Mgogoro wa ardhi Makuyuni na Lotima, Kilimanjaro

KUNA kila dalili ya kuibuka mgogoro mkubwa wa kugombea ardhi kati ya uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini na wananchi wa vijiji vya Makuyuni na Lotima, mkoani Kilimanajaro.

Habari zinasema mgogoro huo unaodaiwa kutishia amani katika vijiji hivyo, umetokana na hatua ya uongozi wa halmashauri hiyo kumega sehemu ya ardhi ya vijiji hivyo bila kuushirikisha uongozi wa vijiji hivyo pamoja na wananchi wao.

Kwa mujibu wa habari hizo, wananchi wa vijiji hivyo vya Makuyuni na Lotima wako katika hatari ya kuingia katika machafuko ya amani endapo Serikali Kuu haitaingilia kati kuzuia mpango huo wa halmashauri unaolenga kumega ardhi yao kwa ajili ya kupima viwanja vya makazi katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Himo.

Mmoja wa wananchi wanaotishiwa kuathirika na mpango huo, Yohana Sawaki, anasema tangu wapokee taarifa hiyo kutoka uongozi wa halmashauri yao Desemba mwaka jana, kumekuwepo na hali tete inayotishia kuleta machafuko na uvunjifu wa amani.

Kwa mujibu wa Samaki, kitu ambacho wananchi wa eneo hilo wanapinga, ni hatua ya halmashauri ya Moshi Vijijini kutaka kupokonya maeneo ya ardhi na pia kutaka kuwaingiza katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Himo.

Baadhi ya maeneo yanayodaiwa kumegwa na uongozi wa halmashauri hiyo, ni pamoja na maeneo ya kilimo na malisho ya mifugo yao, hatua itakayowafanya wananchi hao wakose maeneo ya kilimo na malisho.

Mwanakijiji mwingine, Paulo Petro, anasema wanacholalamikia wao ni utaratibu uliotumika katika zoezi hilo, huku akiwatupia lawama baadhi ya viongozi wa serikali ya vijiji vyao waliochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba mwaka jana, kwamba wameshiriki kwa kiasi kikubwa katika njama hizo za kutaka kuwapora ardhi yao pasipo kuwashirikisha.

Kwa upande wao viongozi wa Serikali za Vijiji wameeleza kusikitishwa na jazba za wananchi hao, ambapo walipotakiwa kutolea ufafanuzi wa malalamiko hayo walikataa kata kata kutokana na kile walichosema wao sio wazungumzaji katika sakata hilo.

Akizungumzia malalamiko hayo ya wananchi wa vijiji vya Makuyuni na Lotima, Mkurugenzi wa Halamshauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini, Fulgence Mponji, anasema sheria na kanuni zilifuatwa katika kufikia uamuzi wa kupandisha hadhi mji mdogo wa Himo.

Juhudi za kumtafuta Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Moshi, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga, ili pamoja na mambo mengine, atolee ufafanuzi suala hilo, bado zinaendelea.

Utata kuhusu majengo ya CCM: Kilimanjaro wachoma moto ofisi baada ya agizo la Mkuu wa Mkoa

WANANCHI wa kijiji cha Aleni wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro, wamevamia jengo la ofisi ya idara ya kilimo na umwagiliaji na kisha kulichoma moto kupinga kuondolewa kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho kwenye jengo la Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuhamia kwenye jengo la idara hiyo.

Kuchomwa kwa jengo hilo kumekuja baada ya kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro aliyoitoa hivi karibuni kupiga marufuku viongozi wa Serikali za Mitaa wanaoishi kwenye nyumba zinazomilikiwa na CCM.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Rombo, Elinas Pallangyo, alisema tukio la kuchomwa moto kwa jengo hilo limetokea baada ya Mwenyekiti wa Kijiji hicho kuagizwa kuondoka kwenye jengo la CCM na kuhamia kwenye jengo la idara ya kilimo.

Alisema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Februari 9 mwaka huu ambapo wananchi hao wanadai majengo ya CCM ni mali ya wananchi kwani yalijengwa kwa michago ya wananchi na si chama.

Alifafanua kuwa ofisi hiyo imeteketea pamoja na mali zote ambapo mpaka sasa thamani halisi haijajulikana na jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini wahusika.

  • Kija Elias, Rombo

Kitime asimulia: Mbongo kupanda ndege ni ishu ya kiukoo


Kupanda ndege sio mchezo ndugu yangu, kwanza ukianza kufikiria katika ukoo wenu watu wangapi wamepanda ndege, ni wachache unaweza hata kuwataja kwa majina na tarehe ambazo walipanda ndege. Kuna wimbo wa kikwetu unamsifu jamaa mmoja toka kijijini kwetu aliyewahi kusafiri na ndege na kutua salama, na hii ni moja ya sifa ambazo ndugu wa ukoo wa jamaa yule huzitaja kama moja ya mafanikio makuu katika ukoo wao kila wanapokuwa wamelewa.

Kwa kawaida Mbongo akiambiwa atasafiri kwa ndege, hasa ikiwa kwa mara ya kwanza, kuna mambo ya msingi ambayo lazima ayafanye. Baada ya kuhakikishiwa safari ni lazima awataarifu ndugu na jamaa , na anaweza kupiga simu mpaka kwa wazazi wake kuwataarifu kuwa atapanda ndege. Zoezi hili huwa na sababu mbili kubwa kwanza ni kuonyesha furaha ya kwa kupanda ndege na kutaka wazazi wao na ndugu kujua kuna mwenzao hatimae kafanikiwa kupanda ndege. Sababu ya pili ni uwoga, unajua kupaa hewani kunatisha, na ukizingatia kila siku tunaona picha za ndege zimeanguka basi kupaa hewani kunatisha sana, sasa inakuwa vema kutoa taarifa kwa ndugu na kuomba wakuombee ufike salama uendako.

