Afisa wa NEC asema wanavyuo wajiandikishe bila hofu ya wapi watakuwa siku ya uchaguzi

Washiriki kutoka vyuo mbali mbali vya Mkoa wa Mbeya.

Wasomi wa Vyuo vikuu Mkoa wa Mbeya wamesema ratiba ya uchaguzi si rafiki kwa wanafunzi na kuwa inawapa mashaka ikiwa wataweza kushiriki kwenye kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Wakizungumza na kwenye mdahalo wa vyuo vikuu uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Chuo kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU) ulioandaliwa na Chama cha Walimu wanaofundisha masomo ya Siasa (CETA), walisema masharti yaliyowekwa na tume ya uchaguzi kwamba ni lazima kila mtu apige kura katika eneo alilojiandikishia linawabagua wanafunzi kutokana na muda wa uchaguzi kuwa eneo tofauti na alipojiandikishia. Walisema asilimia kubwa ya wanafunzi hujiandikisha aidha akiwa chuoni ama nyumbani lakini siku ya uchaguzi huenda akawa sehemu tofauti na alipojiandikishia jambo ambalo linamnyima haki yake ya kupiga kura na kuchagua viongozi.

Wanafunzi hao walishauri kuwa endapo tume itaendelea kusimamia msimamo wake ni bora wanafunzi wakawekewa utaratibu wa kumchagua Rais kwa kuwa ni kiongozi wa Kitaifa tofauti na Wabunge na Madiwani ambao wanapaswa kuchaguliwa na wakazi wa eneo husika.

Afisa Elimu ya mpiga kura na elimu kwa umma kutoka tume ya uchaguzi, Salvatory Alute alisema ni vema vijana wakajitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu bila kuhofia ni wapi watakapokuwepo siku ya uchaguzi.

Alisema zoezi la kujiandikisha ni muhimu kutokana na kutolewa vitambulisho vipya tofauti na ambavyo tayari vipo kwa walioandikishwa zamani na kushiriki chaguzi zilizopita.

Soma taarifa hii zaidi kwenye  Mbeya Yetu blog.

Radi tena yaua 5 Shinyanga

WATU watano wa familia moja wakiwemo wanafunzi wanne wamekufa papo hapo kwa kupigwa radi wakiwa shambani katika Kijiji cha Manungu kata ya Uyogo, Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kahama, Leonard Nyadaho, kwa niaba ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, watu hao walipigwa na radi Februari 28, mwaka huu na kufariki papo hapo kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha.

Nyadaho alisema mvua hiyo iliyoanza kunyesha juzi jioni katika kijiji cha Manungu kitongoji cha Izengwe. Alisema mvua hiyo iliwakuta wananchi hao wakiwa mbugani wakipanda mpunga ndipo walipopigwa na radi na kufariki.

Aliwataja marehemu hao kuwa ni Paulina Williamu (28), Magreth Mayunga (13), Herena Mayunga (14), Flora Mathias (13) na Veronica Mathias (14), wote wanafunzi wa Shule ya Msingi Manungu.

Mashuhuda walisema marehemu hao waliamka asubuhi na kwenda shambani kupanda mpunga, wakiwa huko ghafla lilitanda wingu zito ndipo mvua iliyoambatana na radi ilipoanza kunyesha.

Walisema mvua hiyo kubwa iliyokuwa imeambatana na upepo mkali ilikuwa na muungurumo wa radi wa mara kwa mara. Walisema ilinyesha muda mfupi na ilipokatika walisikia mayowe yakitokea walipokuwa watu hao.

"Baada ya kwenda shambani tulikuta wote hao wameshafariki," alisema mmoja wa mashuhuda hao.

Mtoto ana 'degedege' familia inaenda kwa mganga...

Elimu duni na taabu ya upatikanaji wa tiba rasmi ndiyo kichochezi kikubwa cha imani potofu na kutafuta tiba kwa 'wapiga ramli'...

WATU watano wa familia moja katika Kitongoji cha Benaco, Kata ya Mtandi Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara, wamelazwa katika Hospitali ya Mkomaindo huku hali zao zikiwa mbaya baada ya kunywa dawa ya kienyeji waliyopewa na mganga wa tiba za asili.

Dawa hiyo ya kienyeji inaitwa nyungu, ambayo hutokana na mchanganyiko wa majani tofauti ambayo hupondwa kwenye kinu na kuchanganywa na maji na kuchemshwa.

Mgonjwa hufunikwa kwa nguo nyeupe na kufukizwa na mvuke wa maji hayo kisha huyanywa.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Masasi, Azaria Makubi, alitaja wanafamilia waliolazwa hospitalini ni baba wa familia hiyo Geofrey Evance (43), mke wake, Hadija Salumu (30), dada yake Fidea Evance (40) pamoja na watoto wake wawili, Husna Zuberi (8) na Godfrey Geofrey (10).

Imeelezwa baada ya wanafamilia hao kunywa dawa hiyo, wote hali zao zilibadilika ghafla huku baadhi wakitokwa mapovu vinywani na baadae walipoteza fahamu na kukimbizwa katika hospitali ya Mkomaindo ambako wamelazwa hadi sasa.

Makubi alithibitisha tukio hilo na kusema ni la juzi saa 12:30 jioni katika eneo la Makondeko, Halmashauri ya mji wa Masasi nyumbani kwa mganga huyo.

Alisema wana familia hao walikumbwa na kadhia hiyo baada ya kuitwa na mganga huyo msichana mwenye umri wa miaka 17 (jina tunalihifadhi) kwa lengo la kwenda kumalizia dawa hiyo ya kinga kwa wanafamilia hao kutokana na watoto wao wawili kupewa matibabu na mganga huyo wiki mbili zilizopita.

