Mambo 5 ya msingi ukitaka kufungua au kukuza biashara

(picha: shopify.com)

Je una malengo ya kuanzisha biashara au una nia ya kuikuza biashara yako? Basi ni muhimu sana kufahamu mambo ya kuzingatia katika biashara ili biashara yako iende vizuri. Wakati mwingine unaweza kujiuliza ni mbinu gani utumie ili kukuza biashara, ukweli ni kwamba licha ya kuwa na ushindani mkubwa wa kibiashara bado wewe kama mfanyabiashara una uwezo mkubwa wa kupandisha soko na kukuza biashara yako. Yafuatayo ni mambo 5 muhimu ya kuzingatia unapotaka kufungua au kukuza biashara yako.

1. Fanya biashara ya kipekee


Fikiri na kuwa mbunifu katika kubuni na kuibua biashara mpya. Mfano kama mahali unapotaka kufanya biashara kuna maduka ya nguo na vitu vya makazini na majumbani au biashara nyingine maarufu. Ikiwa mahali pa biashara kuna mzunguko wa watu wengi na kuna mazingira ya kupata faida nzuri unaweza kufanya biashara kama wanazofanya wengine lakini bado una kila sababu ya kuongeza biashara nyingine kwa kubuni na kuibua biashara mpya tofauti na za wafanyabiashara wengine. Kufanya hivyo utaweza kuwa mfanyabiashara wa kipekee kwa kuwa na huduma nyingi ambazo watu huhitaji kuhudumiwa. Moja ya siri ya kuongeza wateja katika biashara yako ni kuwa na huduma nyingi anazohitaji mteja. Kuwa mjanja kwa kujua wateja wako wanataka nini ili uweze kuwasogezea huduma karibu.

2. Pata mshauri wa biashara (business mentor)


Unapokuwa katika wakati mgumu wa kutatua matatizo yako ya kibiashara au unapokuwa na utata katika kufanya maamuzi sahihi ya namna ya kuanza biashara ni vizuri utafute ushauri kutoka kwa watu ambao tayari wamefanikiwa katika biashara kama yako. Pia unaweza kutafuta watu wa kukufundisha jinsi ya kufanya biashara yaani “Business Mentors” ambao watakusaidia kupata ujuzi sahihi na kukupatia maarifa kuhusu biashara yako.

3. Thaminisha bidhaa unazoziuza


Iwe biashara ndogo au kubwa bidhaa unazouza ni muhimu ziwe zenye ubora na mwonekano mzuri utakaomvutia mteja.Watu hupenda vitu vizuri, bora na vinavyodumu hivyo ni vema utengeneze bidhaa zenye ubora na thamani

4. Jiamini na usikate tamaa


Kuna wakati unapoanza biashara mambo huwa mabaya hivyo ni vema ujiamini na utafakari ni wapi umekosea au ni nini cha kufanya ili uboreshe biashara yako. Wakati mwingine unapoanzisha biashara inachukua muda watu kujua unauza nini hivyo swala la muda wa watu kujua biashara yako nalo ni jambo la kuzingatia. Hakuna mafanikio ya haraka hivyo uvumilivu na ukakamavu wako ni muhimu sana katika kukuza biashara yako. Kumbuka usikae na kusubiri sana watu waifahamu biashara yako, weka na bidii zako katika kuongeza na kupanua mtandao wa wateja wako.

5. Fanya biashara uipendayo (find your passion)


Inaaminika kuwa ikiwa mtu atafanya kazi aipendayo basi ataifanya kwa uhodari na utashi wake kuweza kupata mafanikio makubwa, swala hili ni muhimu katika kuamua ni biashara gani unapenda kuifanya. Maendeleo na mafanikio makubwa ya kazi yeyote ile huletwa kwa kufanya kazi unayoiridhia na kuipenda.

