wapo walioondolewa kwa sababu ya shinikizo au maazimio ya Bunge.”

Alisema kitendo cha Rais Kikwete kubadili Baraza la Mawaziri mara saba kinaonyesha wazi kuwa kiongozi huyo anasikiliza ushauri wa wasaidizi wake na malalamiko yanayotolewa na wananchi juu ya wizara au utendaji wa mtu.

“Mfano mzuri ni mwaka 2006, Rais Kikwete alibadili Baraza la Mawaziri kwa sababu wananchi tulipiga kelele kuwa lilikuwa na mawaziri 60 ambao ni wengi. Amekuwa akibadili ili kuongeza utendaji zaidi,” alisema Dk Bana.

Kwa mujibu wa mapitio ya Mwananchi, Rais Kikwete aliachana na mawaziri 63 kwa sababu tofauti, wakati amedumu na mawaziri 16 tu tangu mwaka 2005 alipoingia Ikulu.

Hivi sasa Baraza la Mawaziri lina mawaziri 55, wakiwamo 16 ambao alianza nao tangu alipotangaza baraza lake la kwanza la mawaziri mwaka 2005.

Waliopo sasa ni Dk Binilith Mahenge, Ummy Mwalimu, Saada Mkuya, Mwigulu Nchemba, Adam Malima, Dk Asha-Rose Migiro, Janet Mbene, Dk Seif Rashid, Dk Stephen Kebwe, Jenista Mhagama, Dk Pindi Chana, Dk Titus Kamani na Kaika Telele.

Wengine ni George Simbachawene, Amos Makala, Godfrey Zambi, Juma Nkamia, Lazaro Nyarandu, Mahmoud Mgimwa, Charles Kitwanga, Charles Mwijage, Anna Kilango- Malecela, Angela Kairuki, Stephen Masele, William Lukuvi na Profesa Makame Mbarawa.

Pia wamo Samwel Sitta, Dk Abdulla Juma Abdulla, Mahadhi Juma Maalim, Pereira Ame Silima, Dk Abdallah Kigoda, Dk Fenella Mukangara, Gerson Lwenge, Dk Charles Tzeba, Dk Harrison Mwakyembe, January Makamba, George Mkuchika na Samia Suluhu Hassan.

Mawaziri ambao Rais Kikwete alianza nao na wapo mpaka sasa ni Sofia Simba, Profesa Mark Mwandosya, Stephen Wasira, Dk Hussein Mwinyi, Dk John Magufuli na Aggrey Mwanry.

Wengine ni Profesa Jumanne Maghembe, Dk Shukuru Kawamba, Hawa Ghasia, Dk Mary Nagu na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye katika Baraza la kwanza, alikuwa naibu waziri na baadaye waziri wa Tamisemi.

Mawaziri wengine alioanza nao mwaka 2005 wakiwa naibu mawaziri ni Gaudencia Kabaka, Bernard Membe, Celina Kombani, Christopher Chiza, Mathias Chikawe na Dk Makongoro Mahanga ambaye tangu 2005 mpaka sasa bado ni naibu waziri.

Mawaziri wengine

Mawaziri waliotemwa au kujiuzulu tangu Rais Kikwete aingie madarakani, wakiwamo wale walioshindwa katika kinyang’anyiro cha ubunge ni Edward Lowassa, Antony Diallo, Dk Ibrahim Msabaha, Basil Mramba, John Chiligati, Andrew Chenge, Joseph Mungai, Dk Emmanuel Nchimbi, Lawrence Masha, Mustafa Mkulo, William Ngeleja, Dk Cyril Chami, Omary Nundu, Bakari Mwapachu na Kingunge Ngoimbale-Mwiru.