Mkuu wa kituo, alisema kwa mujibu wa maelezo aliyoyatoa mganga, alitoa dawa hiyo kwa wanafamilia hao waitumie kwa kuoga na kupaka kwenye miili yao na si vinginevyo.

Alijieleza kwamba, baada ya kuwapa, aliingia ndani ya nyumba yake lakini wanafamilia hao walidanganywa na jirani yao (aliyetajwa jina) kuwa ili kinga hiyo iwe ya kudumu na muda mrefu, ni lazima waoge na wanywe maji yake.

Kwa upande wao, wauguzi wa zamu; Prisca Mirumba wa wodi namba moja “B” ya wanaume na Sophia Erasto wa wodi namba sita ya wanawake, walisema waliwapokea wagonjwa hao juzi usiku saa 2:30 wakiwa wamepoteza fahamu huku baadhi yao wakitokwa na mapovu vinywani.

Ilielezwa, walibaini watu hao walipewa kimiminika kinachosadikika kuwa ni sumu. Walipewa matibabu ya awali ingawa hadi sasa kwa mujibu wa wauguzi hao, hali za wanafamilia hao si ya kuridhisha.

Akizungumza kwa tabu akiwa amelazwa kwenye wodi namba sita Hospitali ya Mkomaindo mjini Masasi, baba wa familia hiyo, Geofrey Evance alisema chanzo cha yeye na familia yake kwenda kwa mganga huyo kupata tiba ni baada ya watoto wake kukumbwa na ugonjwa wa degedege.


Alisema baada ya kufika kwa mganga, walipewa dawa hiyo ya nyungu na kisha kushawishiwa na jirani yao wainywe dawa hiyo na kwamba mara baada ya kunywa, walipoteza fahamu na walijikuta wakiwa hospitalini Mkomaindo, mjini Masasi.

Ujumbe kwa aliyeko Tanzania anayehitaji BNF iliyotoka 2014


Kwa mwenye kuhitaji BNF toleo la Septemba mwaka 2014, tuwasiliane 0754876688 au 0715876688. Bei ni shilingi 70,000/= tu.
Evans.

TANESCO yakubali kuwepo 'madudu' kwenye LUKU


Shirika la Ugavi na Usambazaji wa Umeme nchini (TANESCO), limekiri kuwepo na matatizo ya mfumo wa kununua Lipa Umeme Kadiri Utumiavyo (LUKU), ulioanza Ijumaa jioni wiki iliyopita hadi jana na kuwa matatizo hayo yanatokana na mfumo wa kuuza umeme wa LUKU.

Akizungumza na mwandishi jijini Dar es Salaam jana, Meneja Mawasiliano wa TANESCO, Adrian Shogholo alisema ni kweli kuwa tatizo hilo lipo na limetokana na mfumo wa manunuzi wa umeme wa LUKU.

“Ni kweli tunaomba radhi wateja wetu kwamba kuanzia Ijumaa jioni kulianza tatizo la kununua umeme wa luku, kwa wateja wetu, ila tumegundua tatizo na mafundi wetu kwa kushirikiana wa mafundi kutoka Afrika Kusini, ambao walitengeneza mfumo huo, wanalishughulikia tatizo hilo”, 
alisema Shogholo.

Aidha aliahidi kwamba muda wowote kuanzia leo, huduma zitaanza kupatikana na kwamba wakati tatizo hilo likiendelea kushughulikiwa, wateja wa Luku wanaweza kununua umeme kupitia benki ya CRDB, NMB na Max Malipo.

“Kuna wateja wanaotumia simu kununua umeme, wapo waliotuma fedha na hawajarudishiwa majibu ya umeme, na wengine wamepata umeme ila wakiingiza kwenye LUKU hauingii, wasihofu fedha zao ziko salama na watapata umeme, tutawatumia namba nyingine ambazo wakiingiza zitakubali”,
alisema Shogholo.

Mbunge apiga magoti kwa wananchi mbele ya Waziri Mkuu

Mbunge wa jimbo la Songwe Mheshimiwa Philip Mulugo akipiga magoti mbele ya waziri Mkuu Mizengo Pinda katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mbuyuni, Kata ya Gua Wilayani Chunya Mkoani Mbeya

MBUNGE wa Jimbo la Songwe, Mkoani Mbeya, PhilIpo Mulugo, amepiga magoti mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akimuomba waziri huyo kutoa tamko kuhusu ukamilishwaji wa barabara ya Mbalizi - Chunya, kwa kiwango cha lami.

Hali hiyo ilitokea juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mbuyuni Kata ya Gua jimbo la Songwe, alipotakiwa kutoa neno la shukrani na kusalimia wananchi mara baada ya Waziri Mkuu kufika katika halmashauri ya Chunya, ikiwa ni sehemu yake ya ziara iliyolenga kutembelea shughuli mbalimbali za kimaendeleo zinazotekelezwa na serikali pamoja na washirika wa maendeleo katika mkoa wa Mbeya.

Baada ya kupiga magoti huku akimtazama Waziri Mkuu, alisema amekuwa na mtihani kwa wananchi wake kuhusiana na kuanza kwa ujenzi wa barabara hiyo ambayo imekuwa ikizungumzwa mara kwa mara na serikali kuwa ipo katika mikakakati ya kujengwa.

