Katuni ya Wakudata: Haya, mpopoeni tena, ndo kwaaanza katoka bafuni!


Mambo 6 muhimu uyajue ili uboreshe biashara yako
Kuwa na kiu ama shauku ya kufikia ngazi kubwa ya kimafanikio kibiashara, ni hitaji ambalo kila mjasiriamali na mfanyabiashara wa kweli huwa nalo ndani ya moyo wake. Pamoja na kiu hii ya kutaka kufikia mafanikio hayo makubwa kibiashara, wajasiriamali wengi hujikuta wakikwama na kushindwa kutimiza malengo yao.

Kwa kawaida, huwa yapo mambo mengi yanayochangia kutokea kwa hali hii, ikiwemo na kufanya biashara kwa mazoea na matokeo yake kushindwa kuboresha biashara. 

Unaposhindwa kuboresha biashara yako, sio tu kwamba itapelekea wewe kukosa wateja, bali pia itakusababishia kushindwa kufikia mafanikio makubwa uliyojiwekea katika maisha yako. Kwa kujua hilo, ni muhimu sana kwako kuiangalia na kuichunguza biashara yako mara kwa mara na kufanya marekebisho muhimu na ya lazima, ili kupata matokeo chanya unayoyahitaji na si vinginevyo. Lakini, hautaweza kufanya chochote au marekebisho yoyote kama hujui mambo haya.

Haya Mambo 6 Unayotakiwa Kujua, Ili Kuboresha Biashara Yako.

1.Kubali Kuwa Kuna ushindani.


Ni muhimu kujua hili mapema kuwa biashara unayoifanya hauko peke yako, wapo watu pia wanaofanya biashara kama ya kwako. Kwa kujua hilo hutakiwi kubweteka, kujiachia ama kulala na kusubiri wateja waje, utakuwa unapoteza muda na hutapata mafanikio makubwa kama unayoyataka. Badala yake, fanya kazi kwa bidii kuweza kukabiliana na upinzani ulionao na usiogope wala kutishwa na chochote, hapo utakuwa umefanya kitu cha kuboresha biashara yako.

2. Kuwa na malengo na biashara yako.


Ili uweze kufikia mafanikio makubwa unayoyataka katika biashara yako, ni muhimu pia kujiwekea malengo maalum ya kibiashara. Malengo hayo yatakusaidia kujua ni wapi unapotakiwa kufika baada ya muda fulani na wapi ulipokwama. Unapokuwa na malengo juu ya biashara yako, ni lazima nidhamu yako itakuwa juu hasa katika mambo ya pesa na utahakikisha kufanya lolote ili biashara yako ikue. Biashara yoyote unayoifanya kama haina malengo maalumu haiwezi kukua na kufika mbali hata iweje.

3. Jitoe Kufanya kazi kwa bidii.


Kwa kuwa umeamua kuwa mjasiriamali, kitu pekee ambacho kinaweza kufanya biashara yako ing’ae ni kufanya kazi kwa bidii, kwa ubunifu na maarifa makubwa. Nguvu nyingi, mawazo na mwelekeo mkubwa unatakiwa kuupeleka kwenye biashara yako ili ikuletee mafanikio makubwa na si vinginevyo. Kumbuka, wewe ndiyo bosi na mkurugenzi wa biashara yako unayoifanya, ukilala au kusinzia ujue kabisa kila kitu kitaharibika na hutaweza kusonga mbele.

4. Ishi na watu wenye mitazamo chanya.


Itakuwa ni ngumu sana kwako kufanikiwa kama utakuwa una watu wengi wanaokuzunguka ni wenye mitazamo hasi na biashara unayoifanya. Watu hawa watakukatisha tamaa kwa maneno na mienendo yao na utajikuta unashindwa kusonga mbele. Ili uweze kuboresha biashara yako na kufikia mafanikio makubwa, ni muhimu sana kuwa na watu chanya ambao wanauwezo wa kukusaidia kwa hali yoyote ile hata pale ambapo mambo yako yanakwenda hovyo.

5. Badili jinsi unavyojitazama mara moja.


Kuwa na mtazamo chanya juu ya biashara yako ni kitu cha lazima sana kwako, ili iweze kuleta mabadiliko unayatarajia. Biashara yako haitafika popote kama utakuwa mtu wa kuitazama na kuona kuwa haitafanikiwa sana kama unavyoziona za wengine. Kutokana na mitazamo wako huo utaanza kufanya mambo kizembe hali itakayopelekea wewe kushindwa. Kama unataka kuboresha biashara yako, badili jinsi unavyojitazama wewe na biashara kwa ujumla.

6. Jifunze zaidi kuhusu biashara.


Unatakiwa kujifunza na kuilewa vizuri biashara unayoifanya kila siku. Hiki ni kitu ambacho hutakiwi kukwepa kwani kitakusaidia kuiboresha biashara yako kwa sehemu kubwa sana. Kwa kadri jinsi utakavyozidi kujifunza juu ya biashara yako, utagundua mapungufu mengi ambayo ukija kufafanyia kazi, itakusaidia kuhama kutoka ngazi moja na kuelekea ngazi nyingine zaidi ya mafanikio kibiashara.

Kumbuka, ili tuweze kufanikiwa na kufikia mafanikio makubwa, tunalazimika kuboresha biashara zetu kwa sehemu kubwa kila siku. Kama utashindwa kuboresha biashara yako, basi elewa tu hutafika mbali sana kimafanikio kama unavyofikiri, kwani nguvu ya ushindani itakushinda na utajikuta umebaki pembeni na kuwa mtazamaji kwa wengine. Kwa kuanzia, hayo ndiyo mambo muhimu unayotakiwa kuyajua ili kuboresha biashara yako.

Mtwa mpya wa Wahehe na historia ya marehemu Abdul Mkwawa


Adam Abdul Sapi (13) ametawazwa kuwa Chifu mpya wa Wahehe, akirithi nafasi ya baba yake, Abdul Sapi Mkwawa (66) aliyefariki Februari 14, 2015 na kuzikwa katika kijiji cha Kalenga, nje kidogo ya mji wa Iringa ndani ya makumbusho yaliyowekwa fuvu la babu yake, Chifu Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga Mkwawa.