Baada ya kutoa taarifa kinachofuata ni shopping, hapo lazima mswahili akanunue nguo mpya za kupandia ndege, hata kama safari yenyewe ni ile ya saa mbili tu, kutoka Mwanza kwenda Dar, mtu atagharamia suti mpya, shati na tai, viatu soksi nyeupe na bila kusahau san gogoz. Sanduku jipya na hapo anakuwa tayari kupanda ndege.

Usiku wa kuamkia siku ya kupanda ndege, Mbongo halali, usingizi hauji, kila akiwaza kupaa angani haamini, na kingine ni woga kuwa akilala atapitiliza na kuchelewa ndege. Alfajiri saa kumi na moja inamkuta msafiri wetu kisha amka na anaoga, japo ndege itaondoka saa tisa mchana. Siku hiyo ataoga maji ndoo tatu, maji yakiisha anaongeza tena, nyimbo nyingi za furaha, zile za bafuni, utamsikia anaimba ule wimbo wa Tancut Almasi,’Ninakwenda safari safari yenyewe ya masafa marefuuu’. Bafuni kunakuwa raha tupu. Kufikia saa moja asubuhi kisha kunywa chai, tayari kwa safari ya saa tisa mchana, mwenyewe kisha pendeza na suti na tai.

Unajua Mbongo kama anaenda safari kwa basi huwa hana makuu, ataita Bodaboda au Kibajaji apelekwe kituo cha Mabasi, lakini ishu hapa ni kuwa anasafiri na ndege, hivyo itaitwa taxi impelekee mapema uwanja wa ndege, saa nne mbongo yuko tayari uwanja wa ndege.

Baada ya masaa kadhaa kwenye viti vya kusubiria safari, presha inampanda, presha inamshuka, maana ule muda wa kupanda ndege kwa mara ya kwanza katika maisha yake unakaribia. Na utakuta kichwani kishajipangia akiingia tu kwenye ndege atakimbilia kiti cha dirishani, hii itasidia kwanza ataweza kuchungulia nje kuangalia madhari ya miji mbalimbali akiwa hewani, na pili kama kwa bahati mbaya atajisikia kichefuchefu hatasumbua mtu, atafungua tu dirisha na kujisaidia kirahisi unaonae.

Wakati mawazo haya yakiendelea, presha ya msafiri wetu ikapanda ghafla aliposikia, ‘Tangazo, tangazo wale abiria wa kwenda Mwanza tafadhali sogeeni kwenye dirisha la kampuni ya ndege yetu kwa maelezo zaidi’ Jasho likiwa limashamtoka sana kutokana na kuvaa suti na tai kwenye joto, akaelekea kule walikokuwa wanaelekea wengi. Pale wanamkuta binti mmoja kavaa vizuri, analiambia lile kundi la wasafiri, kwa sauti iliyoonyesha kuwa japo anaonekana kama mswahili mwenzetu lakini kuna uwezekano mkubwa kuwa mmoja ya wazazi wake ni Mmarekani ‘Abiria wetu samahani kwa ntakalowaambia, nimetumwa na menejiment ya uongozi wa kampanu yetu niwaambie kuwa bekozi kutokana na matatizo ya kiufundi ambayo ni tekniko, kwenye ndege yetu, safari yenu imeahirishwa mpaka kesho saa kumi na mbili alfajiri……we are vere vere sori, lakini hii ni wa ajili ya usalama wenu nyinyi abiria wetu ambao ndio wafalme.’

Tembelea blogu ya Kitime www.johnkitime.co.tz kwa simulizi zaidi.

Nyota wa soka duniani Kluivert na Rayco Garcia walikutana na Stand United, Shinyanga

Wachezaji wa Stand United wakiwasili Uwanjani

Mji wa Shinyanga jioni ya jana ulitekwa na kocha namba mbili wa timu ya taifa ya Uholanzi 2014 ambye pia alikuwa mchezaji gwiji na nyota wa Ajax Amsterdam, Barcelona ya Hispania na New Castle ya Uingereza, Patrick Kluivert bingwa wa mipira ya vichwa aliyekuwa ameambatana na na gwiji wa zamani wa Barcelona na Real Madrid Rayco Garcia ambaye ni Scout wa Real Madrid kwa kukutana na wachezaji wa Timu ya Stand United ya Shinyanga pamoja na mashabiki wa soka kutoka ndani na nje ya mkoa huo katika kiwanja cha CCM Kambarage.

Tukio zima limefanikiwa chini ya udhamini wa mbunge wa Shinyanga mjini mheshimiwa Stephen Masele ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia Muungano na Mazingira.

Lengo ni kusaka vipaji vya soka kwa ajili ya kucheza ligi za Ulaya, kukuza michezo na kuitangaza Shinyanga nje ya mipaka ya nchi.Kushoto ni Patrick Kluivert akipokelewa uwanjani.


Patrick Kluivert akisalimiana na wapenzi wa soka mkoa wa Shinyanga wakati akipanda jukwaa kuu


Kulia ni Patrick Kluivert akifuatilia mazoezi yaliyokuwa yanafanya na wachezaji wa Stand United katika uwanja wa CCM Kambarage kabla ya kuongea nao na kuwapa siri ya mafanikio katika soka ili waweze kucheza ligi za ulaya
Patrick Kluivert akitoa maelekezo kwa wachezaji wa Stand United wakati wa zoezi maalum jioni ya leo lengo ni kuwanoa ili wawe tishio ndani na nje ya Tanzania


Wa kwanza kushoto ni afisa Habari wa Stand United Isaack Edward akifuatiwa na mkurugenzi wa Malunde1 blog,ndugu Kadama Malunde wakiwa na Patrick Kluivert wakifuatilia zoezi maalum la wachezaji wa Stand unitedMbunge wa Shinyanga mjini Stephen Masele akiwakaribisha magwiji wa soka ili wazungumze na mashabiki wa soka .