Alisema kero kubwa waliyo nayo kwa sasa wananchi wa jimbo hilo ni ubovu wa barabara hiyo kwani ndio kiungo kikubwa cha kusukuma maendeleo katika jimbo lake la Songwe.

Pamoja na hoja hiyo, pia alimuomba Waziri Mkuu kulipa nguvu za kutosha suala la uanzishwaji wa Wilaya katika jimbo hilo ambalo makao makuu yake yamependekezwa kuwa Mkwajuni.

Akizungumzia hoja hizo za Mbunge kwa kuanza na suala la barabara, Pinda alisema tayari hatua za awali zimekwishafanyika kwa kwa kuufanyika upembuzi yakinifu hivyo amewataka wananchi wa jimbo la Songwe pamoja na mbunge huyo kuwa wavumilivu wakati serikali ikiendelea na mchakato huo.

Alsema pamoja na juhudi hizo pia atajaribu kuzunguzma na Waziri Magufuli ili kufahamu kwa kina juu ya kuanza kwa ujenzi wa barabara hiyo ya Chunya - Mbalizi yenye kilometa 60.

  • via Kalulunga blog

Hotuba ya Rais kikwete ya mwisho wa mwezi Februari, 2015


HOTUBA YA MWISHO WA MWEZI FEBRUARI, 2015, YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, ILIYOTOLEWA TAREHE 1 MACHI, 2015

Utangulizi

Ndugu Wananchi;
Kama ilivyo ada tunamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuzungumza kupitia utaratibu wetu huu mzuri wa hotuba za kila mwisho wa mwezi.  Kwa mwisho wa mwezi wa Februari nina mambo matano ninayopenda kuyazungumzia. 

Zoezi la Uandikishaji Wapiga Kura

Ndugu Wananchi;
        Jambo la kwanza ni uandikishaji wa Wapiga Kura.  Tarehe 24 Februari, 2015 Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda alizindua rasmi uandikishaji wa wapiga kura ikiwa ni sehemu ya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura nchini.  Zoezi hili lilizinduliwa Makambako, Mkoani Njombe na litaendelea nchini kote mpaka litakapokamilika kwa mujibu wa ratiba itakayopangwa na Tume ya Uchaguzi.  Uandikishaji unatumia teknolojia ya kisasa ya utambuzi wa alama za vidole (BVR) na macho ya mtu anayeandikishwa.  Teknolojia hii itatusaidia kuondoa kutoaminiana, manung’uniko na madai kuhusu udanganyifu katika chaguzi zetu kwamba wamepiga kura wasiostahili.  Kuanza kutumika kwa teknolojia hii ni kielelezo cha utashi wa Serikali kuwa nchi yetu iwe na chaguzi zilizo huru, wazi na haki.

Ndugu Wananchi;
        Mtakumbuka kuwa, kabla ya uzinduzi wa zoezi hili, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilifanya zoezi la majaribio ya uandikishaji wa wapiga kura kwa kutumia mashine za teknolojia hii mpya katika kata 10 katika Halmashauri za Kinondoni, Kilombero na Mlele kati ya tarehe 15 hadi 23 Desemba, 2014. 

  Habari njema ni kuwa, kwa kutumia mashine za BVR, idadi ya waliojiandikisha ilivuka lengo la uandikishaji kwa kipindi kilichopangwa katika Kata hizo.  Katika Halmashauri ya Kilombero walioandikishwa walifikiaasilimia 110.9 ya lengo, katika Halmashauri ya Mlele uandikishaji ulifikia asilimia 101ya lengo na katika Jimbo la Kawe, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni walioandikishwa walikuwa asilimia 105.67 ya lengo.    Mafanikio haya ni ya kutia moyo pamoja na changamoto za kiufundi zilizojitokeza na zile zinazotokana na upya wa mfumo wenyewe kwa watumiaji.  Changamoto hizo zimefanyiwa kazi na watengenezaji wa vifaa vinavyotumika katika awamu hii ya uandikishaji wa wapiga kura nchi nzima.

Ndugu Wananchi; 
Nimefarijika na taarifa kuwa zoezi la uboreshaji wa Daftari na uandikishaji wa wapiga kura limeanza vizuri Makambako.  Wananchi wamejitokeza kwa wingi kuliko ilivyotarajiwa.  Kati ya tarehe 23 hadi 25 Februari, 2015 kwa mfano, Tume ilitegemea kuandikisha wapiga kura 9,541 lakini kutokana na mwamko wa wananchi kuwa mkubwa wameweza kuandikisha wapiga kura 13,042.  Kila kituo kilikuwa kinaandikisha kati ya wapiga kura 80 na 150 kwa siku.  Lengo la Tume ni kuandikisha wapiga kura 32,000 katika Halmashauri ya Makambako ambako kwa siku wanatarajia kuandikisha watu 4,320.  Naambiwa kuwa hesabu za juzi na jana wameandikisha hadi wapiga kura 6,000kwa siku.  Kwa kasi hii na kama mambo yatakwenda kama inavyotarajiwa, lengo hilo litafikiwa na hata kuvukwa.

Ndugu Wananchi;
        Hatuna budi kutoa pongeza kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa hatua hii ya kutia moyo tuliyofikia katika mchakato huu.  Inaondoa hofu iliyoanza kuingia miongoni mwa baadhi ya watu kuwa huenda zoezi hili lisingefanikiwa.  Tunachokitaka kwa Tume ni kuona zoezi hili linaendelea na kukamilika kama ilivyopangwa. Napenda kurudia ahadi niliyokwishaitoa kwa Tume kwamba Serikali itafanya kila linalowezekana kuiwezesha kirasilimali ili iweze kutimiza jukumu lake hilo.  Nimekwishawakumbusha Hazina kuhusu umuhimu wa zoezi hili kufanikiwa kama ilivyopangwa.  Hivyo basi, nimewataka wahakikishe kutoa kipaumbele cha kwanza katika mgao wa fedha.   Kama haifanyiki nawaomba Tume waniambie mimi mwenyewe.
        