Kabla ya kifo chake kilichosababishwa na maradhi ya sukari na figo, Abdul Sapi Mkwawa aliyekuwa mtoto wa tatu wa Spika wa kwanza mweusi nchini, Adam Sapi Mkwawa, alikuwa akifanyakazi katika kiwanda cha maji Afrika cha Kidamali, Iringa.

Amewahi pia kufanyakazi katika Chama cha Wazalishaji Tumbaku Iringa na Shirika la Elimu Supplies.

Alizaliwa Mei 4, 1949 katika kijiji cha Kalenga na kupata elimu ya msingi katika shule za Kalenga na Tosamaganga kati ya mwaka 1956 na 1963.

Mwaka 1964 hadi 1970 alijiunga na shule ya sekondari Iyunga na Mkwawa, ambako alipata elimu ya kawaida na ya juu ya sekondari kabla ya kujiunga na elimu ya juu ya biashara na utawala 1971 hadi 1973.

Mmoja wa ndugu wa marehemu, Hussein Sapi alisema mpaka umauti unamkuta, Abdul Sapi Mkwawa alikuwa Mtwa (Chifu); alisimikwa mwaka 1999 baada ya kifo cha baba yake, Adam Sapi Mkwawa aliyefariki Juni 25, 1999.

Kabla ya maziko ya Chifu huyo, wazee wa kabila la Wahehe walimsimika Adam ambaye ni mtoto wake wa tano, kuwa Chifu mpya wa kabila hilo.

Hata hivyo, mtoto huyo aliyeko darasa la Saba katika shule ya msingi ya Highlands ya mjini Iringa, atalazimika kusubiri kufanya shughuli za kichifu mpaka atakapotimiza umri wa miaka 20. Badala yake, mdogo wa marehemu, Saleh ndiye atakayeshikilia wadhifa huo mpaka Adam atakapofikisha umri huo.

[video] Taarifa na maoni kuhusu hali ya usalama mkoani Tanga

Watu na vitu kadhaa vyakamatwa Tanga


Serikali imetoa taarifa rasmi kuhusu uhalifu uliotikisa mkoani Tanga, ikisema hali ni shwari na umma wa Watanzania upuuze taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikitia hofu.

Aidha, imesema watu kadhaa wanashikiliwa wakihusishwa na uhalifu huo.

“Tunawashikilia ila mpaka sasa siwezi kukueleza idadi yao na kwamba ni wa kikundi cha ugaidi au la. Hao watu tunafanya nao mahojiano ili kuweza kuelewa kama wanahusika kwenye tukio hilo,” 
 alisema Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Ndaki alisema hali katika kitongoji cha Majimoto, Amboni na mkoa wa Tanga kwa ujumla iko shwari. “Tunaendelea kufanya uchunguzi kubaini hao wahalifu pamoja na silaha zilizoibwa,” alisema.

“Tunaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano wao hasa wanapoona watu wenye majeraha au wanaowahisi kwamba ni wahalifu ili nasi tuweze kuwachunguza kama wanahusika kwenye tukio hili”, 
alisema.

Ingawa Kamanda hakuelezea mazingira ya kukamatwa kwa watuhumiwa, waandishi wa habari waliozuru eneo la Amboni yalikotokea mapigano, waliarifiwa kwamba baadhi ya wavuvi kwenye Mto Zigi, walimkamata mtu wakimtuhumu kukutwa akifua nguo zenye damu.

Katika mapigano hayo baina ya askari na wahalifu, yalisababisha kifo cha askari wa JWTZ, Sajenti Said Kajembe na wengine kujeruhiwa.

“Asubuhi wavuvi kadhaa walikuwa hapo mtoni ghafla walikutana na mtu pembeni ya mto akiwa anafua kanzu pamoja na vifaa fulani kama nguo za kufunika uso ..’maski’ ikabidi wawapigie haraka polisi simu lakini hawakuweza kupatikana na ndipo wakawapigia askari wa JWTZ ambao walifika haraka eneo la tukio na kumkamata mhusika”, 
alisema mkazi mmojawapo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Magalula Said Magalula aliwataka wakazi wa Tanga na vitongoji vyake, kuondoa hofu kwa kuhakikisha wanaendelea na shughuli zao za uzalishaji kwa sababu ulinzi umeimarishwa na hali ya usalama ni shwari.

Pia, aliwataka wananchi na wageni wenye mpango wa kutembelea eneo la kihistoria la Mapango ya Amboni, kuendelea na ratiba zao kwa sababu eneo hilo liko salama na tangu awali halikuhusika kwenye vurugu hizo.
Magalula ambaye pia alikutana na waandishi wa habari, alisema 
“Hali ni nzuri ulinzi na usalama uko imara… naomba wananchi waondoe hofu, wawe na amani na waendelee na shughuli zao za uzalishaji… hakuna tatizo kabisa usalama umedhibitiwa vizuri.”

Mkuu huyo wa mkoa ambaye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, alisisitiza 

 “Naomba Watanzania wenzangu muelewe kwamba eneo lilipofanyika tukio la mapigano na wahalifu si pale yalipo mapango ya Amboni ... maeneo hayo yapo mbali na nitoe mwito kwa wageni wenye mpango wa kutembelea hapo wawe huru kufanya hivyo mahali hapo ni salama.”
“Naomba Watanzania nchini kote kwa ujumla wawe na amani kwa sababu Tanga iko shwari hakuna tena hizo vurugu za wahalifu… naomba wasiamini sana taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii… sisi tuko shwari na shughuli za kijamii zinaendelea kama kawaida ikiwemo Amboni.”

Akizungumzia mapigano hayo yaliyotokea Februari 14, alisema licha ya majibizano ya kurushiana risasi yaliyofanywa na askari wa Polisi kwa kushirikiana na wa JWTZ , uchunguzi unaendelea kuwapata wahusika.

“Vikosi vya usalama vinaendelea na juhudi za kuwasaka pamoja na kutafuta silaha zetu lakini hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa … zipo simulizi mbalimbali zinazoendelezwa kwenye mitandao ya kijamii ila sisi serikali ya mkoa bado hatujathibitisha kwamba watu hao ni wa kikundi gani ila ninachokifahamu hao watu ni wahalifu”, 
alisisitiza.