Hayo ni mambo machache na ya kawaida ya kuzingatia katika biashara yako, kuwa na ndoto kubwa ya kufanikiwa kibiashara ni vizuri lakini pia penda kujua mengi kuhusu mahusiano ya biashara yako na wateja wako kwani biashara ni watu hivyo kuwa makini kwa kila hatua unayopiga kibiashara ili kuepuka hasara.

TUPO PAMOJA
  • Makala hii imeandikwa na Geofrey Mwakatika. Unaweza kutembelea blog yake Geofrey Mwakatika kujifunza zaidi.

Ofisa Ikulu na fedha za Rugemalira: "Nakiri kupokea fedha hizo Sh milioni 80.8, lakini..."

Mnikulu wa Ikulu, Shaban Gurumo mbele ya Kamati ya Maadili kwa Watumishi wa Umma

Mnikulu Shaban Gurumo amekiri mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, kwamba alipokea Sh milioni 80.8 kutoka kwa James Rugemalira na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi, ingawa amekanusha kuomba fedha hizo.

Gurumo alitoa utetezi huo Dar es Salaam jana mbele ya baraza baada ya kusomewa mashitaka ya kutumia cheo chake cha uongozi wa umma vibaya na kujipatia fedha hizo, jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Alikiri kumfahamu Rugemalira, akisema ni rafiki yake kwa zaidi ya miaka 10. Alisema daktari wake, Fred Limbanga ndiye aliyemtambulisha kwa Rugemalira.

“Kama Mnikulu sijawahi kupokea fedha za kiuchumi kwa Rugemalira wala kuwa na mahusiano naye ya kiuchumi, naitambua akaunti ya Mkombozi kuwa ni ya kwangu na niliifungua baada ya James kunishauri,” 
alisema Gurumo.

Alisema awali hakufahamu nani aliyemwekea kiasi hicho cha fedha kwenye akaunti hadi hapo baadaye alipotambua kuwa ni Rugemalira. Alidai hadi sasa hajafahamu sababu za kupewa kiasi hicho cha fedha na wala hakuhangaika kumuuliza Rugemalira.

Pia, alisisitiza kuwa pamoja na kutofahamu fedha hizo alipewa za matumizi gani, ana uhakika si zawadi kama inavyodaiwa.

“Ila nahisi baada ya kuitwa na Kamati ya Uchunguzi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kujibu tuhuma zinazonikabili, huenda Rugemalira alinitumia fedha hizo baada ya kusikia kuwa nina mgonjwa anayeumwa saratani ya mfuko wa uzazi,”
 alisema.

Alisisitiza kuwa hajawahi kuzungumza wala kuomba fedha si kwa barua, simu wala kwa mazungumzo ya ana kwa ana na Rugemalira, ila amekuwa akizitumia kwa shughuli zake binafsi kwa kuwa alizikuta kwenye akaunti yake. “Sijawahi kuomba fedha yoyote kwa Rugemalira wala VIP,” alisema.

Alisema pia hata katika tamko la mali na madeni, aliloliwasilisha Desemba 29, mwaka jana kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, akiwa kama kiongozi wa umma, aliziorodhesha fedha hizo kuwa ni mali yake iliyopo katika akaunti yake ya Benki ya Mkombozi alizopewa na Rugemalira.
Alikiri kuwa alikuwa na matatizo ya kuwa na mgonjwa huyo, aliyempeleka India kwa matibabu na hadi sasa ameshatumia dola za Marekani 40,000 ambayo ni sawa na Sh milioni 73.2, hivyo hakuwa na shida yoyote ya fedha. “Mimi nina fedha zaidi ya hizo za Rugemalira ndio maana sikuomba.”

“Nakiri kupokea fedha hizo Sh milioni 80.8, lakini nilishangaa kwa mara ya kwanza niliposikia kwenye redio iliyokuwa ikirusha hewani kipindi cha Bunge, mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alikuwa akisisitiza nilipewa Sh milioni 800 na kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, jambo ambalo si la kweli,” 
alisema.