Wito wangu kwenu, wananchi wenzangu, ni kujitokeza bila ya kukosa kwenda kujiandikisha kwa mujibu wa ratiba ya uandikishaji katika maeneo yenu kama itakavyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.  Msifanye ajizi maana hakutakuwepo na fursa nyingine ya kujiandikisha kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu baada ya fursa hii kupita. 

Ndugu Wananchi;
Kama ilivyoelezwa na Tume na mimi kusisitiza mara kadhaa kuwa watakaojiandikisha wakati huu ndio watakaopiga kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa na ndio watakaopiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.  Vitambulisho vya zamani vya mpiga kura havitatumika, hivyo watu wote ambao ni Watanzania na wana umri wa miaka 18 au zaidi lazima wajitokeze kuandikishwa upya. Watu pekee ambao hawatapaswa kujiandikisha tena ni wale tu walioandikishwa katika zoezi la majaribio lililofanyika katika zile kata 10 za Halmashauri za Kinondoni, Ifakara na Mlele mwezi Desemba, 2014.  Vitambulisho walivyopata ndivyo vyenyewe.

Ndugu Wananchi;
        Napenda kutumia nafasi hii pia kuwaomba viongozi wa vyama vya siasa, Serikali, dini na asasi za kiraia kuungana na Serikali na Tume ya Uchaguzi katika kuwakumbusha na kuwahamasisha wananchi wakajiandikishe.  Naomba tusiwachanganye wananchi kwa kutoa taarifa zisizokuwa za kweli na kuwafanya wakaacha kujiandikisha. Sisi katika Serikali tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa kila atakayejitokeza kujiandikisha anaandikishwa. Aidha, tutahakikisha kuwa kila panapojitokeza changamoto zinatafutiwa ufumbuzi kwa wakati mwafaka. 

Tunatambua kuwa mfumo huu ni mpya hivyo panaweza kujitokeza changamoto zinazosababishwa na upya wake.  Nawaomba wahusika kuendelea kuwaelimisha watendaji wanaohusika ili wapate uzoefu unaostahili.  Aidha, nawasihi wananchi kuwa wavumilivu na waelewa pale ambapo wakati mwingine watalazimika kukaa kwenye mistari kwa muda mrefu kusubiri kujiandikisha, au wakalazimika kuja siku ya pili.

Ndugu Wananchi;
 Kupiga kura kuamua kuhusu Katiba Inayopendekezwa au kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani ni haki na wajibu wa kila raia.  Lakini, kuipata haki hiyo na kuweza kutimiza wajibu huo kunategemea kuwa na kitambulisho cha mpiga kura.  Bila ya hivyo haiwezekani.  Haya shime jitokezeni, mjiandikishe, ili muweze kuitumia haki yenu na kutimiza wajibu wenu wa kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa na kuchagua viongozi mnaowaona wanafaa kuongoza nchi yetu, jimbo lako na kata yako.

Kura ya Maoni

Ndugu Wananchi;
        Jambo la pili ninalotaka kulizungumzia ni kuhusu Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.  Kama mjuavyo, baada ya Bunge Maalumu la Katiba kutunga Katiba Inayopendekezwa na Rais kuchapisha Katiba hiyo katika Gazeti la Serikali na kutangaza siku ya kupiga kura ya maoni, kinachoendelea sasa ni matayarisho ya kufanyika kwa kura hiyo.  Yapo majukumu ya Serikali, yapo majukumu ya Tume ya Uchaguzi, na yapo majukumu ya Serikali na Tume kwa pamoja.  Utekelezaji umeishaanza na unaendelea.  Miongoni mwa mambo yanayotakiwa kufanyika ni uandikishaji wa wapiga kura ambao umekwishaanza na unaendelea.

Ipo pia kazi ya kuchapisha na kusambaza Katiba Inayopendekezwa ili wananchi waweze kuisoma na kuielewa kabla ya kupiga kura ya maoni.  Tayari Katiba Inayopendekezwa imetangazwa katika tovuti za Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo na katika tovuti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.  Pia imechapichwa magazetini. 

Hadi tarehe 27 Februari, 2015 vitabu 1,558,805 vilikuwa vimechapishwa na nakala 1,341,300 kusambazwa.  Nakala 1,141,300zimesambazwa kwenye mikoa 25 ya Tanzania Bara na nakala 200,000zimegawiwa kwa Zanzibar.  Kwa upande wa Tanzania Bara kila Kata imepewa vitabu 300.  Kwa vile Kata zina wastani wa vijiji vitano (5) hii ina maana kwamba kila kijiji kimepata vitabu 60kwa kila kijiji ambayo si haba. 

Ndugu Wananchi;
Tume ya Uchaguzi itatoa maelekezo kuhusu utaratibu wa kutoa elimu kwa umma.  Nimeambiwa tayari asasi za kiraia 420 kwa upande wa Bara na 75 kwa upande wa Zanzibar zimejiandikisha kwa ajili ya zoezi hilo. Halikadhalika, Tume itatoa maelekezo husika kuhusu kampeni ya Kura ya Maoni wakati ukiwadia.  Naomba watu wawe na subira na kuzingatia masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni na Kanuni zake.  Tukifanya hivyo, zoezi hili muhimu na la kihistoria litatekelezwa kwa usalama na utulivu.  Watu watafanya uamuzi kwa uhuru, uelewa, amani na usalama.  