Kuhusu kuongezeka kwa matukio katika maeneo mbalimbali mkoani humo, alisema kila tukio linachukuliwa kwa uzito mkubwa na linashughulikiwa kwa namna linavyotokea.

Aidha, amewataka wakazi wa Tanga hususan wanaoishi eneo la Amboni na vitongoji vyake kuhakikisha wanaendelea kutoa habari sahihi kuhusu watu mbalimbali wanaowatilia shaka . Alisema taarifa hizo zina umuhimu wa kipekee kwa askari katika kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu hao.

Kutokana na maswali mengi ya wanahabari na wananchi, kudai kutoridhishwa na mwenendo wa utoaji taarifa kuhusu tukio hilo, Mkuu wa Mkoa aliruhusu watembelee eneo la tukio kuthibitisha kama hali ni shwari katika eneo husika.

Timu ya wanahabri takribani 10 kutoka vyombo mbalimbali vya habari, wakiwa chini ya ulinzi wa askari walipelekwa eneo la tukio, ambalo liko umbali wa takribani kilometa tano kutoka yaliko Mapango ya kihistoria ya Amboni.

Eneo hilo limetawaliwa na miamba ya mawe makubwa yenye mapango, ambayo hayatumiki kwa shughuli za kihistoria, kama ilivyo katika kitongoji cha Kiomoni yalipo mapango ya kihistoria ya Amboni.

Shughuli zinazoonekana kufanyika jirani na eneo hilo, ni ulipuaji wa miamba kwa kutumia baruti ambao hufanywa na wachimbaji wadogo kisha kuvunja kokoto kwa ajili ya viwanda vya kutengeneza chokaa pamoja na mawe kwa shughuli za ujenzi mjini hapa.

Eneo wanakodaiwa kuishi wahalifu hao, liko umbali wa meta 300 kutoka upande wa pili zinapofanyika shughuli za upasuaji kokoto zinazoendeshwa na wakazi wa kitongoji cha Majimoto na Mafuriko huko Amboni.

Katika eneo hilo, kulikuwa na ukimya kutokana na kutokuwapo shughuli yoyote hususani uvunjaji kokoto iliyozoeleka kutokana na wananchi kusimamishwa kutokana na tukio hilo.

Waandishi wa habari walilazimika kufuata maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na wanausalama waliokuwa wakiwaongoza kufika ndani ya pango husika.

Mwonekano wa eneo hilo, ulidhihirisha ni la hatari kutokana na mapango kufunikwa na vichaka. Ndani ya pango hilo, upo uwazi mkubwa unaoashiria uwepo wa shughuli za kibinadamu zilizokuwa zikiendelea.

Ndani ya pango hilo, zilikutwa nguo; hususan suruali, madumu ya kuhifadhia maji, vikombe kadhaa vya plastiki, chupa za maji ya kunywa zilizotumika hatua ambayo imedhihirisha kuwapo binadamu waliokuwa wakikaa humo licha ya kwamba, kufika kwake ni kwa shida.

Wakazi wazungumza

Wakizungumza na waandishi, baadhi ya wakazi wa maeneo jirani na eneo hilo, walisema hawajaruhusiwa kufika eneo hilo kwa kuwa linaendelea kulindwa na askari wa Polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) kwa kushirikiana na JWTZ.

“Muda mfupi tu kabla ya ninyi kwenda huko, askari wa FFU walitoka huko , ninyi mnaelezwa kwamba pako shwari lakini sisi bado hatujaruhusiwa kufika kule kwa sababu panalindwa muda wote na askari… ,” 
alisema mkazi aliyejitambulisha kwa jina moja la Mrisho.

Katika hatua nyingine, askari wa JWTZ aliyefariki wakati akitibiwa kwenye Hospitali ya Bombo baada ya kujeruhiwa kwenye mapigano hayo ya mwishoni mwa wiki, mwili wake uliagwa jana mjini hapa kabla ya kusafirishwa kuelekea wilayani Korogwe kwa maziko yaliyofanyika katika kijiji cha Bungu.

Wanne wakamatwa kwa ujambazi Dodoma

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi DAVID MISIME – SACP amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limewakamata majambazi wanne (4) waliomuua ASHELI S/O MAGINA mwenye miaka 40, Msukuma, Mfanyabiashara/Mkulima wa Kijiji cha Bubutole kwa kumkata na mapanga kichwani na mikononi na kufariki papo hapo tukio lililotokea tarehe 11/02/2015 majira ya saa 02:00hrs usiku katika Kijiji cha Bubutole Kata ya Farkwa, Tarafa ya Farkwa Wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma.

Amewataja majambazi hao waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo kuwa ni:
 1. HASSAN S/O MAULIDI @ SALAMA, mwenye miaka 32, kabila Msandawe, Mkulima.
 2. HAMADI S/O HUSSEIN mwenye miaka 25, kabila Msandawe, Mkulima.
 3. RASHID S/O YUSUPH, mwenye miaka 21, kabila Msandewe, Mkulima.
 4. ABDALAH S/O SWALEHE @MUNA, mwenye miaka 25, kabila Msandawe, Mkulima, wote wakazi wa Kijiji cha Porobanguma Wilayani Chemba Dodoma.

Kamanda MISIME amefafanu kuwa majambazi hao walimvamia ASHELI s/o MAGINA nyumbani kwake akiwa amelala dukani na kumshambulia kwa mapanga na kufariki dunia kisha kupora mali mbalimbali ikiwemo pikipiki, mifuko miwili ya sukari ya kilo 25, mifuko miwili ya unga wa ngano ya kilo 25 na soda kreti tatu(3) mali ambayo thamani yake haijafahamika.

Ameendelea kusema kwamba majambazi hao walikamatwa wakiwa na pikipiki yenye namba za usajili T. 449 CQP aina ya SUNLG mali ya marehemu waliyopora eneo la tukio na baadhi ya mali walizopora kama sukari na maharage. Pia waliweza kuonyesha mapanga waliyotumia kumkatakata nayo marehemu ASHELI s/o MAGINA.