Aliomba baraza hilo kuwachukulia hatua na kuwachunguza wale wote waliodanganya, wakiwemo wabunge na vyombo vya habari pamoja na mitando ya kijamii, kuhusu kiasi cha fedha alizopatiwa na Rugemalira ili ifahamike kama wamefanya makusudi, wametumika au la.

Awali, akimsomea mashitaka mbele ya baraza hilo, Mwanasheria wa Sekteratieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Hassan Mayunga alidai mlalamikiwa akiwa kiongozi wa umma, aliomba na kupokea Sh milioni 80.8 kutoka kwa kampuni ya VIP kinyume cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Aidha alidai mlalamikiwa huyo, alipokea kiasi hicho cha fedha kinyume cha sheria hiyo, inayokataza kiongozi wa umma kuomba na kupokea fedha kwa maslahi yake binafsi.

Alidai Februari 5, mwaka jana alipokea Sh milioni 80.8 kutoka kwa VIP kupitia akaunti yake namba 00110102645401 iliyopo katika Benki ya Mkombozi tawi la St Joseph jijini Dar es Salaam.

Shahidi upande wa Sekretarieti hiyo, ambaye ni Ofisa Uchunguzi, Bazilio Mwanakatwe, alidai kupitia kamati ya uchunguzi iliyoundwa na sekretarieti hiyo, walibaini Gurumo alikiuka maadili ya viongozi wa umma, kutokana na kupokea kiasi hicho kikubwa cha fedha bila kukitamka kwa viongozi wake ili kipangiwe matumizi.

“Sheria inatamka wazi kuwa kiongozi wa umma haruhusiwi kuomba au kupokea zawadi kubwa kwa maslahi yake isipokuwa zawadi ndogo isiyozidi Sh 50,000 na endapo itazidi atatakiwa kutamka zawadi hiyo na kukabidhi kwa Ofisa Masuhuli wake ili waweze kuipangia namna ya kuitumia zawadi hiyo,” alisema.

Alidai kamati hiyo ilibaini pia uwepo wa mgongano wa malsahi ambapo Gurumo ambaye ni Mnikulu wa Ofisi ya Rais, kwa nafasi aliyonayo anafahamu siri nyingi na kupata fursa nyingi hivyo kitendo cha kupokea fedha kutoka kwa mwekezaji mkubwa ni kujiingiza katika mgongano wa maslahi.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Getrude Cyriacus, alidai Gurumo, baada ya kuingiziwa fedha hizo, hadi sasa ameshatoa na kutumia zaidi ya Sh milioni 77.

Hoja za kila upande kuhusu shauri hilo, zimepangwa kuwasilishwa tena mbele ya baraza hilo, Machi 13, mwaka huu.

Wakati ofisa huyo wa Ikulu akiwa miongoni mwa viongozi wa umma watano waliokwishafikishwa mbele ya baraza kwa madai ya kukiuka maadili, leo Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Philip Saliboko, pia anapandishwa kizimbani kujibu mashitaka akidaiwa kupatiwa Sh milioni 40.4 kutoka Kampuni ya VIP.

Wakati huo huo, leo baraza hilo linatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu pingamizi lililowasilishwa juzi na aliyekuwa Mkurugenzi wa Ushauri wa Kisheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma aliyetaka shauri linalomkabili la kupokea Sh milioni 423, liahirishwe kusikilizwa kutokana na kesi ya msingi iliyopo Mahakama Kuu.

  • HabariLeo
Habari kuhusu suala hili ipo pia katika tovuti ya MwanaHalisi online

Kambi ya kupima afya bure kwa watoto wa chini ya miaka 5


 

Na Andrew Chale modewji blog

Imeelezwa kuwa, Sensa ya mwaka 2012 ilionesha kuwa asilimia 42 ya watoto chini ya miaka 5 hapa Nchini Wamedumaa, asilimia 16 wana uzito pungufu (wako underweight), asilimia 5 wamekonda (marasmic) wako kwenye kadi nyekundu ya mtoto.