Hali ya Usalama Nchini

Ndugu wananchi;
       
Jambo la tatu ninalotaka kulizungumzia ni hali ya usalama nchini.  Kwa jumla hali ya usalama ni nzuri, hata hivyo kuna matukio ya kiusalama ambayo ningependa kuyazungumzia.  Lakwanza ni mashambulizi yenye sifa za ujambazi na mwelekeo wa kigaidi.  Na, la pilini la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Katika kipindi cha miezi 12 hivi kumekuwa na matukio ya watu kuvamia vituo vya Polisi, wengine wanachoma moto au wengine wanapora silaha.  Pia kumekuwepo na matukio ya kuwashambulia Polisi walioko kwenye doria na wengine kuporwa silaha.  Vituo vya Polisi vilivyovamiwa na silaha kuporwa ni vya Newala Mkoani Mtwara silaha tatu ziliporwa, Ikwiriri katika Wilaya ya Rufiji silaha saba, Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga silaha tano, mbili za polisi natatu za raia waliokwenda kuzihifadhi pale, na Ushirombo Wilaya ya Bukombe silaha 18.  Pugu Machinjioni na Tanga, askari waliokuwa katika shughuli za ulinzi na doria walishambuliwa na kuporwa silaha tatu.  Kule Songea kulikuwepo na matukio mawili ya Polisi kushambuliwa lakini silaha hazikuporwa.

Bahati mbaya, vijana wetu saba wa Jeshi la Polisi walipoteza maisha katika matukio hayo.  Newala alikufa Polisi mmoja, Kimanzichana mmoja, Ikwiriri wawili, na Ushirombo watatu. Wapo Polisi kadhaa waliopata majeraha ya namna mbalimbali katika mashambulizi haya. 

Ndugu Wananchi;
Silaha zote 18zilizoporwa Ushirombo zimepatikana na watu 10wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo wamekamatwa.  Katika tukio la Tanga silaha moja kati ya mbili zilizoporwa imepatikana.  Watuhumiwasaba wametiwa mbaroni, wanne  kati yao ni wale waliokuwa wamejifisha katika mapango ya Kiomoni katika Kitongoji cha Karasha-mikocheni, kilichoko kijiji cha Mzizima wilayani Tanga. Tayari watuwannewanaotuhumiwa kuhusika na tukio la Ikwiriri wamekamatwa.  Polisi wanaendelea na upelelezi kuwapata watu wengine na kuzipata silaha sabazilizoporwa kituoni hapo.  Kwa tukio la Newala silaha zotetatu zimepatikana pamoja na bastola moja ya mtuhumiwa aliyehusikaa  na watu wawiliwametiwa nguvuni.  Hali kadhalika, upelelezi unaendelea wa kuzipata silaha zilizoporwa ambazo hazijapatikana mpaka sasa: yaani Kimanzichana moja, Pugu Machinjioni moja na Tanga iliyosalia moja

Ndugu Wananchi;
        Matukio haya yana sura mbili.  Yana sura ya ujambazi, lakini pia baadhi yake yana dalili za ugaidi.  Vyombo vyetu vya usalama vinaendelea kufanya kazi yake ya uchambuzi wa kila tukio na kulipa nafasi yake stahiki.  Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa Jeshi la Polisi wakishirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na vyombo vingine vya usalama kwa kazi kubwa na nzuri waifanyayo kupambana na uhalifu nchini.  Mafanikio tunayaona, kama nilivyoeleza na kama tulivyosikia kule Tanga hivi karibuni ni matunda ya ushirikiano huo.  Hata hivyo, nimewataka waendelee kuwasaka watu hawa waovu po pote walipo ili wafikishwe mahakamani na kuzirejesha mikononi mwa Polisi silaha zote zilizoporwa. 

Nawaomba wananchi wenzangu wote kushirikiana kwa karibu na vyombo vya usalama hususan Jeshi la Polisi ili tuweze kupata mafanikio zaidi dhidi ya uhalifu huu na uhalifu mwingineo. Nawaomba mfanye mambo mawili:  

Kwanza, toeni taarifa Polisi mnapozipata habari za vitendo viovu au nyendo za watu waovu wanavyokusudia kufanya wahalifu au taarifa za wale waliokwishafanya uhalifu. 

Pili, naomba watu waache kuwashabikia watu hawa waovu wala kueneza taarifa zao potofu kwenye mitandao ya kijamii.  Badala yake tutumie mitandao ya kijamii kuponda fikra zao potofu, fikra zao hasi na vitendo vyao viovu pamoja na kuwafichua wao na mambo yao mabaya wayafanyo.  Napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wote walioweza kutoa taarifa zilizowezesha kuzuia uhalifu usifanyike au zilizowezesha kutiwa mbaroni kwa wahutumiwa wa vitendo vya ujambazi na ugaidi.    Hatuwezi kushinda uhalifu bila ushirikiano baina ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama.

Mauaji ya Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi

Ndugu wananchi;
        Nimesikitishwa sana na taarifa kuwa mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) yameibuka upya baada ya hali kuwa tulivu mwaka 2011.  Mwaka jana (2014) yalitokea matukio matatukatika mikoa ya Mwanza, Tabora na Simiyu na mwaka huu limetokea tukio moja mkoani Geita.