Patrick Kluivert akizungumza na wakazi wa Shinyanga ambapo alisema anataka kuisaidia timu ya Stand United ili iweze kupeleka wachezaji wake kucheza mechi za nje ya nchi.

Orodha ya waliosamehewa kodi Tanzania: Benki yafutiwa hadi kodi "toilet paper"; TRA yajisamehe kodi ya viburudisho...

ORODHA ya walipa kodi wakubwa ambao serikali imewasamehe kodi kwa kipindi cha kati ya Januari 2010 hadi Septemba 2014 imewekwa hadharani, huku matumizi mabaya ya misamaha yakionekana. Baadhi ya makampuni na taasisi hizo yamepewa misamaha hadi ya vitu vya kawaida kama karatasi za kutumia chooni, jambo ambalo linazua maswali kuhusu misamaha hiyo.

Wizara ya Fedha imetoa taarifa hiyo kupitia katika tovuti yake, kutokana na maagizo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuitaka kufanya hivyo, ingawa juzi Jumatatu mtandao ulikuwa umezuiwa kuonyesha taarifa hizo kwa sababu ambazo hazijajulikana. 

Zaidi ya makampuni hayo makubwa kwa kulipa kodi, wizara hiyo ilitakiwa pia kuweka hadharani majina ya watu binafsi na taasisi nyingine ambazo zilifaidika na misamaha hiyo katika kipindi hicho. Katika orodha hiyo ambayo Raia Mwema imefanikiwa kuiona, makampuni ya kuchimba madini, ya kutafuta mafuta, mabenki mbalimbali ikiwamo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Majeshi na Idara mbalimbali za serikali ndiyo walionekana kuwa wanufaikaji wakubwa wa misamaha hiyo. Namba kodi inayosamehewa kwa mujibu wa taarifa ya TRA, kiasi cha shilingi trilioni 1.4 kilisamehewa kulipwa kodi katika mwaka uliopita wa fedha, jambo ambalo lilionekana kuichukiza kamati ya PAC.

Taarifa ya Wizara ya Fedha (MoF) imetoa mwanga wa machache ambayo Raia Mwema imeweza kuyabaini.  Katika ukurasa wa arobaini wa taarifa ya wizara, kuna taarifa za benki ya M (Bank M) ya jijini Dar es Salaam kupewa msamaha wa kodi kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa za kutumia chooni. Zaidi ya bidhaa hizo za chooni, benki hiyo pia iliomba msamaha wa vitu kama tarazi (tiles) na tranfoma. BoT iliomba na kupewa msamaha wa kodi wa vitu kama note book, sare za wafanyakazi, ukarabati wa redio, manunuzi ya kadi za mwaliko na huduma za mwaliko. 

TRA yenyewe ilijiombea na kujipa msamaha kwa ajili ya viburudisho na chakula ambacho walikula katika mojawapo ya mikutano yao. 

Kulikuwa na misamaha mingi pia katika eneo la vinywaji kwa majeshi ambapo soda, bia na vinywaji vikali peke yake viliweza kusamehewa kodi ya zaidi ya shilingi bilioni mbili katika kipindi hicho. 

Kampuni isiyofahamika sana ya Aurum Africa imepewa msamaha wa zaidi ya shilingi milioni 220 kwa ajili ya kuuza dhahabu ghafi (raw gold). 

Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu, pamoja na mambo mengine umeonekana pia kuomba msamaha na kupewa wa samani (furnitures) za ofisini pamoja na ununuzi wa mashati na suruali. 

Mwaka 2012, Benki ya FBME ambayo kwa sasa iko chini ya usimamizi wa serikali, ilipewa msamaha wa kodi wa kiasi cha shilingi milioni 76 kwa ajili ya ununuzi wa samani za ofisini. 

Ingawa baadhi ya misamaha ina thamani ndogo kifedha, lakini Raia Mwema imeamua kuionyesha si kwa sababu ya thamani yake bali kutokana na matumizi mabaya ya fursa hii ya misamaha. Katika orodha hiyo ambayo juzi haikufunguka kwenye mtandao na bado sababu za kuzuiwa kufunguka hazijawekwa hadharani, makampuni yaliyopewa misamaha mikubwa zaidi ni yale yanayojihusisha na uchimbaji madini na gesi. 

StatOil pekee kwa mfano, imepata misamaha tofauti yenye thamani ya shilingi bilioni tatu, bilioni 12, bilioni nne na bilioni tano kwa sababu tofauti kutokana na matumizi yake ya vifaa vya kuchimba baharini, ukodishaji wa helikopta na matumizi mengine. 

Taasisi ambazo zimetajwa katika taarifa hiyo ya Wizara ya Fedha ni Swissport, Mfuko wa PPF, Kundi la Kampuni za Bakhresa, Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli, ABG Exploration, Bomba la Mafuta la Tanzania na Zambia (TAZAMA) na Diamond Trust Bank. 

Makampuni mengine yaliyotajwa ni Kundi la Kampuni za Namera, Benki ya NMB, Jeshi la Magereza, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wakala wa Ujenzi wa Barabara (Tanroads), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Dawasco, Dawasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Takukuru na Kiwanda cha Nguo cha NIDA, Jeshi la Polisi, Mantra Tanzania, StatOil, Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Mradi wa MCC, Petrobas, BG Tanzania, TANESCO, Aurum Africa Limited, African Banking Corporation, AlphaKrust, APM Gold, Bank M, Barrick, BG Tanzania, Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu na Camel Oil. 