Aidha Kamanda MISIME amesema mtuhumiwa HASSAN s/o MAULIDI @ SALAMA alikuwa anatafutwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la mauaji ya IJUMAA S/O SAID mwenye miaka 30, Msandawe Mkulima na Mkazi wa Kijiji cha Monjore Banguma kwa kumchoma na kisu na hili tukio lililotokea tarehe 19/01/2015 majira ya saa kumi na mbiliza jioni katika kijiji cha Porobanguma kwa kile kilichodaiwa kua ni ugomvi uliotokea baina yao. Uchunguzi zaidi unaendelea na ukikamilika watafikishwa mahakamani.

Kamanda MISIME ametoa wito kwa Wananchi waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, kwani wahalifu wanaishi katika jamii na kufanya uhalifu ndani ya jamii. Wahalifu wasifumbiwe macho.

 • Taarifa ya Sylvester Onesmo wa Jeshi la Polisi Dodoma.

Mkuu wa Wilaya aagiza Walimu Wakuu washushwe vyeoZaidi ya watu hamsini wamekamatwa na jeshi la polisi kufuatia vurugu kubwa iliyotokea katika mji wa Katoro mkoani Geita.

Chanzo cha vurugu hizo ni mgomo wa wanafunzi wa shule za msingi Kilimani, Mkapa na Ludete ambapo walilala katikati ya barabara, kushinikiza kuwekewa matuta kutokana na matukio ya ajali ya mara kwa mara hivyo kutishia usalama wao.

Hata baada ya kuwekewa matuta kuzuia ajali vurugu hizo zilipamba moto kutoka kwa wanafunzi na kuingia watu wazima na kuanza kupiga mawe magari yote yaliyokuwa yakipita barabarani na zaidi ya magari saba yameharibiwa vibaya na watu kujeruhiwa.

Baada ya muda kuonekana hali imetulia magari yaliruhusiwa kuondoka hata hivyo hali haikuwa shwari ambapo magari yote yalirudi kituo cha polisi Katoro kwa usalama zaidi.

Mkuu wa wilaya ya Geita ameagiza Walimu Wakuu wote wa Shule za Msingi zilizohusika na uanzishwaji wa vurugu hizo kushushwa vyeo vyao na hatua mbalimbali za kisheria zizingatiwe.

 • Taarifa ya ITV
Polisi wakiwa wamewaweka chini ya ulinzi baadhi ya wananchi walioandamana na kufunga Barabara ya Geita kwenda Bukoba jana.

(picha: Jackline Masinde)

ATCL yazindua ndege 'mpya' nyingine

Meneja wa Air Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Bw James Mbago akizungumza na waandishi wakati wa uzinduzi wa ndege mpya ya shirika hilo aina ya CRJ-100 yenye uwezo wa kubeba abiria 50, mara baada ya ndege hiyo kutua ikitokea mkoani Kigoma. Huo ukiwa ni mkakati wa kimaendeleo wa shirika hilo katika kuongeza idadi ya ndege na safari zake

SHIRIKA la ndege la Taifa (ATCL) mwishoni mwa wiki iliyopita lilizindua ndege yake mpya aina ya CRJ-100 yenye uwezo wa kubeba abiria 50 ikiwa ni sehemu ya mpango wa shirika hilo kuongeza idadi ya ndege zake sambamba na kuongeza idadi ya safari zake.

Shirika hilo ambalo kwa sasa linalotoa huduma zake katika mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Mtwara na visiwa vya Komoro limejipanga kufanya safari za kila siku kati ya mikoa ya Dar es Salaam na Kigoma huku pia likiwa tayari kufanya safari za Mtwara na visiwa vya Komoro mara sita kwa wiki katika siku za Jumatatu, Alhamisi na Jumamosi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mara tu baada ya ndege hiyo kutua kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Meneja wa shirika hilo katika kiwanja hicho, James Mbago alisema ndege hiyo imekodiwa kutoka nchini Afrika Kusini kwa jitihada za Serikali ya Tanzania na sasa ipo tayari kuwahudumia wateja wa shirika hilo.

"Kuja kwa ndege hii kunaongeza idadi ya ndege zetu hadi kufikia mbili na tunashukuru kuona kwamba imepokelewa vizuri na abiria wetu. Ndege yetu nyingine aina ya De-Havilland Dash 8 Q300 kwa sasa inapata matengenezo makubwa kwenye karakana yetu iliyopo hapa hapa uwanja wa ndege,"
alisema Mbago.

Kwa mujibu wa Mbago kupona kwa ndege hiyo inayofanyiwa matengenezo kiwanjani hapo kutalifanya shirika hilo lianzishe tena safari zake za ndani kwa mikoa ya Mwanza, Tabora, Arusha na Mbeya.

"Muda si mrefu mambo yatakuwa mazuri zaidi…inafurahisha zaidi tunapopata mrejesho mzuri kutoka kwa wateja wetu wanaofurahia huduma za shirika lao mama,’’ aliongeza Mbago. Zaidi, Mbago aliongeza kuwa shirika lake linatarajia ongezeko kubwa la abiria kutokana na ukweli kuwa ndege yao hiyo mpya ina uwezo wa kusafiri kwa haraka zaidi ikilinganishwa na ndege nyingine huku safari zake zikiambatana na huduma nzuri inayotolewa kwa wateja wake."

Wakizungumza mara tu baada ya kushuka kwenye ndege hiyo, baadhi ya abiria waliotoka Kigoma walisema licha ya kutumia muda mfupi zaidi lakini pia walifurahia huduma nzuri walizozipata kutoka kwa wahudumu wa ndege hiyo.

Kwa kweli hii ilikuwa ni moja ya safari zangu za ndege ambayo nimeifurahia sana. ATCL wanahitaji pongezi kwenye hili na zaidi wafikirie kuboresha huduma zaidi ya hapa…sisi abiria tupo tayari kuwaunga mkono kwa sababu ndio wanabeba nembo ya taifa letu," 
alisema mmoja wa abiria hao aliyejitambulisha kwa majina Gaudence Kashoka.