Lazima tulaani vikali mauaji ya ndugu zetu albino.  Ni vitendo vya kinyama ambavyo havitegemewi kufanywa au kutokea katika jamii yeyote ya watu waliostaarabika, ya watu wanaomuabudu Mungu.  Watu wenye ulemavu wa ngozi ni wanadamu wenzetu, wenye haki sawa ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yao kama walivyo wanadamu wengine.  Hawastahili kufanyiwa wanayofanyiwa.  Hawapaswi kuishi kwa hofu katika kijiji chao, mtaa wao au katika nchi yao.  Jamii nzima na sisi sote mmoja mmoja na katika umoja wetu, tunao wajibu wa kuhakikisha usalama wa maisha yao na mali zao kama ilivyo  kwa watu wengine wote. 

Kwa kweli, mauaji ya albino ni jambo linalofedhehesha na kulidhalilisha taifa letu.  Ni vitendo visivyovumilika.   Hatuna budi sote kushikamana na kuhakikisha kuwa tunapambana nao kisawasawa na kuwashinda.  Tusikubali kamwe wakaturudisha kule kubaya tulikokuwa zamani.    Naungana na Chama cha Albino Tanzania kulaani ukatili huu na kutaka watu wote wanaojihusisha na ukatili huu wasakwe, wakamatwe, wafikishwe Mahakamani na kupewa adhabu kali inayowastahili wanapopatikana na hatia. 

Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa wakati wote Serikali imelipa uzito mkubwa suala la kudhibiti na kukomesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi au kukatwa baadhi ya viungo vyao wenyewe wakiwa hai.  Tumefanya hivyo bila ya kuchoka tangu tukio la kwanza baada ya mimi kuingia madarakani Aprili 17, 2006 na miezi mitatu tu  kule Nyahunge, Geita alipouawa Alfa Amon ambapo watuhumiwa wawili waliuawa na raia.  Mwaka 2007 kulikuwa na matukio saba.  Mwaka 2008 ndio ulikuwa mwaka mbaya sana walipouawa watu 18. 


Kutokana na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wananchi mauaji yalipungua na kuwa tisa mwaka 2009.  Mwaka 2010 kukawa na tukio moja na mwaka 2011 hapakuwepo na tukio lolote.  Mwaka 2012 kukawa na tukio moja, mwaka 2013 aliuawa mtu mmoja na wawili kujeruhiwa.  Mwaka 2014 waliuawa watu watatu na wawili kujeruhiwa, na Januari, 2015 kumetokea tukio moja kule Geita

Ndugu Wananchi;
        Tangu mwaka 2006 mpaka 2015, watuhumiwa 139 wametiwa nguvuni, miongoni mwao wako watuhumiwa 16 wa matukio ya Desemba na Januari mwaka huu. Mashauri 35yamefunguliwa mahakamani na kati ya hayo 10bado yanaendelea na yapo katika hatua mbalimbali.  Watuhumiwa 73 wameachiliwa na15wamepatikana na hatia.  Kati ya hao waliopatikana na hatia 13 wamehukumiwa kifo na wawili wamepata kifungo cha miezi 6.  Watuhumiwa kwa matukio sita bado wanasakwa.

Matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yametokea katika mikoa kumikati ya mikoa 30 hapa nchini.  Mikoa hiyo ni hii ifuatayo:  Mwanza matukio 13, Kagera sita, Tabora matano, Geita manne, Maramanne, Kigoma manne, Simiyu matatu, Shinyanga mawili, Arusha moja na Mbeya moja.  Utaona matukio41 kati ya 43 yametokea katika ukanda wa ziwa ambapo pia wanaongoza kwa mauaji ya vikongwe na wanawake kwa sababu za ushirikina. 


Ndugu Wananchi;
        Inawezekana kuwa matukio ya hivi karibuni yanaashiria kuwa uhalifu huu unataka kuibuka upya. Napenda kuwahakikishia ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi na Watanzania kwa jumla, kuwa hatutaacha hali iwe mbaya kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.  Tutatumia mbinu na maarifa tuliyoyatumia kukabili wimbi kubwa la mauaji lililokuwepo mwaka 2007 na 2008 na kwa sababu hiyo tukaweza kupunguza hadi kufikia kutokuwa na tukio lolote la mauaji mwaka 2011. 

Tunachokiomba kutoka kwa wananchi ni ushirikiano na msaada wa kuwafichua watu wanaofanya vitendo vya mauaji na kukata viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi.  Pia wasaidie kutoa taarifa kuhusu wanunuzi wa viungo hivyo na waganga wanaochochea mahitaji ya viungo vya albino.  Ushirikiano wa wananchi wa wakati ule uliwezesha kupatikana kwa mafanikio niliyaeleza.  Naamini safari hii tukifanya hivyo tutafanikiwa pia.

Ndugu Wananchi; 
Kutokomeza kabisa matukio ya mauaji na ukataji wa viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi ni jambo linalowezekana.  Hata hivyo, litategemea watu kuacha imani za ushirikina.  Imani potofu, ati kuwa mtu akiwa na kiungo cha mtu mwenye ulemavu wa ngozi atafanikiwa katika shughuli zake za biashara, uvuvi na uchimbaji wa madini ndicho kichocheo cha uovu wote huu unaoendelea.  Ni ujinga ulioje kwa mtu kuamini kuwa mafanikio yake hayatategemea juhudi zake na maarifa yake bali kuwa na kiungo cha mwanadamu mwenzake mwenye ulemavu wa ngozi. 