Wengine ni Ezekiel Maige, Dk Hadji Mponda, Dk Teresa Huvisa, Shamsi Vuai Nahodha, Nazir Karamagi, Dk Mathayo David, Balozi Khamis Kagasheki, Profesa Anna Tibaijuka, Profesa Sospeter Muhongo, Dk Batilda Buriani, Joseph Mungai, Diodorus Kamala, Mohamed Seif Khatib, Mwantumu Mahiza, Profesa Peter Msola na Profesa David Mwakyusa, Philip Marmo na Dk Juma Ngasongwa.

Manaibu waziri ni Dk Luca Siyame, Balozi Seif Ally Idd, Hezekiah Chibulunje, Shamsa Mwangunga, Daniel Nsanzugwanko, Hezekiah Chibulunje, Rita Mlaki, Dk Charles Mlingwa, Zabein Mhita, Dk Athuman Mfutakamba, Dk Lucy Nkya, Goodluck Ole Medeye, Benedict Ole Nangoro, Gregory Teu, Philipo Mulugo, Mohamed Abood, Dk Aisha Kigoda, Omari Yusuf Mzee, Dk Maua Daftari, Zakia Meghji, Joel Bendera, Abdisalaam Issa Khatib na James Wanyancha, Gaudence Kayombo, Mudhihir Mudhihir.

Mawaziri waliofariki dunia katika kipindi hicho ni Salome Mbatia, Juma Akukweti, Jeremiah Sumari na Dk William Mgimwa.

Mwaka 2006

Katika baraza lake la kwanza Rais Kikwete aliteua mawaziri na naibu mawaziri 60 Januari 2006 na ilipofika Oktoba 2006, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya kwanza makubwa ya baraza lake la mawaziri kwa kuwahamisha vituo vya kazi mawaziri 10 na naibu mawaziri wanane. Katika mabadiliko hayo hakuna waziri aliyeachwa.

Mwaka 2007

Februari 2007, Rais Kikwete alifanya uteuzi wa mawaziri wawili na manaibu wawili. Alimteua Dk Buriani kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu) kujaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya kifo cha Akukweti. Ngeleja aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na Kayombo aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwekezaji.

Mwaka 2008

Februari 12, 2008 Rais Kikwete alivunja Baraza la Mawaziri baada ya kujiuzulu kwa Lowassa, Dk Msabaha na Karamagi. Nafasi zao zilizibwa na Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Kamala (Afrika Mashariki), huku Pinda akiteuliwa kuchukua nafasi ya Lowassa.

Mei 2008

Baada ya Chenge kujiuzulu Mei, 2008 kutokana na kashfa ya ununuzi wa rada na nafasi yake kujazwa na Mbunge wa Bagamoyo, Dk Kawambwa, Rais Kikwete pia alibadilisha mawaziri kadhaa.

Mwaka 2012

Rais Kikwete alifanya mabadiliko Mei 2012 kwa kuwaondoa Mkulo (Fedha), Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Maige (Maliasili na Utalii), Nundu (Uchukuzi) na Dk Chami (Viwanda na Biashara). Dk Mfutakamba (Naibu, Uchukuzi) na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Nkya.

Badala yao aliwateua Dk Mgimwa (Fedha), Balozi Kagasheki (Utalii), Dk Mwakyembe (Uchukuzi), Dk Kigoda (Viwanda na Biashara), Dk Mwinyi (Afya), Profesa Muhongo (Nishati na Madini), Dk Seif Rashid (Naibu, Afya) na George Simbachawene (Naibu, Nishati na Madini).

Manaibu wapya walioingia ni Makamba (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Dk Tzeba (Uchukuzi) na Makala (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo). Wengine ni Dk Mahenge (Maji), Masele (Nishati na Madini), Kairuki (Katiba na Sheria), Mbene na Mkuya (Fedha).

Januari 2014

Rais Kikwete alifanya mabadiliko mengine Januari 19, 2014 kwa kuteua mawaziri wapya wawili na naibu mawaziri wapya wanane, huku akiwapandisha vyeo manaibu mawaziri wanne kuwa mawaziri kamili.