Wafaidikaji wengine wa misamaha hiyo ya serikali ni China Geo-Engineering, Commercial Bank of Africa (CBA), Stanbic, Resolute, East Coast Oil and Fats Limited, Ecobank Tanzania, Estim Construction, Etablissement Maurel Et Prom na Ets Maurel et Prom. 

Wengine ni Benki ya FBME, Highland Estate, HTT Infraco LTD, I&M Bank Ltd, Kagera Sugar, Mfuko wa LAPF, Leopard Tours, Mtibwa Sugar, Mufindi Papers, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Shirika la Taifa ya Nyumba (NHC), Mfuko wa NSSF, Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Oilcom, Ophir East Africa, Pangea Minerals na Precision Air Services.


Mkapa, Mwinyi ‘waguswa’ na “SwissLeaks”; Waziri asema "Si kosa Watanzania kuweka fedha Uswisi"


91 client accounts opened between 1982 and 2006 and linked to 286 bank accounts. 
(source: www.icij.org)

UTARATIBU wa Watanzania kwenda kuhifadhi fedha katika mabenki ya Uswisi ulikithiri wakati wa utawala wa marais Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, imefahamika.

Picha za grafu na zilizotolewa na mtandao wa Umoja wa Waandishi wa Habari za Uchunguzi Duniani (CIJ) na ambazo Raia Mwema imefanikiwa kuziona zinaonyesha kwamba wateja wengi kutoka Tanzania walipeleka fedha zao Uswisi katika kipindi cha kati ya mwaka 1988 na 2007. 

Mwinyi alianza kuwa Rais wa Tanzania mwaka 1985 na kumaliza muda wake mwaka 1995 na Mkapa alianza mwaka huo na kumaliza awamu yake mwaka 2005. 

Mtandao huo, kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya duniani, vimeibua taarifa hizo kutoka katika benki maarufu ya HSBC iliyoko Uswisi na habari hizi ni sehemu ya kampeni kali ya kupambana na ufisadi. Mtandao huo tayari umeibuka na taarifa kwamba Watanzania 99 wamehifadhi kiasi cha dola za Marekani milioni 114 katika benki hiyo, huku wakiwa na jumla ya akaunti 286. Hadi kufikia juzi usiku, ni Mtanzania mmoja tu, Sailesh Vithlani, ndiye ambaye anajulikana kuwemo katika orodha hiyo ya watu 99. 

Lakini Raia Mwema limeahidiwa na vyanzo vyake kwamba litapatiwa majina ya Watanzania wengine 98 waliobaki. Taarifa hizo za uchunguzi ambazo zimepachikwa jina la “SwissLeaks” zinaonyesha kwamba katika kipindi cha kati ya mwaka 1982 ambapo ndipo taarifa hizi zimeanza kuvujishwa hadi mwaka 2006, wateja 91 kati ya 99 waliokuwa na akaunti Uswisi ndiyo walifungua kiasi hicho. Kwa maana hiyo, wateja wengine wanane walifungua akaunti zao katika kipindi cha kati ya mwaka 2006 na 2007. Mwezi Juni mwaka 2012, Benki Kuu ya Uswisi ilitoa taarifa iliyoeleza kwamba Watanzania wanahifadhi kiasi cha dola milioni 197 (zaidi ya Sh bilioni 313) katika akaunti mbalimbali nchini humo. 

Kwa taarifa za sasa za SwissLeaks, ina maana kwamba ukiondoa dola hizi zilizopo HSBC, kuna takribani dola nyingine milioni 83 katika benki nyingine tofauti nchini Uswisi. Hii ni kama walioziweka hawajaziongeza au kuziondoa kwenye akaunti zao tangu Junui 2012. Hata hivyo, mwaka juzi, gazeti hili lilibaini kwamba pamoja na ukweli kwamba Uswisi ndiko kunakosifiwa, Watanzania wamehifadhi fedha nyingi zaidi katika Visiwa vya Jersey vilivyo chini ya Himaya ya Waingereza kuliko za Uswisi. 

Gazeti liliwahi kuripoti kwamba fedha za Watanzania pekee zilizoko katika visiwa hivyo zinakadiriwa kufikia kiasi cha pauni za Uingereza milioni 413 (sawa na shilingi za Tanzania trilioni 1.06). Fedha hizo zinatosha kuhudumia bajeti za wizara za Afya, Mifugo na Uvuvi, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Wizara ya Afrika Mashariki kwa mwaka mzima bila ya kuomba fedha kutoka kwa wafadhili na bado ‘chenji’ ikabaki. 

Gazeti hili haliwezi kutaja chanzo cha habari hizi kwa vile taarifa hii ilipatikana katika mkutano uliofanyika Uingereza wiki iliyopita chini ya kanuni za Chatham (Chatham Rules) ambazo zinakataza kutaja vyanzo vya habari zilizopatikana kutoka katika mikutano inayotawaliwa na kanuni hizo. 

Kwa mujibu wa taarifa za uhakika zilizopatikana, Raia Mwema limeelezwa kwamba zaidi ya Jersey, kuna fedha nyingine nyingi katika visiwa vingine kama Cayman na Isle of Man ingawa pia kuna fedha zilizohifadhiwa jijini London, mji mkuu wa Uingereza. 

“Kuna watu binafsi ambao wamehifadhi fedha zao. Kuna fedha za kampuni kadhaa na kuna fedha za inayoitwa mifuko ya hisani. Naweza nikashindwa kuwapa majina haswa ya wenye fedha hizo lakini nadhani inawezekana kuwapa majina ya kampuni na mifuko hiyo ya hisani (trusts),” kilieleza chanzo hicho. 

Kisiwa hicho ni miongoni mwa nchi zinazopendwa na watu, kampuni au taasisi zinazokwepa kulipa kodi au zinazopata mapato yake kwa njia ya kifisadi kwa vile zinatoza kodi kidogo na zina sheria zinazolinda usiri wa walioweka mali zao. Mkutano huo ulielezwa kwamba visiwa hivyo vilivyo chini ya Uingereza lakini vinavyojitawala vyenyewe vimehifadhi kiasi cha pauni bilioni 40 kutoka Afrika na katika hizo, pauni milioni 413 zinatoka Tanzania. 