Nilisema katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi Machi, 2008 kwamba, kama kuwa na kiungo cha albino ndiko kutakakomfanya mtu kufanikiwa katika shughuli zake za kibiashara na kiuchumi basi ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi wangekuwa ndiyo matajiri wakubwa nchini na duniani.  Maana wao sio tu wana viungo bali wana mwili mzima.    Kwa sababu ya kuwepo imani hizi za hovyo, juhudi za kuelimisha jamii kuachana na imani hizi potofu ziongezwe.  Naomba hili ndilo liwe jambo la msingi katika mapambano haya.  Tukifanikiwa katika hili, matatizo yote haya yatakoma.  Serikali na jamii haitalazimika kushughulikia mambo haya ambayo siyo tu ni fedheha hata kumsimulia mtu bali yanatisha na kusikitisha.

Ndugu Wananchi;
        Wiki ijayo nitakutana na baadhi ya viongozi na wanachama wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi.  Nimekubali maombi yao ya kukutana nao ili niweze kusikiliza maoni yao na tubadilishane mawazo juu ya namna bora ya kumaliza tatizo hili.  Mimi naamini kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na jamii utatuwezesha kutokomeza mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi na kuliondolea taifa letu aibu hii.

Ziara ya Zambia

Ndugu Wananchi;
        Tarehe 25 na 26 Februari, 2015 nilifanya ziara ya siku mbili ya kiserikali nchini Zambia kwa mwaliko wa Rais mpya wa nchi hiyo, Mheshimiwa Edgar Lungu.  Ziara ilikuwa na mafanikio makubwa.  Mimi na ujumbe wangu tulifarijika sana kuona kuwa mawazo ya nchi zetu mbili yanashabihiana sana kuhusu namna ya kuimarisha na kuboresha uhusiano wetu na ushirikiano na uhusiano wa nchi zetu mbili.  Kimsingi tumekubaliana katika masuala yote muhimu tuliyoyazungumza.    


Kuhusu TAZARA tumekubaliana kuchukua hatua thabiti kutatua matatizo ya kiungozi, kifedha na kiufundi yanayolikabili shirika letu hilo hivi sasa.  Tumeelewana kuwa hatuna budi kufanya marekebisho ya kimfumo na kiutendaji ili kutatua matatizo ya kimuundo na kimenejimenti yanayochangia kuzorota kwa ufanisi wa Shirika.    Tumekubaliana pia kuwa, Serikali zetu mbili zitekeleze ipasavyo wajibu wake kwa TAZARA ikiwa ni pamoja na kutoa mchango wake wa fedha kwa ajili ya kulifufua Shirika hili muhimu kwa uchumi wa nchi zetu mbili.

Ndugu Wananchi;
Tumekubaliana pia, kwamba, tuangalie uwezekano wa kuruhusu makampuni au mashirika mengine ya reli kutumia reli ya TAZARA kusafirishia mizigo yao kwa kulipa ushuru kwa TAZARA kwa huduma hiyo.  Tumeagiza Baraza la Mawaziri kulifanyia kazi wazo hili jema ili litekelezwe mapema iwezekanavyo. 

Kwa upande wa sekta ya nishati, tumekubaliana  kuwa, nchi zetu mbili ziendelee kushirikiana kuimarisha bomba la mafuta la TAZAMA. Ndugu zetu wa Zambia walitueleza dhamira yao ya kutaka kujenga bomba la kusafirisha gesi kutoka Dar es Salaam hadi Zambia.  Wameomba tukubali kuwauzia gesi asilia.  Niliwaeleza ni jambo linaowezekana, tumekubaliana nchi zetu zilifanyie kazi ombi hilo.

Serikali ya Zambia, imeahidi kuimarisha njia ya umeme kutoka Kasama hadi Mbala Zambia inakoanzia njia inayoleta umeme Sumbawanga.  Kufanya hivyo kutaondoa matatizo ya sasa ambapo umeme unaofika Sumbawanga kutoka Mbala huwa mdogo kiasi kwamba hauna nguvu ya kutosha kwa matumizi ya nyumbani, maofisini na viwandani.  Kwa sababu hiyo, hata mpango wa kuupeleka umeme huo Namanyere, Nkasi na Mpanda haukuweza kutekelezwa kama ilivyokuwa imekusudiwa awali.

Ndugu Wananchi; 
Kuhusu kuboresha huduma kwa abiria na mizigo katika mpaka wa Tanzania na Zambia pale Tunduma, tumekubaliana kuwa, Serikali ya Tanzania ikamilishe ujenzi wa jengo  litakalowezesha huduma zote muhimu za mpakani kutolewa katika jengo hilo (One Stop Border Post).  Wakati tunasubiri kukamilisha ujenzi huo, tumekubaliana tuwe na jengo la muda la kurahisisha taratibu za usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo katika mpaka wetu na Zambia.

Vilevile, tulizungumzia njia za kuimarisha na kuboresha taratibu za forodha kwa mizigo itokayo bandari ya Dar es Salaam kwenda Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia Zambia.  Tumekubaliana kuwa, Mamlaka ya Kodi ya Mapato ya Zambia iangalie uwezekano wa kuwaweka maafisa wake katika Bandari ya Dar es Salaam kama inavyofanyika kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Hii itarahisisha taratibu za forodha kwa bidhaa za Zambia katika bandari yetu.  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeshaanza mchakato wa kupata fursa hiyo.  Kwa jumla, ziara ilikuwa ni yenye mafanikio makubwa.