Taarifa sahihi ya JWTZ kuhusu kifo cha askari wake huko Mbalizi

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania linapenda kutoa taarifa ya kifo cha Askari wake Praiveti Ahadi Mwaka Mwainyokole kilichotokea tarehe 4 Februari 2015 katika mji mdogo wa Mbalizi, Mkoani Mbeya.

Taarifa za mazingira ya kifo cha Askari huyo zimepotoshwa na baadhi ya Vyombo vya Habari na kusababisha mapokeo tofauti kwa wananchi.

Hali halisi ni kwamba, mnamo tarehe 4 Februari 2015 Askari huyo akiwa na Askari wenzake wanne (4) ambao ni Koplo Bedatu Benard Mloka, Praiveti Thani Hamisi Haji, Praiveti Mzee Buan Mzee na Praiveti Mohamed Juma walivamiwa na kundi la wahuni wakati wakitoka matembezini. Chanzo cha vurugu hizo ni kutokana na Praiveti Rashid Maulid wa Kikosi chao kuibiwa samani kwenye nyumba aliyokuwa amepanga uraiani katika mji mdogo wa Mbalizi, Kitongoji cha Shigamba. Samani alizoibiwa ni pamoja na TV aina ya LG “flat screen” “Inch 20”, radio aina ya Sony moja, Deck aina ya Sangsung, flash moja, extension cable moja na fedha taslimu Tshs 30,000/=.

Askari huyo alitoa taarifa Kituo cha Polisi tarehe 03 Februari 2015 na kupatiwa RB yenye Nambari MBI/RB/285/2015, sambamba na kutoa taarifa Polisi. Kituo hicho cha Polisi kilitoa askari mmoja ambae aliungana na askari Jeshi na wenzake na wakaenda eneo la relini ambako vijana wasio na ajira maalumu hushinda. Waliwakamata vijana saba, mmoja wa vijana hao alikimbia na kwenda kuwapa taarifa wenzao ambao hawakuwepo katika eneo hilo ambapo vijana sita walifikishwa kituo cha Polisi.

Ilipofika saa tatu usiku askari hao wakiwa katika matembezi ya kawaida walikutana na kundi la vijana wakiwa na silaha mbalimbali kama nondo na marungu ambao walianza kuwa shambulia huku wakiwashutumu kuwa waliwapeleka wenzao Polisi.

Kwa kuwa kundi la vijana hao lilikuwa kubwa na likiwa na silaha zilizotajwa lilifanikiwa kuwajeruhi, Askari hao akiwemo Praiveti Ahadi Mwainyokole ambae alijeruhiwa vibaya. Askari hao walikwenda Polisi na wakachukuwa PF3 na kisha kwenda katika hospitali ya Jeshi Mbeya baadaye Praiveti Mwainyokole alifariki muda mfupi baada ya hali yake kutokuwa nzuri kutokana na kupigwa na kitu kizito kichwani hali iliyosababisha damu kuvia kwenye Ubongo.

JWTZ linasikitishwa na mauaji hayo yaliyofanywa kwa Askari wake, na mauaji ya askari wengine katika maeneo ambako vitendo kama hivyo vimetokea. Ikumbukwe kuwa JWTZ lipo kwa ajili ya usalama na ustawi wa wananchi, hivyo JWTZ linalaani vitendo viovu vinavyofanyika kwa askari wake na linatoa rai kwa vyombo vya sheria kuchukua mkondo wake.

Kimsingi JWTZ halina ugomvi na wananchi kwani kazi yake ya msingi ni kuwalinda ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kimaendeleo kwa utulivu na amani kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu.

Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Mahusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga

Waziri Sitta: Amsimamisha kazi Mkurugenzi TPA; Ateua mwingine, Aunda timu ya uchunguzi


Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande kutokana na kile kilichoelezwa kuwa uendeshaji mbovu wa utoaji wa zabuni.

Aidha, amemteua Awadhi Massawe kushika wadhifa huo. Kabla ya uteuzi huo, Massawe alikuwa Meneja wa Bandari.

Akizungumza na waandishi wa habari, Sitta alisema uamuzi huo umetokana na kuwapo malalamiko ya kutofuatwa kwa taratibu za zabuni na ucheleweshaji wa barua kwa wanaoshinda.

“Ni muhimu sana taratibu zetu za ununuzi katika bandari ziwe wazi na ziheshimike duniani kote, maana miradi hii ni mikubwa sana inayopitishwa na bodi ya zabuni ya TPA,” alisema.

Sitta alisema, aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Dk Harrison Mwakyembe alianza kushughulikia masuala hayo, lakini hayajakaa vizuri. Alisema hakuna uwazi na kumekuwa na ubabaishaji mkubwa, ikiwemo kubadilika majina ya kamati za kutathmini zabuni.

Wakati huo huo Sitta ameunda timu ya watu sita itakayochunguza tuhuma za Kipande. Imepewa wiki mbili iwe imefanya kazi hiyo.

Timu hiyo itaongozwa na Jaji mstaafu, Augusta Bubeshi na Katibu wake, Deogratius Kasinda ambaye ni mtumishi wa Wizara ya Uchukuzi.

Wajumbe wengine wa timu hiyo ni Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Manunuzi ( PPRA) Dk Ramadhani Mlinga, Samson Lugigo , Happiness Senkoro na Flavian Kinunda ambao walishawahi kushika nyadhifa za juu ndani ya TPA.

“Nimejitahidi kuchukua hawa wastaafu kwa sasa hivi hawatafuti cheo chochote, naamini watatenda haki, watachunguza tu bila kufanya uonevu,” alisema Sitta.

Waziri Sitta alisema bandari ni eneo muhimu, kwani takwimu zinaonesha kwamba asilimia 43 ya makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yanatokana na kodi ya ushuru wa forodha. Kati ya makusanyo hayo, asilimia 87 yanakusanywa kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Kwa upande wa Kipande, alisema hawezi kupinga hatua iliyochukuliwa na Waziri .

Hata hivyo, alisema anaamini kipindi chote cha uongozi wake, alifanya ambayo yalikuwa sahihi na hana wasiwasi na uamuzi huo.