Visiwa vya Jersey vilijipatia umaarufu mkubwa nchini Tanzania miaka michache iliyopita baada ya kubainika kwamba aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania, Andrew Chenge, alikuwa na akaunti katika visiwa hivyo ambayo ndiyo iliyotumika kumwekea fedha (dola milioni moja) zinazodaiwa kutokana na mauzo ya rada ya kampuni ya BAE Systems kwa serikali ya Tanzania.


Mkuya: Siyo kosa Watanzania kuweka fedha Uswisi

99 clients are associated with Tanzania. 20% have a Tanzanian passport or nationality.
(source: www.icij.org)

Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, amesema siyo haramu kwa Watanzania kuweka fedha nje hivyo, Watanzania 99 waliotajwa kuwa na akaunti Uswisi haimaanishi wote wametorosha fedha.

Hata hivyo, amsema serikali inaangalia ripoti ya Swiss Leaks ili kuona uhalali wa akaunti hizo za siri.

“Sisi hatujaona kama ni kosa kwa Watanzania kuwekeza fedha zao kwenye mabenki ya nje na wala isionekane kama ni jambo haramu kabisa.

Kama serikali tungetamani wawekeze kwenye benki nchini ili kukuza sekta ya fedha lakini pia hatuwafungi kutowekeza nje,” alisema.

“Tunachofanya ni kuiangalia hiyo ripoti ili kujua ukweli wa taarifa hizo, lakini taarifa hiyo haimaanishi kwamba ni kosa kubwa kisheria kwa Mtanzania kuweka fedha nje,” alisema.

Mkuya alisisitiza kuwa hakuna shida yoyote kwa Watanzania kuweka fedha kwenye akaunti nje ya nchi.

Waziri Mkuya ameyasema hayo siku moja tu baada ya vyombo vya habari nchini kuripoti taarifa ya kuwapo vigogo 99 wa Tanzania kuficha mabilioni ya shilingi katika benki za Uswisi kutokana na ripoti ya mtandao wa Swiss Leaks chini ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi wa Kimataifa (ICIJ).

Taarifa ya Swiss Leaks iliyotolewa juzi Jumapili, inaonyesha kuwa vigogo hao wa Tanzania wana akaunti za siri zenye Dola za Marekani milioni 114 ambazo ni sawa na Sh. bilioni 199.6.

Msingi wa ripoti hiyo umetokana na aliyekuwa mfanyakazi wa benki ya kimataifa HSBC, Hervé Falciani, kuvujisha siri za akaunti za wateja baada ya kuacha kazi; na mwaka 2008, alivujisha siri za akaunti za siri za baadhi ya watumishi wa umma na wanasiasa kwa Serikali ya Ufaransa ambayo mamlaka za kodi nchini humo ilifanya uchunguzi na kuthibitisha.

Ripoti hiyo ya Swiss Leaks, inaeleza kuwa taarifa za kiuchunguzi kutoka benki ya HSBC nchini Uswisi zinaonyesha kuwa akaunti hizo zinahusishwa na baadhi ya wanasiasa, wafanyabiashara wakubwa na watumishi wa umma ambao wamejipatia utajiri wa siri unaotokana na kampuni hewa (offshore companies).

Meshack aanza kwa vitendo kampeni ya kupanda miti


Mjasiriamali Meshack Maganga ameanza rasmi kampeni ya kupanda miti. Hizi ni picha za kampeni hiyo akipanda miti kijijini kwao Kilangala - Sumbawanga.


The life-saving heart treatment that can kill you


Nd'o ishakuwa fasheni ya kuvalia koti?Augustino Ramadhani aanza kutajwa kwenye Urais Tanzania; Je yeye ni nani? Jaji, Brigedia, Jenerali, Kasisi

Augustino Ramadhani, Jaji, Brigedia, Jenerali, Kasisi
Augustino Ramadhani, Jaji, Brigedia, Jenerali, Kasisi

JAJI Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani, ambaye jina lake limeanza kutajwa kwenye kuwania Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ametajwa kutoa “mojawapo ya maamuzi ya hovyo kabisa” katika historia ya Mahakama hapa nchini, Raia Mwema linafahamu.

Hata hivyo, mwanasheria mkongwe na mmoja wa wanasiasa maarufu nchini, Mabere Marando, amemweleza Jaji Ramadhani kama mmoja wa wanasheria wazuri hapa nchini. 

Mahojiano na watu waliowahi kufanya naye kazi na usomaji wa nyaraka mbalimbali zinazomhusu Jaji huyo, umeonyesha jaji huyo anachukuliwa kwa namna tofauti katika tasnia ya sheria lakini kwenye jamii kwa ujumla uadilifu, uungwana na ucha Mungu wake unaelezwa kama sifa zake kuu. 

Jambo ambalo limeweka doa katika wasifu wa Ramadhani (70) ni kitendo chake cha kutoa hukumu ya suala la mgombea binafsi ambapo alisema suala hilo halipaswi kuamuliwa na Mahakama kwa vile ni la kisiasa na Bunge ndilo linatakiwa kusimamia suala hilo.