Hayo yamesemwa jana Machi 4, jijini Dar es Salaam, na Mkurugenzi Mtendaji wa Kliniki ya kimataifa ya afya ya uzazi kwa baba, mama, mtoto na vijana (AMM), Dk Ali Mzige mbele ya wandishi wa habari wakati wa kutoa taarifa juu ya kambi ya upimaji wa afya kwa watoto wa chini ya umri wa miaka 5, itakayofanyika Jumapili ya Machi 8, katika shule ya Msingi Kibugumu iliyopo Kigamboni, wilaya ya Temeke.

Dk. Mzige alibainisha kuwa kama ilivyo kwa watu wazima, upimaji wa afya ya watoto wenye umri chini ya miaka 5 una manufaa makubwa kwa mtoto, familia na jamii ya watanzania wote.

Ambapo alibainisha kuwa, tatizo la utapia mlo kwa watoto hapa nchini imepelekea Tanzania kuwa nafasi ya tatu katika Bara la Afrika, Lishe duni kwa watoto na wajawazito huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ikiongoza na Ethiopia ikiwa ni ya pili kwa tatizo hilo la utapiamlo.

Pia alieleza kuwa tatizo lingine ni la utapiamlo la kula chakula kupita kiasi kama vyakula vyenye wanga na sukari kwa wingi, mafuta kwa wingi na kuleta maradhi/magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa watoto na watu wazima.

Aidha, Dk. Mzige alisema kuwa elimu sahihi dhidi ya kupambana na maradhi hayo ya utapiamlo, yatatolewa kwenye kambi hiyo huku akisisitiza wazazi kujitokeza kwa wingi siku hiyo, kwani itakuwa ni ya kipekee na faida kwao na kwa watoto wao.

“Tujitokeze kupima afya zetu na pia watoto hasa wadogo. Hivyo kambi hii itakuwa msaada mkubwa kwani tutachunguza yale magonjwa mengi yanayowakabili watoto wengi hapa nchini.” Alisema Dk. Mzige.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kliniki ya kimataifa ya afya ya uzazi kwa baba, mama, mtoto na vijana (AMM), Dk Ali Mzige (katikati) akizungumza na wandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya Kambi ya kupima afya bila malipo kwa watoto wadogo, itakayofanyika Jumapili ya Machi 8 mwaka huu. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa umoja wa jamii ya watu kutoka India Bengali waliopo hapa Tanzania, BANGO SANGHO, Amit Nandy na kulia ni mwakilishi wa shule ya Kibugumu, Mwalimu Mzamili Ally.

Akitoa baadhi ya takwimu zinazowakabili watoto wengi hapa nchini, ni pamoja na :

Watoto 130, walio chini ya umri wa miaka 5 hufa kila siku hapa Nchini kwa ajili ya utapiamlo (Malnutrition-Lishe duni).

Upungufu wa wekundu wa damu asilimia 59 kwa watoto wenye miezi 6 hadi 59. Asilimia 33 ya watoto chini ya miaka 6 wana ukosefu wa vitamin A.

BANGO SANGHO, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa umoja wa jamii ya watu kutoka India Bengali waliopo hapa Tanzania, BANGO SANGHO, Amit Nandy alisema kuwa kwa kushirikiana na Kliniki ya kimataifa ya afya ya uzazi kwa baba, mama, mtoto na vijana (AMM), ya Jijini Dar es Salaam ambapo wameandaa kambi hiyo ya kupima afya bila malipo kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5 ni faraja kwa jamii hiyo kwani watoto wengi hapa Nchini wamesahulika katika kupimwa afya zao.


Amit Nandy aliwataka wananchi wa Kigamboni na maeneo mbalimbali kuwapeleka watoto wao katika shule ya Msingi, Kibugumu kwa ajili ya kupimwa afya zao hizo ikiwemo magonjwa yanayowakabili watoto wengi.