"Mimi sina wasiwasi na hilo sababu huo ni uamuzi wake; lakini nina imani kuwa katika bandari hii, nimefanya kile ambacho nilikuwa natakiwa kufanya, hivyo sina shaka na hilo," alisema Kipande.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto ametaka serikali kujenga matangi ya kuhifadhia mafuta na kujenga bomba la mafuta kwenda mikoani.
Aidha, kamati hiyo imetaka TPA kuangalia uwezekano wa kununua hisa 50 za Kampuni ya Kuhifadhi Mafuta (Tiper) imilikiwe kwa asilimia 100 na Serikali.

Kuhusu ujenzi wa matangi, Zitto alisema hatua ya Serikali kujenga matangi yake ya kuhifadhi mafuta, itasaidia kujua kiasi cha mafuta yanayoingia na kuweza kukadiria kodi kwa uhakika.

Akitoa mfano wa Kenya, alisema Serikali inamiliki matangi ya kuhifadhia mafuta, wanayapima kujua kiasi cha mafuta kilichoingia na kukitoza kodi kabla ya kupelekwa kwenye matangi ya waagizaji.

“ Walichofanya, wamemtaka kila muagizaji kuwa na flow meter yake na yakitoka kwenye meli yanaingia kwenye matangi ya Serikali na baada ya kujua kiasi na kutozwa kodi hupelekwa kwa walionunua,” alisema.
Zitto alisema wakati umefika sasa kwa serikali kujenga mabomba ya kusafirishia mafuta na kwa kuanzia yakawa matatu, ambayo yatasaidia kuondoa mfumo wa sasa wa kusafirisha kwa magari.

“Linaweza kujengwa bomba moja kwenda Mbeya, likawa na matoleo kwa ajili ya mikoa ya Morogoro, Iringa na mikoa iliyo jirani, kwa kufanya hivyo tutaondoka na hali ya sasa ya kusafirisha mafuta kwa magari,” alisema.

Alisema katika kuimarisha reli, ni vyema ukaanzishwa mfumo wa kutoza kodi asilimia 1.5 kwa kila bidhaa inayoingia nchini na fedha hizo ziimarishe usafiri wa reli.

“Kwa sasa asilimia 99 ya mizigo inasafirishwa kwa barabara, hili si jambo jema kwa uchumi, najua nikisema hivyo wenye malori watalalamika, lakini wanaweza kufanya biashara nyingine,” alisema.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa TPA, Awadhi Massawe alisema asilimia 60 ya mafuta yanayoingia nchini hupitia kwenye boya la Single Buoy Mooring (SBM).

Alisema wamejipanga kujenga mita ya kisasa ya kupimia mafuta maeneo ya Kigamboni huku ile ambayo haitumiki, wamepanga kuiboresha na kuwa ya kisasa.

Kuhusu maendeleo ya ujenzi wa gati namba 13 na 14 ambazo zabuni yake iliingia utata, Massawe alisema ripoti ya maandishi wataipeleka kwa Kamati hiyo ya Bunge ifikapo Machi Mosi mwaka huu.

Pia, Massawe alisema hatua ya kitengo cha kupakua kontena kupewa mtu binafsi, inawapunguzia mapato na kuwa hiyo ndio sekta ambayo inaingiza fedha nyingi.

Alisema ili kupambana na hali hiyo, wamejipanga kuimarisha gati namba 1 hadi 7 na kuongeza kina cha bahari ili kuweza kupakua makasha na kuwa kwa mwaka jana waliweza kupakua makasha laki mbili.
Waziri wa Uchukuzi Mhe. Samuel Sitta akizungumza na wanahabari leo bandarini) amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Eng Madeni Shamte Kipande kwa tuhuma za utendaji mbovu, ikiwa ni pamoja na kutokuwepo kwa uwazi kwenye mamlaka hiyo hususani katika michakato ya zabuni mbalimbali zinazotangazwa na mamlaka hiyo.
(picha: Francis Dande)

Rais Kikwete ahudhuria mazishi ya Chifu Mkwawa

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweka udongo kaburini wakati wa mazishi ya aliyekuwa Chifu wa Kabila la Wahehe, Chifu Abdu Mfwimi Adam Mkwawa leo katika eneo la Nyumba ya Makumbusho ya Chifu Mkwawa, Kijiji cha Karenga Februari 16, 2015.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatatu, Februari 16, 2015, ameungana na mamia ya waombolezaji kumlaza katika nyumba yake ya milele, Chifu wa Kabila la Wahehe, Chifu Abdu Mfwimi Adam Mkwawa.
Aidha, Rais Kikwete ameshuhudia kutawazwa kwa Chifu mpya, Chifu Adam Abdu Mkwawa, Mtwa Adam wa Pili, kijana wa miaka 14, ambaye yuko darasa la saba na ambaye anachukua nafasi ya baba yake ambaye aliaga dunia juzi, Jumamosi, Februari 14, 2015.
Mtwa Adam wa Pili ni mtoto pekee wa kiume na pia ni mtoto sita na wa mwisho wa Chifu Abdu Adam Mkwawa ambaye ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 65.
Rais Kikwete amewasili katika eneo la Nyumba ya Makumbusho ya Chifu Mkwawa, Kijiji cha Karenga, kiasi cha saa saba kujiunga na mamia ya waombolezaji na kushuhudia kutawazwa kwa Mtwa Adam wa Pili, ambaye amekuwa chifu kwa kupewa mkuki na ngao, ambavyo vilitumiwa na Chifu Mkwawa mwenyewe, na baadaye kukalishwa kwenye kiti cha uchifu.
Kwa vile hajafikisha umri wa miaka 20 ambao ndio umri rasmi wa kuwa Chifu wa Wahehe, ameapishwa pia chifu wa muda, Chifu Hassan Adam Sapi (Mahinya), ambaye atashikilia kiti cha uchifu kwa niaba ya Mtwa Adam wa Pili, mpaka hapo atakapofikisha umri wa miaka 20, miaka sita kutoka sasa.
Wakati mmoja wakati wa sherehe ya kutawazwa, Rais Kikwete amelazimika kumbembeleza na kumtuliza Mtwa Adam Abdu Mkwawa, ambaye alizidiwa na hisia na kuanza kubujikwa na machozi.
Baada ya kutawazwa kwa chifu mpya, yameanza mazishi ya chifu aliyeaga dunia ambaye amezikwa kwa heshima na taratibu zote za dini ya Kiislam lakini pia akapigiwa risasi tatu kwa kutumia gobole kwa mujibu wa mila na tamaduni za Kabila la Wahehe.
Baada ya kumalizika kwa mazishi ya Marehemu Chifu Abdu Mfwimi Adam Mkwawa, Rais Kikwete amekwenda nyumbani kwa marehemu kutoa pole kwa wafiwa akiwemo mama mjane.
Rais Kikwete amewasili Mkoani Iringa asubuhi ya leo, akitokea Dar es Salaam, ambako anafanya ziara ya kikazi ya siku mbili. Rais Kikwete ataondoka Iringa kesho, Jumanne, Februari 17, kurejea Dar es Salaam.