Jaji Ramadhani alikuwa kiongozi wa benchi la majaji saba wa Mahakama ya Rufani ambayo ilikaa kujadili kesi hiyo ya mgombea binafsi ambayo kwa mara ya kwanza ilifunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila mwaka 1993. Katika hukumu hiyo ya Juni 17, 2010, Jaji Ramadhani ambaye ndiye aliyeiandika alisema;

“Katika kesi hii, suala la mgombea binafsi linafaa kushughulikiwa na Bunge ambalo ndilo lenye mamlaka ya kisheria ya kubadili Katiba na si Mahakama. “Uamuzi wa ama kukubali au kukataa kuanzisha utaratibu wa mgombea binafsi katika chaguzi zote unategemea na mahitaji ya kila jamii kutokana na historia yake. Hivyo, suala la mgombea binafsi si la kisheria bali ni la kisiasa,” 
ilieleza hukumu hiyo. 

Akizungumzia kuhusu hukumu hiyo, mmoja wa mawakili maarufu hapa nchini, Alex Mgongolwa, alisema hukumu hiyo ya suala la mgombea binafsi inatajwa kuwa kama mojawapo ya hukumu za hovyo kabisa katika historia ya Mahakama hapa nchini.

“Mimi ukiniambia ninakumbuka nini kwenye uongozi wa Jaji Augustino Ramadhani kama Jaji Mkuu nitakwambia kuhusu hukumu yake ya mgombea binafsi. Ile ni hukumu ambayo imetia doa heshima yake,”
 alisema Mgongolwa. 

Majaji wengine ambao walishirikiana na Ramadhani kwenye hukumu hiyo ni Benard Luanda, Sauda Mjasiri, January Msoffe, Nathalia Kimaro, Eusebia Munuo na Mbarouk Salim Mbarouk Maamuzi hayo ya Mahakama ya Rufani yalikosolewa na wasomi wengi wa taaluma ya kisheria; ambapo mmoja wao, Profesa Gamaliel Mgongo Fimbo, alinukuliwa wakati huo akiuita ni “disaster” (maafa). 

Hata hivyo, aliyepigilia msumari wa mwisho kuhusu namna hukumu hiyo ilivyokuwa na mushkeli alikuwa ni Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta, ambaye miezi mitano baada ya hukumu hiyo kutoka alitoa maoni yake. Akizungumza katika Chuo Kikuu cha Ruaha Novemba 25 mwaka 2010, Samatta aliichambua huku hiyo kwa mapana, na kueleza kwamba imeipunguzia nguvu Mahakama na kuongeza nguvu kwa Bunge. Akiwasilisha mada iliyojulikana kwa jina la Judicial Protection of Democratic Values (Mahakama na Ulinzi wa Tunu za Demokrasia) ambayo Raia Mwema imefanikiwa kuona nakala yake, Samatta aliileza kesi hiyo ya mgombea binafsi kama “Mojawapo ya kesi muhimu zaidi za kikatiba katika historia ya Tanzania. Katika uamuzi wake huo, Mahakama ya Rufani imeliepa jukumu la Mahakama la kutafsiri sheria ambalo haliwezi kufanywa na chombo kingine chochote isipokuwa chenyewe.

“Suala la mgombea binafsi linagusa haki za msingi za wananchi. Haki ya kugombea, kama zilivyo haki nyingine za msingi, ni haki ambayo Mtanzania anazaliwa nayo na hawezi kunyang’anywa labda kwa sababu ambazo zimeelezwa kwenye Katiba,” 
aliandika Samatta. 

Kwenye maelezo ya kesi hiyo, Jaji Ramadhani aliunga mkono maelezo ya mmoja wa marafiki wa Mahakama, Profesa Palamagamba Kabudi, aliyenukuu maelezo ya Profesa Conrad wa Ujerumani, kuwa “ hakuna hitimisho hadi sasa la wapi zinapoishia haki za msingi”. 

Samatta alifafanua kwamba Ramadhani na Kabudi hawakufafanua vizuri kuhusu maelezo hayo ya Conrad kwa vile yamefafanuliwa vizuri katika baadhi ya hukumu za kikatiba zilizoamuliwa nchini India na ambazo alizinukuu katika maelezo yake. Katika mojawapo ya nukuu kuntu katika hukumu ya Jaji Ramadhani, kwa kufuata ushauri huo wa Kabudi na Conrad, Mahakama ya Rufani ilihoji; “ Suala hili la kudai haki za msingi litaishia wapi? Leo wanadai mgombea binafsi, kesho watadai nini?” 

Jaji Samatta ambaye wanasheria wanamsifu kama mojawapo ya majaji wakuu wanaoheshimika alijibu hoja hiyo kwa kusema;

“ Madai yataisha pale haki zote za msingi zitakapokuwa zimepatikana. Huwezi kumnyima mtu haki kwa madai kwamba akipewa haki hiyo, atadai na nyingine”. 

Akimnukuu mojawapo ya majaji maarufu wa Ghana, Jaji Kayode, Samatta aliandika; “If floodgates it entails, let there be one, once it is a matter of fundamental right(Kama hili litasababisha mafuriko ya haki, basi na yaje tu ali mradi suala linahusu haki za msingi”. 

Akizungumzia hukumu hiyo, Marando alisema suala la mgombea binafsi linategemea na maoni ya mtu kwani wanaopendelea mgombea binafsi wanaweza kuwa na mtazamo tofauti na wasiopendelea suala hilo.

“Nimemfahamu Jaji Ramadhani kwa muda wa zaidi ya miaka 20. Ni mwanasheria mzuri sana. Hukumu zake nyingi zina maamuzi murua kabisa. “Hiyo ya mgombea binafsi inaweza kuwa isiwe kipenzi cha wengi lakini siwezi kuiita ya hovyo. Inategemea tu na mtazamo wa mtu kuhusu suala hilo,” 
alisema. 

Hata hivyo, mmoja wa viongozi wastaafu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) aliliambia Raia Mwema kwamba katika mojawapo ya mikutano ya kuagana aliyofanya na chama hicho, Jaji huyo alieleza kwamba uamuzi huo ulitokana na shinikizo walilopata kutoka serikalini hasa ikizingatiwa kuwa hukumu hiyo ilitolewa katika mwaka wa uchaguzi. 