“wazazi wote tunawaomba kujitokeza kwa wingi, Machi 8, katika shule ya Msingi Kibugumu mukiwa na watoto wenu pamoja na makadi ya kliniki ilikuweza kupata huduma ya matibabu bure.

Madaktari bingwa na matabibu watapima magonjwa mbalimbali ikiwemo Afya ya kinywa, Uzito, Ukaguzi na ushauri wa lishe. Pia watakaobainika kuwa na matatizo maalum ya kiafya watapewa rufaa” alieleza Amit Nandy.

Ambapo alibainisha kuwa, huduma hizo za matibabu zinatarajiwa kutolewa kuanzia asubuhi ya saa tatu hadi saa saba mchana. (Saa 3:30 asubuhi-Saa 7-30 mchana).Dk. Mzige akionyesha mswaki wa mti ambai ni wa asili, ambapo alishahuri watanzania kuwa na tabia ya kubadilisha miswaki yao kila baada ya miezi mitatu, ama kutumia miswaki ya miti ambayo inasaidia kuboresha meno.Dk. Mzige akionesha Yai ambapo alibainisha kuwa Yai sio zuri kwani lina Cholesterol hivyo mtu anashahuriwa kula mayai matatu kwa wiki hasa ya kuchemsha.


Hata hivyo Dk. Mzige alibainisha kuwa, utapiamlo huo unaonekana nchini upo kwenye mikoa inayozalisha chakula na matunda kwa wingi ikiwemo ya Morogoro, Mbeya, Tanga, Rukwa, Iringa na Manyara.Dk Mzige akionyesha soseji ambapo alisema kuwa ulaji wa soseji sio mzuri kwa afya hivyo watu wanatakiwa kuepuka ama kupunguza.Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari waliohudhuria mkutano huo.

Tanzania National Parks fees for 2015/2016


Taarifa kuhusu hali ya afya ya Naibu Spika Ndugai


Zitto: Tuhuma dhidi yangu zichunguzwe

Katika kujitetea mbele ya Baraza la Maadili kuhusu tuhuma dhidi yake za kugawiwa mgawo wa fedha kutoka akaunti ya Escrow, mbunge wa Sengerema Bwana William Ngeleja alisema kuwa ni kawaida wabunge kupewa misaada na wafanyabiashara na taasisi za umma. Katika Maelezo yake alirudia tuhuma za kipuuzi dhidi yangu zilizokwisha tolewa huko nyuma kwamba

1) nilipewa fedha na kampuni ya PAP na
2) nilipewa fedha na shirika la NSSF.


Tuhuma zote hizo nimewahi kuzitolea ufafanuzi na kukanusha kwani hazina msingi wowote na zilikuwa siasa za majitaka. Hata hivyo bado zimekuwa zikijirudia rudia kwa malengo maalumu wanayoyajua wanaotoa tuhuma hizo. Watuhumiwa wa ufisadi wa escrow hawajazoea kuona taasisi za maadili zikifanya kazi kwa namna ilivyo sasa na hivyo wanajaribu na watajaribu kubwabwaja na kuhangaika ikiwemo kutaka kila mtu aonekane ni mtuhumiwa kama wao. Ndio maana Bwana Ngeleja ametaja msururu wa watu wakiwemo wafanyabiashara kwamba huwapa fedha wabunge bila chembe ya ushahidi.

Hivyo narudia kutamka kwamba ninataka uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo ufanyike mara moja, wenye ushahidi wapeleke kwenye vyombo vya uchunguzi na niitwe mbele ya Baraza la Maadili kujieleza. Nikiwa mbunge ambaye maisha yangu yote ya siasa nimeyatumia kupambana na ufisadi na kuchochea mabadiliko ili kujenga misingi madhubuti ya uwajibikaji na kuimarisha taasisi zake, nipo tayari kwa uchunguzi mahususi dhidi yangu dhidi ya tuhuma zilizotolewa na nyingine zozote ambazo mtanzania yeyote anazo dhidi yangu.