Ends
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

16 Februari, 2015
Rais Jakaya Mrisho Kikweteakitia saini kitabu cha maombelezo


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimfariji Chifu mpya wa Wahehe, Chifu Adam Abdu Mkwawa, Mtwa Adam wa Pili (14), wakati wa mazishi ya baba yake aliyekuwa Chifu wa Kabila la Wahehe, Chifu Abdu Mfwimi Adam Mkwawa katika eneo la Nyumba ya Makumbusho ya Chifu Mkwawa, Kijiji cha Karenga leo Februari 16, 2015
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Chifu mpya wa Wahehe, Chifu Adam Abdu Mkwawa, Mtwa Adam wa Pili (14), wakati wa mazishi ya baba yake aliyekuwa Chifu wa Kabila la Wahehe, Chifu Abdu Mfwimi Adam Mkwawa leo katika eneo la Nyumba ya Makumbusho ya Chifu Mkwawa, Kijiji cha Karenga Februari 16, 2015.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimpa pole mjane wa aliyekuwa Chifu wa Kabila la Wahehe, Chifu Abdu Mfwimi Adam Mkwawa leo Kijiji cha Karenga Februari 16, 2015

Sehemu ya III: Mazungumzo na Balozi Mstaafu, Nyang'anyi


Karibu sana na asante kwa kujiunga nasi katika kipindi hiki cha HUYU NA YULE

Tumepata fursa ya kuongea na Mhe. Balozi Mustafa Nyang'anyi

Tumefanya mazungumzo naye ya sehemu nne, kueleza safari yake kimaisha

Tunaendelea na sehemu ya tatu ya mazungumzo yetu, ambapo Mhe Balozi Nyang'anyi anaanza kuelezea namna

 1. Alivyoingia kwenye siasa (ubunge mwaka 1970)
 2. Alivyopata taarifa za kwanza za uteuzi wake serikalini. Hapa napo pana mvuto wake kusikiliza.
 3. Nafasi alizoshika kama naibu waziri na waziri kamili
 4. Nafasi ya ukuu wa mkoa
 5. Na hata harakati zake na pia alivyopata nafasi ya kuja kusoma Chuo Kikuu Havard

KARIBU


Ziara ya Waziri Nagu katika Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango

Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango (Kushoto) akitoa maelezo ya kumkaribisha Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu (Kulia) wakati alipofanya ziara ya kujitambulisha kwa Tume ya Mipango.

Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu amefanya ziara ya kujitambulisha kwa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ambayo ni moja taasisi anazoziratibu.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Dkt. Nagu alitoa wito kwa Tume ya Mipango ijielekeze katika kujibu changamoto kuu za kiuchumi zinazowakabili watanzania kwa sasa ikiwemo umaskini miongoni kwa Watanzania walioko vijijini, ukosefu wa wa viwanda vya kuongeza thamani mazao hasa kipindi hiki Tanzania inapoelekea kwenye uchumi wa gesi.

Dkt. Nagu aliasa Tume ya Mipango kufanya tafiti mbalimbali za kiuchumi na kijamii zitakazotoa majibu ya changamoto hizo.

“Kwa kuwa moja ya majukumu ya Tume ya Mipango ni kuandaa mipango ya maendeleo ya muda mrefu, kati na ile ya kila mwaka na pia kufanya tafiti mbalimbali za kiuchumi na kijamii, napenda kusisitiza kuwa mipango inayoandaliwa ijielekeze katika kujibu changamoto hizo kubwa zinazowakabili wananchi wetu ili kuhakikisha kuwa tunafikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025,” alisema Dkt. Nagu.

Kwa mujibu wa malengo makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, serikali imejipanga kuhakikisha maisha bora na mazuri kwa kila mtanzania, utawala bora unaozingatia sheria, na kujenga uchumi imara, wa kisasa na ushindani.

Akizungumza wakati wa kumkaribisha Dkt. Nagu, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango alisema kuwamajukumu ya msingi ya Tume ya Mipango ni kutoa dira na mwongozo wa uchumi wa Taifa pamoja na kubuni sera za uchumi na mikakati ya mipango ya maendeleo ya Taifa; usimamizi wa uchumi na kufanya utafiti katika nyanja za uchumi na maendeleo ya jamii.

Dkt. Mpango aliongeza kuwa kwa sasa Tume ya Mipango inafanya kazi ya kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/15 pamoja na uandaaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2015/16 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2016/17.

“Vilevile, Tume ya Mipango tumejidhatiti katika kuandaa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 ambao utajikita katika kuifikisha tanzania kuwa ni nchi ya viwanda,” alisema Dkt. Mpango.

Kwa mujibu wa Dkt. Mpango, tangu kuundwa upya kwa Tume ya Mipango mwaka 2008, imefanikiwa kukamilisha kazi kubwa za kitaifa ikiwemo kufanya mapitio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, kuandaa Mpango Elekezi wa Miaka 15 (2011/12 – 2025/26 pamoja na kuandaa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) na kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu 2006.