Aliwapumzisha Dk Huvisa, Teu, Mulugo, Ole-Nangoro na Ole-Medeye.

Mabadiliko hayo yalikuwa yanalenga kujaza nafasi zilizoachwa na Balozi Kagasheki, Dk Nchimbi, Nahodha na Dk Mathayo waliotemwa Desemba 2013 kutokana na kashfa ya Operesheni Tokomeza na nafasi ya Dk Mgimwa, aliyefariki dunia kutokana na maradhi.

Mawaziri wapya walioteuliwa wakati huo ni Dk Migiro, Dk Kamani, Nchemba, Dk Kebwe, Mhagama, Dk Chana, Telele, Zambi, Nkamia na Mgimwa.

Waliopandishwa kuwa mawaziri ni Mkuya, Nyalandu, Dk Rashidi, Dk Mahenge na Dk Mwinyi aliyehamishwa kutoka Afya na Ustawi wa Jamii kwenda Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na wengine kadhaa walihamishwa.

Januari 2015

Rais alifanya mabadiliko yake yanayoweza kuwa ya mwisho Januari 2015, akijaza nafasi zilizoachwa wazi na mawaziri wawili, Profesa Tibaijuka (kufutwa kazi) na Profesa Muhongo kujiuzulu kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Tegeta Escrow.

Walioingia ni manaibu waziri wawili, Mwijage (Nishati na Madini) na Kilango- Malecela (Elimu na Mafunzo ya Ufundi), huku wengine wakihamishwa.

Taarifa ya TCRA kuhusu muingiliano wa masafa ya EATV na ITV via kingamuzi cha Star Media

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
ISO 9001: 2008 CERTIFIED
TAARIFA KWA UMMA

KUHUSU MUINGILIANO WA MASAFA YA EATV NA ITV KUPITIA KING’AMUZI CHA KAMPUNI YA STAR MEDIA KATIKA KITUO CHA KUSAMBAZA MATANGAZO MAKONGO JUU
  1. UTANGULIZI
  1. Masafa ni rasilimali muhimu katika shughuli za Mawasiliano (simu, wavuti, redio, na utangazaji). Masafa ya Mawasiliano (Spectrum) hugawanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) (ikitambuliwa hapa kama Mamlaka) kwa kutoa leseni kwa watoa huduma za mawasiliano nchini kwa mujibu wa sheria na masharti ya leseni. Moja ya kazi za Mamlaka ni pamoja na kupokea na kusuluhisha matatizo ya muingiliano wa masafa kati ya watoa huduma mbalimbali wa mawasiliano kwa kutumia ujuzi na wataalamu na teknolojia ya mitambo maalumu na mahususi ya kisayansi kufanya kazi hiyo. Kazi hizi zimeainishwa katika Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano ya 2003 (TCRA Act of 2003) na Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Electronic and Postal Communications Act (EPOCA) ya mwaka 2010.
  2. Mnamo tarehe 29 Januari 2015, Mamlaka ilipokea malalamiko kuhusu ubora wa matangazo ya vituo vya ITV na EATV yanayorushwa na Kampuni ya Star Media (T) Limited ambaye ni msambaza matangazo ya dijitali. ITV na EATV wana leseni ya Maudhui (Content Service Lisence) na Star Media wana leseni ya Miundombinu ya Utangazaji (Network Facility License as a signal distributor) kutoka TCRA. Leseni zote za Mamlaka zina masharti ya kuzingatia.
  3. Huduma za Mawasiliano hutumia bendi ya masafa tofauti (Spectrum bands). Huduma za mawasiliano ya setilaiti (satellite) hutumia bendi 3.4 mpaka 4.2 GHz, inayofahamika kama C-Band. Ifahamike kuwa masafa ya setilaiti ya kupokea matangazo (satellite downlink frequency) ya 3.644 GHz yanatumika kupokea matangazo kutoka satelaiti ya Intelsat 906 (TP 10) kwa matangazo ya vituo vya utangazaji nchini kupitia mfumo wa dijitali ambao mitambo yake iko katika kilima cha Makongo Juu area. Hata hivyo, sehemu nyingi duniani, ikiwemo Tanzania, hutumia teknolojia ya WiMAX katika bendi 3.5 GHz. Masafa haya yanafahamika duniani kote kwa uwezo wake wa kutumika kiteknolojia kati ya mfumo wa “Fixed Satellite Services (FSS)” na IMT kama vile mwendo kazi wa intaneti bila waya (Broadband Wireless Access (BWA) transmission) ikiwemopia teknolojia ya WiMAX.
4.     Kufuatia malalamiko yaliyopokelewa na Mamlaka, TCRA iliteua timu ya wataalamu Wahandisi wa Masafa kufanya uchunguzi ili kubaini tatizo la muingiliano wa masafa yaliyosababisha ITV na EATV kutokuonekana vizuri katika king’amuzi cha Star Media, kwa kutumia utaratibu na jinsi sheria zinavyoelekeza. Timu hiyo ya wataalamu wa masafa iliwasiliana na Star Media na kutembelea eneo la Makongo Juu kwenye mitambo yao ili kubaini aina ya muingiliano, muda wa muingiliano na maeneo husika. Timu hiyo ilifanya uchunguzi kwa kutumia vifaa maalumu kwenye eneo lenye mitambo ya kurusha matangazo ili kubaini muingiliano wa masafa kupitia watoa huduma wa intarneti za mwendo kasi kupitia teknolojia ya WiMAX katika bendi 3.4 – 3.6 GHz. Aidha timu ilifanya tathmini ya vipimo vya matumizi ya masafa na watoa huduma katika bendi nzima ya C- ya kupokelea matangazo (downlink frequency) kutoka 3.4 GHz hadi 4.2 GHz.