Naunga Mkono kwa nguvu kubwa kazi inayofanywa na Baraza la Maadili. Ni kazi ambayo ilipaswa kuwa imefanyika kwa muda mrefu sana kwa kashfa mbali mbali ambazo viongozi wa umma wamepata kama vile ile ya rada, rushwa katika manunuzi ya mafuta mazito kuendesha mitambo ya Umeme, kujipatia mikopo kwenye taasisi za umma bila kulipa, kujilimbikizia Mali tofauti na kipato nk. Hivyo naiomba Sekretariat ya maadili iyachukue kwa uzito maoni ya Bwana Ngeleja na kama yana uzito kwa mujibu wa sheria na kanuni yafanyiwe uchunguzi. Nipo tayari kufanyiwa uchunguzi.

Katika kujenga Misingi Madhubuti ya uwajibikaji nchini ni lazima kila kiongozi aheshimu taasisi kama Baraza la Maadili. Baraza likiendelea kufanya kazi kama inavyofanyika sasa, vita dhidi ya ufisadi itakuwa imepiga hatua na porojo za kuzushiana mitaani zitapungua.

 - Zitto Kabwe

The Karata TV series pilot episode


We would like to present to you the full pilot episode of the Karata Tv series

Synopsis:

Story of the septuagenarian anti terrorist operative and his team, who are on the tracks of a secret organization plotting to over throw the Tanzanian Government

You can watch on youtube if you click here

If you are also interested in seeing our other projects please find us on Facebook.com/bongosapien enterprises or click here

If you would like to support this project, advertise or have a project of your own call us on +255 714 028989

Also watch below the trailer as well as our video reel...

Katibu Mkuu Kiongozi afurahishwa uwepo wa SACCOs makazini

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue (kushoto) akimsikiliza Mshauri Mkuu na Mlezi wa Ikulu SACCOS Bw Joseph Sanga (wa pili kulia) akimuelezea mikakati ya ushirika huo wakati wa hafla fupi ya kumkabidhi kitabu chake cha uanachama wa ushirika huo Ikulu Dar es salaam. Wa pili kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Ikulu SACCOS, Bw. Deodatus Gaudio, akifuatiwa na Katibu wake Bw. Benedicto Damiano na kulia ni Mtunza Hazina Bi. Judith Medson.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amefurahishwa na uwepo wa vyama vya Ushirika vya Akiba na mikopo (SACCOS) katika taasisi na idara za serikali, akisema kuwa hilo ni jambo la maana kwa kuwa inatoa fursa kwa watumishi kuwa na kipato cha ziada kitachosaidia kuwaletea ahueni kwani mishahara pekee haikidhi matakwa yao yote.

Amesema SACCOS ni ​kama ​benki ya mtu mnyonge, na kusisitiza kwamba mifuko ya aina hiyo inaposimamiwa vizuri faida yake kwa wanachama ni kubwa sana kwani humpa mtumishi ahueni na kumfanya afanye kazi kwa moyo na bila wasiwasi ama usongo wa mawazo.

Balozi Sefue ameyasema hayo Jumanne Machi 3, 2015 jioni alipokuwa akiongea na uongozi wa Ikulu SACCOS, ​uli​omtembelea ofisini kwake Ikulu Dar es salaam kumkabidhi rasmi kitabu chake cha uanachama kufuatia kujiunga kwake na ushirika huo.

“Mishahara yetu ndani ya utumishi wa umma haitoshi kukidhi mahitaji yetu yote, kwa hiyo mipango yote hii ya SACCOS, Mfuko wa Rambirambi na Mfuko wa Ushirika
​iliyopo hapa Ikulu ​inafanya maisha ya mtumishi yawe na ahueni sana na kumfanya afanye kazi kwa moyo.