Kazi nyingine ni pamoja na kuandaa Mipango ya Maendeleo ya Taifa kila Mwaka, kuandaa mfumo wa ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya Matokeo Makubwa Sasa na kuratibu uanzishwaji wa President Delivery Bureau (PDB), Kuandaa Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji katika Sekta ya Umma (Public Investiment Management - Operational Manual – PIM-OM), na kufanya tafiti mbalimbali za kiuchumi na kijamii.


Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu (Wapili kushoto) akizungumza na baadhi ya watendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango alipotembelea na kujitambulisha Tume ya Mipango. Wanaomsikiliza ni Katibu Mtendaji, Dkt. Philip Mpango (Kushoto), Naibu Katibu Mtendaji (Miundombinu na Huduma), Mhandisi Happiness Mgalula (Wapili kulia) na Naibu Katibu Mtendaji (Biashara za Kimataifa na ya Kiuchumi), Bw. Paul Sangawe (Kulia).


Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakimsikiliza Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu (Hayupo pichani) alipotembelea na kujitambulisha Tume ya Mipango.


Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakimsikiliza Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu (Hayupo pichani) alipotembelea na kujitambulisha Tume ya Mipango.


Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu akizungumza na watumishi na viongozi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango (Hawapo pichani) wakati alipofanya ziara ya kujitambulisha kwa Tume ya Mipango.


Baadhi ya viongozi waandamizi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakimsikiliza kwa makini Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu (Kulia) wakati alipofanya ziara ya kujitambulisha kwa Tume ya Mipango.


Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango (Kushoto) akimkabidhi zawadi za vitendea kazi Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu alipofanya ziara ya kujitambulisha kwa Tume ya Mipango.


Naibu Katibu Mtendaji (Miundombinu na Huduma), Mhandisi Happiness Mgalula (Kushoto) akimkabidhi zawadi Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu alipofanya ziara ya kujitambulisha kwa Tume ya Mipango.


Naibu Katibu Mtendaji (Biashara za Kimataifa na ya Kiuchumi), Bw. Paul Sangawe (Kushoto) akimkabidhi zawadi ya kitenge Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu alipofanya ziara ya kujitambulisha kwa Tume ya Mipango. Anayeshuhudia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango.

 • Taarifa ya Saidi Mkabakuli

Tanzania Bloggers Network yamfariji Kitime kwa kufiwa

Mwenyekiti wa muda wa Chama cha Bloggers Tanzania (TBN), Joachim Mushi (kulia) akikabidhi ubani wa fedha shilingi 900,000 na kutoa pole kwa mwanamziki mkongwe, John Kitime (kushoto) ambaye amefiwa juzi na mkewe, tukio hilo lilifanyika jana Kimara eneo la Nguzo ya 800, jijini Dar es Salaam. Mzee Kitime ni mwanachama wa TBN.
Mwenyekiti wa muda wa Chama cha Bloggers Tanzania (TBN), Joachim Mushi (kulia) akikabidhi ubani wa fedha shilingi 900,000 na kutoa pole kwa mwanamziki mkongwe, John Kitime (kushoto) ambaye amefiwa juzi na mkewe, tukio hilo lilifanyika jana Kimara eneo la Nguzo ya 800, jijini Dar es Salaam. Mzee Kitime ni mwanachama wa TBN.

Mwenyekiti wa muda wa Chama cha Bloggers Tanzania (TBN), Joachim Mushi (kulia) akitoa ujumbe wa pole kwa John Kitime na waombelezaji mara baada ya kukabidhi ubani wa fedha zilizotolewa na wanachama wa TBN jana eneo la Kimara Nguzo ya 800 jijini Dar es Salaam. Baadhi ya wajumbe wa TBN walifika kumfariji Kitime ambaye pia ni mwanachama wa TBN.
Mwenyekiti wa muda wa Chama cha Bloggers Tanzania (TBN), Joachim Mushi (kulia) akitoa ujumbe wa pole kwa John Kitime na waombelezaji mara baada ya kukabidhi ubani wa fedha zilizotolewa na wanachama wa TBN jana eneo la Kimara Nguzo ya 800 jijini Dar es Salaam. Baadhi ya wajumbe wa TBN walifika kumfariji Kitime ambaye pia ni mwanachama wa TBN.

Baadhi ya wajumbe wa TBN, wakiwa katika picha na mzee Kitime walipofika kumfariji na kutoa ubani wa TBN. Kutoka kushoto ni Sufian na Othman Michuzi pamoja na Mzee Kitime.
Baadhi ya wajumbe wa TBN, wakiwa katika picha na mzee Kitime walipofika kumfariji na kutoa ubani wa TBN. Kutoka kushoto ni Sufian na Othman Michuzi pamoja na Mzee Kitime.

Kutoka kushoto ni mjumbe mshauri na Kiongozi wa TBN, Issa Michuzi, baadhi ya wanamuziki wa bandi ya Njenje, Mwenyekiti wa TBN, Mzee Kitime na mwanae akipata picha na baadhi ya waombolezaji marafii waliofika kumfariji.
Kutoka kushoto ni mjumbe mshauri na Kiongozi wa TBN, Issa Michuzi, baadhi ya wanamuziki wa bandi ya Njenje, Mwenyekiti wa TBN, Mzee Kitime na mwanae akipata picha na baadhi ya waombolezaji marafii waliofika kumfariji.

Baadhi ya wanamuziki wa Njenje pamoja na wajumbe wa Chama cha Bloggers Tanzania (TBN) wakipata picha ya pamoja na mfiwa mwanamziki mkongwe, John Kitime walipofika msibani kumfariji jana Kimara eneo la Nguzo ya 800, jijini Dar es Salaam. Mzee Kitime ni mwanachama wa TBN.
Baadhi ya wanamuziki wa Njenje pamoja na wajumbe wa Chama cha Bloggers Tanzania (TBN) wakipata picha ya pamoja na mfiwa mwanamziki mkongwe, John Kitime walipofika msibani kumfariji jana Kimara eneo la Nguzo ya 800, jijini Dar es Salaam. Mzee Kitime ni mwanachama wa TBN.[/caption]

Vodacom ZTE ya bei poa imeingia sokoni


Kufahamu duka gani utaweza kuipata simu hii ingia https://www.vodacom.co.tz/productsandservices/devices/vodacom-zte