B.   MATOKEO YA UCHUNGUZI NA YALIYOJITOKEZA

5.     Baada ya uchunguzi huo wa kitaalamu kwa kutumia vifaa maalumu vya teknolojia ya sayansi ya masafa, timu ya wataalamu walibaini kuwa muingiliano wa masafa ulikuwa unatokea kati ya saa 12 jioni hadi saa 6 usiku. Uchunguzi katika eneo la urushaji wa matangazo na mitambo ya Star Media ulibaini kuwa muingiliano ulikuwa katika mfumo wake wa kupokea matangazo (satellite receiver station) iliyoko kwenye eneo (S 06 45’ 736 E 3912’ 632). Mfumo wa kupokea (Low Noise Block down converter - LNB) kutoka bendi 3.4 GHz to 4.2 GHz. Matokeo ya uchunguzi wa masafa ya bendi 3.644 GHz hayakuonesha aina yeyote ya muingiliano. Aidha masafa ya 3.4 GHz hadi 3.6 GHz yalionesha matumizi mbalimbali kutoka masafa ya bendi 3.5 GHz ambayo yanatumika na watoa huduma wanaotumia teknolojia ya WiMAX.

6.     Kutokana na matokeo ya uchunguzi kama ilivyoelezwa katika no 5, ilibainika wazi kuwa hakukuwa na muingiliano katika bendi hiyo (In-band interference) kutoka katika mfumo wa matumizi ya inteneti ya mwendo kasi kwani masafa yote katika mifumo yote ya utoaji huduma haikuonesha muingiliano. Vile vile ilithibitika wazi kuwa hakukuwa na muingiliano katika mfumo huo (out-of-band emissions) Mfumo wa huduma wa mwendo kasi wa inteneti unaotumia masafa ya bendi 3.5 GHz huweza kusababisha muingiliano kwa mtoa huduma anayetumia bendi 3.6 – 4.2 GHz (FSS stations).