Katika gazeti la Raia Mwema toleo lililopita, ilielezwa kwamba Jaji Ramadhani ameibuka kama mojawapo ya kete za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, kutokana na kuwa na sifa mahususi zinazohitajika, ingawa mwenyewe hajaonyesha nia. Sifa hizo ni uadilifu, uaminifu kwa chama na serikali, Uzanzibari wake, Ukristo na weledi wake; sifa ambazo inadaiwa baadhi ya wale ambao wanafahamika kutaka kumrithi Rais Jakaya Kikwete kutoka Tanzania Bara hawana kwa sasa. 

Mmoja wa waliokuwa wajumbe katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba walimweleza Jaji Ramadhani kama mtu aliyekuwa akipendelea muundo wa serikali mbili kama ilivyo sasa ingawa alikubaliana na mapendekezo ya Tume ya Serikali Tatu kwa sababu yalikuwa ni ya wananchi.

“Hii ndiyo sababu humuoni akizunguka mikoani au kwenye vyombo vya habari kupinga Katiba Inayopendekezwa kama baadhi ya wajumbe na Jaji Warioba mwenyewe wanavyofanya.
“Yeye anaamini kwamba kazi waliyotumwa na serikali wameimaliza ingawa pia hakufurahishwa na namna serikali ilivyowatendea wajumbe baada ya kumaliza shughuli za tume.
“Kama ukiniuliza nikutajie watu wawili waliokuwa waumini wa mfumo wa serikali mbili kindakindaki ndani ya Tume ya Jaji Warioba nitakutajia Jaji Ramadhani na Dk. Salim Ahmed Salim,” alisema mjumbe huyo. 

Jaji Ramadhani ndiye Mtanzania pekee aliyeweka rekodi ya kuacha kazi ya Ujaji Mkuu wa Zanzibar na kwenda vitani wakati wa Vita vya Kagera mwishoni mwa miaka ya 1970, ambapo alipigana vita hiyo kwa muda wa miezi kumi. Ni katika maisha yake hayo ya jeshini ndipo alipopanda cheo hadi kufikia kile cha Brigedia Jenerali ambacho ndicho alichostaafu akiwa nacho.

Msaada wa mawazo atimize ndoto yake ya "kuwa na ujuzi wa Medical"

Update:

Maoni kutoka kwa wachangiaji:

  1. Mwambie asome diploma pale Kibaha halafu ajiunge MUHAS/Kairuki/KCMC/ IFAKARA/BUCHS kusoma Udaktari
  2. Asubiri ikitangazwa mwezi wa tano aombe. Changamoto itakuwa alimaliza zamani. Kipaumbele ni kwa waliomaliza 2010 na kuendelea.
  3. Angekuwa ndugu yangu ningemshauri akomae huko aliko

Kuna mdau ametuma ujumbe ufuatao:

MIMI NILIMALIZA KIDATO CHA NNE 2007 NA KUPATA,PHYSICS D,BIOS D, CHEM C, B/MATH D, ENG C.NILIKUWA NA III 23 NIKAENDA UALIMU NA MPAKA SASA NAMALIZIA DEGREE YA ELIMU.NDOTO ZANGU NI KUWA NA UJUZI WA MEDICAL NAWEZA KUFANYA NINI ILI NIWEZE KUTIMIZA NDOTO ZANGU? NAOMBA USHAURI WENU.

Mengi kumzawadia milioni 10/= mshindi wa Wazo la Biashara la 3N


Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Mengi

Mshindi wa Januari 2015 wa shindano la wazo la biashara 3N anatarajiwa kutangazwa siku ya Alhamisi ya Februari 12 kuanzia saa tano asubuhi jijini Dar es salaam.

Kwa mujibu wa Dk. Reginald Mengi kupitia kurasa wake wa twitter, alitangazia umma kuwa Shindano hilo jipya lijulikanalo kwa kifupi -3N, ikiwa ni kifupisho cha ‘Nitabuni wazo la biashara, Nitatekeleza, na Nitafanikiwa’, ambapo mshindi wa kwanza wa mwezi Januari anatarajiwa kutangazwa siku hiyo ya alhamisi Februari 12.

Dk. Mengi aliweka ujumbe huo twittter : “Kutokana na sababu zisizozuilika mshindi wa Januari wa shindano la 3N atatangazwa Februari 12 saa 5 asubuhi. Samahani kwa usumbufu wowote”.

Kwa mujibu wa Dk. Mengi awali mshind I alitakiwa kutangazwa Jumatano ya leo ya Februari 11, kabla ya kusogeza mbele hiyo Februari 12.

Shindano hilo litakuwa linafanyika kila mwezi kwa muda wa miezi sita kuanzia Januari Mosi 2015, hadi Juni 30, 2015, na mshindi wa kila mwezi atajishindia ruzuku ya shilingi milioni 10 atakazozitumia kutekeleza kwa vitendo wazo lake la biashara.

Shindano hilo, linawashirikisha Watanzania pekee, litaendeshwa kwa njia ya mtandao wa kompyuta ambapo mshiriki atatuma wazo lake la biashara kwa anuani ya twita @regmengi Shindano la Wazo la Biashara. Katika mchujo wa kwanza jopo la wataalamu litateua mawazo 10 bora Zaidi na waliotoa mawazo hayo watafanyiwa usaili kwa njia ya simu ili jopo hilo lijiridhishe kama mawazo waliyoyotuma ni yao binafsi, na kama wamejipanga vizuri kutekeleza kibiashara.

Kutokana na mawazo hayo 10 teule, jopo litachagua wazo moja kuwa mshindi. Hii ni mara ya tatu kwa Dkt. Mengi kuendesha shindano kwa kutumia mtandao wa kompyuta wa twitter kwa kuamini kwake kuwa mitandao ya kijamii ina nguvu kubwa katika kuchochea ujasiriamali hasa kwa kizazi cha sasa.