“Hayo ni mambo ambayo nayaamini sana na nayaunga mkono; na naamini hata Mhe Rais mwenyewe anayaunga mkono na ndio maana amekuwa mwepesi kujiunga na ushirika ”, amesema Balozi Sefue baada ya kukabidhiwa kitabu namba 2 na Makamu Mwenyekiti wa Ikulu SACCOS, Bw. Deodatus Gaudio. Kitabu namba moja amekabidhiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Awali, mshauri Mkuu na Mlezi wa Ushirika huo wa Ikulu, Bw. Joseph Sanga, alimfahamisha Katibu Mkuu Kiongozi kwamba mifuko ya SACCOS, Ushirika wa Nyumba na Rambirambi ya watumishi wa Ikulu iko imara na inaendelea kunufaisha wanachama wake kwa ufanisi.

Bw. Sanga amesema malengo makuu ya mifuko hiyo ni kuleta ustawi kwa watumishi na kwamba wote wanaelewa kuwa mikopo ya SACCOS yao sio kwa ajili ya kununulia chakula ama mavazi bali ni ya kuwekeza kwenye miradi itayowaongezea kipato.

“TUnataka kwenda mbali zaidi kwa kushirikiana na mfuko wetu ya Ushirika wa Nyumba ambo tayari umepeleka maombi ya ardhi kwa wanachama wake ambapo viwanja vikipatikana tuna mategemeo ya kuwapa mikopo kuvununua. Mpango huu una faida kwani ni wa amana kubwa na riba ndogo”, alisema Bw. Sanga alipokuwa anafafanua kuhusu mipango ya Ikulu SACCOS.


Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akipokea kitabu chake cha uanachama toka kwa Makamu Mwenyekiti wa Ikulu SACCOS, Bw. Deodatus Gaudio (wa tatu toka kulia). Wengine ni Katibu wa wa ushirika huo Bw. Benedicto Damiano (wa pili kulia), Mtunza Hazina Bi. Judith Medson ( wapili kushoto) na Mshauri Mkuu na Mlezi wa Ikulu SACCOS Bw Joseph Sanga kulia, wakati wa hafla fupi ya kumkabidhi kitabu chake cha uanachama wa ushirika huo Ikulu Dar es Salaam.


Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akionesha kitabu chake cha uanachama baadas ya kukabidhiwa na Makamu Mwenyekiti wa Ikulu SACCOS, Bw. Deodatus Gaudio wakishuhudiwa na Katibu wa wa ushirika huo Bw. Benedicto Damiano, Mtunza Hazina Bi. Judith Medson ( wapili kushoto) Mshauri Mkuu na Mlezi wa Ikulu SACCOS Bw Joseph Sanga kulia,wakati wa hafla fupi ya kumkabidhi kitabu chake cha uanachama wa ushirika huo Ikulu Dar es Salaam.

  • Taarifa ya Ikulu

Maonesho ya utalii ya ITB yaanza Ujerumani

Waonsehaji kutoka Tanzania wakiwa katika mazungumzo ya Kibiashara na wenzao kutoka nchi mbalimbali katika sikuu ya kwanza ya maonesho ya ITB jijini Berlin Ujerumani.

Maonesho ya Utalii ya kimataifa ya ITB ya siku tano yameanza leo jijini Berlin . Maonesho haya yanayofanyika kila mwaka na ambayo ni makubwa kuliko yote duniani yanahudhuriwa na waoneshajio zaidi ya 10000 kutoka nchi 190 duniani.

Tanzania katika maonesho haya inawakilishwa na waoneshaji 160 kutoka katika makampuni 60 kutoka sekta ya umma na binafsi . Taasisi za serikali zinazoshiriki maonesho haya ni Idara ya Utalii ya Wizara ya Maliaslili na Utalii, Bodi ya utalii Tanzania (TTB) ambao ndio waratibu wa ushiriki wa Tanzania katika maonesho haya. Nyingine ni Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Shirika la hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya hifadhi ya ya Bonde la Ngorongoro (NCAA), Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Jumuia ya Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Geofrey Meena Meneja Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania idadi ya makampuni na taaisi yanayoshiriki kutoka Tanzania katika onesho la ITB imekuwa ikiongezeka kila mwaka ambapo mwaka huu washiriki ni sitini (60) wakati mwaka jana jumla ya makampuni yalikuwa hamsini na tatu (53).