7.     Matokeo ya vipimo vilionesha kuwa eneo la Makongo Juu hupokea mawimbi ya Mawasiliano kutoka kwa watoa huduma wote wanaotumia masafa ya 3.5 GHz kutoka meneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kutokana na eneo la Makongo kuwa juu. Hali hii inaweza kusababisha mawimbi ya mwendo kasi wa intaneti katika masafa 3.5 GHzkuibebesha mzigo mkubwa mtambo wa kupokea matangazo ya utangazaji (FSS stations) anayetumia bendi 3.4 – 4.2 GHz kama hakuna wigo wa kuzuia muingiliano kiteknolojia (band pass filter) au mfumo bendi mwembamba (narrow band LNBs).

C.   KUTATULIWA KWA MUINGILIANO WA MASAFA

8.     Kutokana na vielelezo vya matokeo ya uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa masafa kwa kutumia vifaa maalumu, Mamlaka ilitoa maelekezo kwa Star Media ili kutatua tatizo la muingiliano uliokuwepo katika mtambo wake wa urushaji matangazo Makongo Juu. Kwanza, kutumia kifaa kiitwacho IF attenuator/filter katika mitambo yake ya kupokelea mawasiliano ya matangazo ya setilaiti (FSS receiving station); Kutumia LNB converter katika bendi ya masafa 3.7 – 4.2 GHz badala ya kutumia masafa ya (C-band) yote (3.4 – 4.2 GHz); hata hivyo, masafa 3.664 GHz yamehifadhiwa kama wigo unaozuia matumizi kati ya watumiaji wa matangazo ya mitambo iliyosimikwa juu ya ardhi (Terrestrial) - (3.4-3.6 GHz) na yale ya wanaotumia Satelaiti ya kupokelea matangazo (3.7-4.2 GHz). Pili, Mamlaka ingeagiza watoaji wa inteneti ya mwendo kasi katika mitambo yao (BWA) kuwa na nafasi ya kutosha kati ya mitambo ya “FSS” na kufuata utaratibu uliowekwa kulingana na matumizi ya masafa, ikizingatiwa kwamba mawimbi yaliyo mengi katika eneo la Makongo Juu hupokelewa kutoka sehemu mbalimbali kutoka Jiji la Dar es salaam. Tatu, njia mbadala zitumike katika kupokea matangazo ya utangazaji katika kilima cha Makongo Juu kama vile teknolojia ya Mkongo wa Mawasiliano (fiber optic) satelaiti kutumia mfumo wa bendi ya Ku-Satellite band, au “microwave links”.

9.     Baada ya Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kufanya uchunguzi wa kitaalamu kwa kutumia vifaa maalumu vya sayansi na teknolojia mahususi kwa matatizo ya muingiliano wa masafa, imebainika pasina shaka kuwa hakukuwa na hujuma yeyote kutoka kwa Kampuni ya Star Media au kufanya kwa makusudi kwa nia ya  kuharibu muonekana wa vituo husika vya ITV na EATV katika ving’amuzi vyake. Tatizo lilikuwa ni la kisayansi na kiteknolojia ambalo hutokea mara nyingi katika huduma za Mawasiliano kote duniani, na tatizo hilo limemalizika kwa kutumia njia za kisayansi na kiteknolojia kwa watoa huduma wote kwa kushirikiana na Mamlaka..

10.Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) inapenda kutumia fursa hii kuwakumbusha watoa huduma wote wenye leseni za Mamlaka kuwa inapotokea matatizo au malalamiko, basi wafuate taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria na masharti ya leseni pamoja na kanuni zake ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa TCRA na kutoa ushirikiano katika kutatua tatizo husika kupitia sayansi na teknolojia ambayo hutumika katika kutoa huduma za mawasiliano.