Shindano la kwanza na la pili lililoendeshwa mwaka jana lilikusudiwa kushawishi mawazo ya kuondoa umaskini katika taifa lenye utajiri mkubwa, lakini watu wake wengi wakiwa bado wametopea katika lindi la umaskini.

Awali akizungumza katika uzinduzi wa shindano hilo, Dkt. Mengi alisema shindano hilo limelenga kuhimiza watu kuwa na upeo mkubwa wa kuona fursa za kibiashara na kuzitumia kujikwamua kiuchumi. Pia alisema shindano hilo ni mchango wake binafsi wa kuunga mkono jitihada za serikali na sekta binafsi za kuwakomboa wananchi kiuchumi kwa njia za ujasirimali, kwani amesema Sera zote mbili za kitaifa za Elimu ya juu na maendeleo ya viwanda vya kati na vidogo zina vipengele vya kuchochea na kuendeleza utamaduni wa ujasirimali wa mtu mmoja mmoja.

“Kwa muda mrefu nimekuwa nikishawishi uwepo wa moyo wa ujasirimali miongoni mwa wa Watanzania na hasa kwa vijana. Ni ndoto yangu kuona uchumi wetu unakua kwa kasi kiasi cha kuzalisha zaidi ya mamilionea 100 kila mwaka wanaoendesha biashara halali,” alisema.

Alisema kuwa na wazo sahihi la biashara, katika muda muafaka na eneo sahihi ni muhimu zaidi kuliko ruzuku ya fedha.

“Nataka vijana watambue kwamba wanaweza kuanza na kitu kidogo na kukua kufikia kampuni kubwa kabisa ya kimataifa unayoweza kufikiria,” alisema na kusisitiza kwamba anaamini siku moja mazingira ya ujasirimali nchini Tanzania yakuwa miongoni mwa mazingira bora kabisa barani Afrika.

Amesisitiza kuwa Shindano hilo liko wazi kwa watanzania wote na wanachotakiwa kufanya ni kuhakikisha wanapeleka wazo lao la biashara kwa Dk Mengi kupitia mtandao wa kompyuta wa twita, kwa kumtag Dk Mengi kwenye @regmengi.

Aidha amesema ni wale tu watakaomtag ndio watafikiriwa na jopo la wataalamu, na kusisitiza kuwa maamuzi ya jopo la Wataalamu yatakuwa ni ya mwisho.

Washindi wa kila mwezi wataarifiwa kwa kutumiwa ujumbe mfupi kwa kupitia akaunti zao za twita (DM) na kupewa ruzuku yao katika sherehe fupi itakayohudhuriwa na waandishi wa habari.

Call for applications: UN Journalism Fellowships

APPLICATIONS INVITED FOR UNITED NATIONS JOURNALISM FELLOWSHIPS
 
The Dag Hammarskj√∂ld Fund for Journalists is now accepting applications from professional journalists from developing countries for its 2015 fellowship program. The application deadline is March 16, 2015. 
  
The fellowships are available to radio, television, print and web journalists, age 25 to 35, from developing countries who are interested in coming to New York to report on international affairs during the 70th session of the United Nations General Assembly.  The fellowships will begin in early September and extend to late November and will include the cost of travel and accommodations in New York, as well as a per diem allowance.  

The fellowship program is open to journalists who are native to one of the developing countries in Africa, Asia, and Latin America/the Caribbean and are currently working for media organizations. Applicants must demonstrate an interest in and commitment to international affairs and to conveying a better understanding of the United Nations to their readers and audiences.  They must also have approval from their media organizations to spend up to three months in New York to report from the United Nations.

In an effort to rotate recipient countries, the Fund will not consider journalist applications for 2015 from nations selected in 2014:  Nigeria, Tunisia, the Philippines and Vietnam.  Journalists from these countries may apply in 2016. 

Four journalists are selected each year after a review of all applications. The journalists who are awarded fellowships are given the incomparable opportunity to observe international diplomatic deliberations at the United Nations, to make professional contacts that will serve them for years to come, to interact with seasoned journalists from around the world, and to gain a broader perspective and understanding of matters of global concern.  Many past fellows have risen to prominence in their professional and countries. The program is not intended to provide basic skills training to journalists; all participants are media professionals. 

Full fellowship eligibility criteria and documentation requirements as well as the fellowship application form can be found on the Fund’s web site at www.unjournalismfellowship.org

Questions about the program, eligibility and application process can be directed by email to [email protected]unjournalismfellowship.org.  

TBN yamfariji Mwanahabari aliyefiwa na jamaa 6 walioungulia ndani ya nyumbaMwenyekiti wa muda wa Chama cha Bloggers Tanzania (Tanzania Bloggers Network - TBN ), Joachim Mushi (kulia) akitoa poe na kisha kukabidhi ubani wa fedha shilingi laki tano (500,000/-) jana zilizotolewa kwa mwanahabari wa Kitulo FM ya Njombe Bw. Conrad Mpila kama pole toka TBN baada ya kupoteza ndugu watano wa familia moja katika ajali ya moto iliyotokea hivi karibuni na kuua watu sita eneo la Kipunguni jijini Dar es Salaam. Katikati ni mmoja wa wajumbe wa TBN, Dotto Mwaibale. TBN ilishiriki katika mazishi ya marehemu hao sita waliozikwa jana katika makaburi ya Airwing, Dar es Salaam."Tupo nawe katika wakati huu mgumu..." anasema Mwenyekiti wa muda wa Chama cha Bloggers Tanzania (Tanzania Bloggers Network - TBN ) Bw. Joachim Mushi wakati anakabidhi ubani huo.

  • Picha: Francis Dande