Miongoni mwa matukio muhimu yanayotarajiwa ni pamoja na tukio la siku ya Jumuia ya Afrika Mashariki katika maonesho haya litakayofanyika tarehe 6/2/2015 ambapo Tanzania kama mwenyekiti wa jumuia hiyo itakuwa mwenyeji wa tukio hilo litafanyika katika banda la Tanzania. 

Mawaziri wa Utalii kutoka nchi wanachama, mabalozi wa nchi hizo hapa Ujerumani na wageni wengine mbalimbali waalikwa wanatarajiwa kujumuika na mwenyeji wao Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Lazaro Nyalandu katika hafla hiyo katika banda la Tanzania.

Waoneshaji kutoka taasisi za umma wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mweneshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania Bi Devota Mdachi (wa tatu kulia) na Meneja Masoko wa TTB Bw. Geofrey Meena (wa Kwanza kulia) wakiwa katika kaunta ya banda la Tanzania katika maonesho ya ITB Ujerumani.


Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Mh. Philip Marmo katika picha ya pamoja na mabalozi wenzake wanaowakilisha nchi za jumuia ya Afrika Mashariki nchini Ujerumani sambamba na maafisa kutoka Bodi ya Utalii Tanzania na Jumuia ya Afrika Mashariki muda mfupi baada ya kumaliza kikao cha pamoja kujadili imaandalizi ya ‘siku ya jumuia ya Afrika Mashariki’ katika maonesho ya ITB itakayo fanyika tarehe 6/2/2015.

Taarifa ya Geofrey Tengeneza, Berlin

Mwaliko wa mkutano kujadili namna ya kudhibiti mauaji ya albino


YAH: MWALIKO WA KUHUDHURIA MKUTANO WA KUJADILI MIKAKATI YA KUDHIBITI MAUAJI YA KIKATILI KWA WATU WENYE ULEMAVU WA NGOZI (ALBINO), Kayanga Karagwe, Tarehe 17.3.2015 Ukumbi wa Halmashauri ya wilaya KUANZIA SAA 3 ASUBUHI

Rejea kichwa tajwa hapo juu.

Kufuatia ongezeko la kasi ya mauaji, ukatili na vitisho vya maisha dhidhi ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini, sisi Chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi (ALBINO) Tawi la mkoa wa Kagera, tunapenda kukukaribisha katika mkutano ili kwa pamoja kujadili namna ya kukabiliana na hali hii tete inayoendelea katika maeneo mbali mbali nchini kwa sasa dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Pamoja na matukio yaliyokwisha lipotiwa katika maeneo ya Geita, Mwanza na kwingineko nchini, Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa maeneo ambapo kumetokea mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ukichukulia mifano ya Ngara na Chato. Pia yapo matukio ambapo watu wenye ulemavu wa ngozi wameua mfano Kishanda kata ya Bugomora wilaya ya Kyerwa (2008), napengine makaburi yamefukuliwa kama kule Nyakasimbi, wilaya ya Karagwe (2009), Mtoto anusurika kuaua Nyakasimbi (2012).

Watu wenye ulemavu wa ngozi mkoani Kagera hivyo wamekuwa na wasi wasi mkubwa sana na kuhofia maisha yao. Hivyo tunaomba uungane nasi katika kupaza sauti ya pamoja yakukemea mauaji dhidi yetu, katika mkutano ambao umepangwa kufanyika tarehe 17 Marchi 2015 katika ukumbi wa ANGAZA uliopo mjini Kayanga wilayani Karagwe kuanzia majira ya saa tatu asubuhi.

Wako,

Ignas Rugemalira
Katibu
Chama cha albino- Kagera
0752 301351 au 0688 712303