Kwa taarifa zaidi tafadhali wasiliana nasi kupitia [email protected]

Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
 5th February 2015

Rambirambi za Spika kwa misiba ya Mama wa Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa na Jaji Mstaafu

Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Anne Semamba Makinda (Mb), kwa niaba ya Bunge la Jamhuri ya Muungao wa Tanzania anatuma salaamu za rambirambi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Bwana Othman Rashid, kufuatia kifo cha mama yake mzazi, BI. TAJIRI ABDALLAH KITENGE, kilichotokea tarehe 5 Februari, 2015.

Aidha, Spika Makinda anatuma salaamu za rambirambi kwa Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Augustino Ramadhani kufuatia kifo cha mama yake mzazi, BI. BRIDGET RAMADHAN, kilichotokea Februari 3, 2015.

“Nimepokea taarifa za misiba hii kwa masikitiko makubwa na ninawapa pole familia, ndugu, jamaa na marafiki wote. Ninamwomba Mwenyezi Mungu awape faraja wafiwa katika kipindi hiki kigumu.

BWANA alitoa na BWANA ametwaa, Jina la BWANA lihimidiwe. Amina.”

Imetolewa na Ofisi ya Bunge,
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na
Uhusiano wa Kimataifa

DODOMA

Aliyebuni logo aomba namna ya kuonana na Mwenyekiti wa Wakfu ya WAMA

Nimekumbuka nilichora logo ya Wakfu ya WAMA WAMA FOUNDATION : WOMEN AND DEVELOPMENT wakati inaanzishwa. Wakati nimeombwa kuchora (na aliyepewa tenda) nilikabidhi kama michoro 5 hivi kama sampuli, mingine toka kwa watu wengine. Baada ya kupita muda nikaona mchoro mmoja niliochora mimi unatumika ila umeongezwa ile riboni nyekundu tu. Nikashangaa, nikamuuliza niliyempa michoro (nadhani ilikuwa 2007/2008), hakunijibu. Miaka ikapita, miaka ikapita. Mwaka 2013 nikamwomba tena niliyempa michoro yangu anirudishie angalao michoro yangu ya awali. Kimya, miaka ikapita, miaka ikapita, leo ni 2015!

Sasa ni saa za majeruhi, naomba msaada wa kuonana na Mwenyekiti wa WAMA ili angalao nimjulishe kuwa mimi ndie niliyechora logo ya wakfu yake

Mwenye kujua njia rahisi ya kukutana Mheshimiwa Mwenyekiti bila urasimu wa "wewe ni nani, una shida gani, njoo kesho, rudi kesho kutwa" anisaidie

Vicensia Shule 

Rais Kikwete ahudhuria maziko ya mama wa Jaji Mstaafu, Mchungaji Agustino RamadhaniRais Jakaya Mrisho Kikwete na Mama Salma Kikwete wakitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu Bibi Bridget Ramadhani, Mama Mzazi wa Jaji Augustino Ramadhani, wakati wa mazishi Ijumaa Februari 6, 2015 huko Kimara King'ongo jijini Dar es Salaam.Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mama Salma Kikwete wakijumuika wa waomboilezaji wengine katika mazishi ya Marehemu Bibi Bridget Ramadhani, mama Mzazi wa Jaji Augustino Ramadhani, wakati wa mazishi Ijumaa Februari 6, 2015 huko Kimara King'ongo jijini Dar es Salaam.Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mama Salma Kikwete wakiweka udongo kwenye kaburi la Marehemu Bibi Bridget Ramadhani, mama Mzazi wa Jaji Augustino Ramadhani, wakati wa mazishi Ijumaa Februari 6, 2015 huko Kimara King'ongo jijini Dar es Salaam.Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mama Salma Kikwete wakiweka shada kwenye kaburi la Marehemu Bibi Bridget Ramadhani, mama Mzazi wa Jaji Augustino Ramadhani, wakati wa mazishi Ijumaa Februari 6, 2015 huko Kimara King'ongo jijini Dar es Salaam.

Picha: IKULU