Rambirambi

Ndugu Wananchi;
        Wakati tulipokuwa tunajiandaa kurekodi hotuba hii tukapata habari ya huzuni na majonzi makubwa ya kifo cha Mbunge wa Mbinga Magharibi, Mheshimiwa Capt. John Damian Komba.  Kifo chake kimeliondolea taifa letu mmoja wa viongozi wake wazuri, msanii mahiri, raia mwema na mzalendo wa kweli.  Marehemu alitumia muda mwingi wa maisha yake kuelimisha jamii kuhusu mambo mema, amefanya hivyo akiwa mwalimu na baadaye Kiongozi wa Kikundi cha Sanaa cha JWTZ na hapa mwishoni kiongozi wa kikundi cha Tanzania One Theatre cha Chama Cha Mapinduzi.  Kwa kutumia kipaji alichojaaliwa na Mola wake ametoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu na ustawi wa Chama Tawala.  Daima tutamkumbuka kwa mambo mengi mema aliyoifanyia jamii ya nchi yetu na taifa kwa jumla.

Ndugu Wananchi;
        Katika salamu zangu za rambirambi kwa Spika wa Bunge na Katibu Mkuu wa CCM niliwaomba kupitia kwao salamu ziwafikie Wabunge wote na viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi.  Hali kadhalika, niliomba kupitia kwao salamu ziwafikie familia ya marehemu Capt. John Komba.  Kwa familia ya ndugu yetu mpendwa, napenda  kuwahakikishia kuwa tuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na maombolezo.  Tunawaombea kwa Mola awape moyo wa subira na uvumilivu.  Wananchi wa Wilaya ya Nyasa tunawapa pole nyingi kwa msiba mkubwa uliowakuta na pengo kubwa mlilolipata.  Nawaomba watambue kuwa namna bora zaidi ya kumlilia Mbunge wao aliyewapenda ni kudumisha mema yote aliyofanya na kukamilisha zile kazi ambazo alikusudia kuzifanya lakini hakuweza kufanya hivyo kwa sababu ya kukutwa na umauti.
        
Mwisho nawaomba, Watanzania wote tuungane na familia yake kumwombea marehemu Capt. John Damian Komba mapumziko mema.  Amin.

Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibari ki Tanzania!

Asanteni kwa kunisikiliza.

Waziri Nyalandu awaaga wafanyabiashara wanashiriki maonesho ya ITB Ujerumani


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu akitoa nasaha za kuwaaga wafanyabiashara wa Tanzania wanaoenda Berlin, Ujerumani kushiriki maonyesho makubwa Duniani ya biashara maarufu kama ITB kuanzia Machi 4-8 mwaka huu.(picha: modewjiblog)

Na Andrew Chale / modewji blog

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu amewataka wafanyabiashara wa Tanzania wanaoenda kushiriki maonyesho makubwa Duniani ya biashara maarufu kama ITB, mjini Berlin, Ujerumani Machi 4 hadi 8, mwaka huu, kubeba uzalendo na kuitangaza Tanzania hususani vivutio vya Utalii na utajiri wa maliasili ili kuvutia wawekezaji.

Nyalandu aliyasema hayo usiku wa Februari 27, wakati wa halfa fupi ya kuwaaga wafanyabiashara hao ambapo alisema kuwa, kwenda kwao huko kushiriki maonyesho hayo makubwa kabisa duniani, ni fursa kama Tanzania kupata kujitangaza zaidi na kuvutia wawekezaji.

“Leo hii tunawaaga hapa. Nyie ndio Tanzania hivyo mnapokuwa huko mjue mmebeba watanzania wengine zaidi ya Milioni 40. Ni wakati wa kuvitangaza vivutio na uzuri wa Tanzania na ilikuongeza soko letu la Utalii na uwekezaji” alieleza Nyalandu.

Pia aliongeza kuwa, Wizara yake ya Utalii itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha Taifa la Tanzania linafikia malengo yake yaliyokusudiwa ikiwemo kujitangaza ndani na nje ikiwemo kuendelea kuunga mkono juhudi za kupambana na Uharamia dhidi ya meno ya Tembo, wanyama na nyara za serikali kiwemo pembe za ndovu.

Deputy Head of Mission wa Ubalozi wa Ujerumani, John Reyels akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla hiyo.Afisa wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Devota Mdachi (kushoto) akiwa na Dorothy Masawe (Kulia) kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, wakifuatilia jambo kwa makini wakati wa halfa hiyo.Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Lazaro Nyalandu akibdilishana mawazo na baadhi ya wageni waalikwa.Deputy Head of Mission wa Ubalozi wa Ujerumani, John Reyels (kulia), Afisa wa Ubalozi wa Ujerumani kitengo cha habari, John Meirikion (kushoto) wakiteta jambo na mmoja wa wageni waalikwa.CEO wa DHL ukanda wa Eastern Africa, Pramod Bagalwadi, akisalimiana na Waziri Maliasili na Utalii, Mh. Lazaro Nyalandu kwenye hafla hiyo.Baadhi ya wageni waalikwa ambao ni wafanyabiashara katika sekta utalii wakibadilishana mawazo kwenye hafla hiyo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Lazaro Nyalandu katika picha ya pamoja na Afisa wa Ubalozi wa Ujerumani kitengo cha habari, John Meirikion wakati wa hafla hiyo.Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Lazaro Nyalandu katika picha ya pamoja na wafanyabiashara akiwemo Mkurugenzi wa Mauzo wa Hoteli ya DoubleTree by Hilton Bw. Florenso Kirambata ( wa pili kushoto).Mkurugenzi wa Biashara wa Flight Link, Bw. Ibrahim Bukenya akiwa na Deputy Head of Mission wa Ubalozi wa Ujerumani, John Reyels wakati wa hafla hiyo.Wadau wakifurahi